0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Jun 14, 2009

KWA NINI TUWE NA CHUKI DHIDI YA WENGINE?: MAJIBU KWA BWANA FRED KATAWA

Rais mstaafu wa Marekani George W Bush, Je alikuwa na chuki dhidi ya waislamu?

Hivi karibuni nimeandika makala inayozungumzia juu ya watu kujipenda zaidi na kuipa kichwa cha habari kisemacho “KWA NINI TUWE NA CHUKI DHIDI YA WENGINE?”
Miongoni mwa wachangiaji waliojitokeza kuchangia katika makala hiyo, alijitokeza msomaji na mtambuzi mwenzangu Bwana Fred Katawa na kunipa changamoto.
Katika maoni yake Bwana Katawa amedai kuwa mtu anayejipenda iwe kwa kiasi au zaidi hawezi kuwa na chuki na mtu mwingine kwa kuwa upendo upo ndani yake.

Kwa maneno yake mwenyewe Bwana Katawa alisema, naomba nimnukuu,

“Mimi nina mtizamo tofauti na dhana nzima ya kujipenda.Mtu anayejipenda iwe kwa kiasi au zaidi hawezi kuwa na chuki na mtu mwingine kwa kuwa upendo upo ndani yake .Ninavyojua mimi ni kuwa upendo huanza ndani ya mtu kisha hujionyesha kwa wengine kupitia matendo na kauli za mtu husika.Kama mtu ana chuki na wengine au hapendi wengine wafanikiwe siwezi nikamuona kuwa anajipenda zaidi bali nitamchukulia kuwa ni mtu anayejichukia zaidi na chuki hiyo hujidhihirisha pale anapowachukia wengine kupitia kauli zake na matendo yake.” Mwisho wa kunukuu.
Labda nimuulize Bwana Katawa, Hivi mtu anayetaka yeye peke yake ndiye afanikiwe maishani, yeye peke yake ndiye anayepata sifa na yeye peke yake ndiye anayepewa heshima, atakuwa anajipenda au anajichukia?

Au mtu anayetaka watu wengine wawe chini yake, kwa maana kwamba wasifanikiwe, kwa kuwa kufanikiwa kwao kutakuwa na maana ya kumzidi yeye, naye atakuwa anajipenda au anajichukia?

Nimeuliza hivyo makusudi ili kutaka kuuweka mjadala huu sawa, kwani kuna tofauti ndogo sana katika tafsiri ya namna tunavyolichukulia neno kujipenda zaidi na kuwachukia wengine.
Kama unauzungumzia upendo, tafsiri yako ni sahihi kwa sababu huwezi kumpenda mwingine kama wewe mwenyewe hujipendi,
Kujipenda hapa sizungumzii kule kujipenda kwa mtu kuvaa vizuri, kwa maana ya suti au nguo za gharama, kula vizuri, kulala mahali pazuri na mambo mengine yanayofanana na hao.
Nazungumzia kujipenda kwa maana ya mtu kujikubali kama alivyo kujikubali yeye mwenyewe hata kama ana kasoro.

Kama utakuwa unazungumzia kujipenda kwa muktadha huo, basi hilo sina ubishi nalo kabisa, nakubaliana na wewe.

Lakini kama unazungumzia chuki na roho mbaya, basi tafsiri yako inaweza ikaleta maana tofauti na mada yangu ilipolenga, labda kama utakuja na neno tofauti ili kuwasilisha mada yangu bila kupoteza maana niliyokusudia, kwa sababu mtu anayejipenda binafsi na kuwakataa wengine sidhani kama atakuwa hajipendi, na hivyo chuki aliyo nayo kuihamishia kwa wengine.

Maneno kama, “watu wengine hawataki kuwaona wengine wakipata, watu wengine wana roho mbaya, watu wengine wana wivu, watu wengine hawawapendi wenzao, au watu wengine wanataka wapate wao wenyewe” yote hayo yanawakilisha neno kujipenda, kwani kujipenda kwa mwanaadamu kuna maana ya yeye kufanikiwa zaidi ya wengine, yeye kuwa juu ya wengine au yeye kuheshimiwa na kuogopwa na wengine kwa kuwa anawazidi wengine.

Kwa kumalizia Bwana Katawa niliposema kuwa naweza kukubaliana na wewe au kutokubaliana na wewe ni kwamba, ulikuwa sahihi kwa mtazamo nilioueleza hapo juu na pia inawezekana hukuwa sahihi kwa mtazamo wangu.
Mada hii ni ndefu na inaendelea, kwa hiyo sijaifunga, kama una mtazamo tofauti nakukaribisha kuweka changamoto yako hapa, na kama yupo msomaji mwingine ambaye ana mtazamo tofauti, basi na yeye namkaribisha ili aweke changamoto yake hapa kwa ustawi wa wanautambuzi wote.

2 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Nami nina mtazamo tofauti,nijuavyo mimi
  mtu yeyote mbinafsi hana upendo yaani hajipendi na pia hawezi kuwapenda wengine.
  Kuliweka bayana Kaluse unazungumzia
  ubinafsi na si upendo.

  ReplyDelete
 2. Bwana Kaluse nimekusoma tena.Nimekuelewa ulivyoichambua mada yako sehemu hii ya pili.Kwa kuwa umetueleza kuwa mada hii ni ndefu na inaendelea pengine nitakuwa na mengine ya kuchangia mwishoni mwa mada hii.

  Hapo juu umeonekana kuelezea kidogo juu ya mtu anayejipenda zaidi na yule mtu mwenye upendo.

  Kama utapenda au utakuwa na muda,naomba utueleze tofauti au sifa walizonazo watu wafuatao kwa kadiri unavyojua.

  Unaweza kumtambuaje mtu anayejipenda zaidi,mtu anayejichukia au mtu mwenye upendo?

  Ni sifa zipi zinazofanana kati ya mtu anayejipenda zaidi na yule anayejichukia?.Na ni sifa zipi zinazowatofautisha?

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi