0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Apr 2, 2010

MALAIKA WA KIFO! SEHEMU YA PILI


Muuaji Orville Lynn Majors


ILIPOISHIA........


Muuguzi huyo alikiri kwamba kuna wakati walikuwa wakicheza kamari kwa kuwekeana dau juu ya mgonjwa gani atakufa pindi Orville atakapokuwa kazini, na mara zote mshindi alikuwa akipatikana na kujizolea kitita cha fedha. Pamoja na ushahidi huo ambao ulielemea zaidi kwenye minong’ono na maneno ya mitaani, lakini bado wapelelezi walikuwa na wakati mgumu wa kujenga ushahidi madhubuti wa kumtia Orville hatiani.

ENDELEA KUSOMA HAPA………………

Ili kupata ushahidi huo ilibidi wapelelezi wa polisi watumie muda mwingi kuwaita watu ambao ndugu zao walipoteza maisha katika hospitali hiyo na wanao ushahidi kwamba kwa njia moja au nyingine Orville alihusika. Mtu wa kwanza kujitokeza alikuwa ni kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Russell Firestone au kwa jina la utani aliitwa “Rusty”.

Kijana huyu alimpoteza baba yake aliyekuwa na umri wa miaka 74 wakati huo. Kijana huyo akitoa ushahidi wake mbele ya wapelelezi wa Polisi, Rusty alisema kwamba baba yake alilazwa katika hospitali hiyo mnamo December 12, 1994, kwa wiki kadhaa baada ya kusumbuliwa na tatizo la kuzimia ghafla. Kijana huyo aliendelea kuwaeleza Polisi kwamba baba yake alipewa ruhusa kabla ya kulazwa tena siku sita baadae katika hospitali hiyo hiyo.

Baada ya kupata tarifa kuwa baba yake amelazwa tena, Rusty alikwenda kumuona na alipofika hospitalini hapo alimkuta Orville na muuguzi mwingine wakiwa pembeni ya kitanda cha baba yake, alipowakaribia alimsikia yule muuguzi akisema kwa sauti “mwanae huyo anakuja” Alipofika karibu na kitanda alichokuwa amelala baba yake alimuona baba yake akipepesa macho na mara ghafla akaacha kupepesa macho na kubaki kimya kama vile mtu aliyekata roho. Alipowauliza kwamba baba yake amepata tatizo gani, walimjibu kuwa hajui, hata hivyo Orville alitoa mashine yake ya kupimia mapigo ya moyo na kumpima baba yake, lakini kulikuwa hakuna dalili za mtu kuwa hai. Baadae Orville alichukuwa box lake alilokuwa nalo na kuchukuwa sindano kisha akaijaza dawa asiyoifahamu na kumchoma baba yake na kutoweka.

Rusty alimuuliza yule muuguzi kama ile sindano ilikuwa ni ya dawa gani lakini hakupewa jibu na badala yake yule muuguzi aliendelea na shughuli zake. Baadae Orville alirejea na hapo ndipo yule muuguzi alipomuuliza kwamba Rusty anataka kufahamu kama ile sindano ilikuwa ni ya nini?

Kwa maneno yake mwenyewe Orville alimjibu kwa mkato “baba yako amekwisha fariki, je kuna mtu unahitaji kumuita?” kisha wote wawili wakatoweka na kumuacha pale peke yake.
Mtu mwingine aliyetoa ushahidi wake alikuwa akijulikana kwa jina la Robert Doran.

Akiongea na wapelelezi wa Polisi, Robert alisema kwamba anakumbuka baba yao John Andrew Doran aliyekuwa na umri wa miaka 76 wakati huo, alilazwa katika Hospital hiyo mnamo October 1994. Akisimulia zaidi Robert alisema kwamba baba yao alianza kupoteza uzito ghafla na kuwa dhaifu kulikoambatana na kizunguzungu, hivyo walipoona hali ya baba yao imebadilika ghafla vile yeye na mkewe aliyemtaja kwa jina la Marjorie waliamua kumpeleka katika katika hospitali ya Vermillion County kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Walipofika Hospitalini hapo baba yao alilazwa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi. Siku iliyofuata walirejea pale Hospitalini ili kufuatilia vipimo vya baba yao, lakini walipofika walikuta baba yao amehamishiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi. Robert alibainisha kwamba hapo ndio kwa mara ya kwanza alipomuona Orville.

Kwa maneno yake mwenyewe Robert alisema “Huyu kijana mwenye mwili mkubwa(Akimaanisha Orville kwa sababu alikuwa ni mnene) alifika pale tulipo na kutusalimia na kisha alijitambulisha kwetu”

Huku akimnukuu Orville Robert alisema, “Jina langu naitwa Orville Lynn Majors, mimi ndie nitakaekuwa muuguzi wa baba yenu leo, si mlikuwa mkihitaji muuguzi Mahiri?” kwa jinsi alivyokuwa akizungumza alionekana kuwa ni muuguzi mzuri anaeifahamu kazi yake na ambae aliguswa na ugonjwa wa baba yetu, aliendelea kubainisha Robert.

Baadae majira ya mchana Robert alikiri kumuona Orville akimchoma baba yao sindano ambayo wote hawakuifahamu na baada ya sindano hiyo baba yao alionekana kupua kwa shida na kuonekana kama vile anataka kupoteza fahamu. Akiwa amesimama pembeni Orville alikuwa akimpiga piga begani baba yao huku akimwambia “subiri kidogo nakuandalia dawa nyingine”

Baadae baba yao alifariki kwa kile kilichoelezwa na daktari kwamba amefariki kwa ugonjwa wa shambulio la moyo (Heart Attack). Robert aliendelea kuwaeleza wapelelezi wa Polisi kwamba baada ya habari za hospitali hiyo kutuhumiwa kusababisha vifo vya watu wengi kutoka katika vyombo vya habari, yeye na mkewe Marjorie Doran waligundua kwamba huenda na wao walishuhudia mauaji ya baba yao akiuwawa na Orville mbele ya macho yao.
Kwa manaeno yake mwenyewe Robert alisema “ Tulijiona wote tuwajinga kwa kukaa kimya baada ya tukio lile ambalo lilifanyika mbele ya macho yao”

Mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka 1997, bado jopo la wapelelezi walijua dhahiri kwamba isingekuwa rahisi kwao kupata ushahidi wa kina wa kumtia hatiani Orville Lynn Majors.
Kesi ya Orville ilianza kusikilizwa rasmi mnamo December 30 1997 katika mahakama ya Clay County.

Huku akionekana kutokuwa na wasiwasi, Orville alikuwa ametulia wakati Jaji wa mahakama hiyo aliyejlikana kwa jina la Ernest Yelton alimsomea mashitaka ambayo ni ya kuhusika na mauaji ya watu sita, ambapo akipatikana na hatia adhabu yake itakuwa ni kifungo cha miaka isiyopungua 65. Baada ya kusomewa mashitaka hayo wakili wa Orville aliyejulikana kwa jina Marshall Pinkus, alikanusha mashtaka yote yaliyosomwa, kwa niaba ya mteja wake.

Akiongea na waandishi wa habari mara baada ya Orville kusomewa mashitaka, wakili huyo aliwaambia waandishi wa habari kwamba mteja wake amestushwa sana na mashtaka yale.
Wakili yule aliendelea kusema kwamba, anadhani kuwa baada ya miaka mitatu mingine huenda mtu mwingine akafunguliwa mashtaka yanayofanana na yale kwa sababu vifo vyote vilivyotokea katika Hospitali ya Vermillion County kwa jinsi ninavyofahamu vilikuwa ni vifo vya kawaida kabisa. Siamini kabisa kama kuna mtu alihusika na vifo vile.


ITAENDELEA.................

No comments:
Andika Maoni Maoni

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi