0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Jul 31, 2010

NI MAPEPO AU KUSHUKA KWA HISIA?

Kuna wakati huhitaji kuwa peke yao

Wiki iliyopita niliweka hoja ya mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la mama K. mama huyo alitaka ushauri wa namna ya kuiokoa ndoa yake ambayo inaelekea shimoni.

Nisingependa kujadili kile tulichofikia na mama K baada ya kukutana kwetu, lakini ningependa kujadili swala hilo hapa kibarazani ili kujibu baadhi ya hoja za wale waliojitokeza kuweka maoni yao hapa kibarazani na wengine waliamua kuchangia mada hiyo kwa njia ya ujumbe wa simu ya kiganjani.

Naomba nikiri kwamba hoja ile iliwagusa watu wengi ingawa hawakupenda kuweka maoni yao hapa kibarazani, lakini nilipokea maoni mengi kupitia ujumbe wa simu wakiwemo wale waliopiga simu, ambao walioanisha swala hilo na nguvu za giza au mapepo kama walivyoita.

Binafsi nisingependa kulioanisha swala hilo na nguvu za giza au mapepo, ingawa pia kuna uwezekano waliosema hivyo wakawa sahihi. Ningependa kulizungumzia jambo hilo kitaalamu zaidi tofauti na mawazo ya wachangiaji wengi waliojitokeza kuchangia mada hiyo.

Kwa kawaida sisi binadamu tumeumbwa na hisia. Ingawa wote tuna hisia sawa, lakini ikumbukwe kuwa wanawake ndio viumbe pekee ambao huonyesha hisia zao ukilinganisha na wanaume na ndio sababu sisiti kusema kuwa tatizo hilo huwatokea wanawake zaidi ukilinganisha na wanaume.

Hali hiyo inaweza kumtokea mtu yeyote, inawezekana hata wewe unayesoma hapa hali hiyo imeshawahi kukutokea. Inaweza tu ikatokea kwa mwanaume au mwanamke akajikuta hampendi mwenzi wake kiasi cha kutaka kuachana naye. Mara nyingi hali hiyo inaweza kudumu kwa wiki tatu au nne halafu ikatoweka, lakini pia inaweza ikajirudia. Kama itatokea ikadumu kwa zaidi ya mwezi, basi hilo litakuwa ni tatizo lingine.

Lakini pia ningependa kuweka wazi kuwa sizungumzii ndoa au mahusiano ya kufujana, naomba nieleweke, hapa nazungumzia kushuka kwa hisia kimapenzi, kwamba inawezekana ndoa ikawa imara, kwa kiasi fulani, lakini ikatokea kuchafuka kwa hali ya hewa na hivyo ndoa au mahusiano kuyumba, hiyo ni tofauti na ndoa ya kufujwa. Mada ya ndoa ya kufujwa inajitegemea na hiyo nitaizungumzia siku nyingine, kwa kadiri nitakavyopata muda.

Kwa kawaida wapenzi au wanandoa huwa kuna vitu vimewaunganisha, yaani kila mtu kuna kitu kimemvuta kwa mwenzake, haiwezekani wanandoa au wapenzi wakawa wanaishi tu, pasipo kitu chochote kuwaunganisha. Na mara nyingi inakuwa ni namna kila mmoja anavyowajibika kwa mwenzie, kwani hilo na mengine mengi inakuwa ndio chachu ya kurutubisha penzi la wanandoa hao.

Inapotekea upande mmoja ukashindwa kuwajibika kama awali, au ukasahau wajibu wake, basi hiyo inaweza kusababisha kushuka kwa hisia za mapenzi kwa kiwango kikubwa na hivyo kusababisha mke au mume kujikuta akimchukia mwenzi wake na kutamani kuondoka au kuachana naye.

Kushuka kwa hisia husababisha kushuka kwa mapenzi na mtu anayepatwa na tatizo hilo hujikuta akimuona mwenzi wake kama kero na asiyestahili kuishi naye. Wakati huo hujisikia kuwa peke yake tena mbali sana ambapo hataweza kumuona mwenzi wake huyo wala kusikia sauti yake kabisa.

Hali hiyo huitwa kuingia pangoni, ambapo mwanamke au mwanaume hujisikia vizuri zaidi kukaa peke yake kwa siku 3 mpaka 7. Lakini hata hivyo naomba ieleweke kwamba kushuka kwa hisia hakusababishwi na upande mmoja kutowajibika katika ndoa, la hasha, zipo sababu nyingi ambazo zinasababisha kushuka kwa hisia.

Inawezekana wanandoa wakaishi pamoja kwa muda mrefu, lakini kutokana ndoa hiyo kukosa mashamushamu au mbwembwe, ni rahisi kutokea mmoja wa wanandoa akajikuta anakinaiwa na uhusiano huo. Ikumbukwe kwamba uhusiano wowote unapokuwa na kitu kile kile kila siku ni rahisi mmoja wa wanandoa kupoteza hamu kwa mwenzie na hivyo hisia kushuka.

Inashauriwa wanandoa wasiwe wanatabirika, kwa maana ya kukuta kitu kile kile kila siku, kwa mfano kwa upande wa wanawake, mapishi. muonekano na mpangilio wa nyumba, namna ya utandikaji wa kitanda, mavazi na manukato, ni lazima kuwe na mabadiliko ya mara kwa mara, badala ya kuacha kitu kile kile kila siku. Kwa upande wa wanaume nao kama wakirudi kutoka kazini au kwenye mihangaiko wawe wanawa-surprise wenza wao na zawadi tofauti tofauti wanapojisikia kufanya hivyo.

Haihitaji kitu kikubwa, hasa hasa ni kuchunguza kama mweza wako anapenda nini, na bila kumuahidi, unatafuta siku unamletea, kwa kumshtukiza, hiyo inachangamsha na kujenga uhusiano imara.

Lakini pia inawezekana hayo yote yakawepo, na bado ikatokea mwanandoa mmojawapo hisia zake zikashuka kwa sababu tu ya aidha kukinaiwa kumuona mwenzake au kutaka kuwa peke yake kwa kipindi fulani. Hali hiyo inatokana na hisia kuchoka na hivyo kushuka kiasi cha kupelekea mwanandoa kutaka kuwa mbali na mwenzie.

Jambo lingine ni mawasiliano. Ikiwa wanandoa hawana mawasiliano ndani ya nyumba, inasababisha kukandamiza hisia zao, kwa maana ya kila mmoja kutokuwa wazi kwa mwenzie. Wanandoa wanatakiwa kuvunja ukimya na kila mmoja kuwa wazi kusema hisia zake bila kificho, kwani hiyo inasababisha kila mmoja kujua mwenzi wake anapenda nini na anachukia nini. Bila shaka mmeshawahi kuona wanandoa wawapo pamoja hawazungumzi kwa bashasha. Lakini unaweza kumwona mwanandoa huyo huyo ambaye sio mzungumzaji nyumbani kwake, awapo nje ya nyumbani kwake na marafiki zake huongea kwa uchangamfu na bashasha.

Swala la uhuru nalo linatajwa kama mojawapo ya sababu za kushuka kwa hisia. Ikiwa kama mwanandoa mmojawapo atakuwa amejenga tabia ya kumtawala mwenzie na kumyima uhuru kiasi cha kuishi kama mtumwa, ni lazima kuna kipindi mwanandoa huyo atahitaji kuwa huru japo kwa kipindi fulani. Na hapo ndipo hali hiyo ya kufkiria kutoka katika ndoa hujitokeza. Kwani kutokana na kuzikandamiza hisia za kutaka kuwa huru kwa muda mrefu hufikia hatua hisia hizo hulipuka na ndipo hali hiyo hujitokeza. Ikumbukwe kwamba hisia zozote zinapokandamizwa kwa muda mrefu, hufikia kipindi zinalipuka na hapo ndipo mambo yanakuwa si shwari tena.

Hali hiyo inapojitokeza, inatakiwa mwanandoa aliyepatwa na tatizo hilo, apewe nafasi ya kuwa peke yake kwa kusafiri au kuwa mbali na mumewe au mkewe kwa kipindi cha wiki moja hadi mbili, kwani kwa kipindi hicho atajisikia vizuri sana. Kama itatokea mke au mume kupata hisia za kutoka katika ndoa kisha kuanza vituko, si vyema mume au mke kuanza kufanya udaidisi wa kutaka kujua sababu ya mabadiliko hayo, kwani hiyo husababisha hasira zaidi na kupelekea kurushiana maneno hata mbele ya watoto au hata hadharani.

Wazee wetu, enzi hizo, walikuwa na busara sana, na walikuwa na mbinu mbali mbali za kuzifanya ndoa zao kuwa hai wakati wote. Kwa mujibu wa simulizi mbalimbali, ilikuwa kama hali hiyo ikitokea, wazee wetu walikuwa wakiwshauri wake zao wasafiri, kwenda aidha nyumbani kwao au ukweni kupumzika, lakini mara nyingi sababu iliyokuwa ikitolewa ni kuwaambia waende kuwasaidia wazazi shughuli za kilimo.

Kama hali hiyo inampata mume, hivyo hivyo, anatafuta safari ambayo itamuweka mbali na mkewe kwa kipindi fulani, na atakaporudi anakuwa na hisia za mapenzi kama zamani au zaidi ya zamani, kwani katika kipindi hicho kila mtu atakuwa na hamu na mwenzie. Ndio maana kitaalamu hali hiyo huitwa ‘kuingia pangoni’

Hivyo basi, hali hiyo inapomtokea mtu, hakuna sababu ya kushtuka, kwani ni tatizo la hisia kushuka, ambalo linaweza kutibika kwa njia ya ushauri nasaha kwa kumuona mtaalamu wa kutatua migogoro ya ndoa.

1 comment:
Andika Maoni Maoni

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi