0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Dec 29, 2012

NILIMSIKIA AKISEMA, "NI MTU MWEMA LAKINI ATAKUFA KWA AJALI." AKAFA KWELI...!

Mjomba alikuwa akiishi hapa..............!

Ni mwaka 1975 nikiwa sekondari kidato cha nne, nilikwenda Iringa kwa mjombangu kumsalimia. Alikuwa akiishia eneo linaloitwa Ilula, mji ambao uko nje kidogo ya manispaa ya Iringa. Wakati ule mji huu ulikuwa haujapanuka sana, ingawa ulikuwa umechangamka.

Siku moja usiku, tukiwa ndani tunaota moto, alikuja mgeni ambaye alisema anatokea Mikumi. Alisema anamtafuta ndugu yake pale Ilula. Kwa bahati nzuri, mjomba alikuwa ni rafiki wa huyo ndugu wa mgeni yule. Lakini huyo ndugu yake mwenyewe alikuwa amehamia Njombe.

Hivyo mjomba alimkaribisha mgeni yule apitishe usingizi pale nyumbani ili kesho yake aendelee na safari yake, mgeni yule alilala nami chumba kimoja.

Tukiwa tumelala, alishtuka usiku. Siyo kwa kunigusa, bali kwa sauti. Alikuwa akiongea kwa sauti akisema kuhusu familia yetu. Sikujua kabla sijaamka alikuwa akisema nini, lakini wakati naamka nilimsikia akisema. ‘Ni mtu mwema, lakini atakufa, tena kwa ajali. Na familia yake itateketea baada ya muda mfupi kwa kuonewa. Atabaki mtoto ambaye atasumbuka sana. Namwona anasumbua sana, lakini mbona naye haishi kwa muda mrefu? Anapotea akiwa kijana mdogo.”

Aliposema hivyo, aliniomba nimletee maji ya kunywa. Wakati akisema hayo nilikuwa nimeamka namtazama, naye alijua kwamba, nilikuwa macho. Nilimletea maji akanywa na kurejea kulala. Kwa usiku ule niliogopa kidogo. Siyo kwa sababu ya yeye kuzungumza, bali kuzungumzia kifo na matatizo mengine ya kutisha. Kesho yake yule mgeni aliaga na kuondoka kuelekea huko njombe.

Lakini wakati anaondoka alimwambia mjomba, ‘wewe ni mtu mwema sana. Naomba kila wakati uijali familia yako na ukiweza pia weka kila kitu kwenye maandishi maana binadamu siku hizi hawaaminiki.’ Halafu aliondoka.

Mimi niliingia wasiwasi kuhusiana na maneno yale, hasa lile neno la wema. Ule usiku alisema ni mtu mwema….. Halafu sasa pale amelirudia. Pamoja na neno hilo amezungumzia pia haja ya mjomba kuweka mambo katika maandishi, wakati ule usiku alisema mtu huyo mwema akifa familia yake itateketea.

Baada ya yule mgeni kuondoka nilitamani sana kumwambia mjomba kuhusu maneno ya usiku ya yule mgeni. Lakini kila nilipotaka kufanya hivyo, nilijikuta nikijiambia haikuwa na maana. Nilisita hivyo kutwa nzima, hadi nikaamua kwamba, basi sitamwambia chochote.

Amini au usiamini, lakini ukweli ni kwamba zilipita siku saba tu, kabla mjomba hajafariki.

Alifariki kwenye ajali ya barabarani baada ya gari alilokuwa akisafiria na wafanyabiashara wenzake kuja Dar es salaam, kuacha njia na kuanguka kwenye korongo, karibu na mji wa Ruaha Mbuyuni.

Kwa kweli kwa sababu ya ughafla wa kifo sikukumbuka maneno ya yule mgeni. Lakini siku tatu baadaye, baada ya mazishi, ndipo ambapo nilikumbuka maneno yale. Nilijaribu kuzungumza na mama na wajomba wengine, lakini waliona kama nawapotezea muda.

Mjomba mmoja tu ambaye alikuwa amesoma kidogo ndiye alionesha kuvutwa na habari ile, labda akitaka kufanya udadisi wa kisomi.Lakini hata hivyo alipuuzia, kwani siku ya tano, ambapo kikao cha familia kilifanyika, yeye ndiye aliteuliwa kusimamia mirathi ya marehemu.

Kupitia mikono ya huyu mjomba, jambo la pili alilotabiri yule mgeni lilitokea. Kwa nini? Mjomba alichukua fedha za marehemu na kuzitumia. Zilipoisha baada ya mwaka tu alirudi na kuanza kudai nyumba iuzwe ili watoto wasome. Baada ya ushawishi mwingi sana kwa mamlaka kadhaa, mjomba alifanikiwa kuuza ile nyumba ya mjomba.

Hapo sasa ndipo familia ya mjomba ilipoteketea. Labda kutokana na mshtuko, mke wa mjomba alianza kuumwa. Wakati huo, mke wa mjomba na watoto wake walikuwa wamerudi kwa wazazi wake. Wazazi wenyewe walikuwa wako hoi kiuchumi. Walikuwa wanaishi eneo linaloitwa magole, Morogoro.Kwa kukosa huduma za matibabu na hata lishe, mke wa mjomba alifariki.

Miezi sita tu baada ya kifo chake, mtoto wake mwingine akafariki wakati akifanya kibarua cha kupandisha miwa kwenye trekta, mahali panapoitwa Dakawa. Ilikuwa ni miwa ya kupelekwa kiwanda cha sukari cha Mtibwa. Alifariki akiwa na miaka 16. Fikiria mtoto wa miaka 16 na kibarua cha kupandisha miwa!

Mwaka huo huo, mtoto wa pili wa mjomba, msichana wa miaka 14 alipata ujauzito kutokana na kutangatanga kutafuta maisha. Ninadhani kwa sababu umri mdogo, alifariki yeye na mtoto wakati akijifungua. Kwa hiyo akawa amebaki mtoto mmoja wa mjomba.

Huyu naye alikuwa ameanza kuingia kwenye magenge ya wahuni, tangu akiwa na umri wa miaka 12.Kwa kweli akiwa na miaka 16 alikuwa natajwa eneo lote la Magole na Mvomero kwa ujambazi na ukatili. Sifa zake zilienea na akawa anawindwa na wananchi na Polisi.

Ukweli alisumbua sana na wengi ambao wanamkumbuka hadi leo wanaweza kupata jinamizi usingizini.

Huyu alifariki akiwa na miaka 19, baada ya kutegewa mwanamke. Wananchi, walitumia kila aina ya silaha walimuuwa na kuutumbukiza mwili wake uliochomwa moto mtoni. Hapo huo ukawa mwisho wa familia ya mjomba.

Nilianza kujiuliza maswali tangu kifo cha mjomba hadi cha huyu binamu yangu wa mwisho. Utabiri wa yule mgeni ulitimia. Naamini aliitabiria familia ya mjomba. Lakini mbona hakumwambia mjomba moja kwa moja?

Swali hilo sijapata jibu lake hadi leo………….!

No comments:
Andika Maoni Maoni

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi