0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Jul 17, 2010

UMEMFUMANIA, SASA UNASEMAJE?

Huna sababu ya kulia, uamuzi unao mwenyewe

Wiki kadhaa zilizopita niliwahi kuandika kuhusu fumanizi au kutoka nje ya ndoa. Na leo ningependa kuzungumzia jambo hilo kwa kuwa nimekuwa nikipata email kutoka kwa wasomaji wa blog hii wakitaka ufafanuzi zaidi wa kile nilichojadili. Kama hukubahatisha kusoma mada hiyo, unaweza kubofya hapa kujikumbusha.

Hebu fikiria kuwa umedhibitisha kwamba mwenzako sio mwaminifu, yaani ametoka au anatoka nje ya ndoa, utafanyaje? Je, utaondoka, utalipa kisasi na wewe, au utachukua hatua gani?

Kuna mambo ambayo ukiona kwamba yamejitokeza, baada ya fumanizi, unapaswa kujua nafasi yako kwenye uhusiano wako. Kutokea hapo ndipo unapoweza kuamua kama uondoke au hapana.

Kwanza, hebu jikague, Je, umevunjika moyo kupita kiasi? Unadhani itakuwa bora kuvumilia? Unadhani kumvaa na kumwambia umechoka na unataka kuondoka itakuwa ni kujiongezea mfadhaiko zaidi?

Pili, unadhani utaendelea kubaki katika ndoa kwa sababu za kidini? Unataka kufanya kitu kilicho sahihi daima? Uko tayari kuendelea kudhalilika na kuwa hatarini kwa sababu ya imani yako ya kukukataza kuvunja ndoa? Je ni kwa imani yako au wasiwasi wako umelazimika kubaki? Nijuavyo mimi, kosa la kutoka nje halitetewi na dini yoyote linapokuja swala la kuvunja ndoa.

Tatu, unadhani unalazimika kubaki kwa usalama wa watoto? Unadhani ni wewe pekee unawajali watoto na mwenzio hawajali? Inawezekana na mzazi mwenzio pia ni mpenda watoto? Unadhani kuachana kutawaletea watoto matatizo zaidi? Una wasiwasi na maisha ya watoto kama utaamua kuondoka? Kumbuka kuishi kwenye vurugu za ndoa huwavuruga watoto kuliko watoto kuishi na baba au mama wa kambo mwenye upendo.

Nne, unadhani hakuna uwezekano kabisa katika ndoa hii? Umekwama? Umenata kama ulimbona huwezi kuondoka? Unaweza kufikia muafaka kwamba umejitahidi kwa uwezo wako wote kumrekebisha mwenzio lakini wapi. Hivyo umeamua kuishi hivyo hivyo?

Tano, unadhani huwezi kuondoka? Kuna kitu unachodhani kinakuletea ugumu wa kuanza safari? Kuanza maisha mapya? Huna uwezo wa kujiamulia? Kumbuka kwamba, huenda ni mazoea tu yanayokuzuia au utegemezi wa kipato. Lakini, kila binadamu ameletwa duniani ili asimame kama yeye, na siyo kama kipande cha mwenzake.

Sita, unataka kumlinda? Kuna kitu kibaya unachodhani kinaweza kutokea kama utaamua kuondoka? Ataweza kuishi peke yake? Kama utaondoka unadhani itakuwa ni njia ya kumpeleka shimoni zaidi? Umeamua kubaki ukijua kwamba baada ya muda tatizo lenu linaweza kutatuliwa? Inawezekana likatatuliwa, lakini inawezekana wewe ni mtu wa kuumia kwa sababu ya wengine bila sababu.

Saba, unaendelea kuishi naye kwa sababu kuna hatari kumwambia unataka kuondoka? Unadhani atalipuka kwa hasira utakapomwambia unataka kuondoka? Una wasiwasi kwamba una haki ya kuamua kuhusu maisha yako na kuna sheria zinazokulinda.

Je, hujafikiria namna ya kuanza maisha mapya? Hii ni tofauti na hofu ya kuanza maisha mapya. Labda maisha yako, yake na ya watoto yameambatanishwa kupita kiasi, hivyo inakuwia vigumu kujinasua? Pia kuambatanishwa huku labda ndiko kunakokufanya hata usiwe na chembe ya wazo la kutaka kuondoka? Umewahi kufikiria kuhusu utashi wako, ujuzi wako, ndoto zako, matumaini yako na mustakabali wa maisha yako bila yeye, au bila watoto?

Chukua muda wa kutosha kufikiri kwa makini na uyajibu maswali hayo yote ukishayajibu utakuta unatoa uamuzi sahihi utakaokupeleka kwenye maisha uyatakayo. Kumbuka, kila binadamu hukosea na kusamehe kwa aliyekosewa. Lakini kusamehe hakuna maana ya kuendelea kuumia au kuumizwa na uliyemsamehe.

3 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Wapo wengi ambao wanafanya hivyo kuwa hwataki kuondoka na kukubali kupata mateso yaani kuitesa ndoa. Kwa kweli haya si maisha. Lakini kwa nini kila wakati inakuwa ni mke aondoke je kwa nini mume? Nimewza kwa sauti na naacha kuwaza zaidi.

  ReplyDelete
 2. Ni mada nzuri sana kaka Kaluse. Tatizo la kufumania huwaacha njia panda watu wengi sana kiasi cha kutofahamu yepi yatakuwa maamuzi sahihi.

  Nami nazidi kuitafakari kwa sauti kubwa.

  Uwe na Jumapili njema.

  ReplyDelete
 3. Nakushukuru sana na kuwashukuru wengine kwani hizi mada za ndoa na mapenzi zinashika kasi kila ukiingia kwenye blogi zinazowajali wanajamii.
  Hii mada inanikumbusha jamaa mmoja aliyemfumania mke wake. Cha ajabu hakufanya kitu chochote alipowafumania uso kwa uso na kuhakikisha tendo likifanyika.Yeye alirudi sebuleni akawa anajisomea vitabu vyake vya saikolojia.
  Wale hawakuweza kumalizia shughuli yao kwasababu wamefumaniwa kila kitu kilikosa nguvu. Jamaa dume likatoka likiogopa litapata kipigo, lakini hakuna kitu kama hicho kilichotokea. Alipotoka nje yule mume mtu akafunga mlango wake halafu akaenda kitandani kwa mke wake ambaye alikuwa kajifunika gubigubi huku analia. Hakumsemesha zaidi ya salama na pole kwa kazi za mcha kutwa.
  Siku, mawiki na miezi ikapita jamaa hakusema kitu wala hakufanya kitu kama vile hakuna kilichotokea. Mke akaanza kukonda kwa mawazo, akawa hana raha, kila siku anaogopa huenda kipigo kitatokea lakini wapiiii!
  Mke akaona atakufa kwa mawazo na wasiwasi ikabidi yeye aitishe kikao cha wanafamilia. Ndugu walipokuja jamaa akaulizwa nini kulikoni. Yeye akasema mbona hakuna tatizo, mimi nashangaa nyie mumefuata nini hapa, hakuna tatizo.
  Mke ikabidi aeleze ukweli, kuwa alifumaniwa lakini anashangaa mumewe hajamsema wala kumuadhibu.
  Jamaa alisema baadaye kuwa amefurahi sana mke wake kukubali kosa tena mbele ya wazee wote, lakini anaushahidi kuwa hiyo sio mara ya kwanza kwa mke wake kufanya hivyo na kwahiyo yeye na mke huyo basi...akatoa talaka...na nini kilifuata baadaye niulize.
  Sasa kufumaniana ni rahisi kuongea kwa mdomo lakini likikukuta jambo hilo kunahitaji moyo na ujasiri na wa kuvumilia.

  Ni vyema tukajiuliza je mimi sijawahi kufanya kosa hilo ndipo nichukue hatua nitakayochukua. Kama hujawahi mshukuru mungu wako na muombee mwezako , mpe shule kama utaweza, na kama ukiona tendo hilo limefanyika kwa `tabia' mbaya za huyo mwenza ni bora ufikiri mara mbili.
  emu-three

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi