0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Jul 26, 2013

WANAUME HAWAOI SURA TENA BALI UELEWA....!

Wanaume hawaoi sura tena bali uelewa…!

Siku za nyuma, wanaume walijali zaidi uzuri wa sura na mwili wakati walipokuwa wanatafuta mke. Lakini utafiti uliofanywa duniani kote unaonesha kwamba, wanaume hivi sasa wamebadili mitazamo na kuanza kuangalia vitu vilivyo zaidi ya uzuri wa sura na mwili.


Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Grand Valley kilichopo jimboni Michigan nchini Marekani walioendesha sehemu kubwa ya utafiti huo wamesema, wanaume hivi sasa wameanza kujali uwezo wa wanawake katika kufikiri na kujua namna ya kujenga maisha kuliko kujali sura zao na maumbile.Tafiti nyingi, ukiwemo huo wa karibuni wa Chuo cha Grand Valley, zinaonesha kwamba, kwenye miaka hadi 1980, wanaume walikuwa wakioa wake ambao wanaume hao wanawazidi kielimu na hata kimapato. Lakini kufikia mwaka 2002, wanaume wengi walikuwa wameoa wanawake ambao wanawazidi kielimu, kimapato au kukaribiana.
Lakini pia imebainika kwamba, hadi kufikia miaka hiyo, wanaume na jamii nyingi zilikuwa zikimtazama mwanamke anayefaa kuolewa kuwa ni yule mzuri sana kwa sura na umbo. Lakini kufikia mwaka 2002, wanaume wengi na jamii walikuwa wanaamini kwamba, mwanamke mwenye uwezo mkubwa wa kuelewa maisha ndiye anayefaa kuwa mke.
Kwa miaka ishirini hali imebadilika sana. Maisha yamezidi kuwa magumu na uhitaji wa watu kusaidiana katika kuyakabili umeongezeka. Kwa hiyo mtu anapofikiria kuoa huanza kujiuliza atakavyomudu maisha na mke. Kwa hofu za kushindwa, hujikuta akijiuliza namna atakavyoweza kusaidiana na huyo anayetaka kumwoa katika kufanya mambo yaende.


Siku za nyuma, mwanamke mwenye kipato kizuri alikuwa katika ugumu wa kupata mume, lakini siku hizi, bila kujali sura au sifa nyingine, uhakika wa mwanamke kuwa na njia za kipato unampa, nafasi kubwa zaidi ya kuolewa. Kilichokuwa kinaogopwa huko nyuma na wanaume kwa sasa ndicho kinachokimbiliwa.Tafiti hizo zinasisitiza kwamba, thamani ya mwanamke kwenye jicho la mwanaume inaanza kuondoka kwenye uzuri wake wa sura na mwili na kuingia kwenye uwezo wake katika kuyakabili maisha. Hii ikiwa na maana kwamba, kwa kadiri siku zinavyoenda, wanawake ambao watakuwa na nafasi kubwa ya kuolewa watakuwa ni wale waliosoma au wale wenye shughuli za kuzalisha.

Wataalamu wengi wanasema, hivi sasa uzuri unaonekana kabisa kubadilishana nafasi na elimu na uwezo wa ‘kutafuta maisha’ wa mwanamke. Kwa hiyo, sasa siyo suala la uzuri tena, bali mwanamke anajua kitu gani na ana uwezo kiasi gani wa kufanya maisha yawe bora sana.


Hii pia ina maana kwamba, dhana ya zamani ya mwanamke mzuri kuolewa na mwanaume msomi au mwenye fedha imeanza kukosa mashiko. Siku za nyuma mwanamke mzuri sana, angeolewa na mwanaume mwenye fedha, kama zilivyo bidhaa nzuri kuangukia mikononi mwa wenye uwezo kifedha.Lakini leo hii, wanaume wanachoweza kufanya ni kuwachezea kimapenzi wanawake wazuri na siyo kuwaoa. Linapokuja suala la kuoa, kisomo na uwezo wa kuyajua maisha huchukua nafasi. Uzuri wa sura hubaki nyuma kwanza.

1 comment:
Andika Maoni Maoni

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi