0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Nov 25, 2008

MWILI WA AKILI UNAFANYAJE KAZI?Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa mwezeshaji wa utambuzi katika kituo cha FAJI, Dr. John Simbila.

Mwili wa akili:

Akili ni uwezo wa kuelewa na kujifunza mambo au uwezo
wa kufikiri na kuamua kwa busara. Ubongo ni bonge laini la
nyamanyama lenye mishipa ya fahamu lililomo kichwani. Jiulize, je, akili inazalishwa kwenye ubongo au inapitia tu kwenye ubongo ikitokea mahali fulani?

ubongo – ubongo umegawanyika katika sehemu tano:
( I ) Ubongo wa thalamus.
(II ) Ubongo wa hypothalamus.
( iii) Ubongo wa cerebellum.
( iv ) Ubongo wa shina (brain stem )- huu umegawanyika sehemu tatu:
i. Ubongo wa kati ( mid brain ).
ii. Ubongo wa pons valorii.
iii. Ubongo wa medulla oblongata.

(v ) ubongo wa cerebrum.

Huu ni mkubwa kuliko sehemu nyingine za ubongo.
Hutafsiri na kusimamia matendo yaliyo chini ya uamuzi wa mwili kama vile, kutoa sababu, kupanga mipango, kuhifadhi kumbukumbu, kutatua matatizo. Pia ni kitovu cha akili na haiba.

Ubongo huu umegawanyika sehemu 2:

i. Ubongo wa kushoto- husimamia upande wa kulia wa mwili. Hupokea na kutafsiri taarifa pamoja na kuratibu utendekaji kazi wa misuli upande wa kulia wa mwili.

ii. Ubongo wa kulia – husimamia upande wa kushoto wa mwili. Hupokea na kutafsiri taarifa pamoja na kuratibu utendekaji kazi wa misuli upande wa kushoto wa mwili.
Hali hii ( hapo juu ) inatokana na mishipa ya fahamu inapopita kati ya ubongo wa medulla oblongata na uti wa mgongo kupashana kwenda upande wa pili.

Karibu asilimia 90 ya watu wote duniani, ubongo wao wa kushoto unahusika na mantiki – orodha, maneno, tarakimu, mfuatano na uchambuzi. Wakati ubongo wao wa kulia unahusika na ubunifu, mapigo, rangi, kujenga taswira, ndoto za mchana, utambuzi maalumu, muziki na usanii. Lakini kwa baadhi ya watu, utendaji kazi huu wa ubongo huwa ni kinyume, na kwa watu wachache huwa hakuna tofauti.

Uchunguzi wa kitaalamu unaonyesha kwamba:

( I )Ubongo wa kushoto – unafanya kazi zaidi ya asilimia 90 kwa wale wanaotumia mkono wa kulia na asilimia 64 kwa wale wanaotumia mkono wa kushoto.

( ii ) Ubongo wa kulia – unafanya kazi kwa asilimia 10 kwa wale wanaotumia mkono wa kulia ni asilimia 20 kwa wale wanaotumia mkono wa kushoto.

(iii) Asilimia 16 iliyobaki ya watu wanaotumia mkono wa kushoto, ubongo wao wa kushoto na wa kulia unafanya kazi sawa.

Kumbuka kwamba, ubongo wa thalamus, hypothalamus kwa kushirikiana na sehemu za ubongo wa cerebrum kwa pamoja huunda mfumo unaoitwa mfumo wa limbiki (limbic system). Mfumo huu huhusika na kuhifadhi kumbukumbu pamoja na hisia kama vile huzuni, furaha, hasira, hofun.k. Hufanya kazi ya kurekebisha hisia zinazoimarisha uhai ( bila hisia, hakuna uhai).

Milango ya fahamu – hutujulisha kinachoendelea katika mazingira ya nje (mazingira yanayotuzunguka) ili mwili uweze kuchukua hatua zilizo chini ya uamuzi wa mwili au ambazo haziko chini ya uamuzi wa mwili na hivyo kuimarisha mazingira ya ndani ya mwili ( homeostasis) .
Lakini, mbona kuna wengine milango yao ya fahamu haifanyi kazi? Ina maana wao hawafahamu kuhusu mazingira yanayowazunguka? Je, hizi taarifa zinazotolewa na milango ya fahamu zina ukweli kiasi gani? Hebu jiulize kama kweli taarifa zote kuhusu mazingira yanayokuzunguka zinatolewa na milango ya fahamu.

Ulishawahi kusikia kuhusu machale? Ni kitu gani hiki? Ni mlango upi wa fahamu? Wataalamu wanasema kwamba kwenye ubongo wa kulia kuna eneo linaloitwa intuitive area (eneo la machale ) ambalo ndiyo linaloto taarifa za kweli kuhusu mazingira yanayotuzunguka. ( Machale ni mada inayojitegemea nitaijadili baadae katka makala zangu)

Kuna aina kuu mbili ya milango ya fahamu:

1. Milango ya fahamu mjumuisho – iko mitatu

i.Mlango wa joto – huhisi baridi na moto.
ii. Mlango wa mgandamizo na mguso – hihisi mgandamizo na mguso.
iii.Mlango wa maumivu – huhisi maumivu. Maumivu ni
muhimu sana kwa uhai. Hutufahamisha hatari inayotokea kwenye miili yetu ili tuweze kuondoa kihatarishi au tuhitaji matibabu.

2. Milango maalumu ya fahamu – hii ipo minne.
( i ).Mlango wa kunusa ( pua )- husaidia kunusa harufu mbalimbali. Husaidia kuchagua chakula kwa kusaidiana na mlango wa kuonja (ulimi). Tunanusa chakula na wakati huohuo tunaonja chakula. Ukiwa na mafua ladha ya kitu au chakula huwa ikoje?

( ii ) Mlango wa kuonja (ulimi) – husaidia kuonja ladha ya kitu au chakula kusaidiana na mlango wa kunusa(pua). Kuna aina nne za vionjo vilivyopo kwenye ulimi, navyo ni: vionjo vya utamu (mbele ya ulimi) – kuonja vyakula vitamu. Vionjo vya ukakasi (pembeni ya ulimi) - kuonja vyakula vyenye ukakasi. Vionjo vya chumvi (sehemu yote ya ulimi) – kuonja vyakula vya chumvi. Vionjo vya uchungu (nyuma ya ulimi) – kuonja vyakula vichungu.

( iii ) Mlango wa kusikia (sikio) – hufanya kazi mbili: kusikia pamoja na kuweka mwili sawa (kuubalansi) . Mawimbi ya sauti hupimwa kwa kutumia kipimo kinachoitwa decibels scale(Db). Mtu akikaa kwa muda mrefu kwenye eneo au sauti inayozidi 90dB huweza
kusababisha tatizo la kudumu la kutokusikia, mfano: sauti
inayotolewa kwenye amplifaya 120dB, sauti inayotolewa na ndege wakati wa kupaa 140dB. Taarifa ya kusikia kutafsiriwa na pande zote mbili za ubongo wa kulia na ule wa kushoto. Sikio pia hutumika kuimarisha wima wa mwili kwa kusaidia na misuli, viungo ( jointi) pamoja na macho.

( iv )Mlango wa kuona (jicho) – kwenye macho, kuna vipokea taarifa vya mwanga vinavyoitwa rods na cones.
Rods hutumika kuona kwenye mwanga hafifu. Vitamini A husaidia rods kufanya kazi vizuri. Hivyo, upungufu wa vitamini A husababisha upofu wa usiku (night blindness).
Cones hutumika kuona kwenye mwanga wa kawaida/ mkali.

Huonyesha rangi ya kitu. Kuna aina tatu za cones: zile zinazoona vizuri zaidi rangi nyekundu, zile zinazoona vizuri zaidi rangi ya bluu na zile zinazoona vizuri zaidi rangi ya kijani. Kuna aina mbalimbali za upofu wa rangi, inayojulikana zaidi ni ile ya upofu wa rangi nyekundu na kijani. Mtu mwenye tatizo hili hawezi kutofautisha kati ya rangi ya kijani na nyekundu. Tatizo hili huruthiwa, huwapata zaidi wanaume kuliko wanawake.


Kuchanganyika kwa milango ya fahamu (mixed-up senses): hali hii kwa kitaalamu huitwa synesthesia. Tafsiri na taarifa za milango ya fahamu huwa zimegawanyika. Usishangae kusikia mtu akisema, rangi inanuka bluu, jioni ya leo ni chumvi, ladha ya mandazi ni pembe tatu, tatu ni ya njano, ijumaa ni ya kahawia. Yamkini hata ule msemo wa blue Monday uliotolewa na watu wenye hali hii. Mara nyingi, herufi, namba, au muda huwa wanaziona kwa rangi maalumu. Haijafahamika vizuri hali hii husababishwa na nini.

Ingawa inawezekana husababishwa na kutokukomaa kwa mfumo wa fahamu au umeme wa ubongo kupelekea taarifa mahali ambapo ni tofauti kwenye ubongo wa cerebrum. Hali hii huwa inaridhiwa na huwapata zaidi wanawake.

Kutokana na maelezo hayo hapo juu, yametuonyesha kwamba, mwili wa akili ndiyo kitovu, hivyo ni mwili muhimu zaidi. Kama ni lazima tuwe chochote, basi tulipaswa tuwe mwili huu. Lakini hatuwezi kuwa mwili huu kutokana na sababu tutakazoziona baadaye. Mwili huu ndiyo injini ya maisha yetu ( controlling power) – mind (right thoughts), mouth (right speech) na deed (right actions).

Mwili huu unaunganisha mwili wa hisia na mwili unaoonekana. Unaundwa na mfumo wa fahamu (ubongo na milango ya fahamu) pamoja na urazini wa binadamu. Urazini ni sababu za msingi za kufanya jambo, ni maelezo ya kanuni, misingi au sababu.

Ni utambuzi wa ndani yako na nje yako, fahamu upo, nini kinaenda ndani na nje yako. Unapofanya jambo, jitahidi usiwaze kitu kingine ila zingatia tu unachofanya. Jitahidi akili yako ikae mahali ulipo tu. Usipuuze chochote, usimhukumu mtu yoyote ila kuwa na uadilifu (uwezo wa kujibainisha na mtu).

Usiwe na urazini wa viraka, toa fujo zote zilizomo ndani mwako. Kila siku iambie akili yako kwamba, kila kitu kinawezekana, kila kitu ni ok. Futa neno haiwezekani, siwezi, sitaki, sipendi kwenye akili yako.

Mwili huu hutafsiri maisha kwa kwa kadri ya maarifa uliyopewa na vyanzo mbalimbali. Vyanzo hivyo ni wazazi, walimu, mazingira na uzoefu mbalimbali tuliopitia. Maarifa haya ndiyo ambayo leo hii tunayaita akili, fikra au mawazo yetu. Ukweli ni kwamba sisi tunazo akili. Ukweli wenye kuuma zaidi ni kwamba akili hizo ni za kupewa, hivyo hatuna akili kwa sababu siyo za kwetu, ni za kupewa. Sisi ni maroboti/kasuku wa jamii, wazazi, walezi, walimu, marafiki n.k. Yamkini, maarifa hayo yanaweza kuwa siyo ya kweli na mengine yakawa ya kweli ( jiulize, kila unachokiona ni halisi au kwa sababu uliambiwa?).

Ili mwili huu tuweze kuutumia kwa faida yetu, ni muhimu kuufahamu vizuri. Lakini kuufahamu peke yake haitoshi, bali ni muhimu sana kufahamu umebeba taarifa zipi na za vyanzo gani. Mwili wa akili ndipo mahali palipowekwa sauti na taswira ambazo zinatuambia maisha ni kitu gani, sisi ni nani, kipi kifanyike, wakati gani, wapi au kwenye mazingira gani.

Tulipokuwa wadogo, tuliwekewa maarifa na watu tuliowaamini. Kuna mambo mengi ambayo tuliambiwa lakini siyo ya kweli. Ni ukweli wa kimapokeo, mfano: tusi ni kitu kibaya, kuoa au kuolewa ni kuzuri, kuachwa ni kubaya, thamani zetu zinategemea tuna kitu gani au hatuna nini?

Tukaambiwa pia kwamba - mwanamme hatakiwi kulia, fedha haipatikani mpaka uhenyeke sana, biashara ni za wahindi, wapemba na wachaga, ukoo wetu tumelaaniwa, utajiri ni kwa wale waliozaliwa na matajiri tu, maisha ni uwanja wa vita, ndoa ndoano, kumsaidia mkeo kazi za nyumbani ni utumwa au umepewa limbwata, mafanikio ni kwa wasomi tu. Kwa kuwa tunaamini ukweli huu wa mapokeo, matokeo yake tunashindwa kupata tunachohitaji.

Huna budi kuubadili, siyo wa kweli. Na badala yake, tafuta ukweli halisi. Utaupata wapi? Ukweli halisi inabidi tuutengeneze wenyewe kwani tayari tunao ndani yetu. Hii inawezekana tu kama utabadili mfumo wako wa kufikiri, unavyofikiri ndivyo unavyokuwa. Amini kila kitu kinawezekana, ondoa hofu, kubaliana na hali, kuwa mbunifu, usijali muda, usiogope kuhatarisha n.k.

Mwili huu unasimamiwa na fikra na mawazo. mawazo yetu ndiyo yanayofanya mambo yatokee. Mawazo hayataki kuratibiwa (kuwa displined), yanataka yafanye yanavyotaka yenyewe. Yanakuja yenyewe, huwezi kuyazuia wala kushindana nayo ila unaweza kuyaratibu kwa namna unavyotaka.

Tukutane wakati mwingine kwenye mada ya mwili wa hisia.
Kama kawaida nakaribisha maswali na maoni.


4 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. hodi hodi mwenyewe! asante sana kwa darasa nzuri nitarudi tena siku nyingine

  ReplyDelete
 2. Dada Yasinta,

  Karibu sana, yaani nakukaribisha kwa mikono miwili, naomba hii iwe ni blog yako ya kutembelea na kujifunza maarifa mapya, ambayo kwayo huenda yakabadilisha baadhi ya mitazamo yako.
  Watambuzi huwa wanayaaangalia mambo kwa mkabala tofauti.
  karibu sana.

  Shabani Kaluse

  ReplyDelete
 3. Pengine nimeshindwa kuyaelewa vizuri maneno uliyoyatumia katika kutofautisha baina ya milango ya fahamu mjumuisho na milango ya fahamu maalumu. Umetumia vigezo gani kuitofautisha?

  Kazi nzuri.

  ReplyDelete
 4. Mtaalam kwanza nikupongeze kwa elimu nzuri.

  lakini nikuombe kwamba:- ni hatua zipi kwa maana ya process au procedure zinazofanyika katika ubongo mpaka kufikia maamuzi, yaani AKILI kuonekana?

  Lakini pia kuna wataalam wanasema kuna milango mitano ya fahamu yaani minne na wa tano ni kugusa, lakini wewe umeitofautisha! je! ipi ni sahihi?

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi