0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

May 30, 2010

MBARBAIG NA NG'OMBE WAWILI


Mnamo Februari 2, 1985 majira ya saa tisa jioni katika kijiji cha Buguchangaa kilichoko wilayani Kondoa katika mkoa wa Dodoma watu wawili waliotajwa kwa majina ya Iddi Hassani Gwandi na Mussa Amani walikuwa katika mashamba yao ambayo yako jirani wakiendelea na shughuli zao za kilimo.

Mara walimuona mtu mmoja ambaye alikuwa akiswaga ng’ombe wawili majike aliyekuja kutambuliwa baadae kuwa ni Mbarbaig aliyejulikana kwa jina la Kidarbarda Kimawida.
Kidarbarda ambae alivaa vazi maalum linalovaliwa na watu wa kabila la Kibarbaig alikuwa akiwaswaga ng’ombe hao waliokuwa na rangi ya udongo akielekea upande ule waliokuwepo Iddi Hassani Gwandi na mwenzie Musa Amani.

Gwandi na mwenzie Amani walimtilia mashaka Kidarbarda kuhusiana na umiliki wa zile ng’ombe hivyo walimsimamisha na kuanza kumuhoji. Walimuuliza Kidarbarda kama anacho kibali cha kuwamili wale ng’ombe, lakini aliwajibu kuwa hana kibali hicho.

Baada ya kugundua kuwa Kidarbarda hakuwa na kibali cha kuwamiliki wale ng’ombe waliamua kumkamata na kumpeleka katika ofisi ya CCM ya pale kijijini na kumkabidhi kwa katibu wa CCM wa kijiji ambaye alikuja kuwa shahidi wa tatu katika kesi hii. (Ikumbukwe ndugu msomaji kuwa mpaka kufikia miaka ya 1990 kabla ya nchi yetu kuanzisha siasa ya vyama vingi watuhumiwa wa uhalifu walikuwa wanapelekwa kwenye ofisi za CCM ambapo kulikuwa na mahabusu maalum ya kuwafungia wahalifu kabla ya kuwapeleka kwenye vituo vya Polisi ambavyo vilikuwa ni vichache sana wakati huo)

Kwa kuwa giza lilikuwa limeshaingia ilibidi amfungie mtuhumiwa ndani ya chumba maalum kwa kazi hiyo ya kuwafungia wahalifu. Katibu huyo alimuomba Gwandi awachukuwe wale ng’ombe akawahifadhi nyumbani kwake mpaka siku inayofuata waendelee na upelelezi juu ya shauri lile. Siku inayofuata mtuhumiwa yule hakukutwa ndani ya kile chumba alichofungiwa kwani alikuwa amevunja mlango na kutoroka.

Baada ya kugundua kuwa mtuhumiwa ametoroka ilibidi wale ng’ombe wapelekwe katika kituo cha Polisi Kondoa ambapo waliandikisha maelezo kuhusiana na wale ng’ombe pamoja na tukio la mtuhumiwa kutoroka kisha wakarejea kijijini kwao Buguchangaa. Siku ile ile vijana wawili walifika pale kijijini Buguchangaa wakitokea katika kijiji cha jirani cha Tungufu ambapo walikutana na Gwandi , Amani pamoja na Katibu wa CCM wa kijiji aliyejulikana kwa jina la Mohamedi Athumani Mringo. (Majina ya vijana wale hayakutajwa na pia hawakuitwa kutoa ushahidi wao pale mahakamani kwa hiyo maelezo yoyote yaliyonukuliwa kutoka kwa wale vijana yalichukuliwa kama ni ya uvumi na kwa mujibu wa sheria hayachukuliwi kama ni ushahidi wa kumtia mtu hatiani.)

Wale vijana walisema kuwa wametokea katika kijiji cha jirani cha Tungufu na walikuwa wametumwa na wana kijiji wa Tungufu kwenda katika kijiji hicho cha Buguchangaa ili kuwaona ng’ombe ambao walikamatwa kijijini hapo wakiwa na Mbarbaig ambapo wanahisi ndio ng’ombe walioibiwa kutoka kijijini kwao. Vijana hao waliendelea kusema kuwa mnamo Februari 12, 1985 katika kijiji cha Tungufu binti mmoja aliyejulikana kwa jina la Farida Omari aliuwawa wakati akiwachunga ng’ombe wawili majike na muuaji alitoweka na wale ng’ombe. Wale watu watatu ambao ndio waliotumika kama mashahidi wakuu katika kesi hii yaani Iddi

Gwandi akiwa ni shahidi wa kwanza, Musa Amani shahidi wa pili pamoja na shahidi wa tatu Mohamedi Mringo Katibu wa CCM wa Kijiji waliwapeleka wale vijana Kondoa ambapo inasemekana kwamba waliwatambua wale ng’ombe wawili majike kama ndio walioibiwa na mwizi ambaye ndie aliyemuuwa Farida. Baada ya wale ng’ombe kutambuliwa, Polisi waliwakabidhi kwa wale vijana ambapo waliondoka nao.

Baada ya siku kadhaa Gwandi, Amani na Mringo Katibu wa CCM wa kijiji waliitwa katika kituo cha Polisi Kondoa ili kumtambua mtuhumiwa mmoja aliyekamatwa akihusishwa na Mbarbaig anaetuhumiwa kumuuwa Farida na kisha kutoweka na ng’ombe. Walipofika walionyeshwa mtuhumiwa mmoja ambaye alikuwa ni Mbarbaig, alikuwa amewekwa Rumande peke yake na wote walimtambua mtuhumiwa huyo kuwa ndie Mbarbaig waliyemkamata na Ng’ombe siku hiyo ya Februari 12, 1985.

Kesi hii kwa mara ya kwanza ilitajwa katika mahakama ya wilayani kondoa ambapo mtuhumiwa hakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa kesi ile ilikuwa ni ya mauaji na kwa mujibu wa sheria za hapa nchini kesi za mauaji husikilizwa na Mahakama Kuu pekee. Kesi hiyo namba 5 ya mwaka 1985 ambayo inaangukia katika kanuni ya sheria namba 196 ya kesi za mauaji (Murder) ilianza kusikilizwa rasmi katika mahakama kuu kanda ya Dodoma.

Katika usikilizwaji wa awali wa kesi hii ulioongozwa na jaji Samatta, vilitajwa vipengele 9 ambavyo havikuleta ubishi pale mahakamani kati ya pande mbili, yaani ule wa mashitaka na ule wa utetezi. Akiendelea kusikiliza kesi hii jaji Nchalla ambaye alichukuwa nafasi ya jaji Samatta alivitaja vipengele hivyo kama ifuatavyo:

=Ukweli kwamba Farida Omari alikuwa ni mkazi wa kijiji cha Tungufu kilichopo wilayani kondoa mkoani Dodoma.

=Farida alikufa kifo kibaya kwa kuuwawa kikatili mnamo February 12, 1985.


=kabla ya kifo chake alikuwa amewapeleka ng’ombe wawili majike waliokuwa wakimilikiwa na baba yake malishoni.

=Farida na ng’ombe hao wawili aliowapeleka malishoni hawakurejea nyumbani.


=Mnamo February 13, 1985 mwili wa Farida uliokotwa porini akiwa ameuwawa

=Mwili wa Farida ulifanyiwa uchunguzi na daktari Mbwana, hiyo ni baada ya mwili ule kutambuliwa na watu wawili waliotajwa kwa majina ya Omari Mohamedi na Juma Ramadhani.


=Kifo cha Frida kilitokana na kunyongwa.

=Taarifa ya postmortem iliyotolewa na Daktari mbwana ilithibitishwa na mahakama na kuwa Kidhibiti cha kwanza.


=Mchoro wa eneo la tukio ulichorwa na askari polisi aliyekuwa na cheo cha sajenti aliyetajwa kwa jina moja tu la Peter nao ulitolewa pale mahakamani kama ushahidi


Hata hivyo yapo mambo ambayo yalileta utata pale mahakamani baina ya pande mbili.
Utata huo ulikuwa ni huu ufuatao:

=Je haiwezekani kuwa muuaji wa Farida ni mtu mwingine asiyefahamika ambaye ndiye aliyemuuwa na kisha kutoweka?

=Au inawezekana muuaji wa Farida ni mtuhumiwa ambaye inasemekana ndiye aliyekutwa na ng’ombe wawili mnamo Februari 12, 1985 ambao ndio walioibiwa kutoka kwa Farida?


=Je mtuhumiwa huyo aleyekamatwa na ng’ombe wawili mnamo February 12, 1985 katika kijiji cha Buguchangaa ambacho kiko jirani na kijiji cha Tungufu alitambuliwa na mashahidi wote kwa kufuata taratibu?

Utata wa kwanza uliojitokeza wakati usikilizwaji wa kesi hii ni utaratibu uliotumika kumtambua mtuhumiwa yule katika kituo cha Polisi wilayani Kondoa, kwani kwa mujibu wa mashahidi wote wa upande wa mashitaka walidai kuwa walipoitwa kwenda kumtambua mtuhumiwa katika kituo cha Polisi cha Kondoa walimkuta mtuhumiwa Kidarbarda peke yake.

Utaratibu wa namna mtuhumiwa alivyotambuliwa na Mashahidi ulitiliwa mashaka na kuacha maswali mengi pale mahakamani, kwani hakukuwepo na gwaride la uatambulisho kama sheria inavyosema. Kwa mujibu wa maelezo ya mashahidi wote pale mahakamani walikiri kwamba siku hiyo Kidarbarda alikuwa ni mtuhumiwa pekee aliyekuwa amewekwa rumande na walipofika mtuhumiwa huyo aliletwa mbele yao na hivyo kumtambua.

Hivyo katika mazingira kama hayo mashahidi hawakupata tabu kumtambua mtuhumiwa kuwa ndiye waliyemkamata kijijini kwao akiwa na ng’ombe wawili majike mnamo Februari 12, 1985. Utata huo unaungana na utata mwingine uliojitokeza wakati shahidi wa nne katika kesi hii askari wa upelelezi ambaye alikiri kuwa siku hiyo ya tukio la kumtambua mtuhumiwa kulikuwa na hali tete kati ya makabila mawili yaani Warangi na wabarbaig mbapo hali hiyo ilitokana na mauaji ya Farida pamoja na wizi wa hao ng’ombe wawili. Ukweli ni kwamba askari huyo wa upelelezi alikiri kuwa kulikuwa na hali tete kati ya warangi na wabarbaig na si mapigano.

Hata hivyo shahidi huyo aliendelea kuieleza mahakama kuwa shahidi wa tatu Mohamedi Mringo alitaja jina la mbarbaig aliyetoroka akiwa katika rumande ya ofisi ya CCM katika kijiji cha Buguchangaa, na jina linafanana na jina la mtuhumiwa. Shahidi huyo alibainisha kuwa kwa mujibu wa kumbukumbu zake jina la Mbarbaig huyo linafanana na jina la Mbarbaig ambaye amekuwa akikamatwa na kufikishwa katika kituo cha Polisi cha wilayani Kondoa mara kwa mara kwa tuhuma za wizi wa ng’ombe.

Kwa hiyo mazingira hayo yakachukuliwa pale mahakamani na upande wa utetezi kama ni ya kumtuhumu mtuhumiwa Kidarbarda kimakosa kuwa ndiye yule aliyekamatwa mnamo Februari 12, 1985 akiwana na ng’ombe wawili ambao baadae walikuja kutambuliwa na vijana kutoka katika kijiji cha Tungufu ambao hata hivyo majina yao hayakufahamika kuwa ng’ombe wale ndio walioibiwa katika kijiji chao wakiwa wamepelekwa malishoni na Farida ambaye aliuwawa katika uporaji huo.

Nae shahidi wa tatu ambaye alikuwa ni katibu wa CCM wa kijiji cha Buguchangaa, Mohamedi Athumani Mringo katika ushahidi wake alinukuliwa akisema kuwa mtuhumiwa alipelekwa katika ofisi ya CCM ya kijiji majira ya usiku.

Je ilikuwaje ikawa rahisi kwake kumtambua mtuhumiwa Kidarbarda kwa urahisi kiasi kile wakati alimuona usiku ambapo kulikuwa na giza? Utata mwingine ulikuwa ni wa kuhusiana na kujichanganya kwa mashahidi wakati walipokuwa wanelezea vielelezo vya utambuzi wa wale ng’ombe wawili wanaotuhumiwa kuwa walikuwa na mtuhumiwa. Mashahidi kutoka katika kijiji cha Buguchangaa ambao ndio waliomkamata mtuhumiwa akiwa na hao ng’ombe walidai kuwa ng’ombe waliowakamata hawakuwa na utambulisho wa alama yoyote.

Lakini shahidi wa nne askari wa upelelezi aliiambia mahakama kuwa aliambiwa na shahidi wa tatu yaani Mohamedi Mringo kuwa wale ng’ombe walikuwa na alama maalum ya kufyekwa masikioni kidogo, alama ambayo inatumiwa na kabila la warangi kwenye ng’ombe zao.
Naye mtuhumiwa Kidarbarda Kimawida ambaye hakuleta shahidi yeyote alitoa utetezi wake kwa kukanusha kuhusika na kumuuwa Farida wala kuiba hao ng’ombe wawili. Pia Kidarbarda alidai kuwa hakuwahi kutoka katika kijiji chake cha Sambala mnamo Februari 12, 1985.
Akiendelea kutoa utetezi wake Kidarbarda alifafanua kuwa kijiorafia kijiji cha Sambala kiko umbali wa maili nyingi kutoka katika kijiji cha Tungufu na kijiji hicho kiko katika wilaya ya Hanang mkoani Arusha.

Mtuhumiwa huyo aliiambia mahakama kuwa hakuwahi kukamtwa na ng’ombe wawili mnamo Februari 12, 1985, bali anachokumbuka ni kuwa mnamo Februari 15, 1985 aliambiwa mmoja ya ndugu zake kuwa anatafutwa na polisi wa kituo cha Kondoa na mara baada ya kupata taarifa zile alisafiri hadi Kondoa na kuripoti kituoni hapo ambapo aliwekwa rumande. Baadae alijulishwa kuwa mnamo Februari 12, 1985 katika kijiji cha Tungufu alimuuwa binti mmoja aliyetajwa kwa jina la Farida na kisha kutoweka na ng’ombe majike wawili ambao walikuwa malishoni wakichungwa na Farida, mtuhumiwa alikanusha kuhusika na tuhuma zote mbili, yaani ile ya kumuuwa Farida na ile ya kuiba ng’ombe wawili.

Ili Polisi kuthibitisha madai yao waliitwa wanakijiji kutoka katika kijiji cha Buguchangaa ambapo mtuhumiwa aliletwa mbele yao na kuamriwa anyooshe mkono ambapo wanakijiji wale wote kwa pamoja walimtambua kuwa ndiye waliyemkamata na ng,ombe wawili siku ya Februari 12, 1985. Wanakijiji wale walidai kuwa mtu waliyemkamata alikuwa na ulemavu katika vidole vyake vya mkono wa kushoto.

Lakini hata hivyo mtuhumiwa alilalamikia namna alivyotambuliwa, kwani wanakijiji wale hawakutoa vielelezo kuwa mtuhumiwa anafananaje kabla hajapelekwa mbele yao ili wamtambue. Jaji alikubaliana na malalamiko ya mtuhumiwa moja kwa moja.

Wakili wa upande wa utetezi aliyekuwa akimtetea mtuhumiwa aliyetajwa kwa jina moja tu la Mbezi katika majumuisho yake mara baada ya kesi hiyo kuisha kusikilizwa alisema kuwa upande wa muendesha mashitaka umeshindwa kuthibitisha madai ya Kidarbarda kuhusika na mauji ya Farida na wizi wa ng’ombe kwani ushahidi wao ulikuwa na mapungufu makubwa na ulitegemea zaidi ushahidi wa kimazingira katika kuthibitisha tuhuma zinazomkabili mtuhumiwa.

Wakili huyo wa utetezi aliendelea kufafanua zaidi kuwa hata wale ng’ombe wawili wanaotuhumiwa kuwa waliokamatwa wakiwa na mtuhumiwa hawakupata kutambuliwa na mwenye ng’ombe kuwa ndio ng’ombe walioibiwa kutoka kwa Farida siku aliyouwawa.
Wakili huyo aliendelea kubainisha kuwa hata maelezo yaliyotolewa na wale vijana kutoka katika kijiji cha Tungufu yalikuwa ni ya uvumi tu, kwa sababu wale vijana hawakuitwa mahakamani kutoa ushahidi wao.

Nae mwanasheria wa serikali aliyetajwa kwa jina moja la Ndunguru katika maelezo yake ya kufunga kesi alisisistiza kuwa mpaka kufikia hapo imethibitishwa bila shaka yoyote kuwa mtuhumiwa alimuuwa farida na kisha kutoweka na ng’ombe majike wawili. Hata hivyo mwanasheria huyo wa serikali alikiri kuwa wale ng’ombe wawili wanaosemekana waliokamatwa na mtuhumiwa hawakuwahi kutambuliwa na mwenye ng’ombe hao na wala hakuwahi kutoa ushahidi wake mahakamani.

Mwanasheria huyo aliendelea kukiri kuwa hata maelezo yaliyonukuliwa kutoka kwa wale vijana waliotoka katika kijiji cha Tungufu yalikuwa ni ya uvumi. Kesi hiyo iliisha kusikilizwa na siku ya hukumu ilipofika Jaji Nchalla aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo alisoma hukumu.
Katika hukumu yake Jaji Nchalla alisema kuwa baada ya kuijadili ile kesi kwa kina na baraza lake la washauri haikuwawia vigumu kubaini kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha madai ya Mtuhumiwa KIDARBARDA Kimawida kuhusika na mauaji ya Farida pamoja na wizi wa ng’ombe.

Jaji huyo aliendelea kusema kwa maneno yake mwenyewe kuwa “kutokana na mapungufu yaliyojitokeza katika ushahidi uliotolewa hapa mahakamani dhidi ya mtuhumiwa, namuachia huru mtuhumiwa Kidarbarda Kimawida kwa mashitaka ya mauaji ya kukusudia (Murder) na ninaamuru mtuhumiwa atolewe kutoka rumande alikokuwa akishikiliwa”

Hata hivyo Jaji Nchalla alisema kuwa haki ya kukata rufaa kwa upande utakaokuwa haukuridhishwa na hukumu ile iko wazi.

1 comment:
Andika Maoni Maoni

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi