Ilikuwa ni ajali ya kutisha
* Mume alienda mazishini na ambulance kwa upendo wake
* Aliyewauzia gari lililomuua ni miongoni mwa wapenzi wake
* Picha na barua za aibu zikakutwa kwenye droo zake mbili za siri.
Tunaambiwa siku zote tusisemee mioyo ya watu wengine, kwani wao ndio wanaojua hasa nini kinaenda kwenye mawazo yao. Ni hatari kwa mfano, mtu kusema hadharani kwamba mpenzi wake hatoki nje. Anachotakiwa kufanya mtu ni kuamini kwamba mpenzi wake hatoki nje lakini sio kutangaza kwamba mpenzi wake hawezi kutoka nje.
Kuna mambo mengi sana ambayo yanaweza kuwa yanafanywa gizani na wapenzi wetu ambayo tukiyafahamu hutokea kutuumiza sana na kutufanya kuchanganyikiwa. Hebu fikiria, inakuwaje pale mume anapoamini kwamba mkewe ni mwaminifu sana na hawezi kutoka nje, iwe ni kwa jua au mvua. Bila shaka anapong’amua kwamba hutoka sana nje, kunakuwa na kuchanganyikiwa na kuumia kwa kiwango cha juu sana. Lakini jambo la kujiuliza ni hili.
Ni kwa sababu zipi hasa mtu anapendwa na kupewa kila kitu na mpenzi wake lakini bado anakwenda nje na kufanya mambo mengi, makubwa na ya aibu kiasi hiki? Kila kitu hatimaye hujifunua wazi hata kama tumefukiwa makaburini tayari! Utu na uadilifu wetu “feki” hutusuta huko mbinguni tuliko………..
********************************
Ilikuwa ni ajali kubwa na hata mimi sijui niliweza vipi kupona. Dereva na mke wangu walifia pale pale kwenye eneo la tukio. Tulikuwa tukitokea Chalinze kurudi Dar es salaam baaada ya kukagua shamba ambalo ilikuwa tulinunue katika kijiji cha Msata wilayani Bagamoyo. Mbele kidogo ya mji wa Chalinze ndipo ajali hiyo ilipotokea .
Dereva wetu alikuwa akijaribu kulipita lori fulani lakini wakati huo huo gurudumu la mbele la gari letu lilipasuka na kusababisha gari kuyumba ambapo lililivaa lile lori. Kufuatia kuligonga huko, gari letu lilirudishwa katikati ya barabara ambapo liligongana uso kw auso na gari lingine lililokuwa linakuja mbele yetu. Sikujua kilichotokea hadi baada ya siku mbili Muhimbili.
Nilipopata fahamu ilinichukua muda kukumbuka kidogo kilichotokea.
Nilipouliza kuhusu mke wangu hakuna aliyesema kitu kati ya wale ndugu na jamaa zangu waliokuwa pale kando ya kitanda changu. Pamoja na maumivu yangu nilijua kilichokuwa kimetokea. Nilianza kulia , hata kabla hawajaniambia chochote. Kaka yangu aliponiambia “jikaze ni kazi ya Mungu, shemeji mama Rehema ametutoka” Nilipoteza fahamu. Nilipopata fahanu na kukubali kuipokea taarifa ile, niliambiwa kuwa mke wangu alifia pale kwenye eneo la ajali pamoja na dereva.
Mimi nilikuwa nimevunjika mguu wa kushoto, mkono wa kushoto na mbavu mbili na kubanwa kifuani. Hali yangu kwa kweli haikuwa nzuri lakini nililazimika kujikaza. Mke wangu alikuwa amekufa, haikuwa rahisi kukubali. Nilikuwa nampenda na yeye pia alikuwa ananipenda.Ukweli ni kwamba tulikuwa tukiaminiana sana na mke wangu ambaye nitamwita Sia {Jina linalokaribiana na jina lake halisi}. Tulikuwa tumeshibana kiasi kwamba, kulikuwa hakuna ambaye alikuwa hajui.
Nilikumbuka kwamba kwa miaka minane ya ndoa yetu tulikuwa hatujawahi kukorofishana, ukiacha kusigishana kwa hapa na pale. Nilikuwa sijawahi kumsaliti na hata yeye pia. Nilijaribu kukumbuka ahadi zetu kwa kila mmoja na kuhusu watoto wetu wawili mmoja wa kiume na mwingine wa kike. Kwa kweli ilinichukuwa muda wa saa kadhaa kukubali kwamba nilikuwa sina mke, mwili wa yule nimpendaye ulikuwa ukiganda mochuari.
Nilijikuta nikiinuka kwa nguvu na kupiga yowe nikitaka kwenda kumfufua mke wangu. Nilikuwa nimechanganyikiwa kwa kweli! Ndugu zangu na jamaa waliokuwepo pale wodini walinishika nakunituliza. Ilibidi waombe msaada kwa madaktari ambapo nilichomwa sindano iliyonipa utulivu na usingizi. Nilipoamka jioni sana , nilikuwa na utulivu kidogo, kaka yangu aliniomba nijikaze na kumrudia mungu, Aliniambia nijaribu kuukubali ukweli na hali halisi. Nilijikaza na aliniambia kwamba mazishi ya mke wangu ingebidi yafanyike kesho, kwa mujibu wa makubaliano ya ndugu wa pande zote.
Aliniambia dereva wangu alikuwa amezikwa tayari na ndugu zake. Nilimwomba kaka wauache mwili wa mke wangu ili niwe nae karibu kwa muda fulani. Kaka alinishawishi sana nikubali kwa sababu, kama mwislamu ninajua inavyokatazwa kuuweka mwili wa marehemu bila kuuzika kwa muda mrefu, bila sababu.Hatimaye nilikubaliana naye, lakini nilisema ni lazima nami niende kuzika. Kaka alinimbia kwa hali yangu nisingeruhusiwa na madaktari na wala nisingeweza kumudu kwenda makaburini Kinondoni.
Nilimwambia kaka katika yote ningemkubalia lakini sio hilo la kutomzika mke wangu. Nilimwambia, habari ya madaktari aachane nayo na kuhusu mimi kumudu ningemudu tu. Nilikataa katakata hata kusikiliza ilibidi kaka aondoke pale bila muafaka. Walikuja ndugu zangu wengine kunishawishi lakini niligoma kabisa, hadi ikabidi wakubaliane nami. Lakini walijua ingekuwa ngumu sana kutokana na hali yangu.
Kesho yake walikuwa tayari wamepata ufumbuzi. Walikubaliana na uongozi wa hospitali kwamba nipelekwe makaburini kwa gari la wagonjwa. Ni kweli nilikwenda kuzika. Pamoja na kuwa waislamu huwa hatutoi heshima za mwisho kwa kuuona mwili wa marehemu, mimi nililazimisha hadi nikaonyeshwa mwili wa mke wangu.
Alikuwa hana alama hata moja usoni kwani alikuwa ameumia miguuni hadi kifuani. Nilipomwona nilipoteza fahamu………… Tulimzika mke wangu na nikarudishwa hospitalini. Nilitoka hospitalini baada ya mwezi mmoja na kurejea nyumbani. Nyumba yangu mwenyewe ilinitisha na nilihisi simanzi kubwa kuwa mle ndani. Watoto wangu walinisikitisha zaidi. Lakini nilishaamua kuikubali hali halisi. Nilikuwa nimekubali kuanza upya maisha.
ITAENDELEA..................................
mkasa wa kusikitisha huu ati :-(
ReplyDeletenangojea sehemu inayofuata!
naisubiri hiyo siri, iliyofichuka
ReplyDelete