Kwa kawaida mtu anayeamini kwamba, ni dhaifu, hujaribu kwa kila njia kuficha udhaifu wake, na moja ya njia hizo ni kujikweza ili kujaribu kumshusha yule ambaye anadhani anamzidi. Mtu asiye na nguvu anaweza kujitahidi kupiga kelele, kupiga ‘mikwala’ na vitisho, na watu wanapomwogopa, hupata nafasi ya kuwakandamiza hadi pale inapotokea bahati watu hao wakamshtukia kwamba hana nguvu anazodai anazo. Hata hivyo, ule woga kwa mtu huyo utaendelea kuwepo kwa watu wengi.
Kwa miaka mingi mwanaume aligundua kwamba, ni dhaifu mbele ya mwanamke na katika juhudi za kufidia pengo hili alipitiliza mipaka na kujikuta anafanikiwa kumkandamiza mwanamke. Eneo ambalo mwanaume anaweza kusema ni bora kuliko mwanamke labda ni mabavu ya kimwili, ambayo kwa bahati mbaya kwenye zama hizi hayana tena maana, yamepitwa na wakati.
Ukiangalia maeneo mengine yote, mwanamke ndiye bora zaidi. Mwanamke huishi miaka mingi zaidi ya mwanaume (kati ya miaka mitano hadi kumi) na mwanamke huugua au kupata maradhi kidogo zaidi kuliko mwanaume. Wanaume wengi zaidi, kwa kiasi cha mara mbili zaidi hupata matatizo ya kiakili ukilinganisha na wanawake, huku idadi ya wanaume wanaojiuwa ikiwa kubwa zaidi kuliko ile ya wanawake.
Ni kweli, mwanaume anaweza kuringia mabavu yake, lakini huo siyo ubora ambao binadamu anatakiwa kuuringia sasa hivi, kwani unahusu zaidi wanyama kuliko binadamu. Enzi za kuuwa wanyama kwa mawe, mabavu yalikuwa na maana, si leo. Mwanaume kwa karne kadhaa amejitahidi kutumia mabavu yake kumwonyesha mwanamke kwamba, yeye siyo dhaifu. Kwa bahati mbaya mwanamke naye akadhani ni dhaifu. Yeye kukosa mabavu akadhani ni udhaifu. Kwa wakati huo ilikuwa ni sahihi kwa sababu binadamu aliishi kama mnyama. Mtu aliyeheshimiwa alikuwa ni yule aliyekuwa na nguvu za kuuwa mnyama kwa jiwe, lakini bila shaka, leo mambo ni tofauti.
Hebu ona, hadi leo mwanaume anaweza kuhatarisha maisha yake au hata kupoteza maisha akijaribu kutafuta njia za kumfanya mwanamke amwone kuwa ni wa maana. Atasema uongo, atajikweza, atajifaragua, akitafuta kukubaliwa na mwanamke. Huu ni udhaifu mkubwa na unaonyesha ni kwa kiasi gani jinsia hii isivyojiamini. Udhaifu huu na mwingine ndiyo ambao mwanaume amekuwa akitafuta kuuficha ili mwanamke asiuone, ambapo ameamua kumkandamiza kwa mabavu.
Mwanazuoni mmoja wa utambuzi alipata kusema, wale wanaume wote ambao walijitahidi kuifanya dunia hii kuwa mahali penye kupendeza, walikuwa na tabia ambazo ni wanawake zaidi wanaokuwa nazo. Walikuwa na huruma, upendo, unyenyekevu, kusamehe, kusaidia na kujali. Leo hii mwanaume ukitaka kuitwa mwanamke, onyesha huruma, onyesha upendo, onyesha usamehevu. Unaweza kuona ilivyo, kwamba, bila kuonyesha mabavu manaume anahisi kuumbuka.
Kuna wakati tulikuwa tukizungumza na ndugu yangu ambaye alikuwa anatarajia kufunga ndoa. Mmoja kati ya ndugu zangu waliokuwepo alisema, ‘inabidi huyo mchumbako tumuone, kwa upole wako anaweza kukukalia ukimwoa.’ Unaona? Kinachomlinda mwanaume ni kitu kimoja tu, kuwa mbabe na mkali, basi. Hana silaha nyingine na hajawahi kuwa nayo, hivyo akiiachia hii ya mabavu, anajua atakuwa amekwisha……
No comments:
Andika Maoni Maoni