0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

May 24, 2009

HAIWEZEKANI WEWE TU UKAWA SAHIHI

Huna haja ya kujilaumu, ukiwa na subira utafika

Unaweza kufanya zoezi hili na kulimudu? Kujaribu kufikiria na kujiambia kwamba kila mmoja isipokuwa wewe anelewa kuhusu hali halisi na kuichukulia kama ilivyo na anawaelewa watu na kuwachukulia kama walivyo.

Ni zoezi gumu bila shaka, kwa sababu unajipenda sana na usingependa kukubali kwamba ni wewe tu usiyeielewa hali na kuikubali na kuwaelewa watu na kuwakubali walivyo.

Lakini kama ungeliweza kufikiri na hatimaye kuamini hivyo bila shaka ungemudu kujitoa kwenye utumwa ambao hutusumbua tulio wengi nawe ukawa ni mmoja kati yao.

Huu ni ule utumwa wa kudhani kwamba sisi ndio tuko sahihi na wengine wana matatizo bila kujali kama tunavyofikiri ni sahihi au kujipenda.

Huu ni ule utumwa wa kuwatazama wengine kwa jicho la kukerwa pale wanapokosea jambo au wanapotuonyesha tabia za kuudhi au tusizozizoea.
Tukijifunza kuamini kwamba kwamba watu wote tunaokutana nao isipokuwa sisi ni watu wanaoijua hali halisi na kukubaliana nayo na kuwaelewa watu wengine na kukubaliana nao, tutakuwa tumeingia kwenye ukurasa mpya wakuyatazama mambo na kuyapa tafsiri sahihi kwenye maisha yetu

Kwa vipi?

Utajifunza kwamba watu wote unaokutana nao watakuwa wanakufundisha jambo fulani muhimu maishani. Utajifunza kwamba ukikutana na dereva anayeendesha hovyo gari kiasi cha kuhatarisha maisha ya watu au ukikutana na mtu asiye na heshima wala adabu huna haja ya kukereka na kujiingiza kwenye ugiligili wa bure, badala yake unatakiwa kujua kwamba watu hao wanakufundisha kuwa na subira maishani au kuwa mwangalifu kwani dunia imejaa watu wa kila aina ambao hupaswi kulingana nao katika kufikiri wala kutenda.

Ukianza kuamini hivyo utajikuta kwamba unaanza kujiuliza ni kitu gani mtu au watu unaokutana nao maishani wanajaribu kukufundisha. Ukianza kutazama tabia na matendo ya watu ambao unakutana nao maishani wanajaribu kukufundisha.

Ukianza kutazama tabia na matendo ya watu ambao unakutana nao kwenye maisha yako ya kila siku kwa kujiuliza kile unachojifunza kutoka kwao utajikuta unaanza kuyatazama kwa jicho tofauti yale uliyokuwa ukiyaona hapo kabla kama maudhi au yenye kukatisha tamaa. Utaanza kuhisi ukipungukiwa na kiwango cha kukerwa, kuchanganywa na kubughudhiwa na vitendo na mapungufu ya wengine.

Kama tutawatazama wengine na matendo yao kama waalimu wetu tutajikuta tukiondoa hali fulani ya chuki na kukerwa ambayo huwa tunakuwa nayo pale mtu au watu wengine wanapofanya kinyume na matarajio yetu.

Muuguzi anapotutukana au anapotukaripia, badala ya kukasirika inabidi tujiulize tunachojifunza. Huenda tunajifunza kwamba ni hatari kwa mtu kuchagua kufanya kazi asiyoipenda.

Lakini pia huenda tunajifunza huruma, kuwahurumia wengine ambao wanafanya kazi ambazo siyo uchaguzi wao bali kwa sababu ya shida.
Basi linapo haribikia njiani, badala ya kukasirika inabidi tujiulize tunachojifunza. Huenda tunajifunza kuwa ni vizuri kuwa waangalifu tunapoamua kuchukua jukumu fulani kubwa maishani, au huenda tunajifunza kwamba tunaweza kujiandaa na kujiamini lakini mambo yakabadilika bila kutegemea au tunaweza kujifunza kwamba hakuna kitu kisichoweza kwenda kombo hata kama tukiamini kwa kiasi gani.

Mfanyabiashara tapeli anapotuuzia mali mbovu au zisizo zenyewe hatuna haja ya kukata tamaa na kuchanganyikiwa badala yake inabidi tujiulize tunachojifunza kutoka kwake. Huenda tumejifunza hatari ya mtu kujali fedha au maslahi yake zaidi kuliko kujali maisha na matarajio ya wengine. Huenda pia tumejifunza jinsi inavyouma pale tunapowadhulumu wengine.

Inapobidi kusimama kwenye foleni muda mrefu kusubiri huduma fulani, hatuna haja ya kukasirika na kuanza kujilauamu na kuwalaumu wengine. Badala yake inabidi tujiulize kile tunachojifunza katika tukio hilo. Huenda tunajifunza kuwa na subira maishani. Mara nyingi kusimama foleni ni kipimo kizuri sana cha kiwango cha subira aliyonayo mtu.Hii ni nafasi muhimu kwetu kujifunza subira na uvumilivu badala ya kukasirika na kukata tamaa.

Inawezekana wewe unayesoma makala haya unaweza kuliona jambao hili kama kichekesho au lisilowezekana. Lakini kama ambavyo nimekuwa nikiandika kwenye makala zangu nyingi, kuhusiana na nguvu ya subira.
Kama tutajaribu njia hii ya kuvitazama vitendo na tabia za wengine kwa kujiuliza kile tunachojifunza na sio kile kilichotukera, tutaanza kushangazwa na mabadiliko yake.

Pale ambapo wenzetu watakuwa wamekasirika, wamekerwa na kukatishwa tamaa na vitendo au tabia za mtu au watu, sisi tutakuwa tunatabasamu kwa kujifunza jambo.

Maisha ni matamu na rahisi kama nasi tutaamua kila tunapoona jambo lisilopendeza kujiuliza, kama jambo hilo linafundisha nini; badala ya kwa nini ananifanyia hivi.

3 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Ni kweli,
  Hata katika jambo ambalo jamii huona baya bado tunaweza kujifunza na kutengeneza kitu kipya (opportunities)

  Nimeipenda hii mada na nimejifunza kitu na nimekubali kwamaba si mara zote nipo sahihi.

  ReplyDelete
 2. Mvumilivu hula mbivu. Ila siku hizi watu wanatakaka kila kitu kienda haraka haraka.

  ReplyDelete
 3. Unapozabwa kibao basi jiulize ni kwanini umepigwa na ni vipi unaweza kuepusha hilo kutokea hata kama inaweza kuwa kwa kutokutana na mzabaji. Unapoona mtu anaingia na kukutusi, jifunze kuwa watu wa namna hiyo wapo na wapo wengi na pengine wanafanya wafanyayo bila wewe kutaraji, kwa hiyo kuwa tayari wakati wote.
  Ukweli wa mambo ni kuwa katika kila jambo baya litukumbalo, kuna upande chanya unaoweza kuliepusha hilo, na njia nyingine rahisi niliyojifunza toka kwa muumini mmoja wa imani za upole, heshima, amani na upendo ni kuwa "SOMETIMES let someone be right for the sake of peace"
  Nimesema SOMETIMES na nimeiandika kwa herufi kubwa.
  Blessings

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi