0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Jan 28, 2010

SIKUAMINI KAMA NI YEYE

Alikuwa ni zaidi ya mama

Sikumbuki umri wangu kamili wakati ule, lakini bila shaka nilikuwa na umri wa miaka kama sita hivi. Nakumbuka sisi nyumbani tulikuwa miongoni mwa familia za awali kupata simu nyumbani pale Tabora.
Hata hivyo, nilikuwa tu nasikiliza baba au mama akizungumza na simu , kwani ilikuwa ikikaa juu kwenye meza fulani ndefu. Hata hivyo siku moja wakati nikicheza na nyundo, nilijigonga kidole na kuumia. Kwa sababu nilikuwa peke yangu, nilianza kulia kwa maumivu. Lakini, wazo lilinijia ambapo nilikumbuka kuhusu simu.

Baba au mama, mara zote walipokuwa wakitaka kupiga simu, nilikuwa nikiwasikia wakisema, ‘opereta tafadhali.’ Halafu baada ya hapo, wangeuliza au kuomba jambo, ikiwemo kusaidiwa wazungumze na watu fulani.

Nilitafuta stuli na kupanda juu yake. Halafu niliinua simu na kusema, ‘opereta tafadhali.’ Upande wa pili wa simu ulijibu, ilikuwa ni sauti ndogo ya kike. ‘Ehe nikusaidie nini mwanangu?’ Nilianza kulia , labda kwa sababu, sasa nilisikia sauti ya mtu, yaani niliamua kudeka.

‘Nimeumia kwa nyundo, nataka mama aje.’ Ile sauti ya upande wa pili iliniuliza, ‘unatoka damu?’ nilijibu, ‘sitoki damu ila nimeumia ,’ Ile sauti ambayo wakati huo sikuwa najua kwamba ni ya operetta ilijibu. ‘kama kuna friji nyumbani, chukua barafu halafu weka kwenye kidole chako, kitapoa tu wala usilie.’ Nilirudisha mkono wa simu na kufanya hivyo.

Nilikuwa naijua vizuri friji kuliko simu, hivyo sikupata shida. Nilipata nafuu na kujiambia, ‘kumbe hawa maopereta wanajua vitu vingi.’ Kwa hiyo mara kwa mara sasa wazazi wanapokuwa hawapo nyumbani , nikawa nainua mkono wa simu na kumwita operetta , ambapo nilikuwa naongea naye mambo mengi sana. Nilikuwa namuuliza maswali mbalimbali naye akawa anajibu . Basi tukazoeana angalau kwa sauti tu, bila kujuana.

Nakumbuka kuna wakati kasuku wa jirani yetu mmoja mwarabu alikufa. Alikuwa ni kasuku ambaye tulimpenda sana . Alikuwa akijua kuiga sauti hata kuimba . Nilipojua kwamba, kasuku amekufa, niliinua simu na kumwambia operetta juu ya kifo cha kasuku yule. Opereta alisema, ‘kuna dunia nyingine ambapo watu huenda na kuendelea kuimba.’ Nililipenda jibu lake, kwani lilinipa moyo kwamba, kasuku ataendela kuimba huko alikoenda.

Nakumbuka nikiwa darasa la pili, siku moja nilimuuliza opereta maana ya ‘kabwela’ Aliniambia kabwela ni mtu anayeamka akiwa hajui atakavyolala. Lakini usiku ukifika hulala. Sikulielewa vizuri jibu lake lakini nililipenda. Wakati huu nilishajua jina la operetta kuwa ni Marry na mimi alishajua jina langu, ingawa tulikuwa hatujawahi kuonana..

Wakati huohuo nikiwa la pili, baba alipata uhamisho kwenda mkoani Tanga. Nilijua zikiwa zimebaki siku tatu tu kuondoka. Kwa kule kubabaika labda, nilisahau kumwita operetana kumwambia kuhusu kuhama.

Usikuwa kuamkia siku ya safari ndipo nikakumbuka kuhusu opereta wangu. Kwa kuwa wazazi walikuwepo nyumbani nisingeweza kupiga simu. Niliamua kuchukua picha yangu ambayo nilipigwa shuleni na kuiweka kwenye bahasha. Juu ya bahasha niliandika opereta Marry. Kabla hatujaondoka nilikwenda nyumbani kwa rafiki yangu mmoja tuliyekuwa tukisoma naye darasa moja .

Nilipofika nilimkabidhi ile bahasha na kumwomba ampe mama yake aipeleke kwa opereta. Tuliondoka Tabora nikiwa sijui kama operetta yule alipewa bahasha ile au hapana.
Siku zikapita na nilisoma nakumaliza kidato cha nne ambapo nilipata kazi au ajira ya moja kwa moja {direct employment} kwenye shirika la reli {TRC} nilipangiwa Tabora kama kituo changu cha awali cha kazi. Kwa kweli hali haikuwa nzuri kwa sababu ajira ya moja kwa moja haikuwa nzuri kimaslahi hata kiheshima. Kwa vile pia ilikuwa ndiyo mara yangu ya kwanza kuwa nje ya nyumbani , nilihuzunika sana.

Wiki ya pili tu tangu kufika Tabora, nikawa ninataka kupiga simu kwa baba {mama alishafariki}, baada ya kuinua simu nilimuomba opereta . Ajabu ni kwamba, sauti ile niliyoisikia masikioni nilihisi kama sauti niliyowahi kuisikia miaka mingi iliyopita haikuwa ni ngeni kwangu. Kwanza sikuelewa hasa ni kitu gani, lakini baada ya muda nikakumbuka.
‘Nini maana ya Kabwela’ nilijikuta nauliza.

‘Kama hujaumiza kidole chako kwa nyundo na kasuku wa jirani hajafa , usiniambie uko
Tabora,’nilijihisi nikitetemeka. ‘Mama Marry’ niliita nikiwa kama naota . ‘Ni wewe mwanangu Hussein……’ yule operetta alisema.Ilinichukua muda kujibu. Sina haja ya kusema mengi sana, kwani yule mama alinielekeza kwake baada ya kumjulisha kwamba nilikuwa nimepangiwa kazi pale Tabora. Jioni ya siku ile nilikwenda kwake. Kwa mara ya kwanza nilimwona Marry. Hakuwa mtu mzima sana ingawa alionekana kuwa umri umeenda. Lakini kilichonishangaza ni kuona picha yangu ile niliyomtumia ikiwa kwenye fremu nzuri pale ukutani.

Yeye ndiye aliyeniambia kwamba ilikuwa ni picha yangu, vingenevyo nisingeikumbuka. Lakini kwa nini aliiweka pale. Katika mazungumzo aliniambia kwamba hakuwahi kuwa na mtoto maishani mwake na hivyo kule kumsumbua kwangu kwa maswali kulikuwa kukimpa furaha na faraja sana. Alikuwa akijihisi kama vile nilikuwa mwanaye na alikuwa akifurahia sana hali ile. Kuondoka na mumwachia ile picha, anasema kwamba kulimfanya ahisi kwamba kapoteza mtoto, yaani kafa, hivyo akaamua kuiweka picha yangu kama kumbukumbu.
Lakini ukweli ni kwamba, mama yule alikuwa amenivutia sana kwa namna alivyokuwa akijibu maswali yangu na kuvumilia usumbufu wangu. Mama yangu mzazi hakuwa na uwezo ule na wala hakuwa nyumbani muda mwingi. Kwa hiyo akawa zaidi ya mama yangu kwa sauti tu. Nilimpa picha yangu kama zawadi pekee ambayo ningeweza kumpa. Nilihamia pale nyumbani kwake nikawa nimepata mama mpya, naye akawa amepata mtoto.

Niliamini na bado naamini kwamba, usije ukadhani lolote unalomtendea mtu ni dogo. Liwe ni zuri au baya, lolote unalomtendea mtu, jua linamgusa kwa njia ambayo wewe hujui.
Kumgusa kwake huja kujirudia moja kwa moja au kupitia njia nyingine na ni lazima litakuumiza au kukusaidia, inategemea tu ulitenda nini . Leo hii hanidanganyi mtu kuhusu wema au ubaya tunaotenda unavyokuja kuturudia katika mazingira ambapo tunakuwa hatujui kabisa . Lakini, nimejifunza maana ya kuwavumilia wengine
.

3 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Nanukuu "Niliamini na bado naamini kwamba, usije ukadhani lolote unalomtendea mtu ni dogo. Liwe ni zuri au baya, lolote unalomtendea mtu, jua linamgusa kwa njia ambayo wewe hujui.
  Kumgusa kwake huja kujirudia moja kwa moja au kupitia njia nyingine na ni lazima litakuumiza au kukusaidia, inategemea tu ulitenda nini . Leo hii hanidanganyi mtu kuhusu wema au ubaya tunaotenda unavyokuja kuturudia katika mazingira ambapo tunakuwa hatujui kabisa . Lakini, nimejifunza maana ya kuwavumilia wengine." Mwisho wa kunukuu:-

  Ni kweli kabisa na kuna wakati ni afadhali mtendee wema mtu wa baki kulika ndugu kabisa. Ahsante nadhani kuna kitu nimejifunza na inabidi nifanyia kazi kwani simulizi hii imenifungua macho.

  ReplyDelete
 2. Mara nyingi tumeweza kujiaminisha kuwa NYOTA NJEMA HUONEKANA ASUBUHI, japo naamini kuwa kuonekana kwa nyota hiyo hutambulika jioni. Kila kitu tufanyacho duniani twawekeza. Tunalotakiwa kujua ni kama twawekeza kwa wema ama mabaya. Lakini tunalosahau ni kuwa tunapofanya wema si kila wakati waja kujilipiza ndani ya muda tunaodhania. BINAFSI NIMESHUHUDIA "MALIPO" ya wema uliotendwa nami na hata wazazi wangu. Nilipata msaada wa mtu ambaye alisaidiwa na wazazi wangu nikiwa na miaka kama minne. Zaidi ya miaka 14 baadae ndiyo nikaja kupokea msaada huo TENA KWA WAKATI NILIPOKUWA NAHITAJI MSAADA ZAIDI NA NIKIWA SIJUI PA KUUPATA.
  Kwa Hussein kumpata Mama huyo na kurejesha furaha wakati ambao alikuwa hana mtu wa kumpa furaha na faraja ni kitu cha kuonesha nguvu ya wema.
  Walisema WEMA HAUOZI nami naamini kuwa usipokula matunda ya wema wako, ndugu, jamaa, marafiki ama kizazi chako kitanufaika.
  Nakubaliana kabisa na ulichosema kuwa haijalishi ukubwa wa wema, bali wema unaotendwa mara zote hujirudufisha na kukunufaisha.
  Narejea nukuu kama aliyoweka Da Yasinta kuwa "Niliamini na bado naamini kwamba, usije ukadhani lolote unalomtendea mtu ni dogo. Liwe ni zuri au baya, lolote unalomtendea mtu, jua linamgusa kwa njia ambayo wewe hujui.
  Kumgusa kwake huja kujirudia moja kwa moja au kupitia njia nyingine na ni lazima litakuumiza au kukusaidia, inategemea tu ulitenda nini."
  Blessings

  ReplyDelete
 3. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!Sunday, January 31, 2010

  @ Yasinta & Msee ya Changa-Moto: nakubalina nanyi asilimia 100+

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi