0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Jun 2, 2009

SISI KAMWE SIO WAKAMILIFU KAMA WENGINE HAWAJAKAMILIKA.

Hata tukalie viti vya enzi, binadamu wote ni sawa

Sisi kama binadamu tunajipenda na hakuna awezaye kulizuia jambo hili. Lakini kujipenda kwa ziada kunaweza kuzuilika kama mtu ataamua. Kujipenda kwa ziada ndiko ambako kunapelekea dunia kuwa kama ilivyo leo kwa upande wa uharibifu. Yale yote ambayo hayakwenda sawa kufuatana na mpango wa mungu, yamesababishwa na uziada wa kujipenda kwa binadamu. Mpango wa mungu ni kuwa na dunia ambayo haina makovu wala vidonda.

Lakini leo hii, dunia hii tunamoishi imejaa vidonda na makovu zaidi kuliko uzima. Vidonda na makovu haya kama ambavyo nimesema ni matokeo ya binadamu kujipenda kupita kiasi. Kujipenda huku kunamfanya adhani kwamba yeye anastahili zaidi kuliko mwingine na kumemfanaya awe pia mvivu wa kufikiri..

Ni binadamu wachache sana ambao wako tayari kukaa chini na kujiuliza kama wana tofauti na wengine.Ni wachache kwa sababu kila mmoja anaamini kwamba ni tofauti na mwingine, iwe ni kwa mwenye mali au asiyo nayo, iwe ni kwa mwanamke au mwanaume, kila mmoja anaamini kuwa ana tofauti na mwingine. Anashindwa kujua kwamba yeye kama binadamu hana tofauti na binadamu mwingine.

Labda nikumbushe kwamba binadamu hawi binadamu kwa sababu ana magari makubwa na madogo mia moja yenye thamani au ana nyumba za kifahari mji mzima, lakini pia hawi binadamu kwa sababu anashinda na njaa au anatembea makaliao yakiwa nje kwa ukosefu. Binadamu anakuwa binadamu kwa sababu kuna sifa ambazo hupatikana kwake na kwa mwingine bila kujali huyo mwingine yukoje kimwili au kihali.

Kushindwa huku ndiko ambako huwafanya binadamu kuwapa wenzao kile ambacho kama wangepewa wao kungezuka balaa kubwa. Binadamu wamejaribu kuridhisha miili yao na pengine nafsi, kama sio tamaa zao kwa kuwafanyia wengine lile ambalo kwao lingekuwa ni gumu sana kulivumilia.

Leo hii kuna binadamua ambao kwa kujali fedha wanauza sumu kwa binadamu wenzao, huuza vyakula ambavyo wanajua wazi kwamba vinadhuru afya za wengine na kuwauwa au kuwauwa wenzao wenye hali fulani kwa kudhani kuwa watapata utajiri, kama tunavyoshuhudia mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, maalbino.

Kuna wale ambao kutokana na tamaa na kutojitosha wameshiriki katika vitendo vya ufisadi na kujichotea mabilioni ya shilingi huku wakiwaacha binadamu wenzao wakihangaika kwa kukosa huduma muhimu, ambapo hizo fedha zingesaidia kuboresha huduma za afya, miundo mbinu na elimu.

Kuna wale ambao kwa matumizi ya vyeo vyao huwakosesha wengine haki zao kwa sababu tu wengine hao hawana nguvu na uwezo wa kupambana nao. Hawa kwa makusudi huwafanya watu wengi kuishi katika ulitima wa kudumu wakati wangeweza kuinuka na kuishi kama wao.

Kuna kundi kubwa la binadamu ambalo kamwe halijawahi kufanya jema kwa wengine. Halijawahi kutamka jema kwa wengine na halijawahi kufikiri jema kwa wengine. Kundi hili lina watu ambao wao kila siku wanafikiria ni kwa namna gani watatumia ujinga wa wengine kwa manufaa yao. Hutumia ujinga wa wengine kwa kujipatia ziada na “kutanua” huku wengine hao wakiporomoka na kuingia kwenye shimo la kiza cha ulitima.

Imefika wakati ambapo inabidi kuheshimu ubinadamu katika ujumla wake. Inabidi tujue kwamba kinachotufanya tusimame leo na kujidai, kujivuna na kujiona tu bora sana ni kwa sababu kuna binadamu wengine wanaotuzunguka. Kinachotufanya leo hii tutamani kuonekana wakubwa zaidi, wenye uwezo zaidi, wenye heshima zaidi, ni kuwepo kwa biandamu wengine, kuwepo kwa wenzetu. Kwa hiyo sisi sio binadamu hata kidogo kama tunavyodhani, bila binadamu wengine kuwepo.

Mbaya zaidi ni kwamba sisi siyo binadamu kamili kama wenzetu siyo kamili. Ukamilifu wao ndio unaotupa sisi ukamilifu. Ukitaka kuthibitisha jambo hili ni rahisi sana.Hebu anza sasa kutenda yale ambayo hata wewe ungependa kutendewa na kuacha kuwatendea wengine yale ambayo hata wewe usingependa kutendewa. Nina imani baada ya muda fulani utagundua ukweli fulani.

3 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Nimenukuu "Imefika wakati ambapo inabidi kuheshimu ubinadamu katika ujumla wake. Inabidi tujue kwamba kinachotufanya tusimame leo na kujidai, kujivuna na kujiona tu Kwa kweli bora sana ni kwa sababu kuna binadamu wengine wanaotuzunguka. Kinachotufanya leo hii tutamani kuonekana wakubwa zaidi, wenye uwezo zaidi, wenye heshima zaidi, ni kuwepo kwa biandamu wengine, kuwepo kwa wenzetu. Kwa hiyo sisi sio binadamu hata kidogo kama tunavyodhani, bila binadamu wengine kuwepo.

  Mbaya zaidi ni kwamba sisi siyo binadamu kamili kama wenzetu siyo kamili. Ukamilifu wao ndio unaotupa sisi ukamilifu. Ukitaka kuthibitisha jambo hili ni rahisi sana.Hebu anza sasa kutenda yale ambayo hata wewe ungependa kutendewa na kuacha kuwatendea wengine yale ambayo hata wewe usingependa kutendewa. Nina imani baada ya muda fulani utagundua ukweli fulani."

  Kwani haya maneno yako niliyonukuu hapo juu nimeyapenda Ni kweli watu wana ubinafsi/Umimi sana siku hizi. Kazi nzuri kaka Shabani.

  ReplyDelete
 2. Somo lako la leo linahusu binadamu kujipenda zaidi kuliko mwenzake au wenzake.Kwa ujumla linazungumzia upendo na unatushauri tuwe au tujifunze kuwa na upendo.

  Tatizo ni namna gani tutaurudisha au kuurejesha upendo tulokuwa nao tulipokuwa watoto.Ukienda kanisani au msikitini wao watakufundisha upendo ila watakueleza wao ni bora kuliko wengine na wanaweza wakakushauri kutokushirikiana na watu wenye imani au mtizamo tofauti na wao na wanaieleza jamii kuwa wanafundisha upendo.

  Ukija kwenye siasa,shule za msingi na sekondari hadi vyuoni huduma hutolewa kwa ubaguzi wa rangi,imani na uchumi.

  Je ni wapi tutakakojifunza kuwapenda wengine?

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi