0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Mar 25, 2009

BADO WATU WANA HOFU JUU YA KIFO!

Kuna ambao huogopa hata makaburi

Habari niliyoiweka hivi karbuni niliyoipa kichwa cha habari kisemacho “Kama kifo huja hivi, basi kifo ni kitamu” imezua maswali miongoni mwa wasomaji, wengi wakitahamaki kuwa iweje kifo kiwe kitamu? Nimekuwa nikipokea simu na meseji mbalimbali nikitakiwa kufafanua juu ya makala hiyo, nami nimeona ni vyema nijibu hoja za wasomaji hao ambao walikataa kuweka changamoto zao hapa barazani ili kila mtu apate kuchangia kwa uelewa wake.

Kwanza ningependa kuweka bayana kuwa habari ile ilikuwa ni ya kweli kabisa na sio ya kutunga na hata kichwa cha habari ile sikuweka mimi bali muhusika mwenyewe. Labda niweke sawa kuwa kichwa kile cha habari hakikusema kuwa kifo ni kitamu bali kilisema “kama kifo huja hivi basi kifo ni kitamu” kichwa hicho cha habari hakisemi moja kwa moja kuwa kifo ni kitamu, naomba ieleweke hivyo.

Lakini hata hivyo, hata mimi naweza kusema kifo ni kitamu,Je unaweza kunibishia?
Tatizo ni kwamba tumetishwa sana kuhusu kifo kiasi kwamba tumejikuta tukihofia sana kufa. Kama ukisoma mafundisho ya dini nyingi hata yale ya asili utabaini kwamba mbinguni ni mahali ambapo panatakiwa kuogopwa na kukwepwa. Tunaambiwa kuwa kuna pepo lakini pia kuna moto.

Hakuna hata mmoja ambaye amewahi kufa na kurejea na kutuambia kilichotokea baada ya kifo.
Tunahofia kwa sababu hatuna uhakika na kitachotokea baada ya kifo na ndio maana tumebaki kutishwa na maandiko ya dini.
Maandiko mengi ya dini yamejaa vitisho vingi ambavyo ukisoma utaogopa sana kifo, tumetishwa kuhusu kuchomwa moto, kuumwa na majoka, na kuishi kwenye giza milele na mateso mengine ya ajabu ajabu, ikiwa unajihisi una dhambi hofu ndio inazidi kuongezeka maana unajua kuwa hutakuwa salama.

Hivi ni nani kati yetu ana uhakika kuwa akifa ataenda peponi? Naamini hilo ni swali gumu kwa kuwa hakuna hata mmoja kati yetu aliyewahi kujiuliza swali hilo.

Kuna masharti magumu sana yanayosimuliwa katika dini zetu hizi ambayo inabidi yatimizwe ili mtu aweze kufika peponi, na kwa kuwa wengi wetu tunajua kwamba ni vigumu kuyatimiza masharti hayo tumejikuta tukihofia kifo, kwa sababu tunajua kwamba tukifa hatutakuwa salama.

Hivi kama mafundisho ya dini yangesema kuwa huko mbinguni kuna pepo tu, ni nani angehofia kifo?

Watu hawataki kuyaacha maisha hata kama ni mabaya naya kutisha kwa sababu hawana uhakika na maisha yao baada ya kifo, wanajiuliza je huko mbinguni maisha yatakuwaje? Kwa nini mtu afe, halafu akateseke zaidi? Huko hakuna mjadala kama mtu ni wa motoni ni wa motoni tu.

Kama ukimwambia mtu asijali hata kama akifa, kwa sababu kifo kina maana ya kuuacha mwili na sio yeye kupotea, anaweza kukuuliza, “kama nitauacha mwili inamaana gani mimi kuendelea kuwepo? Sitakula, sitafanya mapenzi, sitaendesha gari, sasa ya nini kufa?”
Ni kweli yuko sahihi kwa sababu kipimo chake ni mahitaji ya mwili, kwa kuwa ndiyo anayoyafahamu zaidi.

Kwa bahati mbaya Dini zetu zinawatisha wengi badala ya kuwafundisha kuhusu baada ya kifo.

Ukweli ni kwamba maisha baada ya kifo yapo, lakini hayatakuwa kama haya tunayoishi tukiwa na miili hii inayoonekana. Ni vigumu mtu kuamni kwa sababu tumekuwa tukiishi na miili hii tunayoiona tangu kuzaliwa kwetu na hivyo kukubali nadharia hii ni ngumu kidogo.

Hebu nikuulize wewe unaesoma hapa, Hivi hujasikia watu wakisema “Bora mungu amchukue akapumzike” pale ambapo kuna mgonjwa anayeumwa na ugonjwa unaomtesa na kumpa maumivu makali? Au hujawahi kusikia watu wakisema “ Bora kafa akapumzike kwa amani, ameteseka sana”
Hivi kumbe watu wakifa wanapumzika! Ajabu eeh! Sasa huu moto wa milele na majoka, na mateso mengine tunayoambiwa yanatoka wapi? Je huko kupumzika kunakosemwa kunaweza kuwa ni mahali kwenye nafuu zaidi ya mateso anayoyapata huyo mgonjwa kwa wakati huo? Sidhani kama hilo lina ukweli.

Labda nihitimishe kwa kusema kuwa kufa ni hatua muhimu ya mwanaadamu kutoka katika hatua moja kwenda hata nyingine, ambayo itakuwa ni tofauti na mwili huu tuao uona, mwili ambao hauwezi kujibainisha na mwili huu tulionao, kwa hiyo unapofiwa huna haja ya kuhofu kwani huyo aliyekufa hajapotea bali amechukua mwili mwingine na kuanza maisha mapya.

Ukiujua ukweli huu sidhani kama utaogopa kufa, kwani kifo sio mwisho wako na wala sio mwanzo wa mateso kama inavyosimuliwa. Bado nasisitiza kuwa kifo ni kitamu hakuna haja ya kukihofia.

5 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Shabani hii yote ni imani ya mtu kama wewe unaamini kifo ni kitamu basi inakuwa hivyo, na kama unaamini ukifa kama ulitenda dhambi utaenda motoni basi itakuwa hivyo na kunaoamini kuwa wakifa kama hawana dhambi basi watacheza na malaika wao pia watavaa nguo nyeupe.Nasema tena ni imani ni imani

  ReplyDelete
 2. dada Yasinta,

  Hii sio imani yangu, bali ni imani ambayo wote tunatakiwa tuwe nayo.
  kwani tumetishwa na kudanganywa mno, na ndio maana nimeona niwatoe hofu.
  Bado nasisitiza kifo ni kitamu...

  ReplyDelete
 3. Kaluse, wasiwasi wa Yasinta ni wasiwasi wa wengi tunaoamini hizi dini za kuletwa. Swala linalogmba nadhani si kuogopa kifo bali 'nikifa ntakwenda wapi'. Pengine katika makala bado wengi hawajashawishika na hoja na pia namna ya kuuondoa huo uwoga wa kifo. Nalikuwa mmoja wa walokuwa wanaogopa kifo sana (hata kupita makaburini). Kidogo kidogo uwoga huo umeyeyuka. Lakini baada ya kusoma kitabu kiitwacho 'The power of Positive Thinking' mambo yalibadilika kwani nilikuta kumbe hata madaktari wanaweza kukupa prescription ya kwenda makaburini mara 2 kwa wiki kwa wale wenye msongo wa mawazo (yatokanayo na kuwa busy)ili kuwatafakurisha kuwa 'hao walolala hapo' nao walikuwa hivo, hivo mpira ni wao ama kuucheza wafikie hapo wenzao walipo ama kuacha kuendekeza ujinga na kuishi maisha ambayo ni yenye afya na siha njema.

  ReplyDelete
 4. Habari za hapa kaka Kaluse.

  Nimepita hapa kibarazani kwako kujitambulisha kuwa nimefungua kijibaraza changu kitakachokuwa kikijihusisha zaidi na masuala ya vijana.
  Nimekuwa nimsomaji wa blog yako kwa muda mrefu, na sasa nimeamua na mimi nijitose uwanjani ili kuongeza mchango katika kuielimisha jamii.
  Niko ntayari kuelimishwa na kukosolewa pale nitakapoonekana natoka nje ya mstari.
  Natarajia ushirikiano wako.

  Digna

  ReplyDelete
 5. hapa kuna vitu viwili, kufikiri vibaya, na kudhani kwamba sisis ni miili hii inayoonekana na hivyo watu wanafikiria zaidi kuhusu miili kwa sababu wanaona miili ikichimbiwa kaburi na kutupwa udongoni. hapo ndipo woga ulipo. hawajui kama kufa ni kuvua mwili na kuuacha na hivyo unakuwa mchafu na kama ulivyotoka mavumbini, umeishi kwa kutegemea mavumbi na sasa unarudi mavumbini ili angalau funza na madudu mengine yapate chakula japo sisi tunakuwa mbali sana na mahala pazuri zaidi. mahala pasipohitaji chakula, njaa, mihemko, ngono nk.

  wenmgi mnaogooopa kumbe ni haki yenu ya msingi

  kufikiri vibaya ni kule kutarajia maanguko na matatizo. kwa mfano ukisikia basi limapata ajali unajiuliza kama hakuwemo ndg yako, kama alikuwemo, huulizi kama amepona, bali unauliza 'kafa' au kaumia, au hajafa' hata mitihani yetu huwa tunauliza, nikamatwa au kushidwa mangapi? badala ya kushikilia pazuri tunapopahitaji, tunajiuliza pabaya. unakuta mtu kashida masomo matano kati ya sita na anashikilia moja tu lililomshinda, kama lengo lako lilikuwa kushinda kwanini usijipongoze na kujitia moyo kuwa na hili utalishinda tu wakati mwingine au kwanini usijiabie kuwa hii ni changamoto nzuri au funzo zuri na hivyo kuwa sehemu ya ushindi?"

  ndivyo ilivyo kwa kifo. pamoja na dini zenu, bado mnatarajia kwenda motoni, kuchomwa moto nk. hata hivyo wengi huishi kesho wakijiuliza sasa itakuwaje kwani mazoea yanawadanganya kuwa haya ndiyo maisha pekee na mazuri na mwisho.

  sijui ni nani atakufa nami nikajisikia vibaya kwani hakuna kufa

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi