0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Dec 12, 2008

HADITHI YA KUHESABU VIFARANGA


KUHESABU VIFARANGA KABLA HAVIJAANGULIWA.

Inawezekana hata wewe umeshawahi kuambiwa kwamba usihesabu vifaranga kabla havijatotolewa. Mara nyingi msemo huo hutumiwa katika jamii yetu ikiwa ni njia ya kumwonya mtu kwamba asiwe na matarajio makubwa na jambo ambalo halijafanyika kwa ukamilifu.

Kila mtu, labda ukiwemo na wewe, unajua kuhusu jambo hili na unaliogopa pia. Unaliogopa kwa sababu umeambiwa kwa muda mrefu sana kiasi kwamba limekuwa ni kweli akilini mwako.

Nikisema limekuwa ni kweli nina maana kwamba unaliamini kuwa ndivyo lilivyo.
Hili ni tahadharisho kwamba mtu ukiwa na matarajio makubwa, utavunjika sana nguvu iwapo matarajio hayo hayatazaa matunda yanayotarajiwa.

Bila shaka, waliotuambia hivyo walikuwa wanasema kwa nia njema kabisa.
Lakini je lilifikishwa kichwani mwako kwa njia nzuri, ambayo isingeweza kuzalisha maana tofauti kabisa?
Kila mmoja wetu wakati anakuwa aliwekwa kwenye tahadhari, ambapo alitakiwa bila kujua, kujiweka kwenye mazingira ambayo yatamfanya awe salama kihisia muda wote.

Kwa mfano kutokujenga matarajio makubwa ni ili mtu asije akaumia sana kihisia pale matarajio hayo yakishindwa kufikiwa. Lakini leo ukubwani jambo hilo limekuwa ni sehemu muhimu ya tabia zetu. Hatuko tayari kuwa na matarajio makubwa kwa sababu tunaogopa kwamba kufanya hivyo ni kuingia mahali ambapo tutaumiza sana hisia zetu, pale ambapo jambo tunalotarajia likishindwa kuwa.

Tunaishi kwenye dunia ambayo saikolojia ya binaadamu imeegemezwa kwenye hofu. Hofu ya kupoteza inatusukuma na kutuendesha katika kufanya maamuzi yetu, na katika tabia zetu kwa ujumla.

Kwa sababu ya hofu na mashaka jamii imejitengenezea njia ya kujihami na maneno kama ‘usihesabu vifaranga kabla ya kuanguliwa’ ni moja ya njia hizo ambazo, hutufanya wanajamii kufikiria karibu, kutokuwa na matarajio na kuogopa kutazama mbali.

Kuamini katika msemo kama huo, kuna maana sawa kabisa na kuamini kwamba, mtu anatakiwa kufanya kidogo na kwa karibu ili asije akaumia, endapo atafikiria kufanya kikubwa na kwa mbali halafu kikakwama.
Kila mmoja amefundishwa kujilinda kihisia, kukataa maumivu ya kihisia, pale mambo yatakapoenda mrama.

Kuna baadhi ya maeneo hapa nchini ambapo mtu hatakiwi kusema kwamba at fanikiwa au kupata sana. Kwa mfano kusema atapata mavuno mazuri ni jambo lisilokubalika sana.

Anapokosea na kufanya hivyo, anatakiwa kutema mate chini ili kuvunja balaa ambalo linaweza kutokea.
Anachotakiwa mtu kusema ni kwamba hana uhakika, hajui, ‘ndio hivyo hivyo’, ‘Mungu mwenyewe akipenda nitafanikiwa’.

Kusema kwa uhakika ni jambo linalotisha, lakini pia ambalo linachukuliwa na jamii kama kuringa au kujiona,
Kwa hiyo jamii inaona kufikiria mbali, kuamini kwamba inawezekana ni kuringa.

Unakuta kutokana na mawazo haya, unapoteza kabisa nguvu ya kufanya na kumudu, tunapoteza uwezo wetu kama binadamu ambao tuna vipaji na uwezo mkubwa sana wa kiakili. Hapa ndipo ambapo imani nyingi tulizopewa zinapoonesha udhaifu wake kwetu.
Bila shaka hujui kwamba matarajio ni moja ya rasilimali za nguvu sana ulizonazo.

Hali ya matarajio ya jambo ambalo limetiwa shime linaweza kugeuza kile kilichoonekana kuwa hakiwezekani kikawezekana. Kama una ndoto, una lengo ambalo unataka kutimiza ni lazima uwe na matarajio makubwa, ndipo utakapoweza kulitimiza hasa pale inapotokea kwamba unakutana na vikwazo vikubwa.

Bila matarajio makubwa, utasimama na kuacha, utakata tamaa. Wengi tunakata tamaa kwa sababu hatuna matarajio makubwa. Tulishaogopeshwa kujenga matarajio makubwa. Unapohesabu vifaranga kabla havijaenguliwa unapata nguvu kubwa ya ajabu kwa sababu unaona mafanikio, unajua inawezekana na unajua imekuwa tayari.

Bila kuhesabu au kuogopa kuhesabu kunaweza kukuvunja nguvu na kukufanya uhisi kwamba hakuna la maana, hakuna kutakachozalishwa .
Usije ukachanganya kati ya matarajio na matumaini.
Kutumaini ndiko ambako hakuna maana kwenya maisha. Kutumaini ni kuhisi kwamba kuna siku bahati itatokea na jambo fulani litafanyika na kutakuwa na matokeo fulani siku zijazo.

Kutumaini si lolote bali ni sala dhaifu, kutumaini siku zote huhusisha mafanikio na maanguko. Wakati matarajio yamefungwa kwenye tokeo moja tu-kufanikiwa. Kuhesabu vifaranga kabla kuna maana kujitilia nguvu matarajio yetu.

Kwa kutengeneza matarajio, sio tu kwamba unajipa nguvu ya kusonga mbele, bali pia unapata nguvu mpya, unaona jambo likiwa kama limekamilika, hatua ambayo ni muhimu sana katika kukamilisha malengo yetu.
Kile ambacho mtu anakitaka kwa uhakika na kuamini kwamba atakipata, huo ndio utabiri anaojifanyia , kwani siku zote huwa kweli.

Wengine ili kuwa na uhakika ni lazima kwanza waone na kupata uzoefu wa jambo ndipo waamini. Watu hawa ni wale ambao kila siku wanachozungusha kwenye mawazo yao ni vile vitu ambavyo waliviona vikiwezekana na kupata uzoefu wake, nje ya vitu hivyo, vingine haviwezekani. Kwa nini sasa usianze kuamini kwamba jambo litakuwa, na litakuwa kweli ili uanze kujenga picha ambayo utaiamini ili ufanye kwa mafanikio?

Kwa kuwa na matarajio mtu anajua kwamba jambo litakuwa, litafanyika, anakuwa na matumaini kuhusu uwezekano wa jambo kufanyika. Kwa hiyo kuhesabu vifaranga kabla havijaenguliwa ni jambo zuri sana tofauti na ulivyoambiwa kwamba ni nuksi na halina mwisho mwema.

No comments:
Andika Maoni Maoni

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi