Ndio kwanza mmeanza uhusiano ambapo mnaelekea kufunga
ndoa, wote bado ni vijana wabichi, hamna majukumu makubwa yanayohitaji fedha,
hamna watoto, kwa hiyo fedha mnazopata ni kwa ajili ya kula na kusogeza maisha
kidogo, huku mkipanga mipango yenu ya baadae kuhusu kufunga ndoa. Katika
kipindi hiki kila mmoja anajaribu kuishi kama malaika, hataki kumkwaza
mwenzake. Hata kama mwenzake amemkosea atakaa kimya na kuumia ndani kwa ndani
kwa sababu ya hofu ya kuogopa kuonyesha tabia zake pale akasirikapo.
Tabia hiyo huwapa wakati mgumu wapenzi kujuana tabia,
hususan kwa wanawake ambao hutamani sana kuwajua wapenzi wao jambo ambalo
huwawia vigumu kutokana na sababu nilizozieleza hapo juu. Lakini zipo tabia
ambazo anaweza kuwa nazo mwanaume ambazo ki ukweli hazina maana yoyote kwa
wakati huo lakini zinakupa ujumbe mahsusi kwamba huko mbeleni mwanaume huyo
uliye naye atakuwa mume mwema au hatakuwa mali kitu zaidi ya kuwa sawa na mzigo
usiyo na mwenyewe.
Hapa chini nitaeleza baadhi ya vijitabia ambavyo
vitakufanya umjue mwanaume uliye naye kama atakuwa ni mume wa namna gani:
1.Je huwa anazungumza na watu wazima
wanaomzidi umri?
Wakati mnapokuwa mmehudhuria hafla yoyote ambayo
inajumuisha watu wa rika mbalimbali, Je mwanaume uliye naye huwa anazungumza na
vijana wa rika lake au chini ya rika lake au anajichanganya na watu wazima
waliomzidi umri? Kwa kawaida mwanaume kijana ambaye mara jingi katika mjumuiko
wa marika mbalimbali huwa anazungumza na vijana wa rika lake au chini ya rika
lake anadhihirisha kwamba huyo bado hajakua na hayuko tayari kujifunza kutoka
kwa watu waliyomzidi umri. Lakini mwanaume kijana anayependa kujumuika na watu
wazima waliyomzidi umri ambaye anapenda kusikiliza mazungumzo kuhusu maisha yao
ya mahusiano na mafanikio yao katika maisha ni ishara kwamba anataka kujifunza
na kukua. Hapo ni kama anatafuta maarifa ya kuingia katika maisha ya baadaye.
Pamoja na hayo pia awe na tabia ya kutopenda kwenda kwenye nyumba za starehe
usiku na kujumuika na vijana wenzie na kunywa pombe usiku kucha. Na kama ni
mitoko iwe ni ile ya staha na mapema awe amerudi nyumbani kwake. Kijana huyu awe
na tabia ya kujifunza kutoka kwa watu mbalimbali na pia ajenge mahusiano na
watu waliofanikiwa. Hii ni dalili nzuri kwamba anafaa kuwa mume.
2.Je huwa anakuficha kuhusu mambo yake?
Je huwa anakushirikisha kuhusu madhila yake
yanayomletea msongo wa mawazo? Je huwa anakupigia kukujulisha kuhusu mazonge
yaliyomkuta akiwa kwenye shughuli zake? Kama anakushirikisha hii ni dalili
kwamba ni mtu wa kujali familia. Ni mtu anayemthamini mwenzi wake na anayependa
kumshirikisha mwenzi wake kwenye mambo yanayomletea msongo wa mawazo. Lakini
kama ni mtu ambaye anaficha hisia zake chungu na hapendi kumshirikisha mwenzi
wake kwenye mambo yanayomletea msongo wa mawazo zaidi ya kupendelea kuwa naye wakati
wa siku za furaha, huyo haonyeshi kuwa mume mwema mbeleni kwani kushirikishana
katika hisia ziwe ni chungu au za furaha ni msingi wa kujenga mahusiano imara.
3. Anakuwa na tabia gani baada ya kurudi kazini?
Je yeye ni mtu wa kukimbilia remote na kuwasha TV na
kisha kukaa kitako na kuangalia huku akiwa na kinywaji chake baridi
alichochukua kwenye jokofu? Je ni mtu ambaye mawazo yake yametawaliwa na kazi
au shughuli anazozifanya? Yaani yeye akirudi badala ya kuzungumza na wewe
kuhusu siku yako ilivyokwenda badala yake anazungumzia kazi zake au shughuli
zake kisha anakaa kimya.
Mwanaume, anayejali zaidi kazi yake au mambo yake au
hobby zake hawezi kuwa mume bora na mwenye kujali familia huko mbeleni. Je
atawezaje kujali watoto? Je atawezaje kufuatilia maendeleo ya watoto shuleni?
Je atawezaje kujua hali ya mwenzake kwa muda ambao hawakuwa pamoja. Dalili hiyo
inaonyesha hali ya choyo na ubinafsi na bila shaka kama awali anakuwa na mwenendo
huo basi huko mbeleni hali inaweza kuwa mbaya zaidi.
4.Je ni mtu wa kutapanya pesa au kuweka akiba?
Je bwanako ni mtu wa kujirusha na starehe na mwenye
matumizi yasiyo na tija? Kama ni ndivyo alivyo, Je huwa anajuta kwa matumizi
aliyoyafanya? Kama ni mtu wa matumizi, je huwa anapofanya hivyo huwa anahisi
kushtakiwa na dhamira? Ukweli ni kwamba
kuna aina mbili za watu wenye tabia ya matumizi yasiyo ya lazima. Kuna wale
ambao hujihisi kutawaliwa na matumizi yasiyo ya lazima wanajua kwamba wanatumia
fedha zao vibaya lakini hawana uwezo wa kujiondoa katika hali hiyo na mara
nyingi ni watu wa majuto. Aina ya pili ni ya watu wanaotumia fedha zao bila
kujali lakini wanajiamini kwamba hawatapata matatizo ya kifedha yaani wana
uhakika wa kipato chao. Huyu wa pili hana matatizo kwa sababu ana uhakika wa
kipato na matumizi yake ana uhakika hayataathiri akiba yake aliyojiwekea huyu
utakuwa na uhakika wa kuwa salama kwa sababu anajua kuishi kulingana na kipato
chake yaani anatumia lakini ana uhakika kwamba kipato kipo na akihitaji fedha
hapepesi macho maana zipo tofauti na yule wa kwanza ambaye ni mtu wa matumizi
yasiyo ya lazima wakati kipato chake hakina uhakika ni cha kugongea ulimbo. Huyu
anaweza kukuweka roho juu wakati wowote.
5.Je ni mtu wa kupanga mipango na kuisimamia au wa kungoja kuongozwa?
Je mwanaume uliye naye ni mtu wa kujichanganya na na
makundi ya watu na kuwa mtu wa kutoa mawazo mbalimbali kiasi cha kufanywa
kiongozi kwa kuaminiwa au ni mtu wa kusubiri kupangiwa na kuongozwa kila
mahali? Mwanaume yeyote mwenye kutangulizwa mbele katika jambo lolote anafaa
kuwa si kiongozi tu katika maeneo yake ya kazi bali pia hata katika familia.
Lakini yule anayeongozwa kuanzia kazini kwake na hata katika vikundi vidogo
vidogo vya mtaani huyo atakuwa na shida kidogo katika kuongoza familia yake. Ni
kwamba kuwa na mwanaume wa aina hiyo atakupa wakati mgumu pale ambapo
litajitokeza jambo ambalo litahitaji usimamizi wake au kuingiza familia katika
kufikia malengo fulani.
6.Je ni mtu anayejali afya yake?
Je huwa ana kawaida ya kufanya uchunguzi wa afya yake
mara kwa mara ili kujihakikishia usalama wake kiafya? Je ni mtu wa kufanya
mazoezi madogo madogo hata kama anakuwa amebanwa na shughuli zake? Je huwa anakula vyakula kiafya, yaani siyo
mtu wa KUBUKANYA? Je ni mvutaji wa Sigara? Vipi kuhusu matumizi ya dawa za
kulevya au bangi? Je ni mtu ambaye anatumia kilevi kistaarabu kama ni mnywaji,
au ni mtu wa kukesha kwenye vilabu akilewa bila mpangilio? Kwa kawaida mtu
yeyote anayejali afya yake ina maana kwamba anajua thamani ya mwili wake kwamba
ndiyo unaomfanya yeye aishi kwani mwili huu wa nyama ndiyo unaobeba uhai wetu
kama ukiona mtu anaufuja mwili wake bila kujali kwa ina maana hajui thamani ya
yeye kuishi hapa duniani. Mwanamke tafadhali kuwa makini na mwanaume asiyejali
afya ya mwili wake. Mwanaume asiyejali afya ya mwili wake ni wazi atakuwa hana
malengo katika maisha yek kwani kwa kawaida mtu mwenye malengo anajua thamani
ya kulinda afya ya mwili wake kwa sababu anajua wazi kwamba malengo bila afya
imara ni kazi bure!
7.Je Marafiki zake ni wa namna gani?
Je marafiki zake ni watu wa kuaminika? Au ana kundi la
marafiki ambao wanafanana mawazo na humfanya awe na furaha wakati wote? Lakini
ukweli ni kwamba atika maisha yetu huwa tunaathiriwa na watu wanaotuzunguka.
Kwa hiyo kama marafiki wa mwenzi wako ni wa rila la kwenye miaka ya 30 hivi na
kama bado anaishi ghetto na rafiki au marafiki zake na bado ni watu wa
kujirusha labda pamoja na kuvuta bangi na kukesha kwenye vilabu vya usiku. Hii
siyoa ishara nzuri na inakupa taarifa kwamab huyu mwanaume bado hajajiandaa
kubeba majukumu ya kifamilia. Lakini kama ameshatoka kwenye makundi hayo na
akawa anaishi kwenye chumba chake pake yake na kutumia muda wake mwingi kwa
mambo yanayohusu taaluma yake na kushiriki na marafiki waaminifu lakini kwa
kiasi huku akiweka uzingativu kwenye malengo yake, huyo bila shaka atakuwa ni
mume mwema.
8.Je huwa anajisikiaje kuhusu wazazi wake?
Kama wazazi wake wana uwezo, Je huwa anajisikia na
kuringia uwezo wa wazazi wake kiasi kwamba haonyeshi dalili za kujitafutia
maisha yake mwenyewe? Je ni mtu wa kutegemea kila kitu asaidiwe na wazazi wake
au ni mtu wa kupambana na maisha kivyakevyake na kama ni kusaidiwe kuje
baadaye? Je ni mtu mwenye kuvutiwa na juhudi za wazazi wake na kutaka kuwa kama
wao kwa juhudi zake mwenyewe? Lakini vipi kama wazazi wake ni masikini, Je ni
mtu wa kuonyesha kuchukia umasikini wa wazazi wake kiasi cha kujitoa ili
kupambana na maisha ili kuepuka yale maisha waliyopitia wazazi wake? Je ni mtu
wa kuwasaidia wazazi wake kwa hali na mali? Majibu ya maswali hayo yatakupa
picha kwamba mwenzi uliye naye ni mtu wa namna
9.Je ni mtu wa kusongeka mara kwa mara?
Mtu wa kusongeka (Stressers) mara kwa mara hawezi kujificha, utamjua pale atakapopata
changamoto za maisha ambazo siyo za kuumiza kichwa kivile. Na kama hujamjua mwenzi
wako kama ni mtu wa kusongeka jaribu kusubiri hadi pale atakapopata changamoto
ambayo ni ya kawaida ambayo si ya kuumiza kichwa halafu angalia namna
atakavyoipokea.
Je ni mtu wa kutoa msaada hata bila kuombwa?
Kwa mfano kama kuna rafiki yake anahama. Je ni mtu wa
kujitolea kumsaidia kuhama au mpaka aombwe? Je na kama ni mtu mzito katika
kutoa msaada kwa watu wake wa karibu labdea mpaka aombwe, Je maamuzi yake ni ya
namna gani, anakubali moja kwa moja au ni mtu wa kutoa visingizio au hata kama
anakubali lakini haishi kulalamika awapo mbali na rafiki huyo? Wapo baadhi ya
wanaume si wepesi wa kukubali kutoa msaada hapo kwa hapo mpaka wakajishauri
ndipo hukubali, hao hawana matatizo lakini je hata baada ya kukubali huwa ni
mlalamishi?
No comments:
Andika Maoni Maoni