0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

http://www.serenahotels.com/serenadaressalaam/default-en.html

Dec 29, 2009

KIBAKA ANAPOUAWA DUNIA IMEPOTEZA!

Sasa najua, ni nini maana ya maisha

Ni miaka 16 iliyopita, wakati huo nikiwa ninaishi na wazazi wangu Tandika,Dar es Salaam. Nilikuwa nasoma kidato cha kwanza wakati ule.Nakumbuka siku hiyo nilikuwa nimekaa mahali karibu na soko la Tandika [la zamani]. Nikiwa hapo, kijana mmoja alikurupushwa kutoka huko aliko kurupushwa. Nadhani alikuwa amefanya kosa,ingawa waliokuwa wanamfukuza walikuwa wakipiga kelele za mwizi.

Huyu kijana alipofika pale nilipokuwa, alivua shati na kujifanya kichaa anayechakura takataka zilizokuwa pale, huku akitafuna baadhi. Halafu aliniambia, “wakija waambie mwizi amepita.” Kabla hajamaliza kusema, wale waliokuwa wakimfukuza walifika pale.Kuna waliokuwa na mapanga, marungu, visu, mawe na silaha nyingine.Nilijua yule kijana alikuwa ni mwizi na miaka ile kulikuwa na kundi la vijana wahalifu ambalo lilikuwa likifahamika kama Kiboko Msheli.

Nilikuwa ni miongoni mwa wale ambao waliokuwa wanawaogopa sana hao Kiboko Msheli baada ya shangazi yetu aliyekuwa akiishi Magomeni Makuti kucharangwa mapanga na vijana hao na kuporwa kila kitu nyumbani kwake.Kwa hiyo, nilitaka kuwaambia wale watu kwamba, mwizi wao yuko pale mbele yao.Lakini kitu fulani kiliniambia niache, amekuomba kwa wema, mwache, huenda anastahili kuishi.’Sauti iliniambia kutoka ndani mwangu.

Ni kweli wale watu waliokuwa na hasira waliniuliza, “mwanafunzi, huyu Kibiko Msheli ameelekea wapi?” Waliniuliza kwa sababu, eneo nililokuwepo ilikuwa vigumu kwa mtu kuvuka upande wa pili. “Kaenda huku, karuka hapo akapandia kwenye bati, akaondoka.” Nilisema nikiwa natetemeka.Halafu mmoja kati ya watu wale aliuliza, shati ameliacha hapa.Mbona huyu naye hana shati?’Alisema akimwangalia yule jamaa aliyejigeuza chizi.

Nilisema, “huyu ni kichaa na shati sio lake, shati nila yule Kiboko Msheli, kalivua akaliacha hapa” Kundi lile ambalo tayari lilikuwa limegeuka kumkabili yule kijana, lilibadili mawazo na kuanza kuondoka.Nilikuwa na tetemeka kupindukia.

Yule kijana alipoona watu wale wameondoka kabisa wakiishia kusema, “bahati yake” aligeuka na kunitazama kwa mda mrefu.

‘Umeokoa maisha yangu. Yaani sijui nikushukuru kwa namna gani, sina hata la kusema. Ni kweli, nimemkwapua mama mmoja mkoba, nikakosea stepu.Lakini, kuanzia leo sidhani kama nitaiba tena, sidhani.Unaitwa nani rafiki yangu?’Yule kibaka aliniuliza. Nilikuwa natetemeka sana, hasa baada ya kijana yule kukiri kwamba, ni kibaka na ametoka kufanya jaribio la kumpora mama mmoja. “Naitwa Punja, jina langu Punja…”

Alinitazama huku akiwa anatabasamu. “Umefanya nini shavuni? Aliniuliza, kwani nilikuwa na kovu la duara kwenye shavu. Nilimwambia nilizaliwa hivyo. “Una roho ya kibinadamu, nimeelewa sasa, bado kuna watu wanaopenda watu.” Alisema, ingawa sio kwa maneno kama hayo moja kwa moja. Alizungumza kama vile kwenye maisha yake hajawahi kukutana na mtu anayeweza kumpenda.

Halafu aliniomba fulana. Nilikuwa nimevaa fulana ya michezo ndani ya shati la shule.Kwa hofu zaidi kuliko wema, niliivua na kumpatia.Aliivaa na kumuenea. Hakuwa na mwili mkubwa, bali alikuwa amekomaa.

“Nimebadilika, siwezi kuwa Kiboko Msheli tena.Nakuahidi mwanangu, kweli amini tu…” Alisema kwa lugha ya kihuni, alafu aliondoka akiliacha shati lake pale chini. Nilipumua kwa ahueni.Niliondoka kwenda shuleni huku nikijiuliza ingekuwaje kama ningewaambia wale watu wenye hasira kwamba, yule jamaa hakuwa kichaa bali ndiye kibaka mwenyewe.Damu ilinikimbia, nilipofikiria namna ambavyo wangemuuwa.

Siku zinaenda. Nilimaliza kidato cha nne mwaka 1994, lakini sikufanya vizuri, kwani matokeo yalikuwa ni divisheni ya nne, tena inayokaribia ziro. Nilikuwa nimebakisha point mmoja niingie ziro. Mwaka huohuo mwezi wa Agost baba yangu alifariki.Baba alikuwa akifanya kazi serikalini na mama alikuwa ni mama wa nyumbani, ingawa alikuwa na vijishughuli vyake.

Kufariki kwa baba kuliharibu kila kitu katika mipango yangu ya baadaye, hasa masomo na mambo mengine. Baada ya mazishi ya baba ambayo yalifanyika kijiji cha Ulaya, Kilosa, Morogoro, nilikaa kule kwa miezi mitatu kwa baba mdogo. Baadae nilirudi Dar kuanza kuangalia ningeishi vipi. Lakini mambo hayakuwa rahisi kwani baba hakuwa ameacha kitu cha maana kwetu watoto. Mimi nilikuwa ni mtoto wa kwanza na nilikuwa na wadogo zangu watatu.

Pesa za malipo yake ya kazini zilitumika zaidi kulipa Madeni ya watu na zilizobaki kidogo tulinunua kiwanja eneo la Mbezi ya Morogoro Road. Kwa hiyo kuanzia pale tukawa tunaishi kwa kuhangaika sana.

Maisha yalizidi kuwa magumu na mdogo wangu anayenifuatia aliacha shule kidato cha pili mwaka 1996. Wawili walikuwa shule ya msingi na mmoja alimaliza mwaka huo huo wa 1996. hakufanikiwa kupata nafasi shule ya serikali, hivyo akalazimika kukaa nyumbani.

Mama alilazimika kuuza kiwanja cha Mbezi ambacho kilikuwa hakijafanyiwa chochote ili mdogo wangu aliyesimamishwa shule aweze kuendelea na masomo. Alikiuza, lakini bei ilikuwa ni ndogo sana kwani hakikuwa mahali pazuri sana. Alikiuza kwa shilingi 300,000. Ilibidi bwana mdogo arudi shule. Wakati huu mama alikuwa ameanza kuumwa mara kwa mara. Afya yake ilianza kuzorota siku hadi siku.

Kufikia mwishoni mwa mwaka 1997 hali yake ilikuwa ni mbaya sana. Tulimpima hadi Ukimwi lakini hakuonekana na tatizo lolote. Alikuwa akiumwa mwili mzima na kuna wakati alikuwa akipoteza fahamu. Kwa hiyo alisimama kabisa kufanya chochote.

Kwa kuwa ndiye aliyekuwa akiilisha familia, hali ilianza kuwa ngumu kupita kiasi. Kuna wakati tulikuwa tunashinda na kulala na njaa . Yule mdogo wangu wa Sekondari alisimamishwa tena shule. Ilibidi nitafute vibarua kwa nguvu zangu zote lakini nikawa kama vile nina mkosi, kwani sikuwa napata vibarua hata vile ambavyo tunasema ni vya watu wa chini kabisa.

Labda pia kwa sababu umbo langu lilikuwa ni dogo na vibarua vya aina hiyo vilikuwa vinahitaji nguvu.

Mwaka 1998, mama alikuwa hajiwezio kabisa. Mwenye nyumba naye akawa anatutishia kwani tulikuwa hatujamlipa kwa karibu mwaka mmoja. Pamoja na kumwona mama katika hali ile ya kushindwa hata kusimama, alikuwa akitutishia kututoa kwenye nyumba yake . Kwa kweli nilijua hasa maana ya maisha katika kipindi kile.

Kuna wakati nilikuwa ninakaa chini na kujiuliza ni kitu gani hasa nilichomkosea Mungu au ni laana gani familia yetu ilikuwa imepata.

Mwaka 1998, mama alikuwa hajiwezi kabisa. Mwenye nyumba naye akawa anatutishia kwani tulikuwa hatujamlipa kwa karibu mwaka mmoja. Pamoja na kumwona mama katika hali ile ya kushindwa hata kusimama, alikuwa akitutishia kututoa kwenye nyumba yake . Kwa kweli nilijua hasa maana ya maisha katika kipindi kile.

Kuna wakati nilikuwa ninakaa chini na kujiuliza ni kitu gani hasa nilichomkosea Mungu au ni laana gani familia yetu ilikuwa imepata.

Wadogo zangu wawili nao walijiunga nami kufanya vibarua huku na kule ili kumwezesha mama kupata angalau hata uji. Mdogo wetu wa mwisho ambaye alikuwa wa kike ndiye akawa anamtunza mama.

Kumwogesha na kumbadilisha nguo ikawa ni juu yake, kwani sisi tuliogopa. Ndugu wa mama walikuwa mbali, Sikonge Tabora tena huko ndani vijijini sana. Hivyo ikawa ni sisi wenyewe kukabiliana na hali ile.

Pamoija na kuumwa, mama alikuwa akituambia tusikate tamaa, "Hata nikifa msikate tamaa, mtamudu tu. Nimewalea ili muweze siyo ili msindwe, mtaweza na inabidi msaidiane. Huoni mnaweza kunilea….”

Maneno yake yalikuwa yanatupa moyo lakini yalikuwa yanatuumiza kwa upande mwingine.

Nakumbuka ilikuwa ni February 1999. Ilikuwa jioni saa moja niliporudi nyumbani nilikuta mwenye nyumba ametoa vitu vyetu nje na ametia kufuli vyumba vyake.

Tulikuwa tumepanga vyumba viwili na sebule, pale nje nilimkuta mdogo wangu wa kike akiwa amejiinamia akilia. Jambo la kwanza nililouliza ni mahali alipokuwa mama. Mdogo wangu alisema, “yuko kwa jirani”. Huyu jirani yetu alikuwa ni mtu ambaye hakuwa akielewana na mama sana. Lakini kwa jinsi alivyoiona hali ya mama ya kutupwa nje mchana wa jua kali aliamua kumhifadhi.

Nilikwenda moja kwa moja kumwona. Nilimkuta nje tu ambapo nilimsalimu na kumshukuru kwa wema wake. Alisema kwa kifupi, “nashukuru, lakini nawasaidia kwa siku tatu tu. Baada ya hapo itabidi wenyewe mtafute mahali pengine. Vyombo vyenu mnaweza kuviweka stoo, mkipata pa kuishi mnaweza kuvichukua.” Nilimshukuru hata hivyo. Niliomba kuingia ndani kumwona mama.

Nilimkuta akiwa amegeukia ukutani akiwa analia. Nilimbembeleza na kumwambia "nitapata pa kukaa kabla ta siku tatu na utapona tu ." Sijui hadi leo kwa nini nilisema maneno yale huku nikiyaamini kabisa.

Nilitoka nje baada ya kusema hivyo na nikawa natembea bila kujua ninakoenda. Nilitembea kutoka Tandika hadi nikajikuta niko Temeka, karibu na kituo cha Polisi cha Chang'ombe.

ITAENDELEA..............................

2 comments:
Andika Maoni Maoni
  1. Jamani simulizi inasisimua na inasikitisha hii nasubiri muendelezo wake. kaka Shaban usichelewe kuubadika muendelezo

    ReplyDelete
  2. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!Wednesday, December 30, 2009

    nami nakubaliana na Yasinta. chondechonde kaka Kaluse...nahisi mapigo ya moyo yanakwenda ndiko siko :-(

    ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi