0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

May 17, 2010

MKUTANO WETU NA WANABLOG WENZANGU NA KILE NILICHOKISHUHUDIA BUGURUNI.


Naweza kusema kuwa wiki iliyopita imeacha kumbukumbu kichwani mwangu kutokana na tukio muhimu la kukutana na wanablog wenzangu pale katika Hoteli ya Movenpick.

Ni siku ambayo nilikutana na Chacha o’Wambura Ng’wanambiti na kaka Fadhy Mtanga na Kaka Chib ambapo tulibadilishana uzoefu juu ya Blog zetu hizi.

Mazungumzo yetu yalilenga zaidi katika kupanua wigo wa kublog na kuingia katika utunzi wa vitabu vya maarifa na riwaya. Lengo ni kupanua wigo wa yale tunayoandika ili yawafikie wananchi wengi wasioweza kupata habari za mtandaoni kutokana na ufinyu wa mtandao kutowafikia wananchi wengi vijijini na uelewa mdogo juu ya tasnia hii ya mtandao

Pia tuliazimia kujenga mkakati wa kuwalinda wanablog wa kike ili wasije wakatoweka katika tasnia hii ya blog na pia kuwashawishi wanawake wengi zaidi kujitokeza na kuanza kublog na kuzungumzia matatizo yao na yale yanayoikabili jamii kwa ujumla.

Nisingependa kuzungumza mengi juu ya kukutana kwetu kwani Chacha na Fadhy wameshazungumzia maazimio tuliyofikia katika kikao chetu hicho.

Lakini cha kufurahisha zaidi ni pale Fadhy aliponitembelea nyumbani kwangu maeneo ya Tabata na kupata wasaa wa kukutana na familia yangu.

Tulizungumza na Fadhy hadi saa mbili za usiku na baada ya mazungumzo, nilitoka na mgeni wangu ambapo nilifuatana naye hadi maeneo ya Buguruni, kwani nilikuwa na mtu mwingine ambaye nilikuwa nikutane naye pale Buguruni.

Tulipofika maeneo ya Buguruni kituo cha Sheli tulikutana na mabinti wengi ambao walionekana dhahiri ni wanafunzi kutokana na umri wao kuonekana mdogo. Mabinti hao walikuwa wamevaa vivazi ambavyo viliacha sehemu kubwa ya miili yao ikiwa wazi au tuseme nusu uchi. Walikuwa wakipita pale tuposimama wakiwa katika makundi ya watatu watatu au wanne wakielekea kwenye klabu moja iliyoko jirani na kituo hicho Sheli, maarufu kama Kimboka By Night.

Wakati huo sisi tulikuwa tumesimama kwenye kioski ili kupata maji ya matunda. Nilitumia muda huo kufanya udadisi kwa kumuuliza muuzaji wa kile kioski juu ya wale mabinti wanaopita pale.

Yule muuzaji alitueleza kuwa wale mabinti ni makahaba ambao wanajiuza katika ile klabu ya Kimboka na bei yao inaanzia shilingi elfu tano lakini inategema zaidi na mwonekano wa mtu, na inaweza kupanda hadi shilingi elfu kumi au kushuka hadi shilingi elfu mbili kulingana na hali ya biashara siku hiyo.

Tuliambiwa kuwa mabinti wale hufika pale na mabwana zao ambao huitwa Ving’asti. Vijana hao ambao wengi ni watumiaji wa madawa ya kulevya hutumika kama walinzi wa kuwalinda mabinti hao ili wasidhulumiwe na wanaume wakware, lakini mwisho wa siku hugawana kipato. (Kwa wenzetu wa Ughaibuni huitwa Pimp).

Muzaji yule aliendelea kubainisha kuwa yapo maeneo mawili maarufu kwa ukahaba pale buguruni. Aliyataja maeneo hayo kuwa ni pale Kimboka By night ambapo hukutanisha mabinti wadogo wa umri usiozidi miaka 20 na Sewa Baa iliyoko Buguruni Sokoni ambapo hukutanisha wanawake wenye umri mkubwa wa kati ya miaka 30 na kuendelea. Na wenyewe wamewekeana masharti ya kutoingiliana katika maeneo yao.

Nilipata shauku ya kujua mengi juu ya makahaba hao, na baada ya Kuachana na Fadhy nilikwenda kujionea mwenyewe hali halisi pale Kimboka na kisha nikaeda kule Sewa Baa. Ziara yangu hiyo ilinichukua takribani saa nzima kisha nikarejea nyumbani kutafakari juu ya kile nilichokiona kwa siku ile.

Katika kutafakari kwangu, nilijiuliza swali moja, Je kwa nini mabinti wale wanaitwa ni makahaba? Au ni kwa nini kuwe na makahaba?

Kwa kawaida sisi wanadamu huwa tunapenda kuhukumu matokeo au dalili badala ya kuangalia chanzo. Kwa nini nasema hivyo? Ni kwa sababu wakati tunawazungumzia wale mabinti, muuzaji wa kile kioski alituambia kuwa wale ni makahaba wanaojiuza. Lakini hebu tujiulize, Je wanajiuza kwa nani?

Kama kungekuwa hakuna wanunuzi wa kile kinachouzwa na hao makahaba, ni wazi kusingekuwa na watu hao wanaoitwa makahaba.

Kwa bahati mbaya kabisa ni kwamba wanunuzi wa bidhaa hiyo ambao wengi ni sisi wanaume, lakini sisi hatuna jina la kejeli zaidi ya kuonekana vijogoo.

Inashangaza kidogo kuona kuwa wanaoshiriki katika tendo hilo ni watu wa jinsia zote mbili lakini sifa na jina baya wanapewa mabinti hao.

Hebu tujiulize wote, hivi kwa nini kuwe na makahaba?

Mimi nasema kuwa kumekuwa na makahaba kwa sababu wanunuzi wapo, ambao ni wanaume.

Na imeonekana kuwa soko hilo linalipa na ndio sababu ya mabinti wengi kama wale tuliowakuta pale buguruni wakijiuza, kujikuta wakiingia katika biashara hiyo kutokana na ugumu wa maisha.

Hata hivyo sishangai sana kwani kwa nchi kama Tanzania ambayo hivi sasa inavuma kwa ufisadi, vitendo vya kuvunja sheria na ukahaba ni vya kutarajiwa sana.

Kwa nini tusitarajie vitendo vya aina hiyo wakati wananchi wamekata tamaa kutokana na ugumu wa maisha. Kuna baadhi ya watu wamejilimbikizia mali huku wengine wakishindia mlo mmoja kwa siku.

Hivi sasa kuna wimbi kubwa la mabinti na vijana wa kiume ambao wamejikuta wakiingia katika vitendo vya uvunjaji wa sheria ikiwemo uvutaji wa bangi, matumizi ya madawa ya kulevya na uporaji wa kutumia silaha za jadi kutokana na hali ngumu ya maisha.Wazazi wa watoto hawa wameshindwa kuwalea watoto wao kwa kufuata maadili kutokana na umasikini.

Hivi ni nani asiyejua kuwa pale kipato kinapokuwa kigumu katika familia, wazazi hutokea kuwa wakorofi, wakali na wasiojali sana kuhusu mahitaji ya watoto wao. Kwa kawaida katika ugumu wa mambo, kunakuwa na kutoelewana hata kwa wazazi.

Watoto wanaonekana kwa kiasi cha kutosha kubeba mzigo ambao wazazi wangepaswa kuubeba wenyewe.

Hivi sasa kuna wimbi kubwa la watoto, na hasa wenye kati ya umri wa miaka 13 hadi 19 ambao wamebainika kuwa na sononi, ukatili na kukosa adabu kwa sababu ya umasikini wa familia.

Hivi mnajua ni kwa nini makahaba wengi wanatokea katika maeneo ya uswahilini kama vile Buguruni, Mwananyamala, Tandale, Tandika na kwingineko, na isiwe ni Masaki, Kawe au Mikocheni?

Ni kwa sababu watu wa maeneo hayo, hali zao kimapato ni nzuri ukilinganisha na wale wa maeneo ya uswahilini.

Na msije mkadhani kwamba mabinti hawa wanafanya bishara hii ya ukahaba kwa kupenda? La hasha, sio kweli kabisa, mabinti hawa wamejikuta wakijiingiza katika bishara hiyo kutokna na kukosa namna nzuri ya kujitafutia kipato kwa njia ya halali.

Juzi hapa niliwasikia kinamama ambao hujishughulisha na biashara ya vyakula wakilalamika kuwa wanamgambo wamekuwa wakiwavamia na kuwapora vyakula vyao na hata fedha na kuondoka navyo kusikojulikana, eti kwa sababu wanafanya bishara hiyo katika maeneo yasiyoruhusiwa. Je walitengewa maeneo wakakataa kwenda?

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba kina mama hawa wamekopa katika taasisi za fedha au Saccos, na fedha hizo zinatakiwa kurejeshwa tena na riba juu, lakini bila ya huruma wanamgambo hao wamkuwa wakiwapora vyakula vyao na kuondoka navyo kusikijulikana.

Na ndio maana sikushangaa nilipoelezwa kwamba kuna kina mama ambao ni watu wazima wanajiuza katka Baa ya Sewa pale Buguruni sokoni, kitu ambacho nilikishuhudia.

Kina mama hawa wamelazimika kujiingiza katika biashara hiyo sio kwa kupenda bali ni kutokana na kukosa namna ya kujikimu.

Nilipata bahati ya kuzungumza na mabinti wawili ambapo hata hivyo sikupata muda mzuri baada ya kutishiwa na hao vijana wanaoitwa Ving’asti wao wanaowalinda kutokana na kuonekana kama nawapotezea muda au timing kama wenyewe wanavyosema..

Lakini kwa kifupi waliniambia kuwa walilazimiaka kuacha shule wakiwa darasa la sita na kujiingiza kwenye ile biashara baada ya kushawishiwa na marafiki zao.

Walikiri kuwa hali ya kipato katika familia zao sio nzuri na wanawajibika kujinunulia kila kitu ikiwemo hata chakula.

Kwa upande wa kazi hiyo, ya ukahaba walikiri kuwa ni ngumu sana kwani wanaume wengi hupenda kulawiti tena bila kondom, na wakati mwingine huwadhulumu fedha zao walizopatana.

Kilichonishangaza ni pale waliponieleza kuwa wapo wateja wao ambao wamewazoea wanaopewa huduma hiyo kwa mkopo, wengi wao wakiwa ni vibarua viwandani maarufu kama Day Worker.

Wateja hao hulipa kila mwisho wa juma wanapolipwa fedha zao. Na walikiri kuwa ni waaminifu wakubwa.

Lakini hata hivyo niligundua kuwa mabinti wale ni wavutaji wazuri wa bangi, sigara na ni wanywaji wa Pombe waliobobea.

Nilipowadadisi walikiri kuwa wanalazimika kutumia huo ulevi ili kupata kitu walichoita stimu, yaani kuondoa mawazo.

Walidai kuwa ingekuwa ni vigmu kwao kufanya kazi ile bila kupata hiyo Stimu.

Nilichojifunza kutokana na kile nilichokishuhudia pale Buguruni ni kwamba, kunahitajika mkakati wa kutosha kupunguza pengo kati ya masikini na matajiri. Kuna nguvu kazi nyingi inapotea hivi sasa.

Kujenga shule za kata haitoshi kama hakutakuwa na mkakati maalum wa kupunguza umasikini miongoni mwa jamii ya Watanzania.

Ikiwa kama kila mwaka kuna watoto wanakimbia shule na kuingia katika vitendo vya ukahaba na utumiajji wa madawa ya kulevya, je tutarajie jamii gani itakayoujenga uchumi wetu?

Kelele za majukwaani peke yake hazitoshi kama mikakati na sera maridhawa hazitawekwa ili kukinusuru kizazi hiki kilichokosa mwelekeo.

Katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi mkuu, tutashuhudia kampeni zenye mbwembwe na ahadi kemkem ambazo hazitekelezeki, lengo kuu ni kutaka kujihakikishia ulaji mwingine kwa miaka mitano.

Tunahitaji viongozi watakaoliona hili kama ni janga la kitaifa.

8 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Kukutana kwa wanablogu ni jambo la faraja sana, inaonyesha blogu ni kiungo muhimu cha watu kufahamiana.
  Habari ya makahaba na watumiaji madawa ya kulevya inasikitisha sana.
  Ninaamini mwanaharakati Koero Mkundi atakuja japo na wazo fulani ambalo litatusaidia kutafuta ufumbuzi.
  Ahsante Kaluse kwa mada hii

  ReplyDelete
 2. Ama kweli ni jambo zuri sana mnalolifanya kutuwakilisha wanablog- Ni bahati ya pekee sana kukutana kama mlivyofanya.

  Hili jambo sijui litaendelea mpaka lini nimesoma kwa Mtakatifu Simon mada moja amesema watu kutoa michango ya harusi wanapenda sana lakini kujenga zahanati hakuna. Ni sawa na hapa kuna vijishughuli vingi ambavyo wasichana hao wangeweza kufanya. Saerikali inaona jambo hili lakini halishughulikii kabisa. Kwa kweli kinachotakiwa ni viongozi wapya wenye mawazo mapya waNAOTAKA NCHI YETU IENDELE. Na viongozi hao ni sisi tuamke sasa na mawazo yetu yatoke nje yatumike. Nina huzuni sana kusema haya na kusoma kila wakati habari hizi.

  ReplyDelete
 3. Umenikumbusha sana kaka, PALE Sewa Bar upande wa pili yaani ng'ambo ya barabara pana nyumba ya wageni inaitwa M.K yule mhudum nilikwisha kumhoji siku fulani akanieleza anazo namba za simu za wanawake wanaojiuza.

  Nilimwambia aniitie mmoja. Nikampata na nikaweka mida ya kuzngumza naye. hakika alikuwa mke wa mtu na alinieleza anafanya hivyo baada ya kuchanginyikiwa kidogo baada ya kuchwa. ANAWAITA WANAUME MATAPELI na anaomba mungu arudiane na mumewe. Kwa kweli habari za buguruni ni masikitiko. Nawambia pana gesti naifahamu nilkwisha kufanya upekuzi wa kuhesabu kondomu katika chombo cha taka, lakini hata zingine hazikutumika, nilijiuliza sana. Nilifanya hivyo kwakuwa mmiliki ni mtu aliyepo karibu sana nami. BUGURUNI kipindi cha likizo za wanafunzi pana wanafunzi wengi hujiuza na hii ni mda ndefu sana kuisimulia. Nashukuru kaka umehoji maswali muhimu sana. yanafikirisha

  ReplyDelete
 4. Hiyo ni SIDE B ya stori: Je si kuna wale wadada toka familia bora huko Masaki, maikocheni, mbezi bichi na Ostabei wanaouza 'out of fun, na kujiongezea kipato?'

  HAWAITWI MALAYA, ama?

  Kuna wake za watu tena wengine ni wazito kabisa wanafanya hiyo mineno.

  Kuna wale wanawake wanaokwenda na wachungaji/mapadre na masheikh na utakuta bill za nyumba/shule na matumizi mengine yanatolewa out of our SADAKAz :-(

  Ninazungumza hayo kwa kujua kuna Mama Mchungaji Muamshaji humu kijiweni lakini pia asinihukumu kwa kuwa naongea kutokana na uzoefu wa kufanya kazi na 'Women Engaged in Transactional SEX'

  NA: ni lini wababa nao wataitwa MALAYA. at least mnipe tarehe, ama? :-(

  ReplyDelete
 5. Usiposikia....
  Habari ya hao malaya hapo Bug inatisha sana.

  ReplyDelete
 6. Nawashukuru nyote mliosema. Nyote mnaonesha kuguswa sana na jambo hili. Hali inatisha sana pale Buguruni.

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi