0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Dec 17, 2008

JINSI KUFIKIRI VIBAYA KUNAVYOATHIRI MIILI YETU

Leo nina kisa nataka kuwasimulia.

Bwana mmoja alikuwa amekwenda kazini kama ilivyo kawaida yake, akiwa ndio anafika kazini akapigiwa simu kujulishwa kwamba nyumba yake inaungua.
Bwana yule akarudi nyumabni haraka huku akijaribu kuwasiliana na watu wa zima moto. Alipofika nyumbani akaikuta nyumba yake ndio inazidi kuteketea kwa moto na hakuna kilichosalimishwa hata kitu kimoja na askari wa zima moto walikuwa hawajafika katika eneo la tukio.

Basi yule bwana akawa amesimama akishuhudia nyumba yake ikiteketea asijue la kufanya. Ulikuwa ni msiba mkubwa sana kwake, kwani ile nyumba ilikuwa ni kubwa na ilimgharimu kiasi kikubwa cha fedha.

Wakati akiwa bado amesimama pale nje akiwa anashuhudia lile tukio, mwanae mmoja wa kiume alimsogelea na kumshika bega, kisha akamwambia ‘usijali nilishaiuza tangu jana!, nilikusikia wewe na mama mkilalamika kuwa hii nyumba ni kubwa sana na mlikuwa hamuihitaji tena, nikakutana na tajiri mmoja mwekezaji toka nje ambaye alikubali kuinunua kwa gharama yoyote’

Ghafla sura ya baba yake ikagubikwa na tabasamu la furaha na kumkumbatia mwanae na kumpongeza kwa kwa uamuzi mzuri alioufanya.
Mpaka hapo hakuna kilichobadilika: Nyumba ilikuwa bado inaungua lakini hakuwa mmiliki wa nyumba ile tena, kwa nini ajali, wakati haimuhusu?

Wakati baba akiendelea kumpongeza mwanae huyo, mwanae mwingine mdogo wa kiume aliwasogelea uso wake ukiwa umegubikwa na huzuni, Baba alimwangalia mwanae kwa mshtuko, ‘nini tena?’
“Ni kweli mwekezaji mmoja alikuwa anataka kuinunua hii nyumba’ yule kijana alisema, akimwambia baba yake. Lakini mkataba wa mauzo ulikuwa bado kusainiwa na pande mbili, kwa hiyo hatuna cha kuuza.”

Yule baba aliishiwa na nguvu kabisa, na kukaa chini, mwili wote ulikufa ganzi na hakuwa na la kusema, akabaki kuwaangalia wale wanaye asiamini masikio yake.
Bado hakuna kilichobadilika: Nyumba bado ilikuwa inaungua. Kilichobadilika ni taarifa tu.
Wakati nyumba yake inaungua aligubikwa na huzuni. Alipopata taarifa kuwa nyumba ilishauzwa kwa mtu mwingine, ingawa bado ilikuwa inaungua alifurahi sana kwa sababu haikuwa yake tena.


Zilipokuja taarifa nyingine toka kwa mwanae mdogo kuwa mkataba wa mauzo ulikuwa bado haujasainiwa, baba akataharuki na kurudi kwenye majonzi tena kwa sababu kumbe nyumba bado iko mikononi mwake.
Akiwa bado amegubikwa na simanzi, aliyekuwa mnunuzi wa ile nyumba alifika, ‘najua hii ni bahati mbaya sana kwako, kwa nyumba yako kuungua, hata hivyo nilikuwa nahitaji hii ardhi tu, kwa hiyo nitalipa kiasi kile kile cha fedha tulichopatana’

Kusikia hivyo, uso wa yule baba, ukabadilika tena na kugubikwa na furaha kubwa isiyo kifani, kwani nyumba haikuwa mikononi mwake tena, hakuna haja kusikitika.
Naamini mpaka hapo mmeona mwili unavyopata mabadiliko kulingana na jinsi tunavyotafsiri matukio tunatoyapata.

Ikiwa tutatafsiri tukio vibaya kwa kuanagalia upande mmoja wa hasi, ni wazi tutapata maumivu ya kihisia.
Kwa mfano wa tukio hili la nyumba kuungua, awali yule mzee alikuwa analalamika kuwa ile nyumba haihitaji tena, kwa kuwa ni kubwa na labda ilikuwa ina muundo wa kizamani, kwa hiyo hakuipenda. Alikuwa anatamani kujenga nyumba mpya ambayo ndiyo aliyokuwa akiihitaji.

Niliwahi kuandika kuhusu jinsi mawazo yalivyo na nguvu, kwamba kile tunachofikiri ndicho kinachofanyiwa kazi na akili ya kina (Conscious mind), kwa hiyo, tukio lile ilikuwa ni matokeo ya kile alichokuwa anafikiri.
Lakini kwa bahati mbaya matokeo ya fikra zetu hayaji kwa namna tunavyotaka, yanakuja kwa njia ya ajabu mno ambayo mwenye werevu wa kihisia pekee ndiye atakayeweza kung’amua.
Akili ya kina huwa haileti majibu yakiwa yamevaa suti, mara nyingi yanakuwa na sura isiyovutia na yenye kutia kinyaa, usipoigundua, umekwisha.

Maswali ya kujiuliza:

Hivi kama yule mzee angekuwa na ugonjwa wa moyo, hudhani kama angekufa kutokana na mshtuko wa kuunguliwa na nyumba?

Je ni mara ngapi tunapiga teke yale mambo yanayofanyiwa kazi na akili ya kina na kuja mbele
yetu yakiwa na sura kama hii?

Je hofu na maumivu ya kihisia tunayopata ni kutokana na tukio au tafsiri inayokwenda akilini kwetu?

Je umejifunza nini juu ya kisa hiki?

7 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. This comment has been removed by the author.

  ReplyDelete
 2. Tafsiri tu za NINI ni viatu vizuri ndio zifanyazo baadhi wavae RAIZONI ziumizazo miguu kwa kisa cha kupendeza.

  Naogopa utumwa wa tafsiri uwezeshao NYUMA kutambuliwa kama MBELE.

  ReplyDelete
 3. Binadamu tumeachana kuna wengine wanapopata habari kama hiyo ni kweli kabisa hupata homa kali sana na kuna wengine wanakuwa tu wa kawaida ingawa kuna tatizo. Ni kweli huyu baba angekuwa na ugonjwa moyo kwa kweli nina hakika angekufa. Sijui kama nimeeleweka.

  ReplyDelete
 4. Ubongo hutafsiri taarifa kutokana na habari tunazoupelekea. Ni kama kompyuta unayoijaza taarifa ambazo ndizo utakuja baadae kuiomba kompyuta hiyo izichambue.

  Hitimisho la kipi kinachoonekana ndio kipi, unategemea na viambata zaidi na sio kicho chenyewe kinachoonekana. Lugha ngumu. Ngoja nijitahidi:

  Ili kuelewa unachokiona, kwa mfano, hicho unachokiona si cha muhimu kama viambata vyake. Kisa hiki kimetoa mfano mzuri sana kulielewa hili.

  Kwa hiyo utaona kuwa namna unavyoweza kuhusisha taarifa zinazoingia na viambata vyake, ndivyo unavyoathiri tafsiri.

  Ona hii. Nikandika l3 huwezi kuhitimisha ninaanisha nini kwa sababu hiyo inabaki kuwa alama tu isiyo na maana yoyote mpaka tujue viambata vyake (context). HIvyo nikiongeza A l3 C D hapo utajua alama hiyo ni B. Ila nikibadili viatambata nikasema 11 12 l3 14 unageuza hitimisho na kujua aaah kumbe inaweza kuwa namba.

  Tafsiri haitokani na tukio lenyewe (kwa mfano wangu, alama) bali ni mazingira ya tukio. Kumbe basi unaweza kubadili kila kitu kwa kuliongezea context nzuri unakabaki mwenye furaha!

  ReplyDelete
 5. Nimeandika kwa mwandiko wa mcharazo sana pengine msomaji atapata shida kuelewa baadhi ya maneno. Ila nadhani akitumia kanuni ya 'context' hatakosa kuelewa nilitaka kuandika nini.

  KUna mfano mwingine mzuri kufafanua hili. Zile picha za illusion (?) ambazo kila ukibadili mwelekeo kidogo tu, unaona picha tofauti na uliyoiona mwanzo. Ukibadili umbali wa kuitazama picha hiyo hiyo unagundua picha nyingine tofauti kabisa. Nipatapo fursa nitaambatanisha picha hizo kujaribu kuuunga mkono hoja hii murua sana uliyoianzisha bwana Kaluse.

  Nina hamu ya kuandika sana ila nahisi nitawakosea haki wasomaji wengine wenye maoni mazuri zaidi.

  ReplyDelete
 6. Ahsanteni sana, Kitururu, Yasinta Bwaya na Kamala,
  Maoni yenu nimeyapenda.
  Nisingependa kuhitimisha leo, ili niweze kuwapa wasomaji wengine nafasi ya kuchangia.

  Mada hii haijafungwa.

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi