Kesi hii iliyotokea mwaka 1981 na mshitakiwa katika kesi hii ni Nestory Hussein Chigawa ambaye alishitakiwa kwa kosa la kumuuwa kwa kukusudia Bonifasi Makende. Kesi hii ilifunguliwa kwa mujibu wa kifungu cha sheria ya mauaji ya kukusudia, na ilisikilizwa na Jaji A. Bahati.
Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo ilibainika kuwa mnamo Machi 11, 1981 mtuhumiwa Nestory Hussein Chigawa alikwenda nyumbani kwa Bonifasi Makende na akiwa njiani kuelekea huko alikutana na Paschal Makende, mtoto wa Bonifasi Makende ambaye alikuja kuwa shahidi wa pili katika kesi hii. Alipofika nyumbani hapo mtuhumiwa alimkuta Bonifasi Makende amekaa kwenye kiti nje ya nyumba yake. Katika hali ya kustukiza mtuhumiwa alimzaba makofi mara tatu Bonifasi makende, ambapo alinyanyuka na kuanza kukimbia ili kuepuka kipigo zaidi. Mtuhumiwa alichukuwa mchi na kuanza kumkimbiza na alipomfikia alimpika na mchi huo kichwani mara kadhaa ambapo alianguka lakini mtuhumiwa aliendelea kumpiga mzee huyo hadi akatosheka kisha akautupa mchi ule na kukimbia.
Tukio zima la kupigwa kwa mzee Bonifasi Makende lilishuhudiwa na binti yake aitwae Maria Makende ambaye alikuja kuwa shahidi wa kwanza katika kesi hii. Baada ya tukio lile mtuhumiwa alikimbilia kwa mjomba wake Eduard Chigawa ambaye nae alikuja kuwa shahidi wa tatu katika kesi hii ambapo alimjulisha kuwa amemuuwa adui yake mzee Bonifasi Makende, hivyo kumuomba mjomba wake huyo ampeleke kwa mwenyekeiti wa kijiji. Kwa mujibu wa maelezo ya Eduard Chigawa , mtuhumiwa alikuwa akitetemeka na alikuwa akipumua kwa nguvu huku akiongea kwa sauti ya juu kuwa amemuwa adui yake na hivyo anataka apelekwe kwa mwenyekiti wa kijiji. Hata hivyo Eduard Chigawe alikiri kuwa tangu amfahamu mtuhumiwa hajawahi kumuona akiwa katika hali kama ile; Baada ya tukio lile la mauaji mwili wa Boniface Makende ulipelekwa hospitalini kwa uchunguzi zaidi, ili kujua sababu ya kifo chake.
Mwili ule ulifanyiwa uchunguzi na kwa mujibu wa mtaalam wa kuchunguza maiti (post-mortem) ilibainika kuwa mzee Makende alifariki kutokana na kuvunjika kwa fuvu la kichwa na kuvuja damu kwa ndani. Mtuhumiwa hakukanusha maelezo yote yaliyotolewa na mashahidi wote waliotoa ushahidi katika kesi hii bali utetezi wake ulikuwa kwamba hakujua anachokifanya kwa sababu alikuwa amechanganyikiwa. Akitoa historia ya maradhi yake mtuhumiwa alidai kuwa amekuwa akisumbuliwa na maradhi asiyoyafahamu ambapo kuna wakati mapigo ya moyo wake huenda mbio kunakoambatana na kutetemeka mwili mzima, na hali hiyo inapojitokeza huwa anachanganyikiwa na kutojitambua kuwa yeye ni nani. Mtuhumiwa huyo aliendelea kusema kuwa hapo nyuma aliwahi kwenda kwenye zahanati ili kupatiwa tiba ya tatizo hilo ambapo alipewa vidonge atumie lakini hali yake haikuonyesha kubadilika,hivyo ndugu zake waliamua kumpeleka kwa mganga wa miti shamba. Alipofikishwakwa mganga wa miti shamba alipewa matibabu na kupata nafuu na tangu hapo kila tatizo hilo linapojitokeza huwa anapelekwa kwa mganga huyo na kupatiwa matibabu.
Akizungumzia siku aliyomuuwa mzee Makende,mtuhumiwa huyo alidai kwamba alichanganyikiwa na hakujua ni nini alichokuwa anakifanya na alipokwenda kwa mzee Makende na kumpiga mara mbili kichwani hakuwa anajua anachokifanya, na hakuwa ni yeye kiakili. Mtuhumiwa huyo aliendelea kusema kwamba anachokumbuka ni pale alipojulishwa baadae kuwa ameuwa. Hata hivyo mtuhumiwa alidai kuwa kuna wakati mzee Makende alimwambia kwamba atamloga,na hivyo ndivyo alivyofanya kwani alimloga kweli na ndio sababu akawa mwendawazimu. Katika mahojiano ya awali mtuhumiwa alikiri kwamba wakati anakwenda kumuuwa mzee Makende alikutana na mtoto wa mzee huyo aitwaye Paschal Makende ambaye ni shahidi wa pili katika kesi hii, na mara baada ya kumuuwa mzee huyo hajawahi kuumwa tena.
Mtuhumiwa huyo alizidi kudai kuwa hali yake kiafya imekuwa njema kwa kuwa mtu aliyekuwa anamloga ameshamuuwa kwa hiyo hawezi kuumwa tena, lakini hata hivyo alisisitiza kuwa hakuwa anajua anachokifanya wakati anamuuwa mzee Makende. Naye shahidi wa tatu kwa upande wa mashitaka katika kesi hii mzee Eduard Chigawa aliiambia mahakama kuwa anafahamu kuwa mtuhumiwa alikuwa anasumbuliwa na maradhi asiyoyafahamu ambayo yalikuwa yanamfanya aonekane kama mtu asiye wa kawaida lakini walipompeleka katika zahanati ya kijiji alionekana hana tatizo. Akizungumzia tatizo hilo kwa undani mzee Chigawa alisema kuwa kila mtuhumiwa huyo anapotokewa na tatizo hilo huwa anatetemeka mwili mzima na huwa anazungumza maneno yasiyoeleweka.
Kwa mujibu wa maelezo ya Eduard Chigawa ni kwamba mnamo machi 11,1981 mtuhumiwa alikwenda shambani pamoja nae, na mara baada ya kumaliza shughuli za shamba wote walirejea nyumbani. Walipofika nyumbani mtuhumiwa alitoweka ghafla katika mazingira ya kutatanisha, na aliporejea alikuwa akitweta na kuongea maneno yasiyoeleweka, lakini miongoni mwa maneno yake alisema kuwa amemuuwa adui yake mzee Makende. Katika majumuisho ya ushahidi uliotolewa dhidi ya mtuhumiwa pale mahakamani mwanasheria wa serikali aliyetambuliwa kwa jina moja tu Rutashobya aliieleza mahakama kuwa mtuhumiwa hakuwa mwendawazimu kwani alikuwa na akili zake timamu wakati anamuuwa mzee Makende na alikuwa akijua ni nini anachokifanya kwa hiyo ana hatia kutokana na kosa aliloshitakiwa nalo.
Mwanasheria huyo alinukuu vifungu vya 12 na13 vya kanuni za sheria ambavyo vinafafanua juu ya kumtambua mtu mwendawazimu na asiye mwendawazimu na ili kutetea hoja yake alitoa mfano wa kesi namba 23 EACA 622 ya Muswi Musola na kumalizia kwamba mshitakiwa anapaswa kupatikana na hatia kama alivyoshitakiwa. Katika majibu yake dhidi ya mwanasheria wa serikali wakili aliyekuwa akimtetea mtuhumiwa huyo ambaye naye alitajwa kwa jina moja tu la Bi Humplick aliielezea mahakama kuwa ni kweli mtuhumiwa alikuwa na hali ya kuchanganyikiwa ndiyo sababu alikuwa hajui ni nini anachokifanya.
Ili kutetea hoja yake hiyo naye alirejea kesi namba A 330 ya mwaka 1957 kati ya Jamhuri na Magata Kachehekana. Bi Humplick aliendelea kusema imani juu ya uchawi kwa kawida huwa inaweza kumfanya yule anaeamini kutojua kuwa ni nini anachokifanya. Wakili huyo Aliendelea kubainisha kwamba mtuhumiwa hakuwa anajitambua wakati alipokuwa anakwenda kumshambulia mzee Makende kwa hiyo hana haki ya kushitakiwa. Nao wazee wa Baraza katika kesi hii (Assessors) katika maoni yao mara baada ya kupitia kwa makini kanuni ya sheria namba 12 na 13 iliyotolewa na mwanasheria aliyekuwa akimtetea mtuhumiwa, Bi Humplick, wote kwa pamoja waliridhika kabisa kuwa mtuhumiwa anayo kesi ya kujibu kama alivyoshitakiwa.
Wazee wote wa Baraza hawakuridhishwa na madai kwamba mtuhumiwa hakuwa anajua ni nini anachokifanya wakati anatekeleza mauaji. Mzee wa Baraza wa kwanza aliyejulikana kwa jina la Ramadhani alisema kwamba, kama mtuhumiwa alikuwa na uwendawazimu asingeweza kuzungumza yale yote aliyomueleza Eduard Chigawa kwa sababu alikuwa hajui ni nini anachokifanya.Nae mzee wa pili wa baraza aliyejulikana kwa jina la Martin alisema kwamba kwa mujibu wa vipimo vya hospitalini ilibainika kwamba mtuhumiwa alithibitishwa kuwa alikuwa na akili zake timamu na pia ugonjwa wa uwendazimu aliokuwa anadai kuwa ulikuwa ukimtokea mara kwa mara haukuwa ukifahamika pale kijijini kwao kwa sababu kwa kawaida mtu mwenye ugonjwa wa uwendawazimu angejulikana pale kijijini kwao.
Kwa maneno yake mwenyewe mzee Martin alisema “Hivi inawezekana kweli mtuhumiwa awe anaumwa uwendawazimu na awe na uwezo wa kukumbuka kwamba, kwa kuwa mzee Makende aliwahi kumwambia kuwa atamloga, kwa hiyo ndiye aliyemloga na hivyo aamue kwenda kumuuwa? Zaidi ya hapo mtuhumiwa pia anajua kwa usahihi kabisa kwamba alimpiga mzee Makende na mchi mara ngapi kichwani kitu ambacho hakiwezekani kufanywa na mtu mwenye wendawazimu”
************ITAENDELEA***************
No comments:
Andika Maoni Maoni