0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Mar 10, 2009

KWA NINI TUFIKIRI KUHUSU TATIZO BADALA YA SULUHU?

Hata kama hatupati wateja hakuna haja ya kunung'unika

Ni wangapi kati yetu ambao hatujawahi kupatwa na tatizo au matatizo maishani mwetu? Bila shaka hakuna na kama yupo au wapo ni wazi huyo au watu hao watakuwa ni watu wa historia. Watakuwa ni watu wa historia kwa sababu matatizo ni sehemu ya maisha na kwa hiyo kuwepo kwake ndipo maisha hukamilika.

Maisha haya yangekuwepo bila matatizo ni wazi yangekinaisha haraka sana. Yangekinaisha kwa sababu yasingekuwa na maana yeyote. Maana na utamu wa maisha upo katika kupambana na mazingira na kupata ufumbuzi wa jambo. Kitendo cha kupata ufumbuzi wa jambo na kusonga mbele ni kitendo chenye kushika maana halisi ya maisha. Kitendo cha kupambana na kushindwa pia ndo maisha yenyewe. Kama ingekuwa kila anachotaka mtu anakipata maisha yangepoteza maana yake.

Ina maana kwamba kila mmoja kati yetu ni mtaalamu wa matatizo kwa maana kwamba anafahamu kwa vitendo. Lakini kwa bahati mbaya siyo wote kati yetu ambao tunaweza au kujua namna ya kuyatatua matatizo yetu, lakini mbaya zaidi namna ya kufanya matatizo yasituharibie maisha yetu. Kwa kuwa matatizo ni sehemu muhimu katika maisha yetu ni wazi hatuwezi kuyakwepa. Kwa kuwa hatuwezi kuyakwepa inabidi tujue namna ya kuyakubali bila kutuumiza, ujuzi ambao wengi wetu hatunao.

Tunapopatwa na tatizo au matatizo huwa hatujui kwamba dawa ni kutafuta ufumbuzi wa tatizo au matatizo hayo. Katika kutokujua huko huwa tunajikuta tukichimba na kuchimba hadi ndani kabisa ya tatizo bila kufika mwisho. Tunatumia muda wetu mwingi mwingi kufikiria kuhusu tatizo au matatizo hayo kiasi kwamba inatuwia vigumu sana kwetu kuona kitu kingine ambacho ndicho muhimu zaidi kuliko tatizo au matatizo yanayotukabili.

Kwa kawaida tunapokabiliwa na tatizo kitu ambacho kinatakiwa kuzijaza fikra zetu siyo tatizo hilo bali njia za kupata suluhu ya tatizo. Lakini kwa bahati mbaya kama tunavyobainisha kinachozijaza fikra zetu huwa ni tatizo lenyewe. Kwa hali hiyo tatizo hilo hukuzwa na fikra hizo hadi kufikia mahali ambapo tutaliona tatizo hilo kama dubwana ambalo tayari limeyameza maisha yetu.
Fikira zetu hutuambia kwamba ni lazima tutashindwa na hutuambia na kutushawishi kuamini kwamba ni sisi peke yetu tu ndiyo ambao hupatwa na matatizo. Ili kuepuka uongo huu ambao huletwa kwetu na fikra zetu hatuna budi badala ya kuzijaza fikra hizo na tatizo lenyewe tuzijaze kwa njia ya kufikiri suluhu au ikiwezekana kwa suluhu yenyewe. Kwa kuzijaza fikra hizo kwa njia ya kufikiri suluhu ya tatizo tunajipa moyo kwamba inawezekana na tunajitoa kwenye hofu ambazo zinaweza kutufanya tukashindwa kukabiliana na tatizo ili tuendelee na maisha.

Wengi wetu tuwataalamu wa kuzichosha fikra zetu kwa kuwaza juu ya tatizo tulionalo mkononi badala ya kuzijaza fikra hizo kwa njia ya kufikia suluhu ya tatizo njia za kutuwezesha kulimaliza tatizo hilo. Kama ni hivyo ni kwa nini tusiamue kubadilika sasa hivi.

Kwa mfano kama tuna tatizo la kushindwa kuwapeleka watoto shule kutokana na kukosa fedha za ada hatutakiwi kufikiri kuhusu tatizo hilo yaani kuwaza kuhusu itakavyotokea namna watu watakavyotuona jinsi watoto watakavyokuwa bila elimu na mengine ya namna hiyo. Badala yake tunatakiwa kuwaza namna ambavyo tutajitahidi kuhakikisha kwamba watoto wanakwenda shule. Haya ndiyo maisha ambayo katika mchanganyiko wake ni lazima kuwe na matatizo..

7 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Nimeshawahi kusoma ujumbe fulani,uliandikwa hivi"Usihesabu madhaifu uliyonayo bali hesabu baraka ulizonazo"
  Pengine waweza kusema huna baraka,lakini kama umesoma ujumbe huu tayari una baraka kuna wengine hawawezi wakasoma kwa kuwa hawana uwezo wa kuona!

  ReplyDelete
 2. samahani fungua kurasa ya kuchangia mawazo kuhusu jumuiya ya wanablogu tanzania.

  http://blogutanzania.blogspot.com/

  www.ringojr.wordpress.com

  ReplyDelete
 3. Kaluse, ni kweli matatizo ni lazima ktk maisha kwa sababu kuna wakati utakuta kila kitu unachofanya ni tatizo, hata kupumua ni tatizo yaani kinakuja kipindi hata yule umpendaye ni tatizo. Kwa hiyo ni kweli bila matatizo huwezi kuishi.

  ReplyDelete
 4. Kaka Katawa,

  Popote ulipo naomba tuwasiliane kwa email.
  Unaweza kuwasiliana na mimi kwa email hii: kaluse2008@gmail.com

  ReplyDelete
 5. Hapa nimejifunza kitu.
  Kumbe haina haja ya kuyakimbia matatizo.

  ReplyDelete
 6. "You can't run away from yourself".
  "Binadamu aliyekamilika ni yule ambaye hajakamilika"
  Hizi ni kati ya nukuu kadhaa ambazo natamani kila mtu angezitambua. Tatizo hapa (na nimesoma hii baada ya kuandaa makala yangu) ni kuwa tunataka saana kuwa tunavyotaka tuwe ilhali hali halisi ya maisha inatutaka tuwe tunavyotakiwa tuwe. Ni mkanganyiko wa tunavyotaka kuwa na tunavyotakiwa tuwe unaotufanya tujipoteze kwa kung'ang'ania upande usiostahili.
  Ukweli ni kwamba matatizo yapo popote. Japo yanaweza kuwa matatizo kwa kuwa tu hatujui mwisho wake unanufaisha vipi jamii. Ukiweza kutambua hili, utaona kuwa hata hayo uyaitayo matatizo ni mfumo wa kawaida wa kumaliza jambo moja kuelekea lingine.

  MFANO:Ni mfumko wa bei unaoleta sera bora za kudhibiti, ni kifo cha fulani kinachotupa nafasi ya kumfikiria mwingine ambaye anaweza kuwa na changamoto mpya na za kisasa na sahihi zaidi ziendanazo na mahitaji. Ni makosa ya fulani yanayoboresha sekta nzima.
  Umeshajiuliza ni wangapi walikufa katika kupigania uhuru unao-enjoy sasa? Kwao yale yalikuwa matatizo lakini lengo lilikuwa kuwa na dunia tuliyonayo sasa kwa namna ilivyo.
  Umeshajiuliza ni wangapi walikufa kwa matatizo yaliyokuwepo kwenye ndege za mwanzo? Ni uboreshaji uliotokea wakati ule ambao unatufanya tusafiri kwa haraka na (pengine) salama kuliko wao. Lile lilikuwa ni tatozi kwao japo ni faraja kwetu.
  Unajua ni wangapi wamekufa wakihangaika kuufanya umeme uwe salama na kompyuta zifanye kazi nzuri mpaka ukaweza kusoma "mtazamo" wangu juu ya hili? Ndugu zao waliliona hili kama tatizo japo lengo lilikuwa ni mawasiliano tuliyonayo sasa.
  Na wote hawa na wengine wengi kama wangezamisha akili zao kwenye matatizo na kutojali kutafuta sulhisho pengine tusingekuwepo, ama tungekuwa watumwa, ama tusingeweza kusafiri tusafirivyo ama kuujua ulimwengu na malimwengu kwa urahisi kama ilivyo sasa.
  Ni kweli kuwa kuna yale yaitwayo matatizo (ambayo kwa hakika ndio mafanikio ya wengine). Ninyamaze kwa swali kuwa KAMA NAFASI ULIYOPO SASA KIMAISHA (KUANZIA NYUMBANI MPAKA HAPA UNAPOSOMEA HII) SI YA KWANZA DUNIANI, INGEKUWAJE KAMA LISINGETOKEA LILILOTOKEA KUMTOA ALIYEKUTANGULIA?
  Bushman aliimba kuwa "in order for one to survive, sometimes you gotta take anonter man's life"
  TAFAKARI
  Asante Kaka K na wachangiaji wote

  ReplyDelete
 7. Mzee wa changamoto.

  Hakika maoni yako yamenifikirisha.

  Dada Yasinta na Bwana Katawa:

  Nadhani hii ni changamoto yetu wote.

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi