0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

http://www.serenahotels.com/serenadaressalaam/default-en.html

Mar 6, 2009

ALITABIRI KIFO CHAKE?

Hatuna haja ya kuhofia kifo

Hivi karibuni nimesoma kuhusu mtu anayedaiwa kuwa mzee kuliko wote duniani kwa sasa. Mtu huyu mwenye umri wa miaka 111, ambaye ni Mjapani, alipoulizwa maoni yake, alisema, hataki kufa. Nilianza kujiuliza, hivi ni lini kifo kitakuwa ni jambo la hiari na lenye kupendeza? Lakini, hata hivyo, mbona maisha ni mafupi sana, hata kama mtu atapewa miaka 200 ya kuishi!

Binafsi, napenda kufurahia maisha yangu, lakini najua kwamba maisha ni mafupi sana. Watu wengine wanakiona kifo kama tatizo kubwa linalowazonga.
Watu wengi ambao walishaaga dunia kama vile mababu wa mababu zetu mimi nahisi kama wanaishi vizuri tu huko walikoenda.

Ni kujisumbua kukikataa, kukiogopa au kukiona kifo kama ni tatizo kubwa ajabu. Wengi wa waliokufa wanakiona kifo sawa na mtu aliyemaliza shule na kufuzu. Inabidi hivi sasa tubadilike na tukione kifo kama mtu aliyepitiwa na usingizi wenye jinamizi na kuamkia kwenye ulimwengu wenye amani na usalama.

Lazima wote tufe! Lazima tuishi maisha haya tuliyoyazoea na baadaye tuondoke twende tukaishi maisha mapya ambayo hatukuyazoea. Tujue kwamba maisha tuliyoyazoea ni ya muda tu, na maisha ambayo hatukuyazoea ni ya muda mrefu.
Kama umetafakari kwa makini nafikiri umeshaona kwamba hakuna binadamu anayeishi milele. Mamilioni ya watu wanaoishi duniani ni wafu watarajiwa.

Wengine wanajitahidi kusogeza maisha yao mbele lakini iko siku itawadia na wataondoka, watake wasitake. Nahisi kwamba watu hung’ang’ania maisha ya dunia kwa sababu hawajui maisha baada ya kufa yakoje. Wazo langu ni kwamba kifo si chanzo cha mateso. Chanzo cha mateso ni raha za muda ulizonazo duniani. Unaona kwamba kifo kitakuondolea raha hizo.

Hivi mtu ambaye yuko kwenye maumivu makali ya kupigwa risasi na damu inamwagika kwa kasi bado atatamani aishi? Atataka afe ili aondokane na maumivu makali anayoyapata.
Kifo ni rafiki yetu wa kweli. Kifo kinatutahadharisha kwamba tusiyategemee sana maisha tunayoishi. Kifo kinatukumbusha kwamba kila dakika tuliyonayo inapaswa itumike ipasavyo. Somo kubwa tulipatalo kutokana na kifo, inabidi liwe kwamba maisha baada ya kifo ni ya furaha na watu tukubali kifo, tuwe tayari wakati wowote kufa.

Hebu jiulize swali lifuatalo: ‘Hivi niko tayari kufa sasa hivi?’ Kama jibu lako ni hapana, ni kitu gani kinachokufanya utake kuendelea kuishi? Unaogopa kufa au unaogopa kupoteza mali zako ulizochuma kwa jasho? Ukweli ni kwamba kama kifo kipo na haijulikani kitakufika lini, haina haja wewe kuogopa kwa sababu una umri mdogo au una mali nyingi. Uoga huu ni kwa sababu hatujajiandaa kufa. Kama unataka suluhu na kifo basi jiandae kufa.
Siyo lazima uwe tajiri sana, na baada ya kufikia lengo hilo ndiyo uwe muda muafaka wa kufa.
Hivi sivyo. Sijatimiza yote niliyopanga, lakini niko tayari kufa sasa hivi. Ndiyo maana siogopi kifo na wala sikioni kifo kama janga. Kifo ni sehemu muhimu kwenye maisha yangu!
Kweli kuna mambo mengi sijayafanikisha, lakini juhudi nilizofanya zilikuwa sahihi. Sasa tatizo liko wapi hadi nidhani nastahili kufa baada ya mafanikio tu! Malengo yangu yalikuwa mazuri sana lakini sikuyatimiza kama nilivyopanga.

Hapa cha msingi ni malengo kuwa mazuri lakini kama binadamu nina kikomo cha uwezo wangu. Maumbile hayakutaka kila nililotakla liwe kukamilika.
Hii inatosha kukufariji na kujua kwamba umetenda uliyopaswa kufanya, na hii inatosha kukikaribisha kifo kikuchukue bila woga, kwamba kuna kitu hukukitimiza.
Ukishajua hivi hutakiogopa kifo na utaishi maisha yenye furaha uwe na umri mdogo, maskini au tajiri.

Kuogopa yanayohusu kifo hilo ndilo janga la kweli, lakini kifo kamwe si janga. Kwani, aliyekwambia kwamba, kifo kina ubaya ni nani? Ni dini yako, ambayo inakutishia kuhusu moto, majoka na hasira za Mungu! Dini ingekwambia, baada ya kifo ni amani na furaha tupu isiyo na mwisho, usingethamini maisha haya ya shida ya kidunia.

Maisha baada ya kifo ni ya milele. Kama ni ya milele yataweza vipi kuwa ni maisha ya shida na mashaka? Maisha ya shida na mashaka ni yale yenye muda maalumu, tena mfupi.
Kila mmoja anataka kutimiza jambo fulani na anafukuzana na muda katika kutaka kufanya hivyo. Ndiyo maana kifo kinatazamwa kama adui.

Kama nilivyosema awali, kila mtu amefundishwa kuwa kifo hatima yake ni shida na mateso, ni hofu na vitisho. Mimi siamini kwamba, kwa Mungu mwenye upendo na huruma na usamehevu kunaweza kuwa katika mazingira ya aina hiyo. Jela za binadamu ndiyo ziko hivyo kwa sababu wana visasi, siyo kwa Mungu!
******************************************
Makala hii iliandikwa na hayati Munga Tehenan katika Gazeti la Jitambue, miezi michache kabla ya mauti kumfika na roho yake kuachana na mwili. Elimu ya maarifa haya ya Utambuzi aliyotupatia ndio chachu ya kuwepo kwa blog hii ya Utambuzi na Kujitambua. Kwa hiyo kile wasomaji wa blog hii wanachojifunza humu ni matunda ya hayati Munga Tehenan.

6 comments:
Andika Maoni Maoni
  1. Asante kwa somo hili la kifo. Lakini tutajuaje kama alitabiri kifo chake sawa kabisa nina maana anaweza ametabiri na akachukua sumu na kufa ili iwe utabiri wa kweli. Nawaza tu

    ReplyDelete
  2. Binadamu tupo duniani kwa ajili ya kuishi na si kufanya uchunguzi,kwanini tunaishi.Ukianza kufanya uchunguzi kwanini unaishi,utaanza kutaka kujua mengi kv,ni nani aliyenifanya niishi,kwanini alinifanya niishi,yeye anafanya nini sasa hivi,huyu yawezekana ana nguvu za ajabu.Baada ya kushindwa kupata jibu,wanajamii kupitia watu wengine mnajiwekea utaratibu wenu,mnaweza mkauita dini.Misingi ya kufundisha watoto juu ya kitu mnachokiamini ninyi ambacho kwa ujumla hakipo ni hisia tu, inajengwa.Amri zinatangazwa sambamba na elimu ya maisha baada ya kifo.
    Ndipo taarifa au imani kuwa kuna moto wa milele zinajengwa vichwani mwetu,tunaanza kuogopa kufa kwa kuwa tumeaminishwa kuwa baada ya kifo kuna mateso ya milele.
    Katika imani hizohizo zilizojengwa na wanadamu kuna wengine wapo tayari kujiua na kuwaua wenzao kwa kuwa wanaamini watakwenda peponi.
    Nionavyo mimi sababu kubwa inayotufanya tuogope kifo ni imani tulizolishwa kuhusu maisha baada ya kifo,Vilevile watu wengi tunashindwa kujitambua sisi ni akina nani na badala yake tumeweka nguvu kubwa ktk kujichunguza badala ya kujitambua.
    Inatakiwa tujue kuwa hapa duniani tupo kwa ajili ya kuishi sio kudumu.Mtu anayeishi ni yule anayejipenda,kuwapenda wengine na anakuwa na furaha muda wote na kamwe haogopi kifo.Anayedumu ni yule anayetumikishwa na mwili wake,ana wasiwasi kuhusu uhai wake kila wakati na anaogopa sana kifo.

    ReplyDelete
  3. Niliwahi kusema kuwa kuna watu nawapenda saaana. Nawapenda kiasi kwamba najua wakifa sitalia. Sitalia kwa kuwa wametenda meengi ambayo wameweza na wamekuwa chachu ya maendeleo kwa jamii. Kwa ufupi ni kwamba wametimiza kazi yao.
    Nakumbuka wakati wa kuandaa tamasha la kumuenzi Justine Kalikawe nikiwa na Tanzania Reggae Family, nilimpa pole mmoja wa wanafamilia hao nilipokutana naye kwa mara ya kwanza na pembeni yake alikuwepo Gotha Irie aliyeniambia kuwa hapa hatuko kusikitika, bali tunasherehekea mazuri aliyotenda Justine.
    Iliniingia akilini kutambua kuwa kuna mengi ya kushukuru na kufurahia kuhusu wanaotutoka na si kulia na kulalama kwanini wameondoka.
    Na sisi pia twatakiwa kuwa na imani na maisha tuishiyo. Kuishi maisha yetu sasa na si kuwekeza katika tusiyoyajua. Ninalomaanisha ni kuwa kutenda kila lililo sahihi sasa badala ya kusema ukishapata pesa ndio utafanya hivyo.
    Matokeo ndio hayo sasa kwamba ikitokea kuna tetesi ama dalili za kifo kabla ya kupata pesa unaanza kuogopa.
    Asante K kwa kumbukumbu ya somo hili
    Blessings

    ReplyDelete
  4. Kaka Katawa,

    Popote ulipo naoma tuwasiliane kwa email.
    Unaweza kuwasiliana na mimi kwa email hii: kaluse2008@gmail.com

    ReplyDelete
  5. Bado namkumbuka Munga Tehenan. Riwaya yake ya Rais wa Kesho ni mojawapo ya kazi bora kabisa katika fasihi ya Kiswahili. Alikuwa na kipaji cha hali ya juu. Sikujua kwamba alikuwa amefariki mpaka hivi karibuni. Kifo....

    ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi