0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Dec 31, 2009

KIBAKA ANAPOUAWA DUNIA IMEPOTEZA-SEHEMU YA MWISHO (IMEREKEBISHWA)

Sasa nafahamu, ni nini maana ya maisha.
ILIPOISHIA..............

Nilitoka nje baada ya kusema hivyo na nikawa natembea bila kujua ninakoenda. Nilitembea kutoka Tandika hadi nikajikuta niko Temeka, karibu na kituo cha Polisi cha Chang'ombe.

SOMA HAPA.......

Halafu wazo lilinijia kuhusu jamaa yangu mmoja ambaye tulimaliza naye shule. Nilisikia kwamba alikwenda kusomea upolisi , Moshi na alikuwa pale kituo cha Polisi cha Chang'ombe.

Niliamua kwenda kumuulizia pale. Niliambiwa alikuwa ameshatoka. Wakati namuulizia kulikuwa na raia wengine kando. Mmoja kati yao alikuwa anamwekea dhaman ajamaa yake, aqlinitazama sana na kuniomba nimsubiri amalize shughuli ile ya dhamana. "Ningeomba tuzungumze kidogo, samahani kama nitakuwa nimekusumbua ." Nilimwambia "sawa." Nilitoka nje ya kituo na kumsubiri.

Alitoka na huyo mtu aliyemwekea dhamana. "Nakwambia hivi, hii ni mara yngu ya mwisho kukuwekea dhamana. Ukifanya tena upuuzi wako, usidhani utaniona kuja kuhangaika. Nenda zako, wala sikupi lifti, tutakutana nyumbani." Alimwambia huyo kijana ambaye alionekana wazim kuwa ni mhuni. Yule kijana alisita, lakini aliondoka.

"Ni shemeji yangu, anatusumbua sana, sijui ana laana gani." Yule jamaa alisema akiniambia. Kwa hali yake ambayo ilikuwa inaonesha kwamba alikuwa na uwezo, nilishindwa kujua niseme kitu gani.

Nilijikuta tu nikisema, "atabadilika, maisha yatamfundisha atabadilika siku moja." Yule jamaa alisema , "ni kweli, kama ulivyonibadilisha." Halafu alinyamaza. Nilibaki nimenyamaza, kwani sikumwelewa kabisa.

Halafu aliniambia, "twende tukazungumze mahali penye utulivu, hapa pa wenyewe, unaweza kugeuziwa kibao." Alisema akimaanisha pale polisi . Tuliongozana hadi kwenye gari. Lilikuwa ni gari aina ya Suzuki Escudo la rangi ya dhahabu. "Karibu." Aliniambia. Kama bwege niliingia ndani ya gari na kufunga mlango. Aliwasha gari na kuondoka. Tulienda kwenye baa moja palepale karibu na Chang'ombe polisi upande wa juu tu kidogo.

Tulipokaa tu vitini aliniuliza, "nitakosea nikisema weweni Punja?" Nilishtuka na kushikwa na butwaa zaidi. "Mimi ni Punja ndiyo, ndiyo jila langu…..” Halafu mhudumu alikuja kutruhudumia. Yule bwan alicheka kw afuraha ya wazi kabisa. Halafu aliniuliza kama siwezi kumkumbuka, wakati tulisoma wote. “Wewe ulikuwa darasa la pili, mimi nilikuwa la sita , umesahau, hebu kumbuka.”

Nilijitahidi kurudisha kumbukumbu zangu nyuma enzi za shule, bila mafanikio. Lakini kwa sababu sikutaka kumfanya ajisikie vibaya, nilimwambia, “ni kweli kama nakukumbuka kidogo, sema jina tu nimelisahau.” Yule jamaa alicheka tena na kunigonga mkononi. Alionekana kweli alifurahi.

“Kweli kumbukumbu zako sio kali sana. Umesahau siku moja ulipokuwa sokoni Tandika kuna kibala alitaka kuuawa ukamwokoa…..”
Halafu alinyamaza kama vile naye alikuwa anajaribu kuanza kulikumbuka tukio lile upya. Nilikuwa kidogo nimeanza kusahau tukio lile lakini lilirudi kwenye kumbukumbu zangu haraka. Ndiyo, sura yake haikuja kirahisi, lakini tukio lilinijia akilini kama vile ndio linatokea. Nilitabasamu, lakini pia nikiwa nimeingiwa na mshangao……

“Nakumbuka, nakumbuka vizuri ….Lakini sijui umenikumbuka vipi, maan naona nilikuwa mdogo” Yule jamaa alinikatisha . “Jambo ulilofanya siku ile siyo tu kuokoa maisha yangu, bali ulinibadili kabisa. Ujue nilibadilika kabisa kwa sababu yatukio lile . Nilianza maisha tofauti hadi nimefikia hapa unaponiona.

Siku hizi nnafanya biashara na mafanikio ninayaona. Ulikuwa mtoto, lakini ulikuwa na moyo mkubwa sana, ulikuwa na utu wa kweli. Mtoto wa mjini aone kibaka, aogope kumpigia kelele……”

Kwa kweli kwa sehemu kubwa kwa wakati ule pale, nilikuwa najiona kabisa kuwa ninaota ndoto nzuri halafu yenye utata. Aliniuliza kuhusu maisha yangu, baada ya kuona mshangao wangu umepungua.

Nilimweleza kila kitu kwa kweli. Sikuwa napenda sana kusema matatizo yetu kwa kila mtu, ingawa pale mtaani hakuna ambaye hakuwa anayajua.

“Sikiliza mdogo wangu,” aliniambia baaada ya mimi kumaliza kueleza. “Mimi nihesabu kama kaka yako kabisa, yaani nichukulie hivyo kuanzia leo, matatizo yako yachukulie kama yangupia. Naomba usijali sana , tutasaidiana.”

Bado nilikuwa nahisi kama ninaota na nilitarajia kuwa muda wowote ningeshtuka kutoka usingizini. Lakini, sikushtuka na nilianza kuamini kwamba ilikuwa ni kweli inatokea.

'Nilikuahidi siku ile kwamba, nitaacha kabisa tabia ya wizi. Niliacha kweli na kuamua kuwa mtu tofauti sana. Hata nyumbani walishangaa sana na sikumwambia yeyote niliweza vipi kujitoa kwenye tabia ile. Lakini, siri yangu ilikuwa hapa, moyoni.

Wewe ndiye ambaye ulinifanya nitoke kwenye tabia ile.

“Nilijisikia vibaya sana nilipoondoka na fulana yako siku ile’ Alisema na ilibidi nicheke pamoja naye.

Usiku ule tulitoka pale hadi nyumbani kwa jirani yetu ambapo mama alikuwa amehifadhiwa.

Kufika pale tulikuta ugomvi. Yule jirani aliyemfadhili mama alikuwa akiwafokea ndugu zangu kwamba, wamewaruhusu wageni kuja kumuona mama na hivyo watamletea wezi nyumbani kwake.

Ilikuwa bahati, kwa sababu yule jamaa yangu naye alisikia kila kitu, kwani nilishamwambia kuhusu yule jirani yetu na msaada wake wa masharti.

Ilibidi yule jamaa ambaye sasa nilikuwa namwita kaka, ajitambulishe mwenyewe kwa yule jirani yetu.

Alisema yeye ni mtoto wa dada yake mama na amekuja kumshukuru kwa kutoa msaada ule. Halafu alimuomba kama angeturuhusu tumchukue mgonjwa wetu. Nilishangaa na kuogopa. Tumchukuwe tumpeleke wapi? Nilijiuliza.

Yule jirani alisema ni afadhali na kuanza kuponda kwamba, yule kaka amemwacha mama yake anatimuliwa kwenye nyumba nakudhalilishwa na hadi wakati ule ndiyo anajitokeza.

Yule kaka yangu hakujibu kitu. Aliniomba nikatafute pick-up ambayo ingetosha vitu vyetu.

Nilikwenda kituo cha pick-up haraka na kuchukua gari nikiwa sijui kitafanyika kitu gani. Niliporudi, yule kaka yangu mpya aliniambia nipakie mizigo yetu garini, kwani tungehama usiku uleule. Wakati tuna pakia mizigo alipiga simu kumwita kijana wake mmoja. Alimuelekeza mtaa tuliokuwepo.

‘Akija huyu kijana wangu, atawachukua ndugu zetu hadi Tabata.
Kule kuna nyumba yangu ambayo haina mpangaji, mtaingia mle na tutaangalia baadaye mipango mingine. Kwa sasa mtaishi mle kwanza. Mimi na wewe, akishafika huyu jamaa tuta mchukua mama hadi hospitalini.’ Alisema kwa kujiamini.

Ukweli ni kwamba nilihisi kama, sinema fulani hivi, kama ndoto tupu ambayo ingefika mwisho muda wowote. Bila shaka nawe unaposoma Habari hii sasa hivi unahisi kama ndoto au hadithi tu. Nataka uamini, kwa sababu itakusaidia kwenye maisha, sio hadithi.

Watu walijaa pale kwenye nyumba ya jirani wakishuhudia kuhama kwetu. Bila shaka nao walikuwa wamepigwa na butwaa kuona au kugundua kwamba, kumbe tuna kaka mwenye uwezo.

Natamani siku ile ijirudie tena, kwani ndio siku ambayo nilihisi furaha na hali nyingine ambayo wala nisingeweza kuielezea. Nilihisi hali fulani ambayo naijua mwenyewe huko ndani, siwezi kuisema kwa maneno.

Yule kijana wa kaka alifika na kaka alimpa maagizo ya kuwapelekea wale ndugu zangu kwenye nyumba ya Tabata. “Hakikisha wanapata chakula pale kwa Ben, mwambie malipo kesho.” Alitoa maelekezo.

Yule kijana wake alikubali na kuanza kusaidia kupakia yombo garini. Lakini, kaka alimuita na kumuomba tukasaidiane kumchukua mama ndani.

Tulimtoa mama ndani kwa msaada wa jirani zetu na kumuingiza garini. Ilibidi tuondoke kumpeleka hospitalini. Tulimpeleka mama hospitali ya Agakhan.

Baada ya kufanyiwa vipimo na kupatiwa kitanda, tuliondoka kurudi nyumbani, ambapo sasa ilikuwa ni Tabata.

Yule kaka alinihakikishia kwamba, nisijali kabisa kuhusu yote anayoyafanya, kwani anayafanya kwa moyo mmoja.

Aliniambia kwamba huenda Mungu aliniweka pale sokoni siku ile ili kupitia kwangu, yeye waweze kujifunza ukweli mkubwa kuhusu maisha.

Hivyo kile kilichoniweka pale sokoni siku ile ndicho ambacho kilinifanya kuzurura hovyo hadi tukakutana polisi jioni ile.

Ni kweli huenda. Nilikubaliana naye. Hata hivyo, kunikumbuka, ndilo jambo ambalo lilinifanya nishangae sana. Ni kweli nilikuwa na kovu shavuni lakini hata jina nalo!

Tulihama baadae na kwenda kuishi Buguruni ambako nilipanga nyumba. Hii ilikuwa ni miezi sita baada ya kuhamia Tabata kwenye nyumba ya kaka. Wiki moja tu baada ya kuhamia pale, aliniuliza kuhusu shughuli ambayo ningependa kuifanya.

Nilimwambia ningependa kufanya biashra ya mipakani, Hii ni shughuli ambayo nilikuwa naipenda sana maishani mwangu, tangu utotoni.

Alinipa mtaji na nikaanza biashara. Kwa kweli nilianza na bahati na nimeendelea kuwa nayo.

Mama yangu alipona baada ya kukaa hospitalini kwa wiki tatu. Hadi leo anajiona kuwa anaota kwa kile kilichotokea hajaamini.

Nataka nikwambie ni kwa nini nimeamua kukusimulia kisa hiki.

Hivi majuzi wakati nikiwa natokea Kariakoo naenda Ilala, nilipita mahali ambapo nilikuta kijana mmoja akiwa anaomba asaidiwe na wenye nyumba, pale eneo la Bungoni. Inadaiwa kwamba, huyu kijana alikuwa amempora mtu.

Nilisimama kujua kuna nini. Nilimsikia yule kijana akisema kwa kujiapiza kwamba, hakuwa ameiba ni uongo mtupu.

Aliwaomba wale wenye nyumba wasimtoe kwa vijana kama nane hivi ambao walikuwa wanamtaka kwa madai hayo.

Wenye nyumba hata hivyo walimtoa kijana yule kwa nguvu, kwa kumburuza. Nilishuhudia akipigwa kwa njia ya kutisha.

Siyo wale vijana peke yao, bali walizuka watu wengine ambao walikuwa hawajui chochote kuhusu kijana yule, ambao nao walianza kumshambulia.

Nilondoka eneo lile nikiwa ninadondokwa na machozi. Sijui kama kijana yule alikufa au alipona. Lakini nina uhakika hata kama alipona ni lazima angekuwa na ulemavu wa kudumu.

Najiuliza kila wakati, lini jamii itabadilika na kuyajua matatizo ya wengine kama ambavyo nasi wengine watajua matatizo yetu na kutusaidia ? Ndilo swaIi langu kwa jamii.

******************MWISHO******************

3 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. HIZI SIJUI HADITHI AU HABARI AU KWELI ZINASISIMUA MNO ZINASIKITISHA NA KUTOA MACHOZI MH DUNIANI KUNA MAMBO KILA JAMBO LIKITOKEA LINA SABABU!

  ReplyDelete
 2. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!Saturday, January 02, 2010

  Kaka Kaluse, aksante kwa kisa hiki ambacho ukikisoma hakichuji kwani nishakisoma pahala enzi hizo za Jitambue.

  Hata hivo kinakosa link kati ya sehemu ya kwanza na ya pili hasa kati ya yaliyojiri pale kituoni changombe hadi kufika kule aliko mgonjwa.

  tumegee tafadhali kwani naona kama imesahaulika...lol

  ReplyDelete
 3. Nakubaliana na wewe kaka Chacha.
  Nimeirekebisha, nilighafilika kaka.

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi