May 23, 2012

WANAWAKE WANAVYOIVAA MIKENGE KWENYE NDOA..............!



Ngoja leo niyadadavue makosa yanayofanywa na wanawake wengi pale wanapoamua ni nani wa kuoana naye:

1. Kosa la kwanza, unaolewa na mtu ambaye unajua kabisa ni dhaifu na mkorofi, ukitarajia kwamba ataondoa kasoro zake akiwa ndani ya ndoa. Hili ni kosa kubwa. Kama huna furaha sasa na mtu kabla hujaoana naye, usikubali kuingia huo mkenge. Huwezi kutegemea mtu kuadilika aiwa ndani ya ndoa.

2. Kosa la pili, unaolewa na mtu asiye sahihi kwa sababu ya msisimko wa mwili kimapenzi lakini si kwa sababu ya tabia zake. Kuwa mwangalifu na neno “Nakupenda” neno hili mara nyingi maana yake ni “Nina uchu nawe.” Ndiyo amevutiwa nawekimaumbile, lakini undani wa tabia yake unaujua? Hapa kuna mambo manne… Kwanza, Je anapenda kutomfanyia binadamu mwenzie mabaya kama mabavyo yeye hataki kufanyiwa? Pili, anaishi vipi na watu wengine? Anaishi vipi na watu ambao ana uadui nao, Anawasamehe au analipiza visasi? Je anatoa misaada kwa masikini? Tatu, je ni mkweli, anachokisema ndicho anachokifanya? Je anaaminika? Majukumu anayoahidi kuyafanya anayatimiza? Nne, je anajipenda? Je ni mtu ambaye yuko imara kimapenzi au ni mtu wa kuyumbayumba na asiye na msimamo? Sio mtu akishauriwa na marafiki zake au ndugu zake huko, anakuja na maamuzi yasiyo na kichwa wala miguu

3. Kosa la tatu, unaolewa na mtu ambaye hamna malengo na vipaumbele vya aina moja vya maisha. Je mna utashi wa aina moja? Kwa mfano ni vyema mwanamuziki akaolewa na mwanamuziki mwenzie kwa kuwa anajua mzingira ya kazi ya mwenzie ili kupunguza wivu wa kupindukia usio wa lazima

4. Kosa la nne, unaolewa na mtu asiye sahihi kwa sababu mnakutana kimwili mapema mno. Kukutana kimwili kabla ya ndoa kunaweza kuleta matatizo makubwa mno. Tendo la ndoa kabla ya ndoa hufunika uwezo wa mtu kufikiri. Mtu anabaki kufaidi na kubaki kujali mapenzi ya kimwili na kusahau kukuna ubongo juu ya mambo mengine. Ni lazima mwanamke akune ubongo ili kujua kama huyo mpenzi anakidhi vigezo vyote vya mume mtarajiwa.

5. Kosa la tano, unaolewa na mtu ambaye huna msisimko wa kimwili umwonapo. Kuna uwezekano mkubwa mwanamke akavutiwa na mwanaume kwa sababu ya aina ya gari analomiliki. Hapa hakuna msisimko wa kimwili bali mwanamke kavutwa na gari au rasilimali alizo nazo mwanaume huyo.

6. Kosa la sita, unaolewa na mwanaume anayependa kudhibiti. kuwa na tabia ya kudhibiti wenzako ni ya dalili za mtu jeuri na mwenye kujisikia na mfujaji. Naomba kutofautisha kati ya “kudhibiti” na “kutoa mawazo.” Mtu anayekupa mawazo ni kwa faida yako, lakini anayekudhibiti ni kwa faida yake.

7. Kosa la saba, unaolewa na mtu asiye sahihi kwa sababu unakimbia matatizo uliyo nayo. Unaweza kuwa hujaolewa na huna raha wala amani na ukataka kuolewa. Ndo haiwezi kukutatulia matatizo yako binafsi ya kisaikolojia nay a kimapenzi. Badala a kuyapunguza matatizo hayo, ndoa itayaoneza. Kama huna amani na huyafuahii maisha, chukua jukumu la kurekebisha matatizo hayo sasa kabla hujaolewa. Itakuwa ni faida kwako na kwa mmeo mtarajiwa.

8. Kosa la nane, unaolewa na mtu asiya sahihi kwa kuwa yuko ndani ya pembe tatu. Mtu ambaye anaishi na wazazi wake ni moja ya mfano wa mtu anayeishi katika pembe tatu. Watu wengine wanaoweza wakawa wanaishi ndani ya pembe tatu ni kama wanaofanya kazi saa 24! Huyu mtu halali? Watu wengine walio katika pembe tatu ni watu wanaotumia madawa ya kulevya, mtu anayetawaliwa na “hobbie” zake, anapenda sana michezo (Mpira), kuperuzi mitandao ya kijamii na anapenda sana fedha. Hakikisha kwamba wewe na mpenzi wako , nyote hamtawaliwi na pembe tatu. Mtu ambaye anatawaliwa na pembe tatu hawezi kumtimizia mpenzi wake haja ya upendo atakapokuwa anahitaji. Kama mpenzi wako anatawaliwa na pembe tatu kwa kiasi kikubwa, wewe huwezi kuwa kipaumbele chake.

WANAUME NA WANAWAKE WANAPOLALAMIKA ...........!




Ngoja niyadadavue malalamiko ya wanawake kwanza hapa chini:

1. Wanawake wanalalamika kwamba wanaume sio waelewa wazuri, yaani huwa wanatafsiri mambo tofauti na isivyo.

2. Wanalalamika kwamba wanaume huwa hawajali hisia za wapenzi wao wala hawajali pia kuhusu mahitaji yao.

3. Wanalalamika kwamba wanaume huwa hawajui kuonesha upendo , yaani hata wanapopenda inakuwa kama vile wanajisumbua tu, kiasi kwamba mwanamke anaweza kuhisi kwamba hapendwi.

4. Wanalalamika kwamba wanaume huwa hawana muda wa kucheza na wapenzi wao kabla hawajafanya nao mapenzi yaani hawawaandai kabla ya tendo, wao huwarukia tu na kumaliza haja zao haraka na kugeuka ukutani kabla ya wao (wanawake) hawajaridhika.

5. Wanalalamika kwamba wanaume hawana mawasiliano, huwa hawajui kueleza hisia zao na mawazo yao, bali ni watu wa kunyamaza na kujifungia kwenye dunia yao wenyewe. Wanahisi kama kuelezea hisia zao na mawazo yao ni kuwa dhaifu.

6. Wanawake hulalamika kwamba, wanaume hawana muda wa kukaa nyumbani na familia zao, kwa sehemu kubwa ni watu wa nje tu.

7. Wanawake pia wanawalaumu wanaume kwamba, hawajali mustakabali wa usafi au kupendeza kwa nyumba.

8. Wanawake wanawalalamika kwamba, wanaume huwa wanafanya maamuzi yao bila kujali kuwa wanawake wapo na wanaweza kuwa na michango mizuri sana kwa hicho wanachotaka kukifanya. Huamua kama kwamba wanawake siyo sehemu ya familia.

9. Wanalaumu kwamba, wanaume ndiyo wanaoanzisha au kuendekeza kutoka nje ya ndoa ukilinganisha na wao wanawake.



Malalamiko ya wanaume nayo nayadadavua kama ifuatavyo…..

1. Wanaume wanalalamika kwamba wanawake ni watu wa kulalamika, kukosoa na wenye vijineno vya hapa na pale visivyo na maana na vyenye kukera.

2. Wanaume wanalalamika kwamba wanawake wanajaribu sana kuwadhibiti na kuwakandamiza pale wanapoachiwa nafasi kidogo.

3. Wanaume wanadai kwamba wanawake huwa hawana furaha, mara nyingi wanaonekana kama vile wako kwenye simanzi fulani na wanapenda sana kununanuna hasa pale wanaume wanaposhindwa kuwatekelezea kile walichotaka hata kama hakina umuhimu kwa wakati ule.

4. Wanaume wanalalamika sana kwamba wanawake wanawanyima unyumba kama adhabu ya kuwakomoa. Siyo kuwakomoa tu, bali huwa wanafanya hivyo kwa lengo la kuwashurutisha wakubaliane na utashi wao fulani.

5. Lalamiko lingine la wanaume kuhusu wanawake ni lile la kwamba, huwa hawafikirii kwa mantiki, bali mara nyingi kufikiri kwao huwa kunakumbwa na mhemko. Kwa hiyo, uamuzi wao mwingi hauangalii mantiki bali hujali zaidi hisia zao.

6. Wanawake wanalalamikiwa na wanaume kwamba, hali zao za kihisia huwa hazitabiriki. Yaani huwa zinabadilika kufuatana na mabadiliko ya miili yao ya kihomoni miilini mwao nyakati kama zile za siku zao(hedhi), nyakati za ujauzito na hata wanapokoma kuziona siku zao(menopause) .

7. Wanaume wanawalalamikia wanawake kwa tabia yao ya umbea, kwamba midomo yao huwasha sana hadi waseme kile walichokiona au kukisikia hata kama si lazima na pengine ni hatari.

8. Wanawake wanalalamikiwa pia na wanaume kwamba, huwa wanatoka nje ya ndoa, hasa wanapohisi kukosewa upendo ndani, jambo ambalo haliwezi kuleta suluhu kwa tatizo hilo.

Kama wewe ni mwanaume na umegundua kwamba moja au baadhi ya malalamiko ya wanawake yanakugusa inabidi ubadilike na kufanya kinyume chake. Kama wewe ni mwanamke pia hali ni kama hiyo. Kama kweli una mdomo mwingi kwa mfano, ujue wanaume hawapendi tabia hiyo, hivyo huna budi kubadilika.

May 17, 2012

UNATAKA KUMUACHA MKE MKOROFI? FANYA HIVI.........!






Kuna wanaume ambao wametokea kuoa wanawake ambao wana tabia mbaya . ninaposema kuwa na tabia mbaya sina maana ya mwanamke kuwa Malaya, maana hiyo ni fasili rahisi ya tabia mbaya kwa watu walio wengi. Ninaposema tabia mbaya nina maana kwenda kinyume na matarajio ya mume na pengine hata kwenda kinyume na matarajio ya jamii. Mwanamke ambaye ana tabia kama ghubu, mdomo mdomo (mkosoaji), mtapanyaji wa mali, mpenda makuu na tabia nyingine za aina hiyo, ni mwanamke ambaye kwa kiasi kikubwa anaweza kumsababishia mume matatizo ya kimwili na kisaikolojia. Mwanamke wa aina hii anaweza hata kuathiri makuzi ya watoto na kuathiri uhusiano na mume na watu wengine waliyo karibu yake. Kama mwanamke wa aina hii ameolewa na mume mweledi ndoa inaweza isiyumbe sana, lakini hii ina mipaka na kiwango chake.

Kuna wakati matatizo haya huweza kufika mbali zaidi kiasi kwamba huanza kumwathiri mume. Mwanaume ambaye huchukua kila uamuzi unaohusu maisha yake kwa hadhari kubwa, anaweza kuendelea kuishi na mke huyu. Lakini mara nyingi kuendelea kuishi na mke huyu kuna maana ya matatizo zaidi kuliko ufumbuzi. Bila shaka mmeshawahi kusikia wanaume ambao wanalalamika kuhusu tabia mbaya za wake zao (hata hapa JF wapo wengi sana), lakini huku wakiendelea bado kuwa na wake hao. Ukiacha sababu ya kugawana mali, wanaume wengi huwa wanafikiria mambo mengi ambayo huwazuia kuchukua uamuzi wa kuachana na wake hao.

Nimeona itakuwa vizuri kuwaambia wanaume hawa kwamba, kama ndoa zao zimefikia mahali ambapo zinataka kuwatia kichaa, wakiwa na uhakika kwamba wake zao ndio wenye matatizo na sio wao, (hili inabidi waliangalie kwa makini) inabidi wafanye uamuzi kwa kujiangalia wao na watoto wao zaidi kuliko watu au vitu vingine. Baadhi ya mambo ya kuangalia ni haya:

1. Kuathirika kwao: wajiulize wanaumia kiasi gani kimwili na kisaikolojia kwa kuendelea kuishi kwao na wanwake hawa. Kama ni ghubu na kukosolewa, kunawaathiri kiasi gani,? Na kama ni utumiaji mbaya wa mali unawaathiri kwa kiasi gani? Kama athari za tabia mbaya alizo nazo mwanamke zinafaa kudharauliwa na mume anaweza kuzidharau ni vyema akafanya hivyo, na kuendelea na maisha. Na kama akiona kuzidharau tabia hizo itakuwa na maana ya angamio kwake na pengine mbaya zaidi kwa watoto, inabidi hiyo iwe ni sababu ya msingi kuachana na mke huyo.

2. Ndugu watasemaje: wanaume wengi hukwamia hapo. Kama wake zao wanaelewana vizuri na baadhi ya ndugu, au hata wazazi wao, wanaume hushindwa kutoa maamuzi wa kuwaacha kwa hofu ya kulaumiwa na kushangawa. Wakati mwingine mume huyu anaelewena sana na watu wa upande wa pili, yaani ndugu wa mke na hasa wazazi na pengine wote. Hiki nacho ni kikwazo kikbwa sana, kwani mume hufikiria jinsi atakavyoonekana kwa watu hawa, pale atakapoamua kuchukua uamuzi wa kumuacha mkewe.

3. Sifa moja nzuri: pamoja na kuwa na matatizo, kila binadamu anaweza kuwa na upande mzuri. Kama mwanamke huyu ana sifa fulani ambayo ni nzuri sana, tuseme ni mpishi hodari sana na mkarinu kwa wageni , au labda ni mwaminifu sana katika ndoa, mwanaume anaweza kukwama kutoa uamuzi kwa kudhani au kujidanganya kwamba huenda anaweza asipate mwanamke mwingine mwenye sifa kama hizo. Huku ni kujidanganya kwa sababu kila sifa aliyo nayo binadamu fulani, ya kitabia, ipo kwa binadamu mwingine hata kama siyo wengi.

Ukweli ni kwamba mwanaume anaweza kushindwa kumpa talaka mkewe ambaye anakaribia kumuuwa kwa matatizo yake kwa sababu ambazo mtu mwingine anaweza kuzishangaa. Lakini jambo la msingi kwa mwanaume kama huyu ni kujaribu kupima kwa makini, je hizo sababu zinazomfanya asite kuachana na mkewe huyu zina nguvu au maana kuliko maisha yake, hasa mwili na akili yake?.



Angalizo: Sishauri watu kuachana, lakini nashauri watu kujua kwamba ndoa zenye mashaka makubwa ni hatari kwa afya na maisha yao.

May 16, 2012

WANAWAKE NA KABURI LA MAPEMA.....!






Hivi karibuni nimesoma utafiti katika makabrasha yangu kuhusiana na maradhi mbalimbali yanayowakabili wanawake walioko kwenye ndoa au uhusiano wenye mashaka. Tafiti zinaonyesha kwamba, wanawake wote ambao wana mashaka na wasiwasi kuhusu usalama wa ndoa zao, wasiowaamini waume zao, kwa kawaida, wanakuwa na kinga dhaifu sana dhidi ya maradhi. Haiyumkini hata wale wanawake waliosemwa kuwa wamekufa kwa ukimwi huku waume zao wakiendelea kudunda na maisha na pengine hata kuoa na kuzaa kama kawaida, wake hao walipoteza maisha kutokana na sababu hii.

Mtafiti mmoja Angelo Picardi wa Italia anasema, amethibitisha kuhusu hilo kwa kuwakagua wanawake wapatao 61. Kumbuka kwenye miili yetu kuna seli ambazo kimaumbile kazi yake ni kupambana na maradhi. Kwa wale wanawake wanaoishi kwenye ndoa za mashaka, ambapo hawawaamini waume zao na huku wakihofia kupoteza ndoa zao, mfumo wao wa seli hizo za kinga ni dhaifu, ukilinganisha na wanawake ambao hawana wasiwasi na ndoa zao huvunjika au kuachwa na waume zao.

Maana yake ni nini? Ni kwamba, wanawake ambao wana hofu kwamba, waume zao wanaweza kuwaacha na hivyo kuhisi kutishika na wale ambao wana wivu kwa sababu hawajiamini, hushikwa na maradhi kirahisi sana. Ni rahisi kwao kuwa nyondenyonde kwa sababu mfumo wa kinga katika miili yao umezorota sana. Kuna maradhi ya utegemezi wa kihisia (co-dependence) ambayo ni maradhi ya kiakili, yanayomfanya mtu kuamini kwamba, bila mwingine kuwepo au kuwa karibu naye, hawezi kuishi. Kwa hali hiyo, siwezi kuwalaumu hawa. Lakini napenda kuwaambia kwamba, wanaumwa. Nadhani siyo vibaya kumkumbusha mtu kwamba, tatizo alilonalo ni maradhi, ili atafute tiba.

Bahati mbaya kuumwa kwao huko, huwaletea maradhi mengine, mengi sana kwa sababu ya kushuka kwa kinga ya mwili kama nilivyobainisha hapo awali. Ninavyojua ni kwamba, mtu akiwa na wasiwasi na hofu za kila wakati huharibu kinga na mwili wake kila siku unakuwa kwenye maradhi yasiyoisha. Idadi kubwa ya wanawake wenye shinikizo la damu au hata kisukari, ukichunguza utakuta chanzo cha maradhi hayo ni madhila ya ndoa. Kwenye ukoo hawana historia ya maradhi hayo na staili za maisha yao haziwaweki kwenye uwezekano wa kuyapata, lakini wasiwasi na mashaka ya ndoa, ndiyo chanzo.

Wakati mwingine, mume anaweza kuwa anamwambia mkewe karibu kila siku, ‘nitakuacha mimi’ au ‘nitakurudisha kwenu ukiniletea ujinga.’ Mke huogopa na huanza kujiona akiwa hana usalama tena, kwani akicheza atarudishwa kwao. Naye anaamini kurudishwa kwao ni jambo baya kuliko yote maishani. Hebu nikuulize wewe mwanamke. Hivi ni kitu gani kinachokupa hofu kwamba, mumeo atakuacha na kwenda kuchukua mwanamke mwingine? Lakini hata kama akifanya hivyo, hebu niambie, ina maana ni kweli unaamini hutaweza kuishi? Jaribu kufikiri tena upya, kwa sababu kama unaamini hivyo unajidanganya.

Kumbuka mwanaume huyo anaweza kufa, kama ambavyo wewe unaweza kufa. Hebu fikiria kwamba, mumeo amekufa, ina maana nawe utaona kuishi hakuna maana? Kama ni hivyo, unaumwa, tena unaumwa sana. Unaweza kukuta mwanamke ana ajira yake au ni mjasiriamali aliyesimama kimtaji, na ni yeye mwenye kuilisha familia, lakini anaamini hawezi kuishi bila mumewe. Huu ndio unaitwa utegemezi wa kihisia, sio wa kifedha au kitu kingine.

Wataalamu wanasema, kati ya vifo kumi vya wanawake ambavyo vinatokana na maradhi yasababishwayo na mateso ya ndoa, vitano vinatoka kwenye utegemezi wa kihisia. Mwanamke anaumwa, analazwa hospitalini hadi anatoka, mume hana habari. Lakini, akitoka yeye ndiye mwenye kuhalalisha mumewe kutoenda kumwona wakati alipokuwa anaumwa. ‘Najua ulikuwa na shughuli nyingi, wala usijali mume wangu, mradi nimeshapona.’ Atamwambia mumewe kwa unyenyekevu. Haya ni maradhi mabaya sana na yanahitaji tiba ya haraka kuliko hata Malaria Sugu.

WANAWAKE KUTEMBEA NUSU UCHI, KUMBE WANA LAO JAMBO.....!



Kuna wakati wanaume hudhani kwamba, wanawake wanaovaa nusu uchi huwa wanafanya hivyo kwa sababu ya kutafuta soko kwa wanaume. Inawezekana kukawa na wale ambao wana sababu hizo, lakini wapo wale ambao wanalipa fidia kutokana na kuamini kwao kwamba, sura zao zimewaangusha, hivyo miguu yao mizuri inabidi kuziba pengo au udhaifu huo.


Wakati mwingine hata wanawake wanaodhani au kudhaniwa kuwa ni wazuri, wamekuwa wakivaa nguo fupi zinazoonyesha maungo yao. Hawa nao ni lazima wanalipa fidia ya kasoro fulani waliyo nayo. Inawezekana wameshindwa kulinda ndoa zao, au inawezekana hawajaolewa na sasa wanataka kuonyesha kwamba, pamoja na kutoolewa kwao, bado wao wana sura na miguu au miili mizuri.


Udhaifu wowote ambao unamkera mwanamke iwe ni wa moja kwa moja au kupitia nyuma ya ubongo wake, unaweza kuonyeshwa kwa mwanamke huyo kuyatangaza yale maeneo ya mwili wake ambayo anaamini ni mazuri. Kuyatangaza huko humpa ahueni kwa kuamini kwamba bado anayo thamani, kwani ataangaliwa sana na wanaume, kusifiwa na pengine kutongozwa.


Hebu angalia wanawake ambao wanavaa nguo za kubana huku wakiwa na makalio makubwa. Hawa mara nyingi wana sura ambazo wao au wengi huamini kwamba ni mbaya. Huvaa nguo hizi ili kuonyesha kwamba, pamoja na ubaya wa sura zao, bado wao ni wazuri sana katika maeneo mengine ya mwili ambayo wanaume na hata wanawake wengi huyapenda au kutamani kuwa nayo.


Wengi hawavai tu nguo hizi za kubana kwa sababu ni fasheni, la hasha, wengi hili ni kimbilio la udhaifu wao.


May 12, 2012

WANAUME KATIKA MAPENZI NI KAMA MASOKWE...!


 
Katika utafiti uliofanywa na akina Kruger na wenzake kwa wanyama jamii ya Sokwe, ilibainika kwamba kulikuwa na vifo vingi vya Sokwe madume wenye umri wa miaka 13. Hali hii ilitokana na sababu kwamba, kwa kawaida katika umri huo, Sokwe madume huwa  wamefikia umri wa kupanda na kufanya mapenzi na hivyo huanza kushindana wenyewe kwa wenyewe wakigombea majike na hata kwa lengo la kudumisha hadhi yao miongoni mwa Sokwe wengine.


Katika hatua hii Sokwe hao hufikia mahali pa kupigana na hata kuuana kwa lengo la kujipatia wapenzi na kudumisha hadhi zao. Hali hii haiko kwa sokwe peke yao, bali hata kwa wanyama wengine pamoja na ndege wa aina mbalimbali.


Hata hivyo, pamoja na ukweli huo binadamu naye hajanusurika hata kidogo na purukushani za aina hiyo. Labda kinachomtofautisha binadamu na wanyama hao ni namna wanavyokabiliana na mashindano hayo. Lakini ukweli unabaki palepale kwamba, hata akichagua njia ya aina gani ili kushindana na binadamu wenzake, bado matokeo ya mwisho yatafanana na yale ya wanyama, yaani kifo.


Imeonekana wazi kwamba binadamu wa kiume ndiye mwenye mwelekeo mkubwa wa kupenda purukushani na kuhatarisha maisha yake. Ingawa binadamu huyu wa kiume au mwanaume hahitaji kupigana mweleka na mwanaume mwenzake ili kumpata mwanamke, lakini harakati zake ni zaidi ya kupigana mweleka.


Hata hivyo katika mazingira mengine, mieleka hupiganwa sana katika sura ya mieleka halisi au katika sura nyingine za ushindani wa kutafuta ushindi katika kumpata mwanamke. Wengi tunajua kuhusu habari za kuuawa kwa wanaume kutokana na vurugu za kugombea wanawake.  


Tabia hii ya wanaume ya kuhatarisha maisha si ya leo, bali ni ya tangu kale. Huenda huko nyuma baadhi ya wanaume walitumia silaha kwa lengo la kuwadhulumu ama kuwauwa wanaume wenzao ili hatimaye waweze kuwamiliki wanawake wanaowapenda.
Kwa kawaida, wanaume hushindana wao kwa wao kwa lengo la kumiliki rasilimali na kuhifadhi au kudumisha hadhi na heshima yao ndani ya jamii wanamoishi.


Huu ndio ukweli wenyewe ambao hautofautiani hata chembe na ule wa Sokwe. Ukweli ni kwamba mwanaume anapokuwa na uwezo wa kumiliki rasilimali adimu kama vile fedha na anapoweza kusimika kwa uhakika heshima na hadhi yake, ndani ya jamii iliyomzunguka, mambo hayo humpatia thamani kubwa na kumrahisishia kazi ya kumpata mwanamke anayemtaka.   


Apr 18, 2012

KUMBUKUMBU YA KIFO CHA MUNGA TEHENAN..........!

Kwa wadau wote wa FAJI na waliokuwa wapenzi wa Gazeti la JITAMBUE. Mke wa Hayati Munga Tehenan na wana FAJI, watafanya kumbukumbu ya kifo cha MUNGA TEHENAN. Shughuli hiyo itafanyika katika msikiti wa Kimara na sadaka ya chakula itatolewa katika ofisi za Faji Kimara Rombo.
Bajeti kwa wageni wanaotarajiwa kufikia idadi ya 120 ni Tsh. 631,000. Tunahitaji michango ya wadau kwa hali na mali ili kufanikisha shughuli hiyo. Mtu yeyote mwenye nia ya kuchangia, tunaomba atume mchango kwa M-PESA 0764 461366 au awasiliane na Dr. Johntabata kwa namba hii 0713 250701 au kwa namba yangu 0715 729292

Atakayesoma taarifa hii amjulishe mwenzie……………

Apr 10, 2012

FUMANIZI-MWANAUME ANAPOKUWA KIJOGOO NA MWANAMKE KAHABA

Mara nyingi hujikuta wakiwa na wakati mgumu


Wanaume wengi huwachukulia wanawake kama mali zao, ambazo ni wao tu wanaotakiwa kuzimiliki kwa namna fulani. Mali yako ni mali yako, ikitumiwa na mtu mwingine, huumiza hisia. Lakini, mali hii inayoitwa mwanamke, mbona ina utambuzi wake? Kila wakati ukisoma kuhusu mauaji ya wivu wa kimapenzi, wanawake ndio ambao wanauawa zaidi.


Lakini ukija kusoma takwimu za wanaotoka nje, wanaume ndio wanaotoka kwa kiwango cha juu sana. Kama ni kuuawa, bila shaka wanawake wangekuwa wanawaua wanaume kila siku. Hata ukiangalia kwenye fumanizi nyingi, utashangaa kuona nguvu inapelekwa kwa wanawake, badala ya wote waliofumaniwa.


naonekana kama anayefumaniwa ni mwanamke, yeye ndiye ambaye ametia aibu, na huonekana kama kahaba. Mwanaume ni mara chache sana kukumbana na misukosuko ya fumanizi, hasa kutoka kwa jamii, kwa sababu huonekana kijogoo.


Kwa nini unadhani hali iko hivyo, wakati mwanaume ndiye mtokaji nje mzuri?


Ni kwa sababu wanaume hujawa na wivu zaidi pale suala linapohusu mwili kuliko hisia. Wataalamu wanasema, mwanaume anapofikiria kuhusu kumfumania mke au mpenzi wake, picha zinazoenda kwenye mawazo yake ni zile zenye kuhusu mwili. Atatengeneza picha za mkewe au mpenzi wake na huyo mwanaume wakiwa pamoja kwenye tendo. Ataona kila kitu ambacho hufanya na mkewe kikiwa kinafanywa na mtu huyo na pengine ataona ziada. Lakini, picha zote zitakuwa zinahusu shughuli za kimwili.


Lakini kwa mwanamke picha zitakuwa ni za mwili, lakini pia za kujali. Mwanamke atafikiria au kujenga picha kwamba, mumewe au mpenzi wake ameenda shopping na huyo hawara na anamnunulia vitu vya thamani. Halafu atajenga picha wakiwa pamoja wakiwa wanazungmza kwa furaha na bashasha. Mwanamke huona wivu kimwili na hisia.

Tafiti zinaonesha kwamba, vipigo na vifo vingi dhidi ya wanawake kutoka kwa wapenzi wao hutokana na wivu. Kwa hali hiyo, wivu unaongoza katika kusababisha maumivu ya kimwili na hisia kwa wanawake, na pengine hata kifo………………...

Apr 4, 2012

ASHA MKWIZU HAULI- NA KESI YA KUMUUWA HAWARA WA MUMEWE

Asha Mkwizu Hauli akipelekwa mahakamani


R. v. Asha Mkwizu Hauli, Crim Sessions Case No 3 of 1984 (DSM) (unreported).


Kesi hii niliiandika kwa mara ya kwanza katika mtandao wa Jamii Forum ambapo nina utaratibu wa kuweka kesi mbalimbali kila Ijumaa. Nitakluwa naweka baadhi ya kesi hizo hapa Utambuzi na kujitambua Blog.


Kwa kuisoma na kupata maoni ya wadau mbali mbali wa Jamii Forum waweza kubofya hapa: http://www.jamiiforums.com/mahusiano-mapenzi-urafiki/234276-asha-mkwizu-hauli-na-kesi-ya-kumuuwa-hawara-wa-mumewe.html

Mnamo tarehe 19 Novemba , 1983 mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Mwanahamisi Happiness Senzota alikwenda katika kituo cha Polisi cha Salender Bridge. Alipofika pale kituoni alikutana na askari wa upelelezi aliyejulikana kwa jina la Haruna Masumai ambapo alitoa malalamiko yake kwamba mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Asha Mkwizu ametishia kumdhuru.

Mpelelezi huyo alifanya mawasiliano na mtuhumiwa na ilipofika tena tarehe 21 Novemba wote wawili mlalamikaji Happiness Senzota na mtuhumiwa Asha Mkwizu walifika kituoni hapo kama walivyoelekezwa na askari huyo wa upelelezi. Na kutokana na maelezo yao ndipo askari huyo alipogundua kwamba Happpiness alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mume wa Asha Mkwizu aliyetajwa kwa jina la Dr. Hauli.

Baada ya kuchukua maelezo yao aliwaambia waende lakini waje tarehe 22 Novemba 1983 ambayo ilikuwa ni siku inayofuata.

Kwa mujibu wa house boy wa Asha Mkwizu aliyejulikana kwa jina la Musa James, alidai kwamba mnamo tarehe hiyo ya 22 Novemba 1983, bosi wake Asha Mkwizu alimtuma kwenda kununua mkaa, baada ya yeye Musa kuandaa chai na kumwagia maji katika bustani ambapo alidai pia kuona shimo la urefu wa kama futi tatu kwenda na chini upana wa futi tatu na nusu hapo bustanini. Musa alitakiwa kwenda kununua mkaa Kariakoo na alitakiwa na Asha asirudi kabla ya saa sita mchana. Na baada ya kutoa maelekezo hayo Asha Mkwizu, aliondoka kwenda kituo cha Polisi cha Salender Bridge kama walivyotakiwa na askari wa upelelezi wa kituo hicho.

Walifika hapo kituoni kukutana na askari wa upelelezi Harun. Lakini askari huyo aliwaambia kwamba asingeweza kusikiliza shauri lao kwa sababu Dr. Hauli hayupo nchini kwa hiyo wasubiri mpaka hapo atakaporudi, ndipo wazungumzie shauri lao na kupatiwa muafaka. Askari huyo wa upelelezi aliwasihi wasije wakadhuriana wakati wanamsubiri Dr. Hauli. Baada ya kuwaonya Happiness ndiye aliyekuwa wa kwanza kuondoka na baada ya dakika 10 Asha Mkwizu naye akaondoka. Huo ndio ulikuwa mwisho wa Mwanahamisi Happiness Senzota kuonekana akiwa hai.

Kwa mujibu wa House boy wa Asha Mkwizu, alidai kwamba alirudi kutoka Kariakoo kununua mkaa na alipofika nyumbani alimkuta mdogo wake Dr. Hauli aitwae Robson Hauli akiwa hapo nyumbani, alimkuta bosi wake Asha pia akiwa hapo nyumbani. Asha alimwambia Musa aandae ndizi kwa ajili ya watoto, lakini Musa alishangaa kuona damu pale sebuleni na ilikuwa ni damu nyingi. Asha alimwambia Musa kwamba amejiumiza na alimtaka asafishe ile damu pale sebuleni na kule bafuni pia ambapo damu ilikuwa imeganda ukutani.

Mnamo tarehe 24 Novemba 1983, Asha alimweleza Musa, “Nimemmaliza adui yangu”

Musa alipomuuliza ni nani huyo adui yake aliyemmaliza, Asha alimjibu kuwa ni Happiness Senzota. Asha aliendelea kumweleza Musa kwamba amemuua Happiness na kumzika katika eneo la hapo nyumbani, lakini alikataa kumuonyesha Musa mahali alipouzika mwili huo.

Mnamo 27 Novemba, 1983, Musa alikwenda kuripoti jambo lile Polisi ingawa alionywa na Asha kwamba atunze siri hiyo na asije akamweleza mtu yeyote kuhusu jambo hilo.

Baada ya Musa kuripoti Polisi, Asha alikamatwa na baada ya kuhojiwa alionyesha mahali alipouzika mwili wa Happiness.

Polisi waliufukua mwili huo na baada ya uchunguzi wa awali ilithibitishwa kwamba mwili ule ulikuwa ni wa Mwanahamisi Happiness Senzota. Uchunguzi zaidi ulionyesha kwamba ule mwili ulikuwa na majeraha matatu, jeraha moja katika mkono wa kushoto, na majeraha mawili yalikutwa kichwani, moja likiwa kubwa kwa upana wa sm 5 likiwa na kina kirefu kiasi cha kufumua ubongo. Hili jeraha ndilo lililoelezwa Na Daktari kusababisha kifo cha Happiness Senzota.

Mnamo 29 November 1983 SSP Gewe alimhoji mtuhumiwa na baadae mlinzi wa amani naye alimhoji mtuhumiwa huyo, ambapo maelezo hayo yalitumika kama ushahidi pale mahakamani dhidi yake.

Kesi hii ni ya mwaka 1983 ya Asha Mkwizu Hauli, alishitakiwa na Jamhuri kwa kosa la kumuua kwa kukusudia Mwanahamisi Happiness Senzota hapo mnamo tarehe 22 Novemba 1983 nyumbani kwake katika mtaa wa Lugalo Upanga. Kosa hilo la Kuuwa kwa kukusudia (Murder) limeainishwa kwenye kanuni ya adhabu (Penal Code) kifungu cha 196.

Kesi ilisikilizwa katika mahakama kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam na Mheshimiwa Jaji A. Bahati akisaidiwa na Wazee wa Baraza waliojulikana kwa majina ya Bi. Mwasabuli Ali na mwenzie aliyejulikana kwa jina moja la Mzee Kikoti.

Upande wa mashtaka katika kesi hii waliita jumla ya mashahidi 14.

Hapakuwa na ubishi wowote kwamba, Mwanahamisi Happiness Senzota amefariki na amefariki kwa kuuawa akiwa mikononi mwa Asha Mkwizu Hauli. Mtuhumiwa mwenyewe alikiri kumuua Happiness kwa kumpiga na chuma kizito kichwani ambacho kililetwa pale mahakamani kama ushahidi. Pia mtuhumiwa alikiri kwamba, kutokana na kumpiga Happiness ikawa ndio sababu ya kifo chake. Matokeo ya uchunguzi wa daktari (Post Mortem) ulibainisha kwamba kifo cha Happiness kilitokana na kupasuka kwa fuvu la kichwa na kupelekea athari kubwa katika ubongo.

Mwendesha mashtaka alibainisha pale mahakamani kwamba mtuhumiwa alimuua Happiness baada ya kumshawishi afuatane naye hadi nyumbani kwake na baada ya kumuua aliuchoma mwili wa marehemu moto na kisha kuuzika katika bustani yake na baadae kuondoa ushahidi ili kuficha mauaji hayo. Ili kuthibitisha ukweli wa tuhuma hizo mwendesha mashtaka alileta mashahidi na pia alileta vielelezo pale mahakamani.

Mtuhumiwa utetezi wake ulikuwa kwamba, Marehemu Happiness alimkashifu kupita kiasi wakati alipokuwa hapo nyumbani kwake kiasi kwamba alipatwa na hasira kali zilizopitiliza na kumpiga na kipande cha chuma kichwani mara moja.

Katika maelezo yake wakati anahojiwa, Asha alitoa maelezo marefu kuhusiana na maisha yake na matatizo yake ya ndoa na Dr. Hauli. Aliendelea kueleza jinsi alivyokuja kugundua kuhusu mahusiano aliyokuwa nayo Happiness na Mumewe na jinsi alivyokuwa akipelekwa na Polisi na Happiness mara kwa mara kujibu tuhuma kwamba alikuwa akimtishia kumdhuru yeye Happiness.

Asha alidai kwamba mnamo hiyo tarehe 22 Novemba alikwenda tena Polisi kama alivyoelekezwa, baada ya swala lao kuahirishwa siku moja iliyopita. Alipofika pale alimkuta Happiness tayari ameshafika. Lakini askari huyo aliwaambia kwamba asingeweza kusikiliza shauri lao kwa sababu Dr. Hauli hayupo nchini kwa hiyo wasubiri mpaka hapo atakaporudi, ndipo wazungumzie shauri lao na kupatiwa muafaka. Askari huyo wa upelelezi aliwasihi wasije wakadhuriana wakati wanamsubiri Dr. Hauli. Baada ya kuwaonya happiness ndiye aliyekuwa wa kwanza kuondoka na baada ya dakika 10 na yeye aliondoka na alimkuta Happiness akiwa kasimama kwenye taa za kuongozea magari pale Salender Bridge akiwa anasubiri kuvuka. Walivuka pamoja upande wa pili ilipo Hoteli ya Palm Beach. Ndipo Asha alipomuaga Happiness na kumtaka amfikishie salaam zake kwa mkuu wa shule anakofanyia kazi yeye Happiness aliyemtaja kwa jina la Mwalimu Mpanda. Lakini Happiness akadai kwamba haendi shule. Lakini pia akamwambia Asha kwamba anajisikia njaa na anahitaji kitu cha kula. Asha alimweleza kwamba kwa muda ule hakuna huduma pale katika Hoteli ya Palm Beach kwani ilikuwa ni saa nne asubuhi. Happiness alimuuliza ni wapi anaweza kupata duka la vinywaji baridi na ndipo Asha akamjibu kuwa jirani na anapoishi kuna kioski kinauza vinywaji baridi na kuku wa kukaanga. Happiness alisema ni vyema akioneshwa hicho kioski. Walikubaliana waende pamoja ili baadae yeye Happines awahi kwa dada yake ambaye ilikuwa ampeleke kwa Dr. Mvungi kwa matibabu.

Kwa maelezo hayo Asha alionekana kukwepa hoja kumshawishi Happiness ili wafuatane nyumbani kwake kama alivyonukuliwa katika maelezo ya awali wakati akihojiwa na Polisi. Asha alidai kwamba alikuwa hayuko katika hali nzuri wakati anahojiwa na SSP Gewe na hakusomewa maelezo yake na badala yak alitakiwa kuweka sahihi yake katika sehemu zote zilizowekwa X.

Asha aliendelea kueleza kwamba walifika nyumbani na kumkaribisha Happiness hapo nyumbani kwake ambapo alitoka kwenda kununua chupa mbili za bia na chupa moja cocacola. Alichanganya bia na cocacola kwenye glasi akiwa jikoni kwa sababu Happiness alitaka achanganyiwe vivyaji hivyo kwa mtindo huo. Walikunywa pamoja vinywaji hivyo pamoja na ndizi. Wakati huo walikuwa wakizungumza pamoja. Asha alimweleza Happiness ni kwa jinsi gani wote wawili walivyo na mnasaba na Dr. Mvungi. Na hapo ndipo Happiness aliposema Dr. Hauli ni wake na hawezi kumwacha mpaka kufa. Baadae aliomba aonyeshwe kilipo choo, ambapo alioonyeshwa.
Wakati Asha anaosha glasi hapo jikoni, Happiness alifika hapo jikoni na wakati ananawa mikono yake akaanza kumkashifu yeye Asha kwa kumwambia, “Hivi kwa nini unanifuata fuata wewe kizee, huna thamani tena na umeshakwisha, na umgumba. Kama mumeo angekuwa anakuthamini angekufungia wewe na wanao kuja kupitisa usiku kwangu?” Asha akamwambia, “Happiness, wewe ni kama mwanangu, huwezi kunitusi kiasi hicho.”

Ndipo Happiness akamwambia Asha kwa kipare, “Chebakie ni Kushoshorwa hena mzuti na vichaa.” Maneno hayo yalitafsiriwa kama, “Kilichobaki ni wewe kupata mtu wa kukutia vidole mkunduni.” Na baada kusema hivyo Happiness alimsukuma Asha ambapo shubaka la zana likaangua mguuni mwa Asha, wakati asha anaondoa shubaka lile mguuni mwake, Happiness alimfuata Asha pale alipo na ndipo alipookota kipande cha chuma na kumpiga nacho. Mara aliona damu nyingi ikivuja na alijaribu kumpa huduma ya kwanza lakini haikuwezekana, Happiness Alifariki.

Kuhusu kuuchoma moto mwili wa marehemu kabla ya kuuzika mtuhumiwa alidai kwamba tukio hilo lilitokea kama bahati mbaya.

Mtuhumiwa alikanusha kumwambia house boy wake Musa kuwa asirudi nyumbani mpaka saa sita mchana. Anachojua ni kumweleza Musa kwamba awe makini asije akakamatwa na Polisi kama mzururaji kwa sababu hakuwa na kitambulisho. Pia alikanusha madai ya Musa aliyowaeleza Polisi kwamba yeye Asha alichimba shimo kwenye bustani kabla ya kumuua Happiness, madai mengine aliyokanusha ni kuhusu kumweleza Musa kwamba amemuua adui yake. Alisema alimweleza Musa kwamba kuna tukio limetokea kwa bahati mbaya na amemuua mtu na kumzika katika bustani na alimuonyesha Musa kaburi alipomzikia Happiness.

Asha aliieleza mahakama kwamba kama angekuwa na dhamira ya kumuua Happiness basi angemuua kwa sumu kwa sababu yeye kama Muuguuzi anajua sumu za aina nyingi ambazo angaweza kuzitumia.

Alimalizia kwa kusema kwamba anafahamu kuwa ndugu zake na mumewe Dr. Hauli walikuwa wanataka yeye Dr. Hauli aoe mke mwingine kutoka katika kabila lake na amekuwa akisikia tetesi kwamaba anatakiwa kurudishwa kwa wazazi wake na mumewe.

Mtuhumiwa alifanyiwa usaili kwa muda mrefu kutokana na maelezo yake na alidai kwamba yeye ni mkubwa kwa umri na na kimo zaidi ya Marehemu. Kuhusiana na maelezo ya Musa alidai kwamba Musa anaweza kudanganya kwa sababu ametokea Kusini kama ilivyo mumewe Dr. Hauli. Pia alitaja idadi ya mahawara aliokuwa nao mumewe wakiwemo wanawake wa wazungu.

Alipoulizwa na Mahakama kwa nini mwili wa marehemu ulikutwa na majeraha matatu wakati alidai kwamba alimpiga marehemu kwa pigo moja tu, Asha alijibu kwamba, alimpiga marehemu kwa kile chuma mara moja katika mkono wake na wakati anaanguka alijigonga sakafuni kwa kishindo na ndio akaumia.

Akijibu swali aliloulizwa na mmoja wa wazee wa baraza mtuhumiwa huyo alisema. Mtu akikupeleka Polisi hawezi kuwa rafiki yako, lakini yeye binafsi hakuwa akimchukia marehemu, na hata alipokuja kugundua kuwa marehemu alikuwa na uhusiano na mumewe hakuwa na kinyongo naye.


Alipoulizwa kwa nini katika mahojiano yake na Polisi na pia mlinzi wa Amani hakueleza lile tusi alilotukanwa kwa Kipare na marehemu. Asha alijibu kwamba, Polisi walimwambia hawahitaji maneno mengi na ingawa alilitaja tusi hilo lakini Polisi hawakuliandika katika maelezo yake. Pia Polisi walimwambia aeleze kwa mlinzi wa Amani yale yote alivyowaeleza bila kuongeza kitu.

Katika kesi hiyo kulikuwa na mashahidi watatu wa mtuhumiwa ambao ni Yahaya Mkwizu, kaka yake mtuhumiwa, Benson Hauli, baba mkwe wa mtuhumiwa, na Dr. Rugeyamu mtaalamu wa magonywa ya akili (Consultant Psychiatrist)

Shahidi wa kwanza aliieleza mahakama kuhusu kikao kilichokaa kwa Dr. Hauli na kuamua mtuhumiwa arudishwe kwa wazazi wake. Dr. Rugeyamu alitoa ushahidi kuhusu vipimo alivyomfanyia mtuhumiwa baada ya tukio lile la kuua ili kujua kama alikuwa na matatizo ya akili wakati alipokuwa akitekeleza mauaji hayo. Dr. Rugeyamu aligundua kwamba mtuhumiwa alikuwa na matatizo ya akili ambayo kwa kawaida hutokana na matatizo ya ndoa na pia alikuwa na msongo wa mawazo (Depression) kutokana na matatizo ya kifamilia aliyokuwa nayo. Dr. Rugeyamu alikamilisha ripoti yake kwa kubainisha kwamba yote hiyo ilitokana na kile alichokiita kuondokewa kwa hali ya ubinadamu (diminished responcibility).

Wakimtetea mtuhumiwa katika kesi hiyo pale mahakamani mawakili wa mshitakiwa (Counsels) wote kwa pamoja walikuwa na hoja ya kumtetea mtuhumiwa. Akimtetea mtuhumiwa, mmoja wa mawakili hao (Counsel) aliibua dhana ya Hasira ziliopindukia (Defence of Provocation) na aliungana na ripoti ya daktati wa magonjwa ya akili Dr. Rugeyamu ambayo ilikuwa ndio kielelezo cha tatu (Exibhit 3) pale mahakamani ambacho kilibainisha kwamba mtuhumiwa alikuwa na matatizo ya akili wakati akitekeleza mauaji hayo, na aliendelea kusema kwamba ni hali hiyo ndiyo iliyosababisha mtuhumiwa kushindwa kuzuia hasira zake. Wakili huyo alitoa mifano ya kesi kadhaa ambazo zinakubaliana na nadharia ile. Aliitaka mahakama kukubali kwamba mtuhumiwa alipatwa na hasira zilizopindukia baada ya kukashifiwa kupita kiasi na marehemu na ndio sababu ya kufanya kile alichofanya.

Akijibu hoja hio mwanasheria wa serikali alisema mtuhumiwa alimshawishi marehemu aende naye nyumbani kwake ili aweze kumuua na hiyo dhana ya kukasirishwa kupindukia (Provocation) haiwezi kupewa nafasi katika kesi ile.

Alirejea ushahidi uliotolewa na mashahidi pale mahakamni hususan ushahidi uliotolewa na Musa ili kupinga dhana hiyo ya kukasirishwa kupindukia.

Mwanasheria huyo alisema, na hapa nanukuu,

“Napenda kujumusha maelezo yangu mbele ya wazee wa baraza kwamba sheria inasemaje kuhususiana na dhana ya kukasirishwa kupindukia (Provocation) kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 202 cha kanuni ya adhabu kwa kutofautisha na kifungu cha sheria cha 192 cha kanuni ya adhabu cha mwaka 1945. Ningependa pia kuwaeleza wazee wa baraza nafasi ya sheria kuhusiana na dhana ya kuondokewa kwa hali ya ubinadamu (diminished responsibility) kwa mujibu wa sheria zetu hapa nchini....... I understood the point that in provocation the test used was that of a reasonable of ordinary man, hence an objective test rather than a subjective test.”
Mwisho wa kunukuu.

Mzee wa baraza wa kwanza Bi. Mwasabuli Ali hakukubaliana ushahidi wa dhana ya kukasirishwa kupindukia (provocation) na aliridhia ushahidi wa kwamba mtuhumiwa alipanga kumuua marehemu na alisema mshitakiwa anayo hatia ya kuua kwa kukusudia. Pia mzee wa baraza wa pili mzee Kikoti alikubaliana na mwenzie.

Kesi hiyo iliisha kusikilizwa kwake, na mnamo tarehe October 2, 1985 Mheshimiwa Jaji A. Bahati alisoma hukumu ya kesi hiyo.

Akisoma hukumu hiyo muheshimiwa Jaji A Bahati alisema, na hapa namnukuu, “Sasa nitafanya majumuisho na kuweka maoni yangu katika kesi hii. Ni wazi kwamba hakuna ubishi kuwa Mwanahamisi Happiness Senzota amekufa, na amekufa akiwa mikononi mwa mtuhumiwa Asha Mkwizu Hauli. Na ni dhahiri kuna ushahidi wa kuthibitisha hilo. Kwa hiyo basi ni ukweli kwamba Mwanahamisi happiness Senzota amekufa na kifo chake kilitokana na kuuliwa kikatili na mtuhumiwa. Kilichopo ndani ya shauri na tunachokizingatia katika shauri hili na kutolea maamuzi ni kuangalia kama je mtuhumiwa alimuua marehemu kwa thamira ovu au la.”

Mwisho wa kunukuu...............

Jaji Bahati alielezea ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ambao ulioanisha matukio yaliyofuatana ili kuthibitisha kwamba mtuhumiwa alikuwa amedhamiria kwa makusudi kabisa kumuua marehemu, kuanzia maandalizi ya kaburi lililochimbwa katika bustani kwa ajili ya kumzika marehemu baada ya kumuua na kitendo cha mtuhumiwa kumuonya house boy wake Musa, kwamba asirudi kutoka huko alikomtuma kabla ya saa sita mchana, ili apate muda wa kuuwa na kuzika mwili wa marehemu. Pia kulikuwa na kitendo cha mtuhumiwa kumshawishi au kumlaghai marehemu ili aende nyumbani kwa kwake yeye mtuhumiwa mtaa wa Lugalo, Upanga na baadae huduma ya vinywaji na kitendo cha kukashifiwa na marehemu ambacho kilipelekea kuuawa kwake. Pamoja na hayo pia kulikuwa na kitendo cha mtuhumiwa kuuchoma moto mwili wa marehemu na kisha kuuzika ikiwa ni pamoja na kusafisha nyumba ili kuondoa ushahidi. Pia kulikuwa na taarifa kwa Musa kwamba ameshammaliza adui yake na onyo kwa Musa kwamba asije akamwambia mtu yeyote.

Upande wa mashtaka ulikuwa na hoja kwamba hata kama marehemu alikuwa amemkashifu kupita kiasi mtuhumiwa, lakini bado jambo hilo haliwezi kumkera mtu mzima kufikia kufanya kitendo kama alichofanya mtuhumiwa.

Mahakama ilirejea kifungu cha sheria cha 202 kuhusiana na dhana ya kukasirishwa kupindukia (Provocation).

Hata hivyo mheshimiwa Jaji Bahati alisema atarejea kwenye kanuni ya adhabu baadae.


Akizungumzia utetezi wa mawakili wa mtuhumiwa Mheshimiwa Jaji Bahati alisema.

Namnukuu,

“Upande wa utetezi kwa upande mwingine umekataa kukubaliana na ushahidi uliotolewa dhidi ya mtuhumiwa kwamba alikuwa amepanga kwa makusudi kabisa kumuua marehemu, na badala yake walikuja na madai ya mtuhumiwa kukasirishwa kupindukia (Provocation)”

Kisha Mheshimiwa Jaji Bahati akaendelea,

“nimekuwa nikiwaza sana kuhusu kesi hii, na nimefikia kuamini kwamba hakukuwa na swala la kukasirishwa kupindukia katika kesi hii, na ningependa kuungana na wazee wa baraza kwamba hakukuwa na swala la kuchokozwa katika kesi hii.”

Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Jaji alitoa sababu za kuamini hivyo kama ifuatavyo, kwanza ilikuwa ni maelezo ya mtuhumiwa (Extra Judicial) ambayo yalichukuliwa pale mahakamani kama ni ushahidi wa sita (Exhibit P6) katika kesi hiyo, ambapo mtuhumiwa alimuomba marehemu wafuatane hadi nyumbani kwake ambapo angempatia vinywaji na baadae hela ya taxi. “Je kitendo hiki tukiiteje kama si kushawishi au kulaghai?” Alihoji Mheshimiwa Jaji Bahati, kisha akaendelea..

“Pia katika utetezi wake mtuhumiwa alidai kwamba kitendo cha kushawishi au kulaghai kama ilivyoandikwa katika maelezo yake Polisi ambao ni ushahidi wa tano (Exhibit P5) kuhusiana na swala hilo la kumshawishi marehemu, mtuhumiwa alidai kwamba Polisi ambaye ni shahidi wa 10 (PW 10) aliongeza maneno ambayo hayakutoka kinywani mwake, lakini wakati huo huo, mtuhumiwa hakukanusha madai hayo katika maelezo yake hapa mahakamani kama yalivyonukuliwa katika ushahidi wa sita (Exhibit P6).”

Mheshimiwa Jaji alikubaliana na maelezo ya Polisi kwamba ni ya ukweli kwa sababu Polisi huyo aliyemhoji mtuhumiwa ni mtu mkubwa na kwa nafasi yake hawezi kuandika kitu ambacho hakikutamkwa na mtuhumiwa na badala aliandika kile kilichosemwa na mtuhumiwa na alimsomea maelezo yote kama alivyomnukuu na mtuhumiwa akaweka sahihi.

Akizungumzia juu ya ushahidi huo wa mtuhumiwa kupanga mauaji, Mheshimiwa Jaji Bahati alizungumzia juu ya ushahidi wa house boy wa mtuhumiwa. Kama alivyoileleza mahakama.

Mheshimiwa Jaji alisema. “Lakini katika maelezo yake, Mtuhumiwa alipinga maelezo ya Musa akidai ameidanganya mahakama. Kwa mujibu wa mtuhumiwa alidai kwamba Mtuhumiwa alisema ushahidi wa Musa sio wa kweli kwa sababu, Musa ametoka eneo moja na Dr. Hauli na pia aliogopa kwamba angedhaniwa kuwa yeye Musa ndiye aliyemuuwa marehemu. Pia alibainisha kwamba hakuwa na mahusiano mazuri na Musa.”

Jaji Bahati akizungumzia madai hayo alidai kwamba, maelezo ya Musa hayamshawishi kuamini kwamba ni muongo. Na hata majibu yake wakati akihojiwa pale mahakamani hayakuonyesha kwamba ni muongo. Alichokiona yeye ni kwamba, Musa alikuwa ni shahidi aliyesema ukweli.


Mheshimiwa Jaji alisema kwamba haoni sababu ya Musa kudanganya dhidi ya mtuhumiwa, kwani ni sawa na mtu kudanganya dhidi ya rafiki yake kama ilivyo katika kesi hii, bila sababu ya msingi. Na ndio sababu akakubaliana na ushahidi wa Musa kwamba ni wa ukweli.

Alithibitisha madai ya upande wa mashtaka kwamba mtuhumiwa alipanga kumuua marehemu kama ilivyonukuliwa katika maelezo yake wakati akihojiwa na Polisi, Mheshimiwa Jaji Bahati alinukuu maelezo hayo kama ifuatavyo:

“hapo ghadhabu zilinishika na kwa ghafla nilichukua lichuma fulani fupi ambayo (sic) ilikuwa karibu na mlango wa jiko aliko huyo Manahamisi Happiness Senzota na kumpiga nacho kichwani akiw amesimama kwa nyuma, hapo nilimwona ameanguka chini nilimpiga tenakichwani kwa kutumia hicho hicho chuma ambapo pia ilimpata (sic) sehemu ya mkono..................”

Upande wa utetezi ulidai kwamba SSP Gewe aliongeza hicho kipengele ili kesi hii imuwezesha kupanda cheo. Jaji Bahati hakukubaliana na maoni hayo.

Pia Jaji Bahati alizungumzia ushahidi wa Daktari aliyemfanyia mtuhumiwa vipimo ili kubaini kama mtuhumiwa alikuwa amerukwa na akili wakati akitekeleza mauaji hayo. lengo lilikuwa ni kupinga ile dhana ya kukasirishwa kupindukia (Provocation) kama alivyodai mtuhumiwa. na hapa alinukuu maelezo ya mtuhumiwa kama alivyoeleza katika maelezo yake Polisi:

“........Nilifanya mauaji hayo kwa sababu ya hasira nyingi tokana na marehemu kutaka kuvunja nyumba yangu.”

Mheshimiwa Jaji alisema kwamba maelezo hayo yanathibitisha kuwa mtuhumiwa alipanga kumuua marehemu ili kulipiza kisasi kama alivyonukuliwa na Polisi.

Kilichofuata baada ya mauaji hayo, pia ni muhimu ili kuthibitisha kwamba mauaji yalikuwa ni ya kupangwa. Hapa chini ni maelezo ya mtuhumiwa wakati akihojiwa nna Polisi:

“......... Nilimburuza hadi bafuni ambapo nilichukua mafuta ya taa na kumwaga katika shuka niliyomfunika nayo na kuwasha kibiritiambapo mmoto ulilipuka na kumchoma marehemu sehemu kadhaa za mwili (sic). Na madhumuni yangu ni kwamba akauke damu isizidi kutoka..............niliingia ndani na kuiweka maiti ndani ya jamvina kuiviringisha shuka ya kitandani. Niliiburuza maiti toka ndani hadi kwenye shimo hiyo (sic) na kuitumbukiza.

Maelezo hayo yaliendelea kwamba mtuhumiwa alifanya usafi ili kuficha ushahidi na kisha alienda kazini na kufanya kazi kama kawada na kisha kurejea nyumbani saa nne usiku.

Pia Mheshimiwa Jaji alizungumzia maoni ya mzee wa baraza Bi Mwasabuli Ali. Kwa mujibu wa maoni yake Bi Mwasabuli alisema kwamba, haamini kuwa marehemu ambaye alimshitaki mtuhumiwa anaweza kumuomba mtuhumiwa amwelekeze mahali panapouzwa vinywaji baridi. Alisema, haamini kwamba marehemu ambaye sio mgeni hapa jijini Dar asiwe anajua mahali panapouzwa vinywaji baridi. Bi Mwasabuli alisema pia haamini kwamba marehemu anaweza kumkashifu mtuhumiwa wakati akiwa hapo nyumbani kwa mtuhumiwa. Alikataa kukubaliana na dhana kukasirishwa kwa sababu kama mtuhumiwa alikuwa amekasirishwa kupita kiasi (Provoked) asingeweza kuuburuza mwili hadi bafuni, kuuchoma moto na baadae kuuzika akiwa peke yake, na pia kumwambia house boy wake, “Nimemuua mbaya wangu.” Pia Bi Mwasabuli alishangaa iweje mtuhumiwa amudu kwenda kazini na kufanya kazi kama kawaida kama vile hakuna kilichotokea.

Kwa upande wa Mzee wa baraza wa pili mzee Kikoti pia alikubaliana na maelezo ya mwenzie.

Mheshimiwa Jaji alikubaliana na maelezo hayo ya wazee wa baraza kwamba mauaji hayo yalikuwa hayana maana nyingine isipokuwa dhamira ovu. Mheshimiwa Jaji aliendelea kusema kwamba ingawa mtuhumiwa anadai alipatwa na hasira zilizopitiliza (Provoked) lakini yeye hakubaliani na utetezi huo kwa sababu ushahidi uliotolewa hapo mahakamani hauoneshi kukubaliana na dhana hiyo. Ili kuweka uwiano Mheshimiwa Jaji alitolea mfano kesi kati ya Jamhuri na Stephano Aloys ya mwaka 1972 HCD n. 199.

Jaji aliendelea kusema kwamba, mpaka hapo mashtaka ya kuua kwa kukusudia (Murder) dhidi ya mtuhumiwa yamethibitishwa pasi na shaka yoyote, kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 200 cha kanuni ya adhabu.

Hata hivyo Jaji alieleza kwa kirefu juu ya dhana ya kuondokewa kwa hali ya ubinadamu (diminishing responsibility). Akizungumzia dhana hiyo alitolea mfano kesi ya mwaka 1978 ya Jamhuri dhidi ya Agnes Doris Liundi (Unrepoted), Mheshimiwa Jaji Makame J. Alirejea kesi ya Uingereza ya R.v. Julia Everton ambapo sheria hiyo kwa kule Uingereza inayo nafasi, ambapo mtuhumiwa aliwekwa chini ya uangalizi kwa muda wa miaka mitatu.

Mheshimiwa Jaji aliendelea kusema kwamba, kwa Tanzania hatuna sheria hiyo, na itakuwa ni kinyume na taaluma yake kwenda nje ya mipaka yake.
Kisha akaendelea.......




Kwa heshima na taadhima ninakubaliana na mtazamo wa hapo juu na hata mahakama ya rufaa ya Tanzania katika rufaa ya kesi kama hiyo No. 82 ya 1978 (Haijaripotiwa) inakubaliana na hitimisho la mheshimiwa Jaji katika hilo. Na hivi ndivyo mahakama ya rufaa ilivyosema:




“Inawezekana haswa, kwa kweli kwamba sheria yetu katika suala la kurukwa na akili (Insanity) limepitwa na wakati na ni la kizamani. Katika ushahidi wa Dr. Haule amesema kwamba katika uchunguzi wa kisasa, utofauti kati ya kurukwa na akili na kuondokewa kwa hali ya ubinadamu mkamilifu (diminished responsibility) lipo chini ya mjadala mkubwa kwa sababu halikubaliki. Bunge kwa hekima yake linaweza likataka kurekebisha matawi husika ya sheria na kuyaleta ama kuyaongeza katika mstari utakaoenda sambamba na taaluma za kisasa za kitabibu juu ya suala husika. Na katika nguvu nyingine kimahakama ikiwemo mojawapo hata ya Afrika Mashariki iwe inafanya hivyo. Lakini kama sheria ilivyo tupo katika mchango wa mawazo kuona Mheshimiwa Jaji ameelekea katika hitimisho sahihi”




Huu ulikuwa ni mtazamo wa mahakama ya rufaa.




Katika mahakama ya rufaa ilizingatia rufaa ya kesi ya Agnes Liundi, katika maelezo yake katika kesi hiyo Mheshimiwa Jaji Bahati alikiri kwamba hayatofautiani sana na kesi iliyo mbele yake. Kwa kesi ya Agness Liundi ni kwamba alikuwa ameteswa sana na mumewe kiasi cha kuamua kujiuwa na kuwauwa wanae wote. Siku hiyo ya tukio Agness alinunua sumu pamoja na Juice ya Orange Squash ambapo aliwapa watoto wake wanywe na yeye pia kunywa sumu hiyo. Watoto watatu walifariki lakini yeye na mtoto wake mmoja waliokolewa na madaktari. Katika kesi hiyo mawakili wa utetezi walikuja na hoja ya uwendawazimu (Insanity) wakati mtuhumiwa akitenda kosa hilo lakini mahakama kuu haikuafiki hoja hiyo. Pia kulikuwa na jaribio la kuleta au kuingiza hoja nyingine ya kupoteza hali ya kibinadamu (diminished responsibility,) hoja ambayo pia ilikataliwa na mahakama kuu.

Mheshimiwa Jaji Bahati alikataa kuikubali hoja hiyo ya kupoteza hali ya kibinadamu (diminished responsibility) kama utetezi katika kesi hiyo ya Asha Mkwizu kama ilivyokataliwa katika kesi ya Agnes Liundi.

Kutokana na tafiti za Mheshimiwa Jaji hapakuwa na kipengele chochote cha sheria kinachoeleza juu ya kukasirishwa. Baada ya kukataliwa kwa maelezo ya mtuhumiwa yanayohusu kutukanwa, Mheshimiwa Jaji hakuona umuhimu wa kuhusisha vipengele vya sheria ya kanuni ya adhabu na makosa ya jinai vya 201 na 202 kuhusiana na kukasirishwa. Hapakuwa na umuhimu wa kuoanisha hayo.

Katika hitimisho Mheshimiwa Jaji alisema:

“Nimeridhika na tuhuma za mauaji ya kukusudia zimethibitishwa pasi na shaka yoyote, kwa hiyo basi, mtuhumiwa amepatikana na hatia ya kuuwa kwa kukusudia na ninamhukumu kulingana na sheria kama ifuatavyo;

Mahakama - Hukumu iliwasilishwa mbele ya mahakama ikishuhudiwa na mtuhumiwa, wasaidizi wa mahakama na wazeewa baraza.
Mshitaka - Sina la kusema.

Jopo la mahakimu – Hatuna la kusema.

Mtuhumiwa – Sina la kusema ila nilichosema ni kweli, naiomba mahakama inipunguzie adhabu kwa sababu ya matatizo yote haya, nina mzazi mzee sana na afya yangu ni dhaifu, nimefanyiwa operesheni mbalimbali, ninasumbuliwa na kibofu cha mkojo na uti wa mgongo.

Hukumu - Kwa mujibu wa sheria kuna hukumu moja tu kwa makosa ya kuuwa kwa kukusudia, nayo ni adhabu ya kunyongwa hadi kifo. Alichosema mtuhumiwa katika kesi hii, kinaweza kumsaidia kwa hatua nyingine na si kwa mahakama hii. Kwa hiyo basi, nakuhukumu wewe Asha Mkwizu Hauli adhabu ya kifo kwa kunyongwa”




Haki ya mtuhumiwa kukata rufaa iko wazi.



Jaji A. Bahati
2/10/1985

Sep 21, 2011

NAMNA YA KUTOKA KWENYE UTUMWA WA NDOA…….

Sio lengo langu kuwafundisha wanawake namna yakuachana na wapenzi au waume zao. Lakini hebu fikiria kwamba kila wakati wanandoa au wapenzi wako kwenye vita. Hakuna amani, hakuna masikilizano. Kutwa nzima mtu anawaza kuhusu uhusiano wake mbaya hadi anashindwa hata kufanya kazi. Je, hali kama hii ina maana kwa mtu kuendelea kuwa kwenye ndoa?




Hapa nazungumzia wale ambao wanashindwa kutoka kwenye uhusiano, ambao wanajua kabisa kwamba, unawatesa na kuwaumiza. Kuna sababu nyingi kwa nini watu hawa wanashindwa, lakini nyingine zinatokana tu na kutojua namna ya kutoka, sio utegemezi wa aina yoyote.



Moja ya sababu, ambazo ninaziona sana hasa kwa wanawake ni kujali jamii itasemaje. Mtu anaona kabisa uhusiano haufai na anatamani kutoka . lakini anajiuliza, hivi watasemaje? Kuna wakati ndugu wanamwambia, yeye ndiye mkorofi. Kama hii ndio sababu anachotakiwa kufanya mwanandoa ni kuhakikisha kwamba anajifunza kuishi kama yeye. Nijuavyo mimi, hata wanandugu au jamii hata ikisema vipi, anayeumia au kuepuka kuumia au kuuawa ni yule aliye kwenye mateso ya ndoa


Jambo la kujiliza hapa ni kama, jamii ndiyo inayopigwa, kutukanwa, kutelekezwa au kudhalilishwa? Lakini jambo kubwa zaidi la kufahamu ni kwamba mtu alishaolewa maana yake ni mtu mzima mwenye haki ya kuamua juu ya maisha yake. Akisbiri ndugu wamwamulie, basi huyo bado ni mtoto..



Jambo lingine ni lile la, je nikimwacha nitapata mwingine? kwani wanaume siku hizi ni shida sana? Ni ujinga unaowafanya wengi kuuliza swali hilo. Unahitaji mwingine wa nini? Unahitaji mwingine ili maisha yako yawe ya maana zaidi au? Kama hakuna mwingine ni vyema kwa sababu maana yake ni kwamba hakuna mwingine wa kukutesa. Lakini wanasaikolojia wanaamini kwamba, ‘kila bidhaa ina mnunuzi.’ Kama unataka mwingine, hata ukiwa na miaka sitini utampata. Huwezi kumpata wakati ukiwa ndani ya tanuru la mateso. Ni lazima utoke kwanza.



Kuna wale wanaoshindwa kutoka kwa sababu wanaamini kwamba mwanamke haruhusiwi kutoa talaka. Hi siyo kweli. Kuna wanaoshindwa kutoka kwa sababu dini zao zinakataza kuachana, hii pia siyo kweli. Mwanamke au mwanaume, yeyote anaweza kuomba talaka na ikatolewa, kama kuna sababu zenye kukidhi haja hiyo. Chombo pekee kinachoweza kutoa talaka au kuidhinisha wanandoa kuachana ni Mahakama, siyo dini au taasisi nyingine. Kinachoitwa ‘talaka tatu’ kwa mfano, ni ushahidi tu, na sio talaka.



Kuna wale ambao hawako tayari kutoka kwenye uhusiano mgumu kwa sababu ya mali. Wanaogopa watagawana mali na wenzao, jambo ambalo hawako tayari kulifanya na mara nyingi hawa ni wanaume. Wapo pia wanawake ambao wao ndio waliokuwa watafutaji wakuu. Swali la kujiuliza ni hili. ‘Ni kipi bora, ni mali au ni amani na utulivu na uhai wako?’ kama ni mali, basi hakuna anayeweza kukuingilia kwenye uamuzi wako.



Lakini, kwa ufahamu tu, ni kwamba, pasipo na amani, mali haina maana na pasipo na amani uhai ni wa kubahatisha pia.


Wengine wanashindwa kutoka kwenye husiano kwa sababu wazazi wa mume na ndugu wanampenda sana. Anaogopa kuwaudhi kwa kuondoka kwenye ndoa ya mateso ya mtoto wao na ndugu yao. Anataka wafurahi, hivyo hawezi kuondoka. Huu nao ni upungufu.


Hivi unakuwa umeolewa na ndugu na wazazi au na mume? Lakini, kwani ukiondoka utashindwa kuwa karibu na watu hawa? Hutashindwa na pengine urafiki wenu utakuwa wa kudumu. Ukiendelea kukaa kwenye ndoa ya mateso kuna siku utakosana hata na hawa, maana unaweza ukalipukwa ukamuuwa mtoto au ndugu yao.



Kuna wale wanaoshindwa kutoka kwenye uhusiano mgumu kwa sababu wana watoto na wanaogopa kwamba, watoto wao watateseka. Hivi ni kuteseka kupi kubaya, kule kwa utotoni au ukubwani? Mtoto anayeishi kwenye ndoa yenye vurugu, anaharibikiwa kuanzia utotoni hadi ukubwani. Lakini, hata hivyo kuachana kwa wazazi, sio lazima kuwe na maana ya watoto kuteseka.



Kuna wakati hata watoto wanamwambia mama atoke kwenye ndoa, halafu mama huyo huyo anadai anakaa kwenye ndoa hiyo kwa sababu ya watoto! Kuna haja ya kujiuliza maswali kwa upana zaidi.



Ukitaka kutoka kwenye ndoa ngumu jiulize maswali haya. Je, ndoa hii ni kwa faida ya nani? Je, niliolewa au kuoa ili kupata shida au amani na upendo? Je, bila ndoa,nisingeweza kuishi mwenyewe? Tafuta mifano ya wasio na ndoa ambao wanafurahia maisha.



Jiulize ni kwa kiasi gani wengine wanasaidia kukusukuma zaidi kwenye ndoa hiyo? Jiulize ukamilifu wako. Je, wewe ni nusu mtu au mtu kamili? Kama ni mtu kamili , basi ishi kama mtu kamili.



Sep 14, 2011

THAMANI HULETWA NA UHABA!


Mafuta yalipanda thamani kutokana na uhaba!



Uhusiano wa uhaba na thamani ni mada ambayo ikianza kujadiliwa aina kikomo. Kila mmoja wetu anajua kwamba maji ya mito kwa ajili ya kunywa ni kuhimu kwa maisha a binadamu.


Watu wa vijijini ambako kuna mito mingi hawaoni thamani thamani ya maji na ndiyo maana wanakunywa bure. Kwa maana hiyo pamoja na umuhimu wa maji, watu hao wanaona kwamba hayana thamani kwa sababu ni mengi. Lakini watu wa miji kama Dar wanaona maji ni muhimu kwa sababu kwanza wanayanunua.



Pili, yakikatika kwa muda wa wiki mtu, watu wanatafutana! Ndoo moja ya maji inapanda sana. Kwa hiyo kumbe thamani ya kitu inaongezeka kukiwa na uhaba wa kitu hicho.


Kama kitu siyo haba kama yalivyo maji kwa watu wa vijijini, thamani ya kitu hicho hupungua! Ni kama ilivyotokea hivi karibuni baada ya wauzaji na wasambazaji wa nishati a mafuta walipoanya mgomo baada ya serikali kushusha bei ya nishati hiyo, hali ilikuwa ngumu kweli hapa nchini na ilifikia hatua walanguzi waliuza mafuta kwa bei mbaya ambayo wengi hawakuitarajia, lakini walilazimika kununua.

Hali hiyo inaweza kutokea pia kwenye chakula, madawa na vitu vingine ambavyo vinakuwa haba baada ya janga Fulani kutokea.


Katika nchi kama Marekani umeme haukatiki na hivyo watu hawaoni umuhimu wake kwa sababu sio haba.

Mtu wa Marekani kwa mfano akija huku kwetu ambako umeme ni swala la ‘kukata shingo’ atagundua kwa mara ya kwanza thamani ya umeme. Unapokikosa kitu, kinatengeneza thamani kwa sababu ni haba.



Pia uhaba ni kama mwalimu. Kwa mfano, kama kuna uhaba wa petroli au dizeli. Wenye agari wanakaa kwenye vituo vya mafuta kwa muda mrefu wakisubiri ili wapate huduma hiyo.

Wakati mwingine wanalazimika kupata mafuta kwa njia ya kuruka kama upatikanaji wake unakuwa wa mashaka zaidi.


Lakini uhaba huu kama mwalimu; baadhi ya watu badala ya kukaa kwenye foleni na kupoteza muda wanaamua kutotumia gari katika safari ambazo si za muhimu sana.

Sasa tunakuwa macho kutokana na uhaba. Tunaanza kujua kwamba kila kilometa moja inakula mafuta kiasi gani wakati zamani tulikuwa tunajaza mafuta tani yetu na kwa fujo!



Sasa tunafanya maamuzi kwamba niende na gari au niende kwa miguu! Sasa akili yetu inakuwa na neon uhaba kwa karibu zaidi kuliko neon wingi.
Uhaba maana yake ni umasikini. Uhaba ni neon la kiuchumi lenye maana, mahitaji yamezidi rasilimali. Kitu kikiwa haba bei yake inapanda.
Ndio maan sasa hivi serikali ya Tanzania inadai kwamba bei ya vyakula inapanda kwa sababu mvua haikunyesha na hivyo kuna uhaba wa vyakula.
Pia uhaba unaweza kuoanishwa na upatikaaji wa kazi. Kazi ambazo ni adimu zina mishahara mikubwa kuliko kazi ambazo sia adimu.
Kazi adimu ni zile ambazo mafunzo ake ni magumu na hivyo si kila mtu anaweza kuingia na kujifunza.
Wale wanaojitoa muhanga na kusomea fani hizo ngumu wakishamaliza hupata mishahara minono kuliko wat waliosomea fani ambazo ni rahisi kiulinganifu! Na kama serikali zingeweka mishahara sawa kwa fani rahisi na fani ngumu hakuna mtu ambaye angekuwa anasomea fani anasomea fani ngumu!


Kwa hiyo sababu mojawapo ya kuweka mishahara juu kwa ani ngumu ni kuwavutia watu wajitoe muhanga kusomea fani hizo ili wakihitimu wapate mishahara mikubwa! Kwa hiyo fani zenye wataalamu haba zina mishahara minono kuliko fani zenye wataalamu wengi.


Sasa swali linalobaki kwako ni kwa kiasi gani umejiandaa kifani pale kampuni yako itakapoamua kupunguza wafanyakazi? Uko katika watu wenye kazi adimu katika kampuni yako hata kama leo ukiamua kuacha kazi unaamini kwamba kampuni yako itatetereka? Soma kila wakati ili uwe na moja ya fani ambayo kama janga la kutaka kupunguza wafanyakazi likitokea basi wewe uwe mmoja wa wale watakaosalimika.
Na ndio maana wale wanaotetemeka sana wakati wa kupunguza wafanyakazi ni wale wafanyao kazi zisizo na ujuzi!




Sep 7, 2011

BINTI MSAGAJI KATENGENEZWA NA WAZAZI!

Malezi huweza kuwaathiri!




Mwanamke ambaye ana tabia a kujilaumu yeye kama mwanamke na kulaani kuwa kwake mwanamke, yuko kwenye nafasi kubwa ya kumuuwa mtoto wake wa kike kisaikolojia. Kuna wanawake ambao kwa kuudhiwa na waume zao au hata na wanawake wenzao huwa wanapenda sana kuropoka kauli za kudhalilisha jinsia ya kike.


“Mimi nakwambia sisi wanawake hatufai kabisa, kuzaliwa mwanamke ni jambo baya sana………ningekuwa naweza nimwombe Mungu anibadilishe niwe mwanaume …. Wanawake ni wajinga sana….” Kauli za aina hii zinaporudiwa mara mbili au tatu humfanya mtoto wa kike kuziamini na huanza kuwa na wasiwasi na jinsia yake. Hata watoto wa kiume nao huziamini kauli hizi na kuanza ‘ubabe’ wa kiume kuanzia hapo.


Mtoto wa kike anapozisikia kauli hizi kutoka kwa mama yake na kwa sababu mama yake ndiye ‘shujaa’ wake, huanza kujenga dhana kwamba, kama mama yake hapendi kuwa mwanamke, kwa sababu mwanamke ni mjinga na dhaifu, naye hana budi kuikimbia hali hiyo.


Anaikimbiaje?


Kuna njia nyingi za kukimbia hali hiyo, lakini kubwa na ya karibu ni kwa mtoto huyu kuanza kujibainisha na jinsia ya kiume. Kwa sababu akili ya mtoto haichuji, huanza kuhisi vibaya kuwa kwake mwanamke mbele ya wenzake, hasa wanaume. Kujibainisha na jinsia ya kiume ni pamoja na kufuatana na wanaume, kuvaa kiume, kuongea kiume, kutembea kiume na kufanya kazi za kiume.


Siyo lazima, lakini mtoto huyu anaposhindwa kupata mahali ambapo atadondosha dhana au imani hii, ni wazi atakuja kujibainisha kimapenzi, atajibainisha kama mwanaume. Matokeo ya jambo kama hili ni kuwa na mwanamke ambaye anataka kuwa mwanaume kwa wanawake wenzake kimapenzi.


Kama sio kauli za akina mama kujilaumu, kauli za akina baba kuwalaumu wanawake pia na akina mama kuzikubali kivitendo, zinaweza kuwaathiri watoto wa kike kimakuzi. Baba anapokuwa na tabia ya kutoa kauli kali na chafu dhidi ya mama, na mama kuonyesha kukubaliana na kauli hizo kwa vitendo ni hatari sana.


Hebu sikia kauli kama hii kutoka kwa baba: “Mwanamke gani anayezaa mitoto ya kike tu, ni afadhali kuoa mke mwingine…..” majibu ya mwanamke anayekashifiwa ni haya: “Kwani mimi nimetaka, si Mungu mwenyewe, kwani hata mimi si ninapenda watoto wa kiume……” Kwa mtoto wa kike majibu kama haya, huwa yanasikika masikioni mwake kama, “Hata mimi sitaki watoto wa kike kwa sababu hawana thamani, lakini sina uwezo wa kuwakataa..”


Akina mama, yawapasa kuelewa kwamba, kauli zao na kuzipa kauli za waume zao nguvu, huweza kuwaathiri sana watoto wao. Kila neno wanalotamka kwa watoto ni lazima walikague mara mbili. Waume zenu wanapotoa kauli zinazobagua watoto kijinsia mbele ya watoto hao ni lazima mzikanushe sawia na kuwaeleza watoto ukweli utakaowapa nguvu ya kufurahia jinsia waliyonayo.




Sep 2, 2011

HIVI HUKU SIO KUBAKA KWELI?







Kama kubaka ni hali ya mwanaume au mwanamke kulazimisha kufanya tendo la ndoa bila hiyari ya mwingine, basi wanawake wengi sana walioko kwenye ndoa hubakwa na waume zao kila siku.


Kubakwa huku kunatokana na ukweli kwamba wanawake wengi hulazimika kukubali kufanya tendo la ndoa na waume zao kutokana na mazingira mbalimbali yaliyo nje ya upendo.

Kuna ndoa nyingi ambazo zimekufa, ingawa wanandoa wanaishi pamoja. Zimekufa kwa sababu hazina mawasiliano kabisa. Lakini cha ajabu ni kwamba, watu hawa wanakutana kimwili na pengine kuzaa watoto. Kwa sehemu kubwa kwenye ndoa za aina hii, wanawake huwa hawako kwenye ukamilifu wao kimawazo.


Mara nyingi athari huwa ni kwa wanawake kwa sababu wao kimaumbile huishi kihisia. Kutokana na kuathirika kimawazo hamu yao ya kushiriki tendo la ndoa nayo hupotea.


Kwa kuwa hawana hamu ya kushiriki tendo la ndoa, waume zao wanapowaambia, ‘geuka huku’ (hawaongei zaidi ya hapo kwa sababu hakuna mawasiliano), hufanya hivyo. Na hufanya hivyo huku wakiwa hawataki.


Sio wengi wanaoweza kukataa kwa sababu hawakulelewa katika mazingira yanayoweza kuwafanya wakatae. Wamelelewa kwenye mazingira ambayo yamewaambia, miili yao hawana haki nayo mbele ya utashi wa waume zao!


Ukiacha mawasiliano kuna ndoa ambazo wanaume ni Malaya sana, walevi, au wapigaji. Kwenye ndoa za aina hii unaweza kukuta mwanamke bado anaendelea kuwepo kwa sababu mbalimbali, ikiwemo ya utegemezi au watoto. Pamoja na kuendelea kwao kuwepo, hamu ya tendo la ndoa na waume zao nayo inakuwa haipo


Lakini mwanaume hatakiwi kunyimwa mwili wake anapouhitaji. Kwa hiyo, kinachotokea ni mwanamke kufanya mapenzi kwa kujilazimisha au kulazimishwa..


Kuna kesi nyingi ambapo tumesikia juu ya wanaume kuwauwa wake zao kutokana na kuwakatalia unyumba au wakiwa wanapigana baada ya mwanamke kukataa kushiriki tendo la ndoa.

Kwenye ndoa nyingi wanawake hubakwa, yaani hushiriki tendo la ndoa bila hiyari zao. Hulazimishwa au hujilazimisha kutokana na nafasi ambayo jamii imewapa.


Ni kwa nini basi tunapozungumzia kubaka tusiwaambie wanawake na kuwashauri wawe macho na ubakaji huu ambao una athari kubwa kwao na kwa jamii wakiwemo watoto wanaozaliwa kwenye ndoa hizi za kibabe?