0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Jun 21, 2009

MAJAMBAZI YALIPOTAKA KUNIULIA MWANANGU USIKU WA JANA

Abraham akitatafakari tukio la jana

Kuna wakati mambo mengine inabidi yatokee ili maisha yaendelee.
Katika kujifunza kwangu maarifa haya ya utambuzi nimegundua kwamba
Matukio yote tunayokutana nayo yanakuwa yanatufundisha jambo fulani muhimu maishani.
Kama ukianza kutazama matukio na matendo ya watu ambao unakutana nao kwenye maisha yako ya kila siku kwa kujiuliza kile unachojifunza kutoka katika matuki hayo utajikuta unaanza kuyatazama kwa jicho tofauti yale uliyokuwa ukiyaona hapo kabla kama maudhi au yenye kukatisha tamaa. Utaanza kuhisi ukipungukiwa na kiwango cha kukerwa, kuchanganywa na kubughudhiwa na vitendo na mapungufu ya wengine..
Hapa ninapoandika makala hii siamini kabisa kama niko hai mimi na familia yangu.
Usiku wa jana majira ya saa tisa za usiku tulivamliwa na Majambazi zaidi ya kumi wakiwa na silaha mbali mbali kama vile mapanga, marungu na Bastola .
Nyumba ninayoishi iko maeneo ya Tabata Bima na ni Non Crime area kwa maana kwamba hakuna uhalifu wa kutisha na tukio hili la jana limemuacha kila mtu mdomo wazi, kila mtu alikuwa akijiuliza KULIKONI JAMANI!!!!

Jana nlikuwa kazini na nilirudi nyumbani majira ya saa tatu za usiku nikiwa nimechoka ile mbaya, na hata mwanangu Abrahamu nilimkuta alikuwa hana furaha kabisa kama kawaida yake.
Nilipanda kitandani kulala sa nne na nusu usiku baada ya kupata mlo wa usiku.

kama unaamini katika maono, au njozi basi tukio hili nilifahamishwa kabla hata halijatokea

Ilikuwaje?

Ngoja niwasimulie. Katika hali ya kuashiria kuwa kuna jambo baya litatokea, nikaota ndoto ya kushangaza sana.
Niliota kwamba nilitoka kwenda katika kampuni fulani kufuatilia masoko na huko wakanipa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kilikuwa na mchanagnyiko wa Dola za Kimarekani na za Shilingi za Kitanzania ambazo nilitakiwa kuziwasilisha kazini, kwani lilikuwa ni deni ambalo kampuni ninayofanyia inaidai kampuni hiyo.

Nilipewa lifti na mmoja wa wafanyakazi wa kampuni ile na alinishusha karibu na kazini kwangu, nilipovuka barabara, nikakutana na watu wawili wakiwa na bastola wakataka kuninyang'anya ule mkoba wenye hela, sasa nikawa navutana nao huku wapita njia wakipita bila hata kutoa msaada na walikuwa wakiona kila kitu, nikawa nawaonyesha ishara walinzi wa kampuni ninayofanyia kazi kuwa naibiwa lakini nao hawakunijali hata sikumbuki ile ndoto iliishaje nikastukia kishindo cha mlango ukivunjwa.
Nilipoamka nikajikuta nimewekewa bastola kichwani na mwanangu Abrahamu kashikwa kichwa chini miguu juu, huku wakitishia kuniua mimi na mwanangu pamoja na mke wangu, kama sitawapa pesa.
Mke wangu alizimia ghafla kwa hofu.

Nilinyanyuka huku nikipigwa na mapanga kwa ubapa mgongoni na kuwapa pochi iliyokuwa na kiasi cha shilingi elfu sabini.

Wakakataa wakidai kuwa hawawezi kuvunja nyumba kwa elfu sabini na nisiwatanie kwani taarifa walizonazo ni kwamba sisi wapangaji wa nyumba ile tuna hela sana na wakatishia kumkata kichwa mwanangu.

Kuona hivyo nikajua kuwa hawatanii kwani walikuwa ni wengi sana, nikawapa mkoba wangu mweusi uliokuwa na vijisenti vyangu vya akiba, hawakuridhika na kuanza kunipiga kwa ubapa wa panga nikawaambia kuwa kama wanataka kuniuwa basi wafanye hivyo kwani sina hela tena.

Basi wakachukua TV, Deki ya DVD, Mobile phone 3 na Music System, lakini walishindwa kubeba Computer yangu kwa madai kuwa itawapotezea muda kuchomoa nyaya, niliposikia hivyo nilishukuru sana kwani kile kitendea kazi changu kingechukuliwa, ningeadimika mtandaoni, na blog ya Utambuzi na Kujitambua ingesinzia kidogo.

Kumbe walianzia kwa wapangaji wenzangu. Nyumba yetu ina wapangaji wanne.
Baa day a kuchukua kile walichoamini kuwa kingewasaidia kusogeza maisha yao mbele walitoka na kutufungia mlango wa chumbani kwa nje ili tusitoke kuwasaidia wenzetu, kwani walikuwa wakiendelea kuvunja vyumba vingine.

Majambazi hayo yalitumia takribani nusu saa katika kuvunja na kuiba kisha yakatoweka.
Niliungana na wapangaji wenzangu pamoja na majirani waliojitokeza baada ya tukio lile kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi kilichopo jirani, Pale kituoni tulishauriwa twende kituo cha polisi Buguruni kwani ndipo tunapoweza kufungua faili na kupewa RB.

Mpaka sasa Polisi bado wanaendelea na uchunguzi na watuhumiwa hawajatiwa mbaroni.
Hali ya familia yangu na ya familia za wapangaji wenzangu tulioibiwa pamoja bado ni tete na bado nina maumivu ya mapanga ya mgongoni.

Napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru mungu muumba kwa kutuponya katika kadhia ile na kuepuka kifo, kwani roho zetu zilikuwa mikononi mwa majambazi hayo.

17 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Pole sana kaka kwa mkasa mzito ulokukumbwa pamwe familia yako.
  Nimesoma huku mwili ukinisisimka mno. Tunamshukuru Mungu mu salama. Vitu vilivyochukuliwa si hoja ingawa umerudishwa nyuma. Cha muhimu mmenusurika.
  Mungu awape faraja na kuwaongeza maradufu ya pale mlipodhulumiwa.

  ReplyDelete
 2. Naungana na kaka Fadhy kuwa habari hii kuisoma inasisimua.
  Kaluse,
  Nimesoma kwa masikitiko makubwa sana kisa na mkasa ulioikumba familia yako. Imenikumbusha sana uvamizi uliofanyika katika nyumba yetu ningali mtoto mdogo (miaka 11), tukio lile lilinipa wasiwasi mkubwa kwa miaka takriban kumi iliyofuatia, usiku ulikuwa adui yangu kwani nilikuwa nashindwa kupata usingizi na kuweweseka, hadi sasa nimekuwa mtu ninayependa kuwa macho zaidi usiku na kulala mchana hata kazi ninayofanya ni ya zamu ya usiku badala ya mchana.
  Poleni sana ila ashukuriwe Mtoa Uhai na Uzima aliyeinusuru familia yako mbali na mauaji.
  Ni vyema ulivyofanya kuripoti polisi, tafadhali fuatilia na uweke kumbukumbu ya safari za polisi ili iwe rejea kwa maisha ya mbeleni (kwako na watu wengine pia).
  Vitu vimepotea lakini vitarejea uhai ungalipo.
  Pia, Heri kwa sikukuu ya Baba duniani.

  ReplyDelete
 3. Namshukuru Mungu kuwa mko maishani. Hivyo vifaa sio kitu kwani utanunua vingine lakini roho hazinunuliwi. Hata nami nimesoma huko nasisimka. Pole sana

  ReplyDelete
 4. Pole sana bwana kaluse kwa mkasa uliokupa.

  ReplyDelete
 5. Tumshukuru Mungu kwamba roho yako hawajaichukua, vitu walivyochukua mungu atakupa tena zaidi ya hivyo. pole sana kwa mkasa huo

  ReplyDelete
 6. Pole sana kaka.Mungu hakukutupa nawe usimtupe pia maana amekuwekea kusudi la kitendea kazi ili ukitumie kwa kurudisha vilivyopotea.jamani kamalaika hako kana kosa gani? Thx to Gud!

  ReplyDelete
 7. Pole sana kwa yaliyokusibu. Mali zinaweza kununulika upya, cha msingi ni uhai wako na familia yako.

  ReplyDelete
 8. Pole sana Bwana Kaluse. Kwa kuwa wewe ni mtu wa Utambuzi natumaini tukio hili unaliangalia kwa mtazamo unaofaa zaidi. Bora uzima tu.

  ReplyDelete
 9. dah pile sana ndugu yangu yaani sina hata la kusema, nchi yetu!!!

  ReplyDelete
 10. Pole kaka na masahibu yote,mungu atakufanyia wepesi kupata vilivyopotea ktk tukio hilo.

  ReplyDelete
 11. Duh!Hii iansikitisha na kuhuzunisha, Yaani kama alivyosema dada Yasinta na dada Subi, hata miimi nlikuwa nasoma huku mwili ukinisisimka na mapigo yangu ya moyo yakienda kasi.
  Hawa watu ni wabaya na sitsiti kusema kama wakipatikana wanstahili kifo, hivi kutaka kumuaa malaiaka wa watu Abrahamu ndio nini?
  Pole sana kaka Kaluse kwa mkasa huo na mungu atakurudishia vitu vyote vilivyoibwa na ziada pia, na hao maharamia mungu atawaangamiza...
  habari hii imenisikitisha sana

  ReplyDelete
 12. Nianze kwa kusema SHUKRANI KUWA U-MZIMA NA UNGALI HAI na tunaweza kusoma tukio halisi toka kwa mtu aliyekumbwa na ambaye bado yu-hai. Pili nasema POLE SANA kwa mkasa huu na kwa kumbukumbu mbayailiyoachwa akilini mwako, mkeo na kwa mtoto Abrahamu. Lakini kama "Katika kujifunza kwangu maarifa haya ya utambuzi nimegundua kwamba
  Matukio yote tunayokutana nayo yanakuwa yanatufundisha jambo fulani muhimu maishani." Japo kujifunza huku kwaweza kutofautiana kulingana na mtazamo, lakini tukubaliane kuwa YAONESHA PESA IMETANGULIZWA MBELE KULIKO UHAI WA WATU. Na sitashangaa kama polisi nao watataka uwalipe kitu kidogo ili kuweza kuwasaka waliokuibia. Yaani dunia imeingizwa katika akili za kufikiri pesa ndio kila kitu na kudharau maisha na madhara ya kisaikolijia yanayoweza kuwawinda watu na hasa watoto kama Abrahamu. Aliyosema Da Subi ni kweli kuwa yaweza kuchukua miaka kadhaa kwa taswira mbaya za hivyo kutoka ama kuzoeleka akilini mwa shuhuda.
  Pole sana na naamini utafanya ustaarabu wa kumsaidia mwana kuepukana na njozi mbaya za hili tukio.
  POLE KAKA

  ReplyDelete
 13. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wasomaji na wanablog wenzangu wote walioungana nami katika kunipa pole juu ya mkasa huu ulionipata.
  Kikubwa kwangu ilikuwa ni uhai wangu na wa familia yangu, pesa na makorokoro mengine yaliyochukuliwa si kitu kikubwa kwangu.
  Hii kwangu ni kama chngamoto na nimejifunza kitu kimoja muhimu sana kutokana na mkasa huu, kuwa hata kama eneo unaloishi lina usalama kiasi gani, swala la kuchukua tahadari pia ni muhimu sana,kama nilivyosema kuwa huwa tunajifunza kwa kila jambo, liwe baya au zuri, pia nimejifunza kuwa pengo kati ya walio nacho na wasio nacho linapokuwa kubwa, usitegemee kuwa majambazi watawafuata wale wenye ukwasi mkubwa pekee, hata sisi tunaoonekana tukitoka asubuhi na mikoba kwenda makazini na kurejea jioni tutaonekana tumeyamudu maisha kwa mtazamo wao.
  Kuna kujifunza kwingi juu ya tukio hili, na hili kwangu litaendele kuwa somo muhimu.
  familia yangu bado haijarudi katika hali ya kawaida kutokana na kukumbwa na jakamoyo tangu kutokea kwa tukio hilo na bado tunajiuguza taratibu huku tukiendelea kufarijiwa na majirani zetu.
  Nawashukuru sana.

  ReplyDelete
 14. Pole haichelewi. Nadhani bado sijachelewa kuungana na wafariji wote waliopita kukupa pole.

  Nilizipata habari hizi kupitia barua pepe ya mwanablogu mmoja aliyejua sikuzipata habari hizi kupitia blogu.

  Tukio hili linasikitisha. Linaumiza kimwili na kiufahamu. Pole sana Shabani.

  Nimeshukuru kuona umelichukulia tukio hili kwa mtazamo wa 'zaidi ya kinachoonekana'.

  Nakutakia utulivu katika kipindi hiki kizito. Vilivyopotea, utavipata maadam u hai.

  Pole sana wewe na familia yako.

  ReplyDelete
 15. aisee, siui nikupe pole au hongera kwa kupata somo jipya? yamenikuta nami kama hayo hivi karibuni.

  ni mambo ya kawaida tu kwani yapo

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi