0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

May 15, 2010

FUMANIZI: EPUKA WANAOSHAURI KUACHANA.

Huna haja ya kuwaza sana

Fumanizi husababisha hisia zenye maumivu, hasira, kutokuaminiana, woga, aibu na kujilaumu. Lakini kufumania au kufumania hakupaswi kuwa sababu wa kuwa mwisho wa ndoa yenu, ingawa kunaweza kuwa pia.

Baada ya fumanizi, inabidi ujitahidi kuelewa na kuweza kujenga tena ndoa yako, pengine sasa ikiwa ni ndoa imara zaidi. Hata hivyo hii inataka kujituma kwingi na uvumilivu na subira .

Ndoa inaweza kuendelea hata baada ya fumanizi kwa kutumia ushauri, kupeana muda na kushirikiana. Kuna ndoa ambazo zimeweza kudumu zaidi baada ya fumanizi kutokea.

Pale kutoka nje kwa mwanandoa mmoja kunapogundulika hupelekea hisia kali kwa wanandoa wote, mshtuko, aibu, kujilaumu, kujiona mkosaji, hasira kali na wasiwasi. Kutokana na hisia hizi zote mara nyingi wengi hufanya maamuzi yasiyo mazuri kama kutengana au kuachana kabisa.

Badala ya kufanya hivyo katika kipindi kile cha muda mfupi baada ya fumanizi, tunahitaji kuwa watulivu sana ili tuweze kuchukua hatua zinazofaa.

Kupata msaada: Kwa uzima na afya yako mwenyewe, tafuta msaada kutoka kwa familia, rafiki, mchungaji, shekhe au mshauri yeyote unayemwamini wewe na kujihisi huru kwake. Kuongea kuhusu hisia zako kwa wale unaowapenda sana itakusaidia wewe kupunguza nguvu za hisia za maumivu ya tukio hilo. Kuongea na watu wengine kunaweza kukupa wewe uwezo wa kuelewa zaidi hisia zako na kupata mtazamo mwingine kuhusu tukio.

Pengine aliyetoka nje inawezekana hatosheki katika mahusianao katika ndoa yake au hawajibiki vizuri katika ndoa. Au pengine hawezi kudhibiti mihemko yake.

Mabadiliko ya maisha kama kuzaliwa mtoto au upweke wa aina fulani, unaweza kuwa ndio sababu ya kutoka nje. Inabidi haya yatazamwe kabla mtu hajaamua lolote.

Kwa hiyo kujua sababu ya mwingine kutoka nje ni muhimu sana na hii inaweza kukupa ahueni, kwani unaweza kubaini kitu ambacho kinaonesha kwamba, kwako pia kuna matatizo.

Hatua zitakazokusaidia kujenga upya ndoa yako baada ya fumanizi ni nyingi. Lakini hizi ni baadhi tu ambazo kwa mazingira yanayokukabili, zinaweza kukusaidia.

Kuacha kutoka nje ya ndoa:
Hatua ya kwanza ni kwa mwanandoa kuacha tabia ya kutoka nje ya ndoa kiukweli. Mwanandoa anatakiwa kuacha kabisa mahusiano na mawasiliano na wapenzi wao wa nje, kujirudi kiukweli katika ndoa hakuwezekani bila kufanya hivyo.

Kukubali kuwajibika:
Kama umetoka nje ya ndoa, kuwa tayari kuwajibika katika vitendo vyako. Kama ulikuwa unadanganya, fikiri kuhusu matokeo ya vitendo vyako, fikiri kuhusu furaha uliyoiondoa kwa vitendo vyako, kubali kubadilika.

Onyesha nia ya malengo yako:
Kuwa na uhakika kuwa wote wawili mko tayari kujenga upya ndoa yenu. Inawezekana kuchukua muda kuondoa yote yaliyotokea na kuona kuwa mnaweza kuponya ndoa yenu tena. Kama wote mmefikia muafaka wa kujenga upya ndoa yenu basi ni vyema mjue kuwa itachukua muda, nguvu na kujitolea sana.

Onana na mshauri wa wanandoa:
Mtafute mshauri wa ndoa ambaye atakusaidia kujenga upya ndoa yako kama itakuwa inahitajika. Onana na mshauri wa ndoa ambaye alishawahi kukutana na kusaidia kutataua matataizo ya fumanizi. Mwepuke mshauri ambaye anaamini kumfumania au kufumania ndio mwisho wa ndoa yenu.

Kuchunguza tatizo:
Kufumania au kufumaniwa huzua matatizo katika ndoa. Chunguzeni kwa makini mahusiano yenu ili uweze kujua nini kilichosababisha au kilichopelekea kutoka nje ya ndoa na nini mfanye ili kuzuia kutoka nje ya ndoa tena. Epuka kutafuta msaada kwa watu ambao huwaamini na anajua hawawezi kukupa msaada mzuri kwa sababu itakuzidishia hisia za maumivu.

Kila mmoja apewe nafasi:
Kila mwanandoa anahitaji kupumzika kwa ajili ya kuondoa msongo na wasiwasi kutokana na tukio la fumanizi, hii ni kwa sababu huwa ni vigumu kusikiliza ushauri wakati mihemko iko juu sana.

Pata muda:
Epuka kujua undani zaidi kuhusu fumanizi la mwenzi wako kwa wakati wa mwanzoni. Ahirisha mjadala huo kwanza mpaka uzoee ile hali ya kumfumania mwenzi wako.

Fumanizi ni nini kwako?
Fumanizi sio kitu kimoja chenye maelezo au hali ya kueleweka kirahisi. Kuna aina nyingi za fumanizi. Kitu ambacho kinaweza kisikubalike kwa wanandoa fulani, kinaweza kukubalika na kuvumiliwa na wanandoa wengine kwenye fumanizi. Suluhu kwenye masuala ya fumanizi haifanani.

Kurudi katika hali ya kawaida baada ya fumanizi ni hali ambayo kiukweli ni ngumu sana, lakini inawezekana mmoja kuvumilia baada ya mmoja kutoka nje ya ndoa. Ushauri wa mambo ya ndoa utakusaidia kuliona tatizo hili kama matatizo mengine ya ndoa, jifunze jinsi ya kujenga tena ndoa yenye nguvu na mahusiano mazuri na epuka suala la kutalikiana, labda tu ama inabidi.

Kuelewa kwa nini mwenzi wako ametoka nje ya ndoa ni hatua muhimu katika kuweza kurejea tena katika ndoa na kuwa na furaha.

Kutoka nje ya ndoa huweza kutokea kwenye ndoa yenye furaha na isiyo na furaha na sababu zinatofautiana.

Baada ya mshtuko ule wa mwanzoni kuisha, zungumzeni kwa uwazi na upendo kuhusu kilichotokea, usijali ugumu katika kuongea au utakachosikia kuhusu tukio. fahamu kuwa unaweza kuhitaji msaada kwa mshauri au mtu yeyote unayemwamini ili uweze kuongea kwa uwazi zaidi.

Kama wewe ndiye uliyetoka nje ya ndoa unaweza kutengeneza ratiba kwa ajili yako wewe kuweza kujirudisha katika hali ya kawaida tena. Mara nyingi yule aliyetoka nje ya ndoa huwa na wasiwasi sana kuhusu tukio hilo. Kila mmoja anahitaji muda wa kuweza kujitibu mwenyewe.

Kwa watu wengine kusamehe ni suala gumu katika kujenga ndoa upya baada ya fumanizi.

Kusamehe siyo suala rahisi na la haraka. Inaweza kuwa kitu cha muda mrefu katika maisha, lakini kama umejitolea kwa mpenzi wako hili ni suala rahisi sana.

Mwisho wa ndoa au hapana ?
Siyo kila ndoa iliyoguswa na suala hili la fumanizi ni lazima imalizike kwa kutokuachana. Wakati mwingine kunakuwa na uharibifu mkubwa na wanandoa hawana budi kuachana na pia kama wanandoa hawako tayari kuwa pamoja tena.

Lakini kama wote mko tayari kujenga upya ndoa yenu, basi suala hili huwa rahisi sana na uhusiano utaendelea kuwa mzuri na wa amani zaidi.

3 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. ni habari nzuri sana nimeipenda na nimejifunza kitu ahsante sana kaka Kaluse. Nitaiomba niiweke pale kibarazani kwangu pia. Upendo daima!!!

  ReplyDelete
 2. Big up.
  Hii ndio watu wanaiita habari yakinifu

  ReplyDelete
 3. Kaluse,,fumanizi na hatua ya maisha ndani ya ndoa,,,bila fumanizi unakuwa hujakomaa ndani ya ndoa yako,,,lazima hitilafu itakuwepo tu,,,cha msingi ni kuwai lile fumanizi kabla halijajipeleka mbali,,,

  Lucy

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi