0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Apr 26, 2011

NI MBAYA KWA KULINGANISHWA NA NINI HASA?

Kuna mengi tusiyoyajua!


Miongoni mwa wanafalsafa maarufu duniani ni mgiriki Socrates. Kwa wale wanaosoma na kufuatilia maisha ya wanafalsafa wa kale hapa duniani, huenda watakuwa wanajua kuhusu ndoa ya mwanafalsafa huyu maarufu.


Wanaofuatilia maisha ya wanafalsafa hao watakubaliana nami kuhusu mke wa Socrates. Watu au wenzake Socrates walipokuwa wanamuuliza kuhusu mke wake, wakitegemea kusikia akilalamika, kwa sababu mama huyu alikuwa na ghubu sana, hawakusikia malalamiko yoyote. Badala yake aliwauliza, ‘mnataka kujua yukoje kwa kulinganisha na nini?’


Je, wewe umeshagundua mahali ambapo falsafa imejificha kwenye swali hilo la Socrates la ‘kwa kulinganisha nanini?’ Ni hivi, iwe ni kwa watu, maeneo, hali, matukio, na hata hisia zetu vyote hivyo havina maana yenye kulingana kwa watu wote. Vyote hivyo ni vizuri au vibaya kwa viwango kwa kutegemea tunavilinganisha na nini.


Kwa mfano nikisema mke wangu ni mgomvi sana na ana ghubu ni lazima niwe ninawajua wanawake ambao ni wagomvi au wana ghubu kidogo. Kwa kuwajua hao ndipo ninapojua viwango vya ghubu au ugomvi. Hivyo hapo ninaweza kusema kiwango cha ugomvi au ghubu kwa mke wangu. Kama sina cha kulinganisha, maana yake sina mahali pa kupimia.


Kwa kujua ukweli huu kutoka kwa Socrates, tunaweza kupata utambuzi mkubwa zaidi na mbinu za kumudu kuishi bila matatizo na watu wakorofi, penye matatizo, penye hali ngumu au mbaya na matukio ya kila siku kwenye maisha yetu. Tunapata uwezo wa kuyapa hayo yote majibu mazuri baada ya kufikiri vizuri.


Hebu fikiria kuna aina ngapi za watu? Kuna aina nyingi sana, kama ilivyo idadi ya watu, kwa mfano, kwa Tanzania kuna aina za watu kiasi cha milioni 30! Kama tunashindwa kuwavumilia watu wakorofi kama tunavyowaita, inabidi tujiulize kwanza, watu hao ni wakorofi kwa kulinganisha na kitu gani? Kama kila mtu ana tabia, mienendo na mitazamo yake, ukorofi wa hawa unaupima kutokea wapi? Kwa kulinganisha na akina nani wakati kila mmoja ana tabia tofauti na mwingine?


Hebu tuchukue vikombe vya aina moja, kama kimoja kimebenduka, tunaweza kusema hakiko kamili. Ni rahisi kusema hivyo kwa sababu, tuna mahali pa kulinganisha, ambapo ni kwenye vile vikombe vingine vizima. Kwa binadamu hali ni tofauti kabisa, kwa sababu wote ni tofauti.


Hebu fikiria kuhusu tukio fulani kwenye maisha yako. Unasema kwamba, hili ni tukio baya. Lakini bado kuna swali, kwa kulinganisha na tukio lipi? Kila tukio linatokea mahali pake, muda wake na kwa sababu fulani au maalumu ili maisha yaendelee kuwepo. Kwa nini kama ni hivyo udhani tukio fulani ni baya au zuri? Huu ubaya au uzuri ni kwa kulinanisha na tukio lipi wakati kila tukio lina mahali, muda,na sababu ya kutokea kwake?


Tunaambiwa kwamba kila jambo ambalo linaingia kwenye mfumo wetu wa kufikiri ni vizuri au vema likawa limepimwa kwa mujibu wa tafsiri zetu ambazo hazipaswi kutuumiza. Unaona jambo ambalo linataka kukuumiza kihisia, ni kwa nini usijiulize kama jambo hilo ni baya, ni kwa kulinganisha na lipi?


Kumbuka ni lazima kuwe na mahali ambapo tunasimama ili kupima uzuri au ubaya wa jambo kwa kulinganisha na mengine, ambayo kwa kawaida hayatarajiwi kubadilika.


Kama yanabadilika, basi ni vigumu kusema kuwa ni mabaya au mazuri, kwani hatuna mahali pa kuyalinganisha. Kama vikombe vinavyofanana kabatini vingekuwa wakati mwingine kimoja kinakuwa kirefu kingine kifupi au kinaadilika rangi, tusingeweza kuvilinganisha pia. Binadamu kila mmoja ana haiba yake, kila mmoja ni yeye kwa tabia, mienendo na hata miili.

4 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Hakika leo nimelipenda sana somo hili maana hili ni darasa kabisa. Nimefurahi sana kusoma hapa nilikuwa nikisoma na mara nikastukia nasoma kwa sauti jinsi nilivyostukia uliyoyaandika ni kweli kabisa katika dunia hii hakuna watu waliofanana kwa tabia, mienendo au miili ..labda sura lakini hata hivyo lazima kuna kitu kitakuwa tofauti. Mnajua mara nyingi nimekuwa nikijiuliza kama Mungu angeumba watu tuofanana kitabia kwa mfano wenye tabia kama yangu wangekuwa hamsini je dunia hii ingekuwaje? Ukweli sina jibu....mmmhhh ngoja niache...

  ReplyDelete
 2. Blog ya Yasinta ni Mbaya kwa kulinganishwa na nini? Blog ya Matondo, no...Mubelwa......Oh!nooo Ah! ya Markus Mzee wa Nyasa ni mbaya....kwa kulinganishwa na nini?.......LOL

  Nimeona nitoe mfano wa Blog ili kujaribu kupanua wigo wa mada hii, kwani naamini hata mitizamo yetu katika blog zetu hizi nayo haifanani na haitoweza kufanana, na ndio maana wakati mwingine unaweza kukuta mada moja inaweza kuleta mlolongo wa changamoto hasa kutoka kwa akina ANNONY, na kama una moyo mwepesi waweza kupata Presha.
  Ni kweli kaka tuko tofauti kabisa, yasinta sio Koero, Mubelwa sio Matondo, Ansberti Gurumo sio Evarist Chahali, Makulilo sio Kamala, Mzee wetu Prof. Mbele sio Fred Macha, Kaka Fadhy sio Markus Mpangala......mlolongo unakuwa mrefu kama reli ya Tazara, na kamwe tabia hazilingani.....

  Nimejifunza mengi kwa mada hii...

  ReplyDelete
 3. Koero umetoa mifano mizuri sana kwa nini tuende mbaliiiii wakati mifano tunaiona kama Koero alivyosema ...asiyejifunza hapa kwa kweli atakuwa .....jaza mwenyewe hapo kwanye deshi

  ReplyDelete
 4. Shule nzuri , tunafaidika na mafunzo unayotupa mkuu!

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi