0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Apr 11, 2011

KUNA AMBAO HAWAJUI TOFAUTI YA FEDHA NA UPENDO

Wanahitaji malezi mazuriKuna wazazi ambao pengine kwa kutofahamu hupenda kutamka maneno kama haya mbele ya watoto, ‘bila fedha dunia hii nani atakujua, ni nani atakuthamini,’ watoto waliolelewa wakiyasikia maneno au kauli kama hizi mara kwa mara ndio wale watu ambao leo hawawezi kuthamini mtu mwingine hadi mtu huyo awe na fedha. Ndio wale ambao leo wanapoona mtu ana fedha hata akiwatemea machoni hufurahi na kuona fahari, wale ambao hujipendekeza kwa watu wenye fedha ni sehemu muhimu ya maisha yao.


Hawa ndiyo wale watu ambao wanapokosa fedha huwa kama wagonjwa, ndoa zao huwa ngumu, uhusiano na wenzao huwa mgumu na kukata tamaa huwafikia haraka. Hii ni kwa sababu wazazi wao waliingiza akilini mwao imani hii ya kwamba mtu kutokuwa na fedha si lolote si chochote na kwamba mtu mwenye fedha ndiye binadamu zaidi na anastahili kunyenyekewa kwa sababu thamani yake ni kubwa.


Kuna wakati wazazi huwa wanaamini kwamba mtoto hapaswi kuambiwa hapana kwa kila anachokihitaji kama uwezo wa kumpa kitu hicho upo. Wazazi hawa humpa mtoto kila anachokitaka bila kujali kama kinamsaidia katika makuzi yake au hapana.


Tabia hii ni mbaya na ya hatari sana katika makuzi ya mtoto, kwani mtoto anayelelewa katika mazingira haya huja kuwa na wakati mgumu sana maishani kuhusiana na fedha. Bila shaka umeshawahi kusikia kuona watu ambao hawako tayari kusikia neno ‘hakuna’ hasa kuhusu fedha.


Hawa ni wale watu ambao walipokuwa watoto hawakunyimwa kitu, walipewa na wazazi kila walichohitaji. Kwa sababu hiyo wakakua wakiamini kwamba binadamu anapaswa kupata chochote kila anapokihitaji.


Hebu fikiria kuhusu mtu ambaye anaamini akilini mwake kwamba kila anachohitaji ni lazima kipatikane. Lakini siyo kuhitaji kutoka kwake mwenyewe, la hasha bali kuhitaji kutoka kwa mwingine.


Kuna watu ambao wanapokuomba kitu au fedha na ukawaambia huna, inakuwa tayari umeshajenga uadui mkubwa nao kwa sababu wao hawajui neno ‘hapana’. Wakati wanapohitaji kitu, wazazi wao waliwajaza akilini mwao dhana kwamba mtu ni lazima apate kila anachokiomba au kukitaka kutoka kwa mwingine.


Kama ni ndani ya ndoa wanawake waliopata malezi haya huwa wanasaidia sana kuzilegeza au hata kuzivunja ndoa zao. Kwa kuwa wamelelewa kwa kupewa kila walichokihitaji.


Wanapoolewa huwa hawategemei hata siku moja waume zao kuwaambia ‘sina’. Wanapoambiwa ‘sina’ na waume zao, wanatafsiri kauli hiyo kama ukosefu wa upendo. Kwani wazazi wao waliwapa kila kitu kwa sababu waliwapenda. Hivyo wao wanavyoamnini ni kwamba upendo ni sawa na kutoa kila kinachoombwa na mwingine.


Bila shaka umeshawahi kusikia jinsi baadhi ya watu wanavyolalamika wanaponyimwa kitu walichoomba kutoka kwa mwingine. Hata ukiangalia mtindo wao wa kuomba ni kama vile wanatoa amri au kulazimisha wapewe, iwe ni haki yao au siyo haki yao. Hii ni kwa saabu katika makuzi ao hawakufundishwa kutofautisha kati ya utashi na hitaji.


Ili kupunguza watu wa aina hii katika jamii inabidi wazazi wawe makini sana katika malezi ya watoto wao kuhusu fedha. Mtoto ni lazima aonyeshwe kwa upendo kwamba kuna wakati hawezi kupewa kila anachohitaji. Kuna wakati ni lazima anyimwe kwa upendo kitu anachohitaji hata kama wazazi wana uwezo wa kukipata kirahisi. Kunyimwa huku kutamfanya mtoto aingize akilini dhana kwamba katika maisha siyo lazima tupate kila kitu tunachokihitaji.


Mtoto ni lazima aonyeshwe tofauti kati ya utashi na mahitaji. Kuna mahitaji ya msingi ya binadamu ambayo ni lazima mtu ayapate. Lakini kuna tamaa ya kimwili ambayo humpelekea kutaka kila anachokiona. Ni lazima mtoto aambiwe ni kwa nini inabidi mtu afanye uchaguzi wa kupata mahitaji kwanza na baadae ndiyo afikirie kupata utashi.


Mtoto asipofundishwa kwa vitendo au hata kwa kuelekezwa kuhusu ukweli huu ndipo pale anapokuja kuwa mkubwa hushindwa kujua anunue au atafute nini kwanza na nini baadae katika mahiaji yake. Unaweza kukuta mtu ana gari la bei mbaya asana lakini mahali pa kulala ni tabu. Unaweza kukuta mtu anavaa nguo za bei mbaya sana, lakini kwake hata mahali pa kukaa hakuna. Watu kama hawa hawazuki tu, bali huzushwa na malezi haya mabaya.


Malezi mazuri ni yale ambayo mtoto hupewa au huonyeshwa upendo kukubaliwa na kuungwa mkono kwenye mambo anayoyafanya na siyo yale ya kupewa fedha badala ya mambo hayo. Fedha ikichukua nafasi ya mambo hayo mtoto anapokuja kukua atashindwa kutofautisha kati ya fedha na upendo au mapenzi.


Kama ni mtoto wa kike ndiyo wale ambao hawawezi kukaa na mume ambaye hana fedha. Hawawezi kwa sababu pasipo na fedha hakuna mapenzi au upendo kama walivyolelewa kwa kuamini hivyo.2 comments:
Andika Maoni Maoni
  1. Kaka Shaban! Afadhali umeliandika hili nakumbuka kuna wakati niliandika. kwa kweli asilimia ya watu wa aina hii inazidi kuongezeka yaani watu wanaishi kwa kupenda mali si UPENDO. Na hii ni hatari sana maana mtu anaishi na mtu kwa vile ana mali? anampenda mtu kwa vile ana mali? akiishiwa naye anatoka... Sijui tuendako ni wapi na ni kweli hii inawaathiri sana watoto wetu kwani watoto ni wepesi sana kuiga...TUPENDANA KAMA SISI SI KWA AJILI YA MALI.

    ReplyDelete
  2. kweli kaka kaluse leo umenigusa ulivyoandika hapo juu ni yakweli kabisa kuna wazazi baadhi utakuta mzazi ana watoto wengi tu katika hao watoto wake kuwa nakipato kizuri nawengine hawakujaliwa sasa mzazi atakuwa upande wa yule mwenye nacho atasikilizwa kwakila kitu atakacho sema hata kama akiongea pumba itasikilizwa na kupewa heshima na yule asiye nakitu hata kama kitu atakachozungumza kinapoint hasikilizwi anapuuzwa kisa hana kitu na kumbe hata na yeye hakupenda iwe hivyo hio kitu inanikera sana

    ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi