Leo nina kisa nataka kuwasimulia.
Bwana mmoja alikuwa amekwenda kazini
kama ilivyo kawaida yake, akiwa ndio anafika kazini akapigiwa simu kujulishwa
kwamba nyumba yake inaungua.
Bwana yule akarudi nyumbani haraka
huku akijaribu kuwasiliana na watu wa zima moto. Alipofika nyumbani akaikuta
nyumba yake ndio inazidi kuteketea kwa moto na hakuna kilichosalimishwa hata
kitu kimoja na askari wa zima moto walikuwa hawajafika katika eneo la tukio.
Basi yule bwana akawa amesimama
akishuhudia nyumba yake ikiteketea asijue la kufanya. Ulikuwa ni msiba mkubwa
sana kwake, kwani ile nyumba ilikuwa ni kubwa na ilimgharimu kiasi kikubwa cha
fedha.
Wakati akiwa bado amesimama pale nje
akiwa anashuhudia lile tukio, mwanae mmoja wa kiume alimsogelea na kumshika
bega, kisha akamwambia ‘usijali nilishaiuza tangu jana!, nilikusikia wewe na
mama mkilalamika kuwa hii nyumba ni kubwa sana na mlikuwa hamuihitaji tena,
nikakutana na tajiri mmoja mwekezaji toka nje ambaye alikubali kuinunua kwa
gharama yoyote’
Ghafla sura ya baba yake ikagubikwa
na tabasamu la furaha na kumkumbatia mwanae na kumpongeza kwa kwa uamuzi mzuri
alioufanya. Mpaka hapo hakuna kilichobadilika: Nyumba ilikuwa bado inaungua
lakini hakuwa mmiliki wa nyumba ile tena, kwa nini ajali, wakati haimuhusu?
Wakati baba akiendelea kumpongeza
mwanae huyo, mwanae mwingine mdogo wa kiume aliwasogelea uso wake ukiwa
umegubikwa na huzuni, Baba alimwangalia mwanae kwa mshtuko, ‘nini tena?’
“Ni kweli mwekezaji mmoja alikuwa
anataka kuinunua hii nyumba” yule kijana alisema, akimwambia baba yake. “Lakini
mkataba wa mauzo ulikuwa bado kusainiwa na pande mbili, kwa hiyo hatuna cha
kuuza.”
Baada ya kupata taarifa ile, yule
baba aliishiwa na nguvu kabisa, na kukaa chini, mwili wote ulikufa ganzi na
hakuwa na la kusema, akabaki kuwaangalia wale wanaye asiamini masikio yake.
Bado hakuna kilichobadilika kwani
nyumba bado ilikuwa inaungua. Kilichobadilika ni taarifa tu.
Wakati nyumba yake inaungua
aligubikwa na huzuni. Alipopata taarifa kuwa nyumba ilishauzwa kwa mtu
mwingine, ingawa bado ilikuwa inaungua alifurahi sana kwa sababu haikuwa yake
tena. Zilipokuja taarifa nyingine toka kwa mwanae mdogo kuwa mkataba wa mauzo
ulikuwa bado haujasainiwa, baba akataharuki na kurudi kwenye majonzi tena kwa
sababu kumbe nyumba bado iko mikononi mwake.
Akiwa bado amegubikwa na simanzi,
aliyekuwa mnunuzi wa ile nyumba alifika. “Najua hii ni bahati mbaya sana kwako,
kwa nyumba yako kuungua, hata hivyo nilikuwa nahitaji hii ardhi tu, kwa hiyo
nitalipa kiasi kile kile cha fedha tulichopatana”
Kusikia hivyo, uso wa yule baba,
ukabadilika tena na kugubikwa na furaha kubwa isiyo kifani, kwani nyumba
haikuwa mikononi mwake tena, hakuna haja kusikitika.
Naamini mpaka hapo mmeona mwili
unavyopata mabadiliko kulingana na jinsi tunavyotafsiri matukio tunatoyapata.
Ikiwa tutatafsiri tukio vibaya kwa kuanagalia upande mmoja wa hasi, ni wazi
tutapata maumivu ya kihisia.
Kwa mfano wa tukio hili la nyumba
kuungua, awali yule mzee alikuwa analalamika kuwa ile nyumba haihitaji tena,
kwa kuwa ni kubwa na labda ilikuwa ina muundo wa kizamani, kwa hiyo hakuipenda.
Alikuwa anatamani kujenga nyumba mpya ambayo ndiyo aliyokuwa akiihitaji.
Tumejifunza jinsi mawazo yalivyo na
nguvu, kwamba kile tunachofikiri ndicho kinachofanyiwa kazi na akili ya kina
(Subconscious mind), kwa hiyo, tukio lile ilikuwa ni matokeo ya kile alichokuwa
anafikiri. Lakini kwa bahati mbaya matokeo ya fikra zetu hayaji kwa namna
tunavyotaka, yanakuja kwa njia ya ajabu mno ambayo mwenye werevu wa kihisia
pekee ndiye atakayeweza kung’amua.
Akili ya kina huwa haileti majibu
yakiwa yamevaa suti, mara nyingi yanakuwa na sura isiyovutia na yenye kutia
kinyaa, usipoigundua, umekwisha. Je ni mara ngapi tunapiga teke yale mambo
yanayofanyiwa kazi na akili ya kina na kuja mbele yetu yakiwa na sura kama hii?
Je wewe umejifunza nini juu ya kisa
hiki?
Je hofu na maumivu ya kihisia
tunayopata ni kutokana na tukio au tafsiri inayokwenda akilini kwetu?
UFAFANUZI ZAIDI:
Kwa ufafanuzi zaidi ni kwamba tunapaswa kujipa majibu chanya
pale tunapopata jambo linalotutatiza, kwani hiyo ndiyo njia pekee
itakayotufanya tuishi kwa amani.
Kwa mfano iwapo utampigia mpenzi wako simu halafu hapokei na
simu yake ikawa inaita mara kadhaa bila kupokelewa, hapo unapaswa kujipa jibu
kwamba, "labda atakuwa ameiweka simu kwenye chaji na yeye yuko nje ya
hapo nyumbani au ofisini kama ni mfanyakazi."
Kama unadhani atakuta missing call zako na kukupigia lakini
asifanye hivyo, basi jipe jibu kwamba, "Labda hana salio"
Kama ukipiga simu tena ukakuta simu yake iko bize muda wote
anaongea na mtu mwingine, jipe jibu kwamba, "Labda anaongea na wazazi wake au bosi wake kama ni
mfanyakazi" hata kama ni saa sita usiku hilo jibu linatosha
kujifariji na kuepuka msongo wa mawazo!
Kama ukipiga tena ukakuta simu imezimwa, basi jipe jibu
kwamba, "Labda simu yake imeisha chaji"
Kama ukipiga simu baadaye ukakuta inaita halafu akapokea
lakini akakupa majibu yenye kukera, basi jipe jibu kwamba, "labda
amekumbwa na msongo wa mawazo"
Je si mmeona jinsi ilivyo rahisi kuepuka kukerwa na mtu kwa
kujipa majibu chanya?
Dumisha furaha yako kwa kujipa majibu chanya na kuepuka maradhi yatokanayo na kusongeka.....
Dumisha furaha yako kwa kujipa majibu chanya na kuepuka maradhi yatokanayo na kusongeka.....
No comments:
Andika Maoni Maoni