0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

http://www.serenahotels.com/serenadaressalaam/default-en.html

Apr 17, 2010

THAMANI YAKO UNAYO, HAIWEZI KUCHUKULIWA NA YEYOTE!

Rais Obama wa Marekani anajua siri ya kujiamini na ndio sababu akafika hapo

Mhubiri mmoja maarufu nchini kwenye moja ya semina zake alifungua semina kwa kuishikilia noti ya shilingi 10,000 mkononi. Kulikuwa na watu zaidi ya 500 kwenye ukumbi alimokuwa akifanyia mahubiri yake. Aliinua noti hiyo na kuuliza ‘ni nani anayeitaka noti hii?’

Mikono karibu yote ukumbini ilinyooshwa. Mhubiri aliendelea kusema, ‘nitampa mmoja wenu noti hii, lakini kwanza ngoja nifanye hivi.’ Alipomaliza kusema hivyo aliikunjakunja noti ile. Baada ya kuikunjakunja aliuliza tena, ‘ni nani anayeitaka bado noti hii?’ vidole karibu vyote vilinyooshwa tena.

‘Sawa,’ alisema, kabla hajaendelea, ‘Je kama nikifanya hivi?’ Alipomaliza kuuliza hivyo aliiweka noti ile chini na kuisigina kwa mguu bila kuichana, halafu aliiokota ikiwa imechafuka na kuikunjakunja. Aliuliza tena, ‘sasa ni nani ambaye bado anaitaka noti hii?’ vidole vilinyooshwa tena juu.

‘Rafiki zangu, wote leo mmejifunza somo la maana sana. Bila kujali nilichokifanya kwenye noti hii, lakini bado mmeendelea kuitaka, kwa sababu kuikunja kwangu na hata kuikanyaga, hakukuondoa thamani yake. Bado imeendelea kubaki noti ya shilingi 10,000.’

Bila shaka hata wewe utakubaliana na kauli hii ya mhubiri huyu, kwamba noti ile iliendelea kubaki noti ya shilingi 10,000 na kwamba thamani yake iliendelea kubakia pamoja na kukunjwa na kukanyagwa kwake.

Mara nyingi kwenye maisha yetu huwa inatokea tukaangushwa na kukunjwakunjwa na penngine kugalagazwa kwenye vumbi la fedheha na dhalilisho kwa uamuzi ambao huwa tunauchukua na mazingira ambayo huja au kutujia kwenye njia zetu kimaisha. Katika nyakati kama hizi hutokea tukajihisi kuwa hatuna thamani. Lakini tusichokijua ni kwamba, hata kama kingetutokea kitu gani, hatuwezi kamwe kupoteza thamani zetu.

Tuwe wachafu au wasafi, tuwe tumekunjwakunjwa na kutupwa kwenye vumbi la dharau na kejeli au tuwe tumetakaswa kwa kila aina ya usafi, bado thamani yetu haiwezi kununulika.

Kwa nini?

Ni kwa sababu thamani yetu haiji kupitia au kutokana na kile tunachokifanya au kutokana na akina nani tunaowajua au wanaotujua, bali jinsi tulivyo.

Thamani yetu iko ndani mwetu, kama ambavyo thamani ya noti iko kwenye noti yenyewe bila kujali kama imekunjika au ni safi. Tukiamua kwamba thamani yetu iko nje yetu, ni wazi tukikejeliwa au kuvurugwa kwenye dhalilisho na dharau, tutajikuta tukijidharau na kudharauliwa kikweli na hata wale waliokuwa wakituheshimu.

Lazima tujue kwamba, sisi ni watu maalum. Kati ya watu bilioni sita na nusu tuliopo duniani hakuna mwingine kama sisi, nasi kila mmoja kama yeye ndiye anayekamilisha idadi hiyo. Kama tumeshazaliwa ni lazima tujue kwamba hakuna mwingine tena atakayezaliwa kama sisi na hajawahi kuwepo mwingine anayelingana nasi.

Tukitukanwa, tukasingiziwa, tukaharibiwa jina, tukaaibishwa na kufanyiwa ubaya, bado thamani yetu itaendelea kuwepo. Kama tutalijua hilo, basi hakuna dhalilisho au kashfa ambayo itaweza kutufanya tuone kwamba tumevunjiwa heshima au kudhalilishwa. Hii ni kwa kuwa thamani yetu haiwezi kuguswa na mtu kwani iko ndani mwetu.

Ni sisi tu tunaoweza kamua kuitoa au kubaki bila thamani na sio mtu mwingine wala mazingira yoyote.

Kwa nini basi tuamue hivyo?

Kuna wakati huwa tunajiingiza mahali ambapo tunajiumiza bure kwa kudhani kwamba thamani yetu wanayo watu wengine. Watu hao wanapotuita wajinga au wanapotuita masikini au wanyonge, huwa nasi kwa kutojua tunakubaliana nao kwamba sisi kweli tuko hivyo na hao wanaotuita hivyo ndio ambao ni wajanja, matajiri na wenye nguvu. Hatujui kwamba kwa kufanya hivyo tumejiondolea wenyewe thamani yetu.

Lakini pale ambapo watu hao wanapotushusha na kutubeza, sisi tutawachukulia kama mkono wa mhubiri au mguu wake ambao unatukunjakunja na kutukanyaga bila kumudu kuondoa thamni yetu, hatutajisikia vibaya kwani hatutakubaliana nao.

Wengine wanasemaje kuhusu maisha yetu na wanatutendea kitu gani, sio kinachotuumiza, bali kinachotuumiza ni namna tunavyoamini. Kama tunaamini kwamba thamni yetu inapimwa nao, kuwekwa au kuondolewa nao, ni lazima watatupangia tuishi vipi. Hapo tutakuwa hatuna thamani tena kama binadamu kamili au halisi.

4 comments:
Andika Maoni Maoni
  1. Bwana Kaluse;
    Nilikuwa ninatazama hapa dakika chache tu zilizopita kipindi cha Mtambuzi mmoja anayeitwa Dr. Wayne Dyer na alikuwa anaongelea jambo hili hili. Bila kutambua thamani yetu tunajiweka katika nafasi ya kupoteza muda wetu katika mambo yasiyo na faida, tukijaribu kuwafurahisha watu huku tukidhani kwamba thamani yetu inaamuliwa nao. Pia tunapoteza uwezo wa kujiamini na wakati mwingine maisha yetu yanakosa mwelekeo na mwishowe tunashindwa kufika tunakopaswa kufika.

    Nilimuuliza swali hili Kamala jana. Lile gazeti lenu la Jitambue lililokuwa likichapisha makala za Munga Tehenan lingalipo? Kama limekufa pengine itabidi mfanye mkakati mlifufue. Makala kama hizi zina nguvu za kubadilisha maisha ya watu na inabidi ziwafikie wasomaji wengi kwa kadri inavyowezekana. Msichoke wala kukata tamaa!!!

    ReplyDelete
  2. Nasema kama Pro. Matondo ni kweli habari kama hii inabidi watu wengi wasome ni habari nzuri sana na inafundisha- Kwani ni kweli kuna watu ambao wanajisona haweana thamani hhata bila sababu. Kaka Kaluse ni kweli hilo gazeti la jitambue lifufueni na muandike habari kama hizi. Natumaini ujembe huu wengi watasoma.
    Na halafu kaka Kaluse umenikumbusha mbali kweli hiyo picha wakati nilipokuwa mdogo baba alipokuwa anatoka kazini duh! mpaka raha, Ahsante kaka:

    ReplyDelete
  3. Kaka Kaluse, sitokosea kuungana na kaka Matondo na da Yasinta.
    Unajua mara nyingi huwa tunajipotosha kuona fulani ni mtu muhimu sana na sisi tupo alimradi tupo. Kumbe tunasahau hata sisi tuna thamani kubwa pasipo kujali hali yetu kwa wakati huo.
    Ahsante sana kwa somo zuri.
    Ni post inayofaa kusomwa na kila mtu.
    Jumapili njema kaka.

    ReplyDelete
  4. hii inanikumbusha story ya mtoto mmoja ambaye alikuwa anataka kujinyonga kutokana na kuwa alikuwa hapendwi na kila mmoja, si katika familia bali pia shuleni na ktk jamii nzima.

    akasikia toka redioni juu ya washauri nasaha naye akaenda kupata ushauri utakaomsaidia aharakishe ama aahirishe kwa muda alichokuwa anataka kukifanya.

    Daktari wa masuala ya akili aliposikia akashindwa kujua amsaidieje. Wakati akiwa hajui anusuruje maisha ya kijana huyu mdogo ambaye alikuwa na akili sana darasani akatoa noti 2 za $100. Moja akaiweka ktk matope na kuitoa.

    Kisha akamuuliza mtoto: ni ipi kati ya hizi noti mbili (bill) inaweza kununua vitu zaidi ya nyingine?

    Mtoto akajibu: ZOTE ZINA THAMANI SAWA!

    Dkt akamjibu kuwa wewe sasa uko ktk stage hii ya matope kwa hiyo hata iweje THAMANI YAKO IKO PALE PALE kama wengine!

    Mtoto akaondoka zake akiwa na taswira mpya kuhusu yeye.

    Yes: HATA IWEJE, thamani yetu iko palepale!

    Asikudanganye mutu YOYOTEEE!

    ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi