0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Jul 20, 2010

UMESHAWAHI KUONA MTU ANAFUMANIWA KWA MKEWE WA NDOA?

Mwanamke haolewi mara mbili.
Picha kwa hisani ya Blog ya Maisha na Mafanikio


Je, umeshawahi kusikia mtu anashitakiwa kwa kuzini na mke wake wa ndoa? Ni swali la kuchekesha kidogo, lakini ukweli ni kwamba, jambo hilo, limeshawahi kutokea.


Wapi na kwa nani? Ilikuwa kwenye kesi ya Ramadhani dhidi ya Mohamed ya mwaka 1983 ukurasa wa 309 wa ripoti za sheria Tanzania (Tanzania Law Report).


Kesi hii ilianzia mahakama ya mwanzo ambapo mtuhumiwa alishitakiwa na Mohamed kwa kuzini na Mwanaidi wakati mwanaidi alikuwa ni mke halali wa ndoa wa Ramadhani. Katika kesi hii Ramadhani alishinda, lakini Ramadhani alikata rufaa katika mahakama ya wilaya na rufaa hiyo alishinda.


Lakini hata hivyo kwa uchungu wa kuporwa mkewe, Ramadhani naye alikata rufaa katika Mahakama kuu. Je, hukumu ilikuwa ni nini? Hebu tupate kwanza historia kamili ya kesi hii.


Hukumu katika mahakama kuu ilitolewa tarehe 29 mwezi Julai mwaka 1983, na katika hukumu hiyo, jaji alisoma historia ya kesi na historia hiyo ilianzia Desemba 1978 ambapo Ramadhani alimuoa Mwanaidi Mwiru na walikuwa wanakaa wote kwa wazazi wa mwanamke na Ramadhani alimlipia mkewe mahari ya ng’ombe wawili.


Mwaka 1980 Ramadhani alipata safari ya kibiashara na kwenda Endasak (bila shaka mkoani Arusha). Lakini mara tu bwana Ramadhani alipoondoka ndugu wa mke waliingiwa na tamaa na wakaamua kumwoza kwa mwanamume mwingine aliyeitwa Mohamed na ndoa ilifanyika tarehe 9 Julai 1980 kwa mahari ya ng’ombe watatu. Hata hivyo, ndoa hiyo haikudumu kwani mwezi Oktoba, 1980, walishindwana na Mwanaidi alirudi kwao na Mohamed aliahidiwa kurudishiwa ng’ombe wake.


Mwezi wa Novemba, mwaka 1980, Ramadhani alirudi nyumbani kutoka katika safari yake ya kibiashara na alishangaa kuambiwa kuwa ndani ya miezi kadhaa aliyokuwa hayupo, mkewe alishaozwa kwa bwana mwingine. Ramadhani hakutaka maneno mengi, bali alichofanya ni kwenda nyumbani kwa kina Mwanaidi na akamchukua Mwanaidi na kuondoka naye hadi nyumbani kwake.


Mwezi Aprili, mwaka 1982, Mohamed alimshitaki Ramadhani kwenye mahakama ya mwanzo, akidai kuwa Ramadhani alizini na mkewe (Mwanaidi)na hivyo anamdai fidia ya ng’ombe saba.Hata hivyo, madai yake hayo yalitupiliwa mbali na Ramadhani alishinda kesi hiyo na hakimu wa mahakama ya mwanzo alidai sababu ya kumpa ushindi Ramadhani ni kuwa ndoa yake ilitangulia, ingawa ndoa zote ni halali.


Mohamed hakupendezwa na kushindwa kwake katika kesi hiyo, hivyo alikata rufaa kwenye mahakama ya wilaya na katika mahakama hiyo mambo yaligeuka na Mohamed alishinda kesi na sababu ya kushinda, hakimu alisema ni kuwa ndoa ya Ramadhani ilikuwa ya kimyakimya yaani haikuwa na “shangwe za harusi,” hivyo ilikuwa ni batili na hata jamii haikufahamu kama Ramadhani alimwoa Mwanaidi, wakati ya Mohamed ilikuwa na shangwe na zaidi ya hapo ilifanyika baada ya matangazo ya siku 21 na ilifuata taratibu zote na hivyo ikajulikana na jamii nzima.


Katika kipindi hiki kulikuwa na mvutano kati ya wanasheria, kama ili ndoa itimie ni lazima kuwe na sherehe. Wapo waliosema kuwa, sherehe ni lazima ili ndoa iwe ndoa, lakini wengine walisimamia zaidi vifungu vya sheria na kusema shangwe si lazima alimradi tu kuwe na makubaliano huria na ndoa iwe kati ya jinsia mbili tofauti zilizodhamiria kuishi maisha yote pamoja.


Ramadhani hakufurahishwa na maamuzi hayo ya kuporwa mke wake yaliyofikiwa kwenye mahakama hiyo ya wilaya, hivyo naye alikata rufaa Mahakama Kuu.


Katika mahakama kuu suala lililokuwa katika mgongano lilikuwa ni ndoa ipi ni halali kati ya ile ya Ramadhani na ya Mohamed? Na katika kufikia maamuzi, Jaji alitumia sheria kama inavyosomeka, ‘literal meaning’ na hakuruhusu au hakutazama mazingira mengine katika kutafsiri maana ya ndoa.


Katika sheria ya ndoa ya mwaka 1971 aliyotumia Jaji, kifungu cha 9 (1) ndoa inatafsiriwa kama muunganiko huria kati ya mwanamume na mwanamke waliodhamiria kuishi pamoja kwa maisha yao yote. Zaidi ya hapo Jaji alisema kwamba katika jamii ambazo zinafuata sheria za kimila, ndoa halali huweza kufungwa kwa kutumia sheria za kimila na kutokuwepo shangwe za harusi na kutokufuata milolongo mingine, hakuwezi kubatilisha ndoa hiyo kama viini vyote vya ndoa halali halali kama ilivyotafsiriwa kwenye kifungu cha 9 (1) cha sheria ya ndoa ya mwaka 1971 vipo.


Jaji aliendelea kusema kuwa Ramadhani na mashahidi wake, akiwemo mshenga wake walithibitisha kuwepo kwa ndoa kati yake na Mwanaidi. Zaidi ya hapo Mwanaidi mwenyewe pia alikiri kuwa walifunga ndoa ya kimila na Ramadhani. Kwa kuongezea Mwanaidi alisema kuwa ndoa kati yake na Mohamed ilifanyika baada ya kulazimishwa na wazazi wake.


Hivyo, kutokana na sababu hizo hapo juu, Jaji alisema kwamba, ndoa kati ya Mwanaidi na Ramadhani ilikuwa halali japokuwa haikuwa na shangwe na aliibatilisha ndoa kati ya Mwanaidi na Mohamed.


Kwa kuongezea Jaji alisema kuwa sheria zetu haziruhusu mwanamke kuolewa na wanaume wawili kama inavyoonekana kwenye vifungu 15 (3) na 152 (1) vya sheria ya ndoa ya Tanzania ya mwaka 1971.

Kwa kumalizia Mahakama Kuu ilisema kwamba mahakama ya mwanzo haikufanya makosa kwa uamuzi iliyotoa, ingawa ilikosea pale tu iliposema ndoa zote ni halali. Hivyo, rufaa ilikubaliwa na Ramadhani alirudishiwa mkewe na Mohamed alitakiwa kulipa gharama za kesi hiyo.


6 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Jamani eeeeeeh, yaani humu duniani kuna visaaa.

  ReplyDelete
 2. Kweli dunia ina mambo.

  Ila nilipoiona picha ya mdada huyo hapo juu wa Kimasai mzungu nikajua ndi Mwanaidi mwenyewe. Kumbe ni mawazo tu siyo lazima yawe halali.

  ReplyDelete
 3. Aaah, mimi nafikiri wangefuata dini isingekuwa na tatizo si kuna kuulizwa `nani mwenye pingamizi' kukiwa kimya mara tatu jamaa ni wake, lakini sasa mpangaji na aliyekuwa kaoa awali alikuwa safari iweje!
  Mimi kwanza nashngaa watu hufungwa ndoa za kidini wakigombana wanaenda mahakamani ili iweje, mahaka ndio iliyowafungisha ndoa, nafikiri wangerejea kwa waliofungisha ndoa wakahukumiwa huko...naona wanaogopa manake ukienda kwenye dini ndoa sio rahisi kuvunjika

  ReplyDelete
 4. CRAZY WOMAN,,YUPO TUU NAYE HUYO MWANAMAMA ANAFANYWA KAMA MPIRA MBOVU,,HANA SAUTI WALA MSIMAMO ..INASIKITISHA KUWA NA KESI ZA KITAPELI KAMA HIZI,,PIA KATIKA UPANDE MWINGINE,,HUYU MWANAMAMA ANAWEZA AKAWA TAPELI...

  Il

  ReplyDelete
 5. Nilichoona zaidi hapa ni ugumu wa maisha na kumfanya mwanamke kuwa kama bidhaa katika jamii. Kwanini aozwe kwa mtu mwingine kwa tamaa?? Hata inavyoonyesha ni kwamba mwanamke hakuolewa kule kwa kupenda nandio maana haikumchukua muda kurudi. Wakati sasa umefika wa kuacha kuwafanya wanawake kama bidhaa na hili linaweza kufanyika kwa kushusha mahari na kuwa kitu kidogo kinachoashiria heshima kwa mila zetu. Mfano mzuri ni ule ambao juzi juzi kuna kijana alichajiwa shilingi elfu kumi na tano za bongo na ndoo ya plastiki!! Hii ni katika kuonyesha heshima yetu kwa mila zetu na si sababu za kiuchumi...

  ReplyDelete
 6. Na huyu Ramadhani naye,....! si alimshindwa akamrudisha kwao, sasa nini tena. Mwanamke nae anavutwa vutwa tu na yeye yumo tuuuu, aaaargh!

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi