0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Feb 21, 2009

MAZUNGUMZO YANGU NA MALISA

Mfumo wetu wa elimu bado hauwasaidii kujitambua

Hivi karibuni nilitembelewa na msomaji wa blog yetu hii ya utambuzi na kujitambua pale katika kituo chetu cha FAJI Kimara kona. Malisa alikuwa ni msomaji wa gazeti la jitambue ambalo siku hizi halichapishwi tena kutokana na sababu za kiufundi. Kutokana na gazeti hilo kutokuwepo mitaani kwa kipindi cha muda mrefu, Malisa akajikuta akiwa ni mmoja wapo wa wasomaji wa blog hii baada ya kukutana nayo kama bahati mtaandaoni.

Mazungumzo yangu na Malisa yaligusia mambo mengi sana kuhusiana na yale ninayoyaandika humu na yale niliyokuwa nikiyaandika katika gazeti la Jitambue wakati ule. Ukiongea na Malisa, kwa mtu mwenya maarifa haya ya utambuzi ataamini kabisa kuwa ni mwanautambuzi mzuri ingawa hajawahi hata mara moja kuhudhuria darasa hata moja na kujifunza maarifa haya ya utambuzi.
Hakusita kukiri kwamba hajawahi kukutana na Hayati Munga Tehenan ambaye ndiye mwalimu wetu aliyetumia muda wake mwingi kutufundisha maarifa ya utambuzi, ambapo sasa tunayasambaza kwa watu wengine kwa njia mbalimbali.

Malisa ni mmoja wa wasomaji wa Gazeti la Jitambue aliyeamua kutenda yale yaliyokuwa yakiandikwa katika gazeti hilo na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kubadili mfumo wake wa maisha na kuacha kuishi kimazoea. Miongoni mwa mambo tuliyozungumaza, mojawapo ni kuhusu mfumo wetu wa elimu hapa nchini. Malisa anabainisha kwamba elimu yetu hapa nchini ina kasoro kubwa, jambo ambalo liliwahi kuzungumzwa na mwanablog mwenzagu Koero Mkundi katika kijiwe chake cha VUKANI, pale alipoweka makala yake iliyohoji kuwa Msomi hasa ni nani?

Malisa anabainisha kwamba mfumo wetu wa elimu umefinyangwa kwa kuchanganywa na elimu iliyokuwa ikitolewa na wajerumani ambayo ilikuwa ikituandaa kuwa makarani wao. Mfumo wa elimu iliyokuwa ikitolewa na Wajerumani haukuwa na lengo la kuzalisha wasomi ambao wangeweza kujitegemea kwa kufikiri, ambapo kwa kupitia elimu wangeweza kujua wao ni nani na malengo yao ya kuwepo hapa duniani ni yapi.

Malisa aliendelea kusema kwamba Elimu iliyotolewa na wajerumani wakati ule wakitutawala ilikuwa kuwawezesha kupata makarani ambao wangesimamia kodi unyapara kwenye mashamba ya Pamba na Mkonge, walimu wa kutia wengine ujinga huo ili kuwatenga na wanajamii walio wengi ambao hawakuwa wamesoma. Hakuna aliyepata elimu ya kumwezesha kusimama na kujijua ili kujisaidia na kuwasaidia wengine kujikomboa kifikra na baadae kwenye nyanja nyingine kimaisha.

Malisa alibainisha kwamba Wajerumani walikuwa ni wajanja kwani kama wangeanzisha mfumo wa elimu wa kutukomboa kifikra ingekuwa ni kutupa njia ya kuwaondoa wao kirahisi kwenye utawala. Mtu anayekutawala kutokana na ujinga wako, atakuwa ni mjinga zaidi yako kama atakuruhusu kujua kama anakutawala. Wajerumani hawakuwa wajinga kiasi hicho.

Kwa hiyo mfumo huo wa elimu wa wajerumani haukuishia hapo, uliendelea, kwani baada ya uhuru wa nchi hii uhaba wa wasomi wazalendo ulilazimisha vijana wengi kusomeshwa kwa lengo la kuchukuwa nafasi za wazungu katika utawala , kama vile wakuu wa wilaya , wakuu wa mikoa, mameneja, makarani na wanyapara.

Mfumo ule haukubadilishwa kabisa, ili kupata mfumo bora utakaotuwezesha kujijuwa na kufikia malengo yetu. Leo hii hali ni mbaya, mfumo wetu umevurugwa kiasi kwamba unatia aibu. Pamoja na kubadilishwa mara kadhaa, hakuna jipya lililoongezwa zaidi ya kuboresha yale yale aliyoyaacha Mjerumani. Mpaka leo hii wote tumepitia na wengine wanaendelea kupitia barabara ile ile aliyoitengeneza Mjerumani katika mfumo wa elimu.

Tulisoma na tunasoma ili kuajiriwa, na ndio maana si ajabu kukuta mwanafunzi kwa mfano aliyemaliza chuo kikuu na kupata shahada ya kilimo anatafuta kazi ya kuajiriwa, tena unaweza kukuta anatafuta kazi ambayo sio taaluma yake kwa sababu ya taaluma yake labda haina maslahi, kwa maana ya mshahara na marupurupu hautoshelezi. Mtu kama huyo ukimuuliza, kwa nini asijiajiri kwa taaluma yake ya kilimo, kwani tunayo ardhi yenye rutuba hapa nchini huku tukiwa na mito na maziwa, ambapo anaweza kuanzisha kilimo cha umwagiliani, mtu huyo anaweza kutafsiri ushauri wako kama matusi kwake, kwani amesoma, lakini elimu aliyosomea haijamsaidia kujua ni kwa nini aliisomea.
Malisa alimalizia kwa kushauri kwamba, inabidi wanafunzi walioko mashuleni na vyuoni waanze kujiuliza wanasoma kwa ajili gani, na kwa manufaa ya nani?
Bila kujiuliza wanaweza kujikuta wakielemewa na elimu waliyoipata badala ya kuwapa nafuu.

No comments:
Andika Maoni Maoni

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi