0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Jun 7, 2009

KWA NINI TUWE NA CHUKI DHIDI YA WENGINE?

Hata kupendeza kwa wengine hujenga chuki
Hivi karibuni nimepata bahati ya kuzungumza na kijana mmoja ambaye ni mwanafunzi katika madarasa yetu ya Utambuzi pale Kimara Rombo.

Kijana huyu anakiri kuwa Gazeti la Jitambue kwa kiasi kikubwa ndilo lililombadilisha na kuwa kama alivyo sasa, anabainisha kuwa tangu Gazeti hilo liache kuchapishwa baada ya Mwandishi wa gazeti hilo Hayati Munga Tehenen afariki, anaona kama vile amepungukiwa na kitu.

Hata hivyo anasema kuwa ujio wa blog hii ya Utambuzi na Kujitambua umeweza kwa kiasi fulani kuziba pengo la Gazeti la Jitambue ingawa sio wasomaji wengi waliokuwa wakisoma gazeti hilo wana uwezo wa kuwa na uwezo wa kusoma blog hii.
Nakumbuka siku moja kijana huyo alinipigia simu akiniomba tuonane ili tubadilishane uzoefu na baada ya kukutana kwetu, nilimshauri ajiunge na madarasa ya Utambuzi pale Kimara ili kujiongezea uzoefu wa masuala haya ya utambuzi kitu ambacho alikiafiki na kujiandikisha.

Katika mazungumzo yetu kijana huyo alinisimualia jinsi maisha yake ya nyuma yalivyokuwa kabla ya kujifunza haya mambo ya utambuzi.
Alikiri kuwa alikuwa ni mtu mwenya hasira za ziada na asiye na subira.
Kwake yeye kugombana na mtu lilikuwa ni jambo la sekunde tu, alikuwa hawezi kumvumilia mtu pale anapomletea ujinga au kumkosea japo kidogo.

Anasema baada ya kumaliza elimu yake na kuingia katika ajira alijikuta akiwa mdandiaji wa ajira, yaani kwa muda wa mwaka mmoja alijikuta akiwa amepita katika kampuni zaidi ya tano katika vipindi tofauti tofauti.
Tatizo kubwa lilikuwa ni kutovumilia majungu na kusengenywa.
Wakati naingia kwenye ajira miaka ya tisini nilikuta ajira nyingi zimeshikiliwa na Watanzania wenye asili ya Kiasia, kwani ajira za hawa wenzetu zilikuwa ni ngumu na zilizojaa ubaguzi kupindukia. Alisema kijana huyo.

Alikutana na watu ambao kutokana na labda njaa zao wamejikita katika kuwafanyia wengine fitina ili kujipendekeza kwa wajiri hao wanaopenda fitina na majungu kazini, lengo kubwa likiwa eti kulinda maslahi yao, kwani kwao kufitiniana ni kinga tosha ya kuhami maslahi yao.

Kijana huyo anabainisha kuwa katika muda mfupi aliofanya kazi katika makampuni hayo mengi yakiwa ni ya Waasia ndipo alipokuja kugundua kuwa kuna wanaadamu wenye chuki na roho mbaya hasa.

Kuna wakati alijikuta akimpiga mtu au kupigana nje ya kazi kutokana na kutovumilia ujinga wa hao wapambe ambao walikuwa wako tayari kumfitini mtu kwa kumsingizia jambo ilimradi kumuharibia.
Kutokana na utendaji wake mzuri wa kazi na nidhamu aliyokuwa nayo, alikuwa na bahati ya kupendwa na kila bosi aliyewahi kufanya kazi naye, lakini kumbe hiyo ilikuwa haiwafurahishi baadhi ya wenzake aliowakuta pale kazini na hivyo kumzulia jambo na kumsabishia matatizo.
Kutokana na tabia ya kutomvumilia mtu alijikuta akiingia katika mzozo na wenzake na hatimaye kupoteza ajira.

Siku moja alimtembelea rafiki yake mmoja ambaye alimuahidi kumtafutia kazi, kwa bahati mbaya alipofika hakumkuta bali alimkuta mkewe ambaye alimkaribisha sebuleni na kumwambia kuwa mumewe ametoka mara moja na angerejea muda si mrefu. Wakati akiendelea kumsubiri rafiki yake huyo huku akiangalia TV, mara aliona gazeti lililoandikwa Jitambue.

Ukweli ni kwamba alikuwa akiliona gazeti hilo mitaani lakini hakujishughulisha kulinunua kwa kudhani ni magazeti ya udaku, kwa kuwa hakuvutiwa na vipindi vilivyokuwa vikioneshwa kwenye TV, hakuwa na jinsi aliamua kupitishia macho lile gazeti japo kupoteza muda.

Habari alizokutana nazo humo ziilimfumbua macho na kumzindua. Wakati akiwa bado amezama kwenye gazeti hilo mara mwenyeji wake akafika. Alitumia muda huo kuzungumza na mwenyeji wake juu ya yale aliyoyasoma katika gazeti lile na kwa kuwa rafiki yake huyo alikuwa ni msomaji mzuri wa gazeti hilo alimsimulia uzoefu wake juu ya gazeti hilo na jinsi hata yeye lilivyoweza kumbadilisha kimaisha.
Tangu siku hiyo akawa ni msomaji wa gazeti hilo, ana alipopata kazi, hakupata tena taabu ya kuishi na watu wenye tabia alizokuwa akizikimbia. Sio kwamba hakuwakuta watu wa aina hiyo katika kampuni hiyo aliyoajiriwa, la hasha alikutana nao tena wengine walikuwa na tabia za ajabu kupindukia, alichofanya ni kubadili namna yake ya kufikiri na kumchukulia mtu kama alivyo. Anasema siri kubwa aliyojifunza ni kwamba sisi kama wanaadamu hatuwezi kumbadilia mtu kitabia bali kila mtu anaweza kubadili tabia mwenyewe akitaka.

Hata hivyo hajutii yote yaliyotokea na wala hawalaumu waliokuwa wakimfanyia hivyo, kwani yote hayo ilibidi yatokee ili ajifunza jambo.

Kuna wakati niliwahi kuandika katika mojawapo ya makala zangu kuwa sisi binaadamu tunajipenda sana, katika kujipenda kwetu ndio maana tuko tayari kuwaona wengine wakiumia ili sisi tuone raha, yaani kuna watu wengine hufurahi sana kuwaona wengine wakiumia kihisia.

Kwa kujipenda kwake binadamu anataka aone kuwa yeye peke yake ndiye anafanikiwa maishani, yeye peke yake ndiye anayepata sifa na yeye peke yake ndiye anayepewa heshima.

Ili hayo yatimie ni lazima binaadamu wengine wawe chini yake, kwa maana kwamba wasifanikiwe, kwani kufanikiwa kwao kutakuwa na maana ya kumzidi yeye.

Wote tunajua maana ya chuki, ingawa kuna uwezekano mkubwa wengi wetu hatujui ni kwa kiasi gani chuki dhidi ya wengine hutuharibia maisha yetu na kutufanya kila siku kubaki katika hali duni tuliyomo.

Hebu jaribu na wewe kufanya utafiti mdogo. Ni mtu au watu gani ambao wewe unawafahami vizuri kuwa wana chuki dhidi ya watu wengine?
Ninaposema chuki nina maana ya watu ambao wenzao wakipata wao hujisikia vibaya, wenzao wakifanikiwa wao huponda na kudharau mafanikio yao, wenzao wakijitahidi kupanda kimaendeleo wao huwashusha, wenzao wakisifiwa kwa jambo zuri wao hujitahidi kuwaharibia majina na tabia nyingine za namna hiyo.

Hebu waangalie watu hao ambao wana tabia kama hizo, halafu uangalie au upime kiwango cha maendeleo yao, unaweza ukapima pia aina ya maisha wanayoishi. Bila shaka utagundua kwamba kwa kiwango kikubwa ni watu ambao wana maisha duni siku zote na ni watu ambao maisha yao yanaonekana yamejaa nuksi na hawana furaha katika maisha. Sisemi hata hivyo kwamba watu wote wasio na kitu wana chuki, au sisemi kuwa watu wote wenye uwezo hawana chuki, hapana. Kuna watu wenye chuki lakini ambao wana uwezo, ingawa uwezo huo kwa kawaida huzongwa na mikosi tele na kukosa amani ya nafsi.

Kuna watu wasio na kitu ambao hawana chuki hata asilani, lakini hawa maisha yao siku zote yamejaa matumaini na furaha ya kweli
Chuki kwenye maisha ina kazi moja tu, nayo ni kuhakikisha kwamba anayeifuga hata siku moja hapandi juu kimafanikio, na anaishi kwenye fadhaa, wasiwasi na kukosa furaha siku zote.

Chuki hupoteza muda wetu, hutuharibia mahusiano na watu, hutukosesha bahati na baraka, sasa kwa nini mtu usiamue kubadilika?
Ukianza kuondoa chuki moyoni au rohoni mwako ni wazi utaanza kujisikia mwepesi zaidi kimwili na kiakili na ninachoweza kukuhakikishia ni kwamba utaanza kuona mabadiliko kwenye shughuli na mambo yako.

5 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. "Chuki hupoteza muda wetu, hutuharibia mahusiano na watu, hutukosesha bahati na baraka, sasa kwa nini mtu usiamue kubadilika?
  Ukianza kuondoa chuki moyoni au rohoni mwako ni wazi utaanza kujisikia mwepesi zaidi kimwili na kiakili na ninachoweza kukuhakikishia ni kwamba utaanza kuona mabadiliko kwenye shughuli na mambo yako".Ni kweli kabisa usemavyo. Hili darasa nimelipenda sana nadhani itabidi nami nianza kusoma mambo ya utambuzi.

  ReplyDelete
 2. karibu sana dada yasinta.
  maarifa ya utambuzi unaweza kuyapata hata hapa blogunin kama utakuwa mfuatilliaji wa makala za utambuzi zinazotoka hapa,au kwa kamala

  ReplyDelete
 3. Mimi ninapata shaka na matumizi ya neno
  'KUJIPENDA ZAIDI".Umesema mtu anayejipenda zaidi mara nyingi huwa ni mbinafsi na hujenga chuki dhidi ya yeyote anayeonekana kumzidi.

  Mimi nina mtizamo tofauti na dhana nzima ya kujipenda.Mtu anayejipenda iwe kwa kiasi au zaidi hawezi kuwa na chuki na mtu mwingine kwa kuwa upendo upo ndani yake .Ninavyojua mimi ni kuwa upendo huanza ndani ya mtu kisha hujionyesha kwa wengine kupitia matendo na kauli za mtu husika.

  Kama mtu ana chuki na wengine au hapendi wengine wafanikiwe siwezi nikamuona kuwa anajipenda zaidi bali nitamchukulia kuwa ni mtu anayejichukia zaid na chuki hiyo hujidhihirisha pale anapowachukia wengine kupitia kauli zake na matendo yake.

  Nahitimisha kwa kupinga kuwa kujipenda zaidi hakuwezi kukasababisha uwachukie wenzako bali anayejenga chuki dhidi ya wenzake ni yule ambaye anajichukia zaidi yeye mwenyewe.Kauli na matendo ya mtu huonyesha nini kinachoendelea ndani ya mtu huyo.

  J

  ReplyDelete
 4. Bwana Katawa,
  Kwanza nikushukuru kwa changamoto yako.
  Ukweli ni kwamba siwezi kukupinga wala kukubaliana na wewe moja kwa moja, nitakueleza sababu.
  nisome katika makala ijayo.

  ReplyDelete
 5. Nasubiri kwa hamu

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi