Huu utakuwa ni msiba mkubwa kwa wanafamilia ya Jitambue, baada ya serikali kuweka alama ya X kwenye nyumba ambayo ndipo kilipo kitivo chetu kikuu cha kukutana na kuelimishana juu ya Utambuzi na Kujitambua.
Kituo hicho ambacho kilianzishwa na Mwasisi wa madarasa haya ya Utambuzi Hayati Munga Tehenan ambaye alifariki hapo mnamo tarehe 5 Mei 2008, kimekuwa ni chachu ya mabadiliko ya kitabia na mienendo kwa wanachama wake na wapenzi waliokuwa wakihudhuria madarasa hayo na wale waliokuwa wakisoma vitabu na magazeti ya Jitambue.
Baada ya kifo cha mwasisi huyo, ni madarasa pekee ndiyo yaliyokuwa yamebaki pamoja na blog hii yaliyokuwa yakiendelea kuelimisha juu ya maarifa haya ya utambuzi.
SIku ya Alhamisi ya tarehe 7 April 2011, tulikutana katika kituo hicho ili kujadili mustakabali wa umoja wetu na kuweka mikakati ya kuboresha uendeshaji wa kituo chetu ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kuhama katika jengo hilo kabla ya utekelezaji wa bomoa bomoa.
Katika mjadala huo Katibu wa kikundi Dada Tafsiana alieleza changamoto kubwa mbili zinazoikabili familia yetu ya Jitambue.
Kwanza alizungumzia juu ya wanachama wengi kutojihusisha katika shughuli mbalimbali za umoja wetu, inawezekana wakawa aidha wamejitoa, au wameamua tu kukaa pembeni kwa sababu zao wanazozijua. Alibainisha pia kuwa mahudhurio kwa wanachama katika vikao muhimu vya maamuzi ni hafifu mno kiasi kwamba viongozi wanashindwa kupitisha maamuzi mbali mbali kwa kuhofia kuonekana kuungwa mkono na idaidi ndogo ya wanachama. Akitoa mfano alisema kuwa kati ya wanachama 70 aliowatumia ujumbe wa simu ya kiganjani kuwaalika katika kikao hicho ni wanachama 9 tu ambao tulihudhuria.
Pili alizungumzia juu ya kukwama kwa miradi mbalimbali ya umoja wetu kutokana na ukosefu wa fedha, hiyo imekuwa ni changamoto kubwa kwa sababu wanachama wameshindwa kuwasilisha michango yao ambayo ndio chanzo kikuu cha mapato katika kugharamia uendeshaji wa kituo chetu.
Mwenyekiti ndugu Fred Mbeyela Aliwaomba wanachama waliohudhuria katika kikao hicho kutoa mawazo yao ya namna ya kukiendesha kituo chetu ambacho kwa kweli kinaonekana kukosa mwelekeo kwa sasa.
Wanachama tuliohudhuria tulikubaliana kwa pamoja kubadili muundo wa uendeshaji wa kituo chetu.
Kwanza tulikubaliana kwamba tutafute ofisi mahali pengine ili kupisha bomoa bomoa
Pili tulikubaliana kwamba katiba ya umoja wetu ibadilishwe na kuboreshwa zaidi na pia kuwe na masharti ya uanachama yatakayowafanya wanachama wawajibike katika umoja wetu.
Nitaendelea kuwajuza zaidi kila hatua tutakayopiga katika jitihada hizi tuliyoianzisha ya kutaka kuboresha kituo chetu cha Wanafamilia ya Jitambue
Mimi naitwa Lucas Haule. Nimekuwa mwanachama wa FAJI kwa muda mrefu, lakini alipouacha mwili wmasisi wetu, nikawa pembeni.
ReplyDeleteIla nimefurahi kuwa iletiba ya akili bado inapatikana, naomba kuwa nashiriki na kushirikishwa. No yangu ni 0754805111.