0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

May 15, 2009

KUWA NA AKILI NYINGI SIO KUWA TAJIRI!

Huwa hawachagui aina ya biashara

Hata mimi nilikuwa nikiamini katika jambo hili, kwamba watu wenye uwezo mkubwa kiakili huwa na mafanikio katika maisha.
Nilikuwa nikiamini hivyo kwa sababu nilikuwa nikijua kwamba ni wale wenye uwezo mkubwa darasani ndio pekee wenye uwezo wa kufanikiwa katika maisha, lakini hivi karibuni baada ya kusoma tafiti kadhaa na kuangalia maisha ya wale niliosoma nao ambao darasani walikuwa wakituburuza kwa kupata maksi za juu na kufaulu sasa hivi maisha yao ni ya kawaida kabisa na wengine wameshindwa kabisa katika maisha wamebaki kubaingaiza tu mitaani.

Wale ambao tulikuwa tukiwaita mbumbumbu, ambao hawakuwa na uwezo kabisa darasani na wengine walishindwa kabisa kuendelea na masomo wakiwa hata hawajafika darasa la tano, ndio ambao wamefanikiwa na kumudu kuwa na kipato cha kuridhisha na wengine wakiwa wanamiliki biashara kubwa kubwa.

Na ndio maana kuna wakati unashangaa sana kusikia watu wakisema, ‘fulani alikuwa bomu kabisa darasani, hata la nne hakumudu kumaliza, lakini sasa ana fedha kama nini!’ Kwa nini kauli kama hizi zimebeba mshangao mkubwa? Ni kwa sababu, tumefanywa kuamini kwamba, uwezo wa kiakili, ndiyo unaoamua mtu apate fedha kiasi gani maishani mwake.

Ninavyojua mimi ni kwamba, kuna watu kwa mamilioni ambao wana akili sana, kuanzia za darasani na zile za nje ya darasa. Lakini, ukiangalia kipato chao, kila siku ni kile cha kubangaiza. Ukweli ni kwamba, hakuna uhusiano kati ya akili nyingi na upataji wa fedha.

Watu wenye uwezo wa kawaida kiakili wanaweza kuwa na mali sawa na wenye uwezo mkubwa. Haijalishi uwezo wako wa kiakili linapokuja suala la mafanikio ya kiuchumi. Kama una mtazamo chanya na unahitaji mafanikio kiuchumi, haihitaji uwezo mkubwa kiakili kuvipata hivyo.

Hata hivyo imebainika kwamba watu wenye uwezo mkubwa sana kiakili pia wana matatizo kiuchumi kiasi cha kushindwa kabisa kulipia bili na za vitu kama umeme, maji, simu na vingine hata vidogo zaidi.
Matatizo kiuchumi yanaweza kuhusishwa na uwezo mdogo wa kutunza pesa. Tafiti za nyuma zilionesha kwamba, uwezo wa kiakili huathiri pato au pesa ambayo mtu hutengeneza kwa mwaka.

Watu wenye uwezo mkubwa kiakili huwa na mafanikio ya juu kielimu, kicheo na hii hutokea mara nyingi. Hata Ruth Spinks, mwanasayansi wa neva (neuroscientist) anathibitisha jambo hilo na kusema, halina majadala. Na anasema, kwenye pato la kifedha, akili kubwa haina nafasi kubwa.

Lakini pia mtu kuwa na kazi inayomlipa vizuri haimaanishi kuwa ni tajiri. Mtu anaweza kuwa na mshahara mzuri sana kwa sababu ya elimu na cheo chake, lakini je, umeshawahi kujiuliza kuhusu namna watu hawa wanavyodaiwa? Wanadaiwa sana, kwa sababu hata kutunza fedha, kwao ni shughuli pevu.
Kwa mfano,, ingawa wanasayansi waliogundua roketi walikuwa wakipata mapato makubwa haikumaanisha kwamba wao ni matajiri kwani hawakuwa na akiba ya kutosha kulidhihirisha hilo.

Utafiti mpya wa Zagorsky unaonesha kwamba watu wenye uwezo mkubwa sana kiakili huwa hawana tabia ya kutunza pesa nyingi. Wengi wanaonekana kujali zaidi sifa za kiakili kuliko zile za kifedha. Ndiyo maana, ni vigumu kukuta wanataaluma wakiwa ndiyo matajiri katika jamii.

4 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Nashukuru umeandika mada hii kwani kuna wengi wanafikiri hivyo. Hawajui kwamba hata aliye mbumbumbu ni mtu pia, na kuwa tajiri hii sio kwamba mtu atakuwa na maisha mazuri siku nzuri nk.

  ReplyDelete
 2. Kaka Kaluse, nakubaliana na wewe kwa umantiki wa hoja hii. Nawafahamu watu wengi walio na uwezo mkubwa kitaaluma lakini ni hohehahe wa kutupwa. Wengi ni wahadhiri na maprofesa, na sio kwamba hawapati pesa, la hasha, wanapata sana lakini huishia kufanyia mambo wanayojua wao, ile elimu ya ujasiriamali ambayo hata wewe huizungumza, hamna kwao, wapo busy na miradi, pesa inaingia kila mara, lakini maisha yao kama ya fukara wanaonyonywa na kugandamizwa na mfumo...hujui kesho utakula nini

  ReplyDelete
 3. Tujiulize lakini usahihi wa hivi vipimo vya akili!

  Kwa mfano vigezo vya IQ test ukimuuliza maswali mtoto wa Matombo Mororgoro na wa Kibaha kuhusu Dar unaweza kufikia hatima ya kudhani wa Kibaha anaakili zaidi, kumbe ni kwa sababu yeye ana acess na Dar kuliko wa Matombo kwa hiyo ujuzi wake wa Dar unamzidi mtoto wa Matombo.


  Halafu tujiulize ni nini lengo na kimfarijicho mwenye akili kwa kuwa kuwa na fedha sio lengo la watu wote.

  Kubwa kabisa tukumbuke mwenye pesa labda hiyo ndio akili na kipaji chake-kupata pesa. Kwa hiyo kama umsifiavyo awezaye fizikia kuwa ana akili sana, labda tunasahau kumsifia mwenye pesa kuwa ana akili sana ingawa yake ni ya kujijazia ngawira pesa.

  ReplyDelete
 4. Dah! Kwanza ninafarijika kurejea "nyumbani" hapa kuweza kuchangia.
  Najua ukweli juu ya hili na nimekuwa nikiamini kuhusu usemalo. Lakini pia Kaka Simon kanichangamotoa kidogo na vu-maswali vwake vuzuuri ambavyo vunatufanya tujiulize kama tunatafsiri haya kisahihi. Lakini bado ukweli unabaki kuwa akili nyingi si kigezo sahihi za kuwa na pesa nyingi, lakini kwa aliye nje ya Tanzania anaweza kuamini kuwa wapo watu ambao kwao pesa si muhimu kuliko sifa na kudhihirisha uwezo wao katika mambo fulani fulani.
  Kwa hiyo Kaka Kaluse umenena mema kuwa hatuwezi kupima uwezekano wa mtu kuwa na pesa nyingi kwa kutumia vipimo vya uwezo wake darasani, kama ambavyo Kaka Simo amesema kuwa kuna ugumu wa kuoanisha mafanikio ya mwenye akili na mwenye pesa.
  Dah! Kaazi kwelikweli.
  Blessings to y'all

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi