Hivi sasa katika jamii yetu kuna kundi la wanawake ambao wana watoto
lakini hawajaolewa lakini pia lipo kundi kubwa la wanawake ambao wako kwenye
ndoa au mahusiano kwa muda mrefu lakini hawana watoto, hawa wamekuwa ni wahanga
wa kubwa wa makanisa na hizi kliniki za tiba mbadala zilizosheheni hapa nchini
zikidai kwamba zinasaidia wanawake kupata watoto.
Kundi hili la wanawake ambao hawajajaaliwa kupata watoto kwenye ndoa
zao wamejikuta wakipoteza fedha nyingi sana ili kupata watoto.
Dunia yetu imebadilika, mitindo ya maisha nayo imebadiliaka, mila desturi
zetu nazo zimebadilika pia. Zamani vijana walikuwa wanalazimishwa na wazazi
kuoa mapema na kama kijana akifikisha umri fulani hajaoa alikuwa anaonekana mtu
wa ajabu tofauti na siku hizi shinikizo la vijana kuoa halipo tena kama zamani
vijana wanawajibika kuamua wenyewe ni wakati gani waoe kwa sababu hata hivyo
huduma ya ngono inapatikana hovyo.
Kwa upande wa wanawake nao shinikizo limebaki kwao, kwa kadiri umri
unavyosonga ndivyo wazazi, jamii iliyomzunguka inavyozidi kumpa shinikizo la
kuhoji kwa nini haolewi huku wanaume wakizidi kubaki huru na maamuzi yao.
Kwa wale ambao waliamua kuzaa kabla ya ndoa iwe ni kwa bahati mbaya au
kwa kukusudia ambao wamebaki kuwa na watoto kabla ya ndoa wanao mtihani mwingine
wa kupata wenza. Wanaume wengi wanashikwa na kigugumizi cha kuoa wanawake
waliokwisha kuzaa.
Lakini wanaume hao hao unaweza kukuta nao wana watoto waliowazaa nje ya
ndoa wakawatelekeza kwa mama zao. Hapo ndipo ilipo hadithi ya kuku na kifaranga
haijulikani kipi ni kipi.
Bila shaka wengi wetu tumeshakutana na wanawake wenye kutafuta watoto
wakiwa tayari umri umeshawatupa mkono. Ukweli ni kwamba, umri wa kupata watoto
kwa wanawake umepungua sana tofauti na zamani.
Hivi sasa kutokana na mtindo wa maisha na vyakula tunavyokula watoto wa
kike wanavunja ungo mapema hivyo wanaanza kushiriki ngono mapema, na hivyo
kutokana na utoaji wa mimba holela au kutumia vidonge vya kuzuia mimba mapema
wengi wamejikuta wakikosa uzazi pale wanapokata shauri ya kutafuta watoto.
Lakini pia maradhi ya ngono yaliyoachwa kwa muda mrefu kabla ya kutibiwa
yameathiri via vya uzazi vya wasichana wengi na hivyo kupoteza uwezo wa kuzaa.
Lakini pia vyakula tunavyokula na madawa tunayotumia yanayotibu maradhi
mbalimbali nayo yana mchango katika tatizo hilo.
Sasa basi labda changamoto tuliyo nayo kwa sasa ni je kuna haja kweli kwa
wanawake kuwa na ulazima wa kusubiri mpaka kufunga ndoa ndipo wapate watoto au
wanaweza kupata watoto kabla ya ndoa kutokana na kuepuka umri kuwatupa mkono na
kupoteza kabisa uwezo wa kuzaa.
Je jamii inawachukuliaje wanawake wenye watoto kabla ya ndao? Je
hawastahili kuolewa?
No comments:
Andika Maoni Maoni