0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Nov 27, 2009

BINTI ALIYESHANGAZA FAMILIA KWA VISA-SEHEMU YA MWISHO

ILIPOISHIA.........

Alikuwa na kila aina ya visa. Alikuwa akitukana waalimu,kupiga wanafunzi wenziena kuanzisha vurugu za aina mbalimbali. Ajabu ni kwamba, ukiwa umekaa naye na kuzungumza naye, anakuwa mtoto mzuri na msikivu sana. Anaweza hata kulia, kujutia makosa yake. Lakini baada ya hapo ndio anakuwa ametiwa moto.

ENDELEA KUSOMA HAPA..................

Kwa mwaka mmoja wa kidato cha kwanza, tulimbadilisha shule kiasi cha sita. Alipoingia kidato cha pili ndio vurugu zikawa kubwa zaidi. lakini sasa hapa akawa ameanza tabia za uhuni, yaani kushiriki ngono.

Hali hii ya kupenda kushiriki mapenzi ilitukera sana na tulijua kwamba tumeshapoteza mtoto tayari. Lakini katikati ya tatizo hili, likazuka lingine. Hili ndilo lilikuwa kubwa zaidi. Alikuwa mara nyingi akidai kwamba ana hamu na mama yake. Tulipokuwa tukimwambia kwamba mama yake yupo hapo nyumbani, yaani mke wangu, alikuwa akisema hana uhakika sana kama hadanganywi.

Kusikia hivyo, nilijua yule mama aliyenisaidia kumpata alikuwa amemwambia siri yote. Nilipomwendea na kumuuliza alisema asingeweza. Lakini alisema hata mama yake halisi na yule mtoto, kabla hajafa alikuwa akiropoka mambo mengi makubwa na ya kutisha.

Ilibidi sasa niombe ushauri kwa watu mbalimbali, kuanzi kwa mashehe, mapadri, waganga na madaktari. Lakini hakuna kilichobadilika. Kila mmoja alijaribu kumsaidia kwa namna yake lakini, bila mafanikio.

Pamoja na Vituko vyake na kauli za kutisha, hasa hizo za kumtaka mama yake na kusema anahisi haambiwi kweli, bila kufafanua, alimaliza kidato cha nne mwaka 1999. Wakati huo alikuwa anaumwa sana hata hivyo. Tulijaribu kumsaidia sana kwa matibabu na kumtunza.

Tulikuwa tunampenda sana pamoja na visa na vituko vyake. Mwaka 2000 alizidiwa sana na maradhi na tulilazimika kumfanyia vipimo zaidi na alibainika kwamba ameathirika kwa ukimwi..

Hatukumpa matokeo ya vipimo hivi awali, lakini alitushangaza aliposema, 'mnanificha kitu gani, siogopi kama mnavyofikiria. Kwani mtu kwenda kuungana na mama yake kuna tatizo?' Kwa kuwa nilishamzoea kwa visa vingi lukuki, sikustuka sana, ingawa mke wangu alishtuka kupindukia.

Mwaka 2001 alizidiwa kabisa na sasa alikuwa akikaa nyumbani tu. Siku moja mwezi wa Juni aliomba apewe jina la ukoo wa mama yake, kabla hajafa. Hapo tuliogopa vizuri sana kwa kweli na siwezi kuisahau siku hiyo. Tulimpa jina la ukoo wa kwa mke wangu, alikasirika sana na kusema anataka jina la ukoo wa kwao.

Alisema akifa bila jina hilo, mambo yasiyopendeza yangetokea na kwamba asingepaswa kulaumiwa kwa hilo, kwani kazi tuliyofanya ingekuwa imepotea bure.

Tuliogopa sana na ilibidi niende kwa yule mama aliyenifanyia mpango wa kumpata binti huyu na nilizungumza naye. Alisema, ingekuwa ni vigumu kwake kupata taarifa za yule mama yake. Lakini kwa bahati alikumbuka jina na ubini na kwamba, yule mama alimwambia alikuwa ametokea kijiji cha Puge, Nzega, Tabora.

Alimwambia alifika Dar es salaam kwa kudanganywa na mtu ambaye alimleta Dar na kumtelekeza baada ya ujauzito. Nililazimika kusafiri hadi huko Puge, nilipofika hapo kijijini {Ni kijiji lakini ni kama kamji kadogo} nilidadisi na kupata taarifa kumhusu yule mama. Sikusema chochote, zaidi ya kurejea Dar es salaam. Nilivyoambiwa kule ni kwamba, yule mama wa mtoto wetu alikuwa apewe kitu walichoita Mkoba {Uganga bila shaka} ya bibi yake mzaa baba, lakini akakataa na kukimbilia kusikijulikana.

Huku Dar es salaam alikuja mwenyewe na kukutana na huyo tapeli aliyempa ujauzito. Inaelezwa kwamba, bibi yake alikufa akiwa hajakabidhi mikoba ya uganga kwa yeyote. Hayo niliyaamini ingawa kabla ya tukio hili, kama ungenitajia jambo kama hilo, ningekutemea.

Nilirudi Dar na nilipofika nyumbani, hali ya binti yetu ilikuwa mbaya sana. Nilimsalimia na kumwambia kwamba tunampa jina {Naomba nisilitaje}. Aliposikia jina hilo aliinua kichwa, jambo ambalo alikuwa hajawahi kulifanya tangu kuzidiwa kwake na ugonjwa.

Halafu alirudisha kichwa kwenye mto na kufariki hapohapo. Naomba uniamini kwa faida yako, kwani hilo, lilitokea mbele ya macho yangu. Sioni faida ambayo mimi au wewe utaipata kwa uongo ambao nitaufanya katika suala hili.

Mwaka huo huo akiwa na miaka 41 mke wangu alijifungua mtoto wa kike. Ilikuwa kama ajabu kwetu na mshangao huo hauwezi kututoka hata siku moja. Lakini hata kama atakuja mtu gani tukubali kuwa hakuna miujiza na nguvu za ajabu kwenye maisha, tutambishia hata kwa thamani ya damu yetu, kwa sababu tumeona kwa macho yetu.

Mimi na mke wangu tumeumizwa sana na kilichotokea na hasa matukio ya yule binti yetu ambaye tulimlea kwa upendo. Tumekuwa tukijiuliza kilichotokea bila kupata jibu. Tunapata majibu mengi kuhusu jambo lile, lakini tulipofika kwenye ofisi za Gazeti la Jitambue, ndipo tulipopata majibu yenye ridhiko ambalo limeanza kutupa nafuu kubwa.


*******************MWISHO******************

7 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. HII HABARI INASIKITISHA NA KUSISIMUA!! JE HABARI YA KWELI?? MAKE IMAISHA WAKATI IMEANZA KUNOGA. NAOMBA NIJUE HILO. NA PHCHA ILIYOKO KWENYE HABARI NDO BINTI MWENYEWE ALIYEKUWA NA VISA KWA FAMILIA YAKE??

  ReplyDelete
 2. Ndugu usiye na jina, habari hii ni ya kweli kabisa na iliwahi kuandikwa katika gazeti la Jitambue Kitambo kidogo...ila kwa kutaka kuwakumbusha wasomaji wa blog hii nimekuwa nikiweka baadhi ya ushuhuda uliwahi kuandikwa katika gazeti hilo ambalo mimi nilikuwa ni mmojawapo wa waandishi wake kabla ya kusitishwa kuchapishwa kwake kutokana na kifo cha mmoja wa wamiliki na aliyekuwa mhariri mkuuu wagazeti hilo, hayati Munga Tehenan.

  Kuhusu Picha, kwa kweli haina uhusiano wowote na habari hiyo ila niliweka tu kama taswira ya kunogesha makala hiyo.

  Unakaribishwa kama unao mchango au maoni yoyote juu ya mada zangu.

  ReplyDelete
 3. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!Friday, November 27, 2009

  kazi nzito hiyo

  bila shaka alikufa huyo mtoto akaamua kuleta faraja kwa wanandoa hao

  miujiza? pengine ipo

  ReplyDelete
 4. To become a parent is also a challenge. Ni fundisho kwa ulimwengu

  ReplyDelete
 5. Hii habari inasikitisha sana, ila huyu mtoto alikuwa kama ni neema kwa wao kupata mtoto wao halisi.
  Ahsante kwa kuweka hapa, maana mie sikuwahi kusoma.
  Dada F.

  ReplyDelete
 6. ni habari nzuri na ya kufundisha, kumbuka Mungu Mwenyewe ndo agawaye

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi