0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Feb 16, 2009

KWA MGONJWA HAPANA, ILA KWA MAITI!

Je mmeniona?

Kila mmoja wetu ameshawahi kwenda kwenye misiba na baadhi yetu tumeshahudhuria vikao vya harusi. Bila shaka tumeshashuhudia pia mambo ambayo huwa yanatuacha na maswali kwenye misiba au vikao hivyo. Miongoni mwa vile ambavyo tumevishuhudia inaweza kuwa ni watu wanaojionyesha.

Hivi inakuwaje mtu anatoa fedha kwa ajili ya msiba katika njia ambayo inaonyesha anataka kila mtu amuone? Kuna njia nyingi zenye kuonyesha kwamba mtu anatoa ili watu wamuone na sio kwa sababu ya kusaidia shughuli za msiba.

Kwenye vikao vya harusi ni hivyo hivyo, mtu hutoa ahadi kwamba atatoa kiasi fulani cha fedha, kiasi kikubwa sana. Lakini hata hivyo baada ya kikao huzungusha kutoa kile alichoahidi. Anaweza akatoa kile alichoahidi, lakini huwa ni kwa njia ambayo ni yenye kuomba watu watambue kwamba ana uwezo.

Watu hawa utakubaliana na mimi kwamba kama watafuatwa na wahusika yaani waliofiwa au wenye harusi wakiwa peke yao na kuombwa fedha, ama watakataa au watatoa fedha kidogo sana kuliko zile ambazo wangezitoa hadharani.

Inawezekana mtu akafuatwa na mtu mwenye kuuguliwa akaombwa shilingi 10,000 akasema hana, lakini mgonjwa huyo anapokufa saa chache baadae mtu huyo akatoa shilingi 50,000.

Hivi unadhani hii inatokana na nini?

Kuna maelezo mengi kuhusiana na tabia hizi, lakini kubwa zinaweza kuwa zinatokana na nadharia za ngazi ya mahitaji ya binadamu.

Kwa nadharia ya mahitaji ya mwanadamu ni kwamba, binadamu anapofikia mahali ambapo amepata mahitaji yake ya msingi huhama na kuanza kutafuta mahitaji mengine, ikiwemo kutambuliwa. Kutambuliwa hutafutwa kwa namna mbalimbali mtu anaweza kufadhili timu ya mpira ili atangazwe na vyombo vya habari au kufanya jambo ambalo litamfanya aonekane kwamba amevuka hatua ya chini, ya kutafuta kula kulala na kuvaa.

Utakubaliana nasi kwamba watu wote wenye tabia hii ya kutaka kujionyesha kwenye misiba au harusi ni wale ambao chakula kuvaa na kulala haviwasumbui. Kwa kuwa wamekidhi mahitaji hayo ya msingi husumbuliwa na maumbile ya binadamu ya kutafuta hitaji lingine.kwa hiyo watu hawa siyo kwamba wanafanya hivyo kwa kuwadharau wengine hapana. Hufanya hivyo ikiwa ni juhudi yao kutaka watu wengine wawapende au kuwatambua.

Ndiyo maana muoaji au mfiwa akienda kwake wakiwa wawili kunakuwa ni vigumu kumsaidia kwa kiwango kikubwa kama ambavyo angefanya hadharani. Hii ni kwa sababu wakiwa wawili kutambuliwa au kupendwa kwake kutakuwa hakuna kishindo wengine hawatamtambua hawatampenda wakati yeye anataka auwe ndege wengi kwa jiwe moja. Vivyo hivyo kwa kuangalia sababu zinazowafanya watu kusaidia utagundua kwamba kuna watu ambao husaidia ili kuziba udhaifu wao. Wachunguze sana watu wa aina hii utagundua kwamba wana udhaifu mwingi kwenye nyanja nyingine hasa za kisaikolojia. Unaweza kukuta ni watu wasiyo jiamini ni watu wakorofi ni watu wenye sifa ya umalaya au nyingine mbaya kwa mujibu wa maadili ya jamii na ni watu ambao tafakari yao ni ndogo.

Hivyo hutoa fedha kwa kujionyesha wakidhani hilo litaweza kuziba udhaifu wao. Hebu jaribu kuchunguza watu ambao wameanza kushika fedha juzijuzi kama watu hawa sio waangalifu ni
lazima watakuwa na vituko vya namna hii. Hii yote ni kutokana na kushindwa kwao kujiamini wanataka kuwaonyesha wengine kwamba wao siyo wale wa zamani. Lakini ukiwauliza wenyewe watakana sana kwa sababu kila kitu hufanyika nje ya urazini wao, yaani kwenye mawazo yao ya kina.

Kwa hiyo unapokutana na watu wa aina hii usiwashangae kwani wanahangaika katika kupanda ngazi ya mahitaji ya binadamu au wanajitahidi kuficha au kuziba udhaifu wao. Badala yake inabidi ujiulize nawe kuwa huwa hufanyi vituko kama hivyo mahali pengine. Je ukipokea mshahara au kuuza mazao yako na ukipata fedha, huwa huwafanyii hivyo wenzako kwenye maeneo mbalimbali ya kadamnasi

1 comment:
Andika Maoni Maoni
  1. haswaaaaa walimwengu tunashangaza kila kukicha ni mambo ya ajabu kama hayo

    ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi