0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Dec 15, 2008

JE BIBLIA ILIUFAGILIA UBEPARI? MAJIBU KWA KAMALA


NADHARIA YA MWENYE NACHO KUONGEZEWA

Hivi karibuni mwanautambuzi mwenzangu Kamala katutolea fungu moja katika biblia akidai kwamba Biblia inaufagilia ubepari.

Ingawa fungu lenyewe alilinukuu kwa kiingereza, nimeona nilitafsiri kwa Kiswahili ili niweze kumjibu vizuri.
Fungu lenyewe ni kutoka katika kitabu cha Marko mtakatifu, 4 fungu la 24 mpaka 25.
Nitanukuu fungu hilo:

‘akawaambia angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa.
Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu hata kile alicho nacho atanyang’anywa’
Mwisho wa kunukuu.

Je fungu hili linamaanisha kile alichosema Kamala, Kwamba Biblia Iliupendelea ubepari?

Kwa mujibu wa Mwanasaikolojia mmoja aitwae Dr. Sigmund Freud katika mojawapo ya tafiti zake aliwahi kusema kuwa watu wamegawanyika katika makundi mawili,
Kundi la kwanza ni lile la watu walioshindwa katika maisha na kundi la pili ni lile la watu walifanikiwa.
Dr Sigmund Freud anazidi kubainisha kwamba tofauti iliyopo katika makundi hayo mawili ni namna kila kundi linavyofikiri.

Kundi la wale walioshindwa katika maisha linakuwa ni la watu wanofikiri juu ya kushindwa, ni kundi la watu wasioamini katika kufanikiwa,.
Watu wanoangukia katika kundi hili kufanikiwa kwao ni jambo lisiliwezekana kutokana na namna wanavyofikiri.
Kundi hili ndio lile la asiyekuwa nacho kupokonywa hata kile kidogo alichonacho kama lilivyozungumziwa katika biblia na bwana Yesu.
Kwa nini hata kile kidogo alichokuwa nacho anyang’anywe?
Kwa kawaida kama unafikiri na kuamini katika kushindwa, sio tu kwamba kufanikiwa kwako itakuwa ni msamiati mgumu, bali pia kutofanikiwa huko kutakugharimu, kwa sababu, utakuwa kila unachojaribu kufanya ambacho umetumia gharama katika kukianzisha hakifanikiwa na hivyo ile gharama uliyotumia kupotea.
Ndio kunyang’anywa kwenyewe hata kile kidogo ulichonacho.

Kundi la watu waliofanikiwa ni lile la watu ambao mawazo yao yote yapo katika kufanikiwa, kundi hili ni la watu makini ambao kwao anguko moja ni kama ngazi ya kuelekea katika kufanikiwa.
Kundi hili ni la watu wenye moyo wa kuthubutu, halijali kuhatarisha mitaji yao, kwa kuhofia kupata hasara.
Watu wanaoangukia katika kundi hili hawachoki kujaribu hata wanapopata maanguko kadhaa hujipa moyo na kusonga mbele, hawana muda wa kukaa na kunung’unika, kwa kuwaza kuhusu maanguko yaliyopita, kwao huo ni mzoga ulishakufa na kuoza.
Watu wa namna hii pia wanayo sifa ya kuwa na subira, na hii ndio nguzo muhimu sana wanayoitumia, ndio sababu wanafanikiwa.
Kundi hili ndilo lile la walionacho kuongezewa, kama ilivyoandikwa katika biblia.

Kama unafikiri katika kufanikiwa utafanikikiwa na kuwa tajiri kwa jinsi unavyotaka na kama unafikiri katika maanguko, basi wewe utavuna umasikini wa kutosha, na usimlaumu mtu.
Yesu hakuwa mnafiki, alikuwa muwazi, alijitahidi sana kuwafundisha wafuasi wake namna ya kufanikiwa, lakini tafsiri iliyokwenda vichwani mwao ilikuwa ni tofauti.

Ndio sababu watu wengi walipotoshwa na mojawapo ya mafundisho ya Yesu aliposema kwamba tajiri kuuona ufalme wa mbinguni ni sawa na ngamia kupenya katika tundu la sindano.
Fungu hili lilipotoshwa na wahubiri wengi kiasi cha kuwafanya waumini wao kuuogopa utajiri.

Naomba kuwasilisha.

7 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Kazi nzuri Kaluse. Ninarudi baadae naona muda umeniishia kwa sasa naomba kutafakari majibu yako

  ReplyDelete
 2. Mmh...! Hivi kumbe, kumbe ndivyo inavyokuwa (ga?)
  yap, nakumbuka niliwahi soma pahala kuwa wakoloni walikuwa wakipenda kutumia mistari kama hiyo. Wakapenda kusema pia, "tiini mamlaka, mamlaka zote zatoka kwa Mungu"
  Kwa bahati mbaya, mimi si mtaalamu wa Biblia, nashindwa kufahamu kwanini wamishenari kama vitangulizi vya ukoloni walipenda zaidi hayo.
  Wakati mwingine huwa napata taabu kufahamu kwanini kina Lenin na wakomunisti wa China hawakuipenda dini.
  Mimi (kwa mtazamo wangu) sioni kama Biblia iliufagilia ubepari. Nadhani ni falsafa tu kama alivyoichambua kaka hapo juu, ndiyo inayotugharimu.
  Lakini siku zote huwa naamini kuwa sisi Waafrika, hususani Watz, Mungu hakutuumba tuwe masikini. Vinginevyo asingetupa mito itiririshayo maji nyakati zote, milima iliyofunika madini ya kila aina, mbuga zilizohifadhi hadi viumbe adimu duniani, na mengine lukuki.
  Ila wajanja wachache ndo wanaleta dosari. Samahani nimekosea, hawana sifa ya kuitwa wajanja. Mafisadi.
  Natamani kuandika mengi lakini nashindwa.
  Naandika tu kuwa Biblia haiufagilii ubepari, isipokuwa sisi ndo tunaoukuza unyonyaji na ufisadi na kila uchafu.
  Eeh Mwenyezi Mungu utunusuru waja wako.
  Amina.

  ReplyDelete
 3. Tukumbuke lakini mtu aliyenacho si lazima iwe ANACHO katika mfumo wa mali.

  ReplyDelete
 4. Ahsante, Mtanga, Bwaya na Bwana Kitururu, kwa maoni yenu.
  Nimefurahi sana kuwa wote mliielewa mada hii kwa ufasaha.
  Ningependa kukubaliana na bwana Kitururu kwamba, kuwa nacho si lazima kiwe katika mfumo wa mali, hiyo ni kweli. lakini kwani mali ni nini?
  Mali ni Fedha au ni rasilimali?
  Kama inavyofahamika kuwa Bwana yesu alifundisha kwa kutumia njia kuu tatu, yaani Methali, Mafumbo, na kujifananisha.
  Ndio dababu wakati mwingine hata wanafunzi wake walikuwa na wakati mgumu sana kumuelewa.
  Nilichokuwa najaribu kubainisha ni ile tafsiri potofu iliyowekwa vichwani mwetu, ambayo ilitufanya tuwe tunafikiri kama wao walivyotaka.

  Bwana Mtanga kumbuka kwamba hawa ndio waliotuletea haya mafundisho ya Yesu na ndio hao hao waliotutawala kwa miongo mingi barani Afrika.

  Hivi kweli walitaka tuufahamu ukweli au walitaka kututawala kwa njia ya maandiko matakatifu?

  Bado tuna maswali mengi ya kujiuliza ambayo majibu yake ni kitendawili.
  nawashukuruni sana tena sana kwa kuchangia mada hii.
  Ahsanteni sana

  ReplyDelete
 5. Kaluse, mjadala usifungwe mapema hivi. Mijadala kama hii si kama ile ya kujadili watu maarufu kwenye baadhi ya blogu ambayo haihitaji muda kuelewa picha ni ya nani. Mijadala hii, kwa hakika ya mawazo, inahitaji tafakuri za kina. Nashauri mjadala usifungwe tafadhali hata kama itachukua miezi kuuhitimisha. Maoni ya msomaji wako.

  ReplyDelete
 6. Bwaya bado sijafunga mjadala, wasomaji wengine wanaweza kuchangia.
  karibuni sana.

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi