0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Dec 11, 2012

THAMANI YETU IKO NDANI YETU....!


Mhubiri mmoja maarufu nchini kwenye moja ya semina zake alifungua semina kwa kuishikilia noti ya shilingi 10,000 mkononi. Kulikuwa na watu zaidi ya 500 kwenye ukumbi alimokuwa akifanyia mahubiri yake. Aliinua noti hiyo na kuuliza ‘ni nani anayeitaka noti hii?’

Mikono karibu yote ukumbini ilinyooshwa. Mhubiri aliendelea kusema, ‘nitampa mmoja wenu noti hii, lakini kwanza ngoja nifanye hivi.’ Alipomaliza kusema hivyo aliikunjakunja noti ile. Baada ya kuikunjakunja aliuliza tena, ‘ni nani anayeitaka bado noti hii?’ vidole karibu vyote vilinyooshwa tena. ‘Sawa,’ alisema, kabla hajaendelea, ‘Je kama nikifanya hivi?’ Alipomaliza kuuliza hivyo aliiweka noti ile chini na kuisigina kwa mguu bila kuichana, halafu aliiokota ikiwa imechafuka na kuikunjakunja. Aliuliza tena, ‘sasa ni nani ambaye bado anaitaka noti hii?’ vidole vilinyooshwa tena juu.

‘Rafiki zangu, wote leo mmejifunza somo la maana sana. Bila kujali nilichokifanya kwenye noti hii, lakini bado mmeendelea kuitaka, kwa sababu kuikunja kwangu na hata kuikanyaga, hakukuondoa thamani yake. Bado imeendelea kubaki noti ya shilingi 10,000.’ Bila shaka hata wewe utakubaliana na kauli hii ya mhubiri huyu, kwamba noti ile iliendelea kubaki noti ya shilingi 10,000 na kwamba thamani yake iliendelea kubakia pamoja na kukunjwa na kukanyagwa kwake.

Mara nyingi kwenye maisha yetu huwa inatokea tukaangushwa na kukunjwakunjwa na pengine kugalagazwa kwenye vumbi la fedheha na dhalilisho kwa uamuzi ambao huwa tunauchukua na mazingira ambayo huja au kutujia kwenye njia zetu kimaisha. Katika nyakati kama hizi hutokea tukajihisi kuwa hatuna thamani. Lakini tusichokijua ni kwamba, hata kama kingetutokea kitu gani, hatuwezi kamwe kupoteza thamani zetu.

Tuwe wachafu au wasafi, tuwe tumekunjwakunjwa na kutupwa kwenye vumbi la dharau na kejeli au tuwe tumetakaswa kwa kila aina ya usafi, bado thamani yetu haiwezi kununulika.

Kwa nini?

Ni kwa sababu thamani yetu haiji kupitia au kutokana na kile tunachokifanya au kutokana na akina nani tunaowajua au wanaotujua, bali jinsi tulivyo. Thamani yetu iko ndani mwetu, kama ambavyo thamani ya noti iko kwenye noti yenyewe bila kujali kama imekunjika au ni safi. Tukiamua kwamba thamani yetu iko nje yetu, ni wazi tukikejeliwa au kuvurugwa kwenye dhalilisho na dharau, tutajikuta tukijidharau na kudharauliwa kikweli na hata wale waliokuwa wakituheshimu.

Lazima tujue kwamba, sisi ni watu maalum. Kati ya watu bilioni saba tuliopo duniani hakuna mwingine kama sisi, nasi kila mmoja kama yeye ndiye anayekamilisha idadi hiyo. Kama tumeshazaliwa ni lazima tujue kwamba hakuna mwingine tena atakayezaliwa kama sisi na hajawahi kuwepo mwingine anayelingana nasi.

Tukitukanwa, tukasingiziwa, tukaharibiwa jina, tukaaibishwa na kufanyiwa ubaya, bado thamani yetu itaendelea kuwepo. Kama tutalijua hilo, basi hakuna dhalilisho au kashfa ambayo itaweza kutufanya tuone kwamba tumevunjiwa heshima au kudhalilishwa. Hii ni kwa kuwa thamani yetu haiwezi kuguswa na mtu kwani iko ndani mwetu.

Ni sisi tu tunaoweza kamua kuitoa au kubaki bila thamani na sio mtu mwingine wala mazingira yoyote.

Kwa nini basi tuamue hivyo?

Kuna wakati huwa tunajiingiza mahali ambapo tunajiumiza bure kwa kudhani kwamba thamani yetu wanayo watu wengine. Watu hao wanapotuita wajinga au wanapotuita masikini au wanyonge, huwa nasi kwa kutojua tunakubaliana nao kwamba sisi kweli tuko hivyo na hao wanaotuita hivyo ndio ambao ni wajanja, matajiri na wenye nguvu. Hatujui kwamba kwa kufanya hivyo tumejiondolea wenyewe thamani yetu.

Lakini pale ambapo watu hao wanapotushusha na kutubeza, sisi tutawachukulia kama mkono wa mhubiri au mguu wake ambao unatukunjakunja na kutukanyaga bila kumudu kuondoa thamni yetu, hatutajisikia vibaya kwani hatutakubaliana nao.

Wengine wanasemaje kuhusu maisha yetu na wanatutendea kitu gani, sio kinachotuumiza, bali kinachotuumiza ni namna tunavyoamini. Kama tunaamini kwamba thamni yetu inapimwa nao, kuwekwa au kuondolewa nao, ni lazima watatupangia tuishi vipi. Hapo tutakuwa hatuna thamani tena kama binadamu kamili au halisi.

1 comment:
Andika Maoni Maoni
  1. Kweli mkuu umenena kweli, thamani ipo ndani mwetu, hata tuchafuliwe vipi mwilini mwetu bado thamani itabakia ile ile.

    Je thamani hiyo inaingiaje ndani mwetu inakujaje, inakuja hivi hivi tu..ni swali hilo kwa kila mmoja wetu.

    ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi