0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

http://www.serenahotels.com/serenadaressalaam/default-en.html

Mar 27, 2009

UMASIKINI SAWA, LAKINI KWA NINI TUWACHUKIE WALIOFANIKIWA?

Hatuna haja ya kuchukia hali zetu

Ni kitu gani kinachotofautisha binadamu yaani kutoka binadamu mmoja hadi mwingine? Ni wazi ni vitu vingi sana kiasi kwamba haiwezekani kwa kuvitaja vyote na kuvimaliza katika nafasi hii ndogo. Lakini bila shaka inatosha kusema kwamba kama binadamu hatuwezi kulingana.
Kuna miongoni mwetu ambao tuna mafanikio makubwa kimaisha na wengine tukiwa katika kukubali ugumu mkubwa kimaisha. Katika hali hizo mbili kila mmoja wetu ana namna anayoichukulia hali yake. Kati yetu hufurahia na na kuringia mafanikio yetu huku tukitaka zaidi na zaidi wakati wengine tukichukia na kujichukia kutokana na ulitima tuliokuwa nao.

Hebu tujiulize sisi ambao tunaishi katika ulitima au ufukara huwa tunajitazama vipi, huwa tunaichukulia vipi hali yetu na kuiamulia vipi? Tukijiuliza kwa makini tutagundua kwamba kwa sehemu kubwa huwa tunaichukia hali yetu ya ulitima au ufukara. Kuichukia hali hii siyo kuichukia kwa kwa kufanya juhudi kuiondoa, bali ni kuichukia kwa kutafuta ‘mchawi’ ambaye tunadhani ndiye anayetusababishia hali hii.

Kwa kawaida kwa kuzingatia kanuni za mfumo wa mawazo ya binadamu ni kwamba tunapochukia hali zetu ina maana pia kuwa tunajichukia wenyewe ingawa huwa hatujui kwamba tunajichukia. Kwa kuwa tunajichukia wenyewe siyo rahisi kubaini kwamba mitazamo yetu kuhusu hali zetu ni kioo cha sisi na udhaifu wetu. Tunapotafuta mchawi wa hali zetu huwa tunafanya hivyo kwa sababu ya udhaifu wetu ambao kamwe hatuko tayari kuukubali.

Inapotokea tukaanza kuchukia ufukara tulio nao kwa njia ya kulalamika na kulaani ama kukata tamaa tukafikia mahali pa kujidharau na kujibeza na huku tukiamini kwamba hatuna thamani ndipo ambapo hufikia mahali pa kuanza kuwachukia wale wote ambao wana mafanikio maishani. Tunawachukia hao kwa kudhani kwamba wao wana thamani kubwa kuliko sisi kwa hiyo wanatubeza. Tunawachukia hawa kwa njia ya kujaribu kupunguza ugigili tulionao kwa hali zetu.

Tunajisikia ahueni kuwachukia na kuwasema vibaya huku tukijaribu kurusha ‘dua za kuku’ ambazo ni wazo haziwezi kuwapata kwa sababu hawako kama sisi tunavyowatazama. Kile tunachokiona kwao ndiyo udhaifu wetu tukiona kujichukia kwetu kupitia kwao kwa sababu kama binadamu tunajipenda sana na hivyo kuwa vigumu kwetu kujichukia.

Ni kweli kwamba wengi wetu tusio na uwezo kamili ambao ni mafukara, wengi wetu tusio na elimu, tusiojua au kutumia vipaji vyetu huwa tunawachukia wale wenye uwezo waliosoma na wenye vipaji au wanaojua kuvitumia. Chuki hizi huwa tunazitoa kwa kutamani kwetu kuona wakianguka kujaribu kuwaharibia majina kufurahi wanapoingia kwenye matatizo na kuwapiga vita ya moja kwa moja..

Siyo kweli kwamba ufukara wetu ndiyo unatufanya kuwa na tabia hiyo, bali namna tunavyoutazama na kuutafsiri ufukara huo. Kama tunaamini kwamba ufukara wetu siyo jambo la ajabu na wala hautuondolei thamani yetu na kuwaona waliofanikiwa kama watu sawa na sisi hatuwezi kuwajengea chuki na kuwapiga vita. Kama tukiuchukulia ufukara wetu kama jambo la kawaida na la muda mfupi ambalo litarekebishwa na kuondoka siku fulani hatuwezi kuwachukia waliofanikiwa.

Badala yake tutawatazama kama kioo cha kuonea udhaifu wetu na kuwakubali. Tutawatazama na kujiuliza ni kwa vipi wao waweze, tutajaribu kuiga au kuuliza mbinu zao za mafanikio tutawachukulia kama mfano hai wa uwezo wa binadamu kupata akitakacho maishani na tutawapenda kwa sababu hatuna sababu ya kuwachukia. Kwa kufanya hivyo nasi tutajikuta tukipambana na maisha ili kutoka katika hali tulionayo. Tutafanya hivyo kwa sababu tutakuwa tumekubali kujifunza kutoka kwao.

Lakini kama hatutakuwa tumewatazama kwa njia hiyo na badala yake kuwatazama kinyume tutajikuta tukiwajengea chuki tukiwaona wanaringa tukiwaona ni wajuaji na kuwaona wakiwa na kila kasoro. Chuki ni kama tulivyobainisha ni kujichukia kwetu kwa kushindwa kwetu kujua namna ya kusogea hivyo kwa kujichukia kupitia kwao tunapata ridhiko na kuendelea kubaki katika hali zetu. Tunabaki katika hali zetu kwa sababu hutujifunzi kutoka kwao udhaifu wetu na kuukubali bali tunajifunza uongo kwamba watu hao ndiyo dhaifu au wenye matatizo na kasoro.

Jaribu kufanya uchunguzi au utafiti utagundua kwamba watu wote fukara wenye chuki dhidi ya wale waliofanikiwa kamwe maisha yao hayawezi kubadilika hadi wanakwenda kaburini. Hayawezi kubadilika kwa sababu badala ya kujifunza na kuujua udhaifu wao kupitia kwa wengine waliofanikiwa wao hujifunza kuukimbia udhaifu wao kupitia kwa hao waliofanikiwa.

Ni vizuri tukawaambia wale ambao wana hali mbaya kimapato kwamba hiyo siyo hali yao. Hakuna binadamu ambaye ameandikiwa kuwa kama alivyo leo bali kila mmoja kwa sehemu yake kubwa huamua mwenyewe awe vipi. Tunapotaka kujitoa katika ulitima tuliyomo inatubidi tuwe na ruwaza nzuri ya kufikiri kama tunaamini kwamba ufukara wetu ni kwa sababu tumeandikiwa hivyo, ni kwa sababu tumelogwa ni kwa sababu hutukusoma ni kwa sababu hii au ile hivyo hatuwezi kutoka humo kamwe hatutatoka na kuendelea kuwachukia wanao vuka vizingiti vya ufukara.

Lakini tukiamua kwamba wanaopata wamepata kutokana na kuamua kwao kupata na hivyo hata sisi tunaweza kupata kwa kukagua njia na mbinu walizotumia ni wazi hatuwezi kujichukia na hivyo kuwachukia hao bali tutajifurahia na kujifunza mengi kutoka kwao na ni dhahiri tutakuja kuvua koti la ufukara..

2 comments:
Andika Maoni Maoni
  1. Kuchukia mtu mwenye uwezo ni kukosa au kutotaka wengine waendelee. Na hii ipo sana watu wanajengeana chuki. Kwani maisha ni kuridhika ridhika na ulichonacho kama huna uwezo sio kujenga chuki.

    ReplyDelete
  2. Chuki chuki, kila mtu anamchukia mwenzie, hata masikini anamchukia masikini mwenzie.
    Je huu ni uungwana?

    jamani tupendane.....
    Kujengeana chuki hakufai ni kujiongezea msongo wa mawazo kwani kila unavyozidi kumchukia anayefanikiwa na ndio anazidi kufanikiwa, sasa si utajinyonga bure......

    ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi