KESI ILIYOZUA UTATA:
ILIPOISHIA.......
ENDELEA KUSOMA HAPA.................
kwa kipindi cha miezi tisa kilikuwa ni cha kuchapa kazi kama kawaida na katika kipindi hicho aliweza kufichua kashfa kadhaa za rushwa na uhalifu zilizotamalaki katika jiji la Dublin.
Kutokana na kufichua uozo huo, Veronica alijitanabahisha kama adui namba moja aliyekuwa amejijengea maadui wengi miongoni mwa wahalifu wakubwa. Mnamo mwaka 1995 Septemba, Veronica aliona huo ndio wakati muafaka wa kulivaa gwiji la uhalifu liitwalo John Gilligan ili amhoji maswali kadhaa.
Historia ilikuwa inamuonesha John Gilligan kama mhalifu mzoefu ambaye si chini ya miaka mitatu iliyopita ndio alikuwa ametoka jela, lakini kwa kipindi kifupi akawa amefungua mradi uliogharimu mamilioni ya dola.
Veronica alitaka kujua amewezaje kufungua mradi mkubwa vile na kwa muda mfupi kiasi kile, tangu alipotoka jela? Alikwenda kwa Gilligan bila taarifa na kwa mujibu wa maelezo yake, alipofika nyumbani kwa Gilligan alikutana naye mlangoni akiwa na vazi la kuogea.
Inasemekana Gilligan alikuwa mkali na alipomkaribia alimsukuma na kofi la uso na baadae la kifuani huku akimwambia, 'kama ukiandika jambo lolote linalonihusu mimi, hakika nitakuua wewe, mumeo, mtoto wenu, familia yako na kila mtu anayekuhusu.'
Alipomaliza kusema hivyo alimsukumia kwenye gari alilokuja nalo kisha akamchania nguo zake ili kuangalia kama veronica alikuwa na mashine ya kunasia sauti ambayo hata hivyo hakuwa nayo. Baada ya kuhakikisha kama hakuwa na kinasa sauti alimuamuru aondoke pale haraka sana. Kwa vile lilikuwa ni shambulio la moja kwa moja, ukweli ni kwamba lilimtisha sana Veronica kushinda matukio mawili ya nyuma yaliyohusisha silaha.
Baada ya kuripoti tukio lile kwea bosi wake, ilibidi washauriane na mwanasheria wa gazeti na hatimaye walifungua kesi ya shambulio dhidi ya Gilligan.
Kutokana na shambulio lile Veronicas alianza kufikiria kuacha kazi ile ya uandishi wa kiuchunguzi, hasa baada ya kuona familia yake nayo iko hatarini kwa sababu ya kazi anayoifanya. Siku ya jumanne ya tarehe 25, Juni 1996 John Gilligan alifikishwa katika mahakama ya Dublin akishitakiwa kwa kosa la shambulio la aibu dhidi ya Veronica Guerin.
Gilligan alikanusha mashitaka na kuachiwa kwa dhaman akisubiri kesi kusikilizwa rasmi tarehe 9 Julai, 1996. Baada ya kesi hiyo kuahirishwa, Gilligan aliondoka mahakamani moja kwa moja na kuelekea uwanja wa ndege na kupanda ndege kuelekea Amsterdam, safari ambayo aliieleza kama ya kibiashara.
Gilligana alijua dhahiri angehusishwa na mauaji ya Veronica, hivyo kuwepo kwake nje ya Ireland alijua kungemsaidia kutohusishwa na mauaji yale.
Alipopigiwa simu na mwandishi wa gazeti la Daily Mail alijibu kwa mkato, ‘sijafanya jambo lolote baya na wala sina ushahidi wowote kuhusiana na mauaji hayo, na ninadhani mauaji hayo yamepangwa na kutekelezwa ikiwa ni mpango maalum ili nihusishwe.
Wakati Gilligan akiwa ni mtuhumiwa katika mauaji ya Veronica, polisi wa Dublin waliingia katika operesheni maalum ya kuwasaka watuhumiwa wakubwa na waliokuwa kama miungu watu. Katika operesheni hiyo iliyohusisha wapelelezi maalum wapatao 50, walifanikiwa kuwahoji washukiwa zaidi ya 1,000, miongoni mwao watuhumiwa 60 walitiwa nguvuni lakini hakuna aliyeshitakiwa kwa kosa la mauaji ya Veronica Guerin.
Hata hivyo polisi hao walifanikiwa kikamata fedha zenye thamani ya dola 200,000 na silaha zilizokuwa zikimilikiwa kinyume cha sheria.
Mnamo tarehe 8 October 1996 John Gilligan alikamatwa na askari wa ushuru kwenye uwanja wa Heathrow jijini London akiwa njiani kupanda ndege kuelekea Amsterdam, huku akiwa na kiasi kikubwa cha pesa kinachokadiriwa kufikia dola 500,000.
Alishitakiwa kwa kifungu cha sheria ya usafirishaji wa dawa za kulevywa pamoja na kiasi kikubwa cha pesa. Gilligan aliwekwa kwenye gereza lanye ulinzi mkali la Belmarsh, ambapo alihojiwa na maofisa kadhaa wa polisi kuhusiana na tuhuma zinazomkabili ikiwemo ya mauaji ya Veronica Guerin, lakini alikanusha kuhusika na mauaji hayo.
Siku kumi baada ya Gilligan kukamatwa, kijana mmoja aitwae Paul Ward, aliyekuwa na umri wa miaka 32 alikamatwa na kushitakiwa kwa kosa la la kula njama na kutekeleza mauaji ya Veronica Guerin, pamoja na kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la utani kama Tosser ambaye ndiye aliyeaminika kuwa aliendesha pikipiki siku ya mauaji. Watu hao wawili walifikishwa mahakamani ingawa vielelezo kama vile pikipiki na silaha iliyotumika havikupatikana.
Mnamo November 1998 Paul Ward alipatikana na hatia ya mauaji ya Veronica Guerin na kuhukumiwa kifungo cha maisha. Wakati akiendelea kutumikia adhabu yake ya kifungo cha maisha, mtu mwingine aliyejulikana kwa jina la Brian Meehan naye alipatikana na kosa la kushiriki katika mauaji ya Veronica Guerin.
Kama vile Paul Ward, naye alihukumiwa kifungo cha maisha. Kwa upande wa John Gilligan, kesi yake iliendelea kuunguruma nchini Uingereza na hatimaye alihukumiwa kifungo cha miaka 28 kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya, adhabu ambayo ilipunguzwa hadi miaka 20 baada ya kukata rufaa.
Tukio la kuuawa kwa mwandishi huyu wa habari lilipelekea kutengenezwa kwa filamu mbili zilizojizolea umaarufu ambazo ni When the Sky Falls iliyotengenezwa mwaka 2000 na nyingine iliyopewa jina la mwandishi huyu, iitwayo Veronica Guerin iliyotengenezwa mwaka 2003.
Hata hivyo yupo mwandishi mmoja wa habari nchini Ireland aitwae Emily O’Reilly ambaye ametunga kitabu kinachozungumzia maisha hadi kifo cha Veronica Guerin alichokitoa mwaka 1998 na kukipa jina la Life and Death of a Crime Reporter.
Kitabu hicho ambacho kinaonekana kinamsimanga Veronica na waajiri wake, kwamba Veronica binafsi alikuwa mzembe na aliyejisababishia umauti wake mwenyewe, kimeshutumiwa na watu wengi, kiasi cha kumuita mama huyu aliyetunga kitabu kwamba ana roho mbaya na anatafuta umaarufu kupitia mgongo wa Veronica Guerin baada ya kifo chake, madai ambayo, Emily binafsi aliyakanusha wakati alipohojiwa na BBC.
***************MWISHO*******************
Kuna watu wanafanya lolote jema kwa wengine na kitakachotokea na kitokee na kuna wengine wanakuwa wabinafsi sana. Namsifu Veronika kwa ujasiri wake.Upumzike kwa amani peponi amina.
ReplyDeleteTuko pamoja katika uhalisia wake...!
ReplyDelete