Siyo kila dalili ya mwanaume kupenda ni ya kweli…!
Kuna wakati ambapo, wanawake wanajikuta wakikabiliwa na swali la, je, mwanaume huyu ananipenda kweli? Hii hutokea pale anapokutana na mwanaume ambaye, huenda amevutiwa naye. Pengine mwanaume naye anaweza kuonesha kuvutiwa na mwanamke huyo.
Kwa hiyo, mwanamke hujiuliza kama akubali ombi la mwanaume huyo na kukubali kuzungumza naye au kuanzisha naye uhusiano, kama mwanaume atakuwa amezungumza naye kuhusu jambo hilo. ni kweli kwamba, kuna ugumu kwa mwanamke kujua hasa ni kwa namna gani anaweza kujua kwamba, huyo mwanaume amempenda kweli au hapana.
Kuna vitu vingi ambavyo vinaweza kuwa ni dalili ya kumpenda mwanamke, lakini wakati huo huo vinaweza visiwe.
1. Hebu tuchukulie kwamba, mwanaume ameonesha kuwa na tabia tunazoziita nzuri. Labda amekumbuka kirahisi jina la mwanamke, ameonesha kuwa msikilizaji mzuri, ameonesha kuwa anajali kuhusu kinachosemwa na mwanamke, na amekuwa anamuuliza maswali kwa dhati na utulivu. Hapa mwanamke anaweza kuamini kwamba, huyu mwanaume anampenda. Lakini ukweli huenda ukawa ni kinyume chake. Inawezekana huyo mwanaume ni muungwana tu, na anaonesha tabia hizo kutokana na uungwana wake na siyo kutokana na kumpenda kimapenzi mwanamke.
2. Kuna watu ambao wana upendo, wamekomaa kihisia na wanajua kuhusiana vizuri na watu. Hii haina maana kwamba, kumwonesha mtu tabia hizo, kuna maana ya kumpenda au kumpenda sana mwanamke. Dalili hizi ni nzuri na inawezekana zikawa zinaonesha mwanaume kumpenda mwanamke, lakini mwanamke asilichukulie jambo hilo kwa namna hiyo.
3. Mwanaume anaweza kuonesha kuwa na udadisi kuhusu mwanamke kwa maana kwamba, kutaka kujua mambo yake, kumfuatilia au kuulizauliza kuhusu habari za mwanamke. Hii haina maana kwamba mwanaume amempenda kimapenzi. Inawezekana mwanaume akawa amevutiwa kimapenzi na mwanamke ndiyo maana akaonesha tabia hizo, lakini siyo lazima iwe hivyo. Kumbuka kwamba, mwanaume anaweza kuvutiwa na mazungumzo ya mwanamke, akavutiwa hata na namna alivyo usoni, hivyo akapenda kuzungumza naye lakini siyo kwa sababu anampenda.
4. Kuna wanaume ambao wana wake au wapenzi, lakini wanajisikia vizuri kusikiliza wanawake wengine au kujua tu habari za wanawake wengine, bila kuwa na haja ya kuanzisha uhusiano nao. Mwanaume anapompa mwanamke ‘ofa’ hasa ya chakula cha mchana au usiku, ni dalili ya wazi ya kuvutiwa naye. Hapa kuna uhakika mkubwa zaidi, labda tu kama mazungumzo yanayotajwa kufanywa wakati huo wa chakula yanafahamika, na ni ya shughuli maalum. Kwa hiyo ‘ofa’ ya chakula ni dalili nzuri na yenye uhakika. Lakini kuna jambo ambalo ni muhimu kwa mwanamke kulifahamu katika hali kama hii. Kuna wakati mwanaume kumpa ‘ofa’ mwanamke kwa chakula cha mchana au jioni, kunaweza kusiwe na maana ya moja kwa moja kwamba, uhusiano utaundwa. Inawezekana katika kutoka outing huko, mwanaume akaghairi. Kwa wengine huchukua muda hadi kuamua kuhusu kuunda uhusiano au hapana.
5. Hata mwanaume kuamua kumpeleka mwanamke kwa familia yao na kumtambulisha kama rafiki yake, ni hatua yenye kuonesha kwamba, mwanaume ameamua kumpenda mwanamke huyo. Lakini wakati mwingine hii inaweza ikawa ni janja yake kutaka tu kumthibitishia mwanamke ili amhadae vizuri, na wala hakuna maana ya uhusiano wa kudumu.
6. Kuzungumza kwa pamoja kuhusu masuala ya baadaye ya kiuhusiano, kama vile, idadi ya watoto na mambo mengine ambayo mara nyingi huzungumzwa na watu ambao tayari wako kwenye uhusiano ni dalili ya mwanaume kuvutiwa mwanamke. Lakini tatizo la jambo hili ni kwamba, kuzungumza masuala ya baadaye inaweza kuwa ni njia ya mwanaume kutaka kujisikia au kujua jinsi inavyokuwa katika mambo hayo. Inaweza kuwa pia ni njia yake ya kutaka kupima wanawake wanavyosema kuhusu masuala hayo. Lakini inaweza ikawa mwanaume huyo anatafuta kujua misimamo ya mwanamke huyo ili hatimaye afanye uamuzi. Kwa hiyo, bado haioneshi kuwa amevutiwa na kuamua tayari.
Mara nyingi wanawake hudanganywa na dalili fulani zinazooneshwa na wanaume wakati wanapoanza kuzoeana nao. Dalili hizi huwafanya kuamini kwamba, wanaume hao wamewapenda tayari, wakati siyo kweli. Kwa kuangalia baadhi ya dalili hizo kama nilivyozitaja, mwanamke anaweza kuwa makini wakati anapoanzisha uhusiano, ili asikurupuke na kujikuta amedanganyika. Ni kweli, kuna wakati ni dalili zinasema kweli, lakini kuna wakai zinadanganya kuhusu kupenda au kupendwa.
No comments:
Andika Maoni Maoni