0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Nov 20, 2008

ZIJUE CHANGAMOTO ZA KUFIKIRI VIZURI


Kama ulikuwa umepanda mbegu hasi, kufikiri kwako vizuri kutatawaliwa na changamoto, zisikutishe na usishindane nazo,ziache zipite.

Jana usiku nimepokea ujumbe kwenye simu yangu ya mkononi kutoka kwa msomaji wa blog hii.
Msomaji huyo alisema kwamba amefurahishwa sana na ujio wa blog hii ya utambuzi, hapo kabla alikuwa anasoma Gazeti la jitambue ambalo kwake lilikuwa ni kama dawa, kwani kila akikumbana na changamoto za maisha, basi akisoma gazeti la jitambue anapata majibu ya matatizo yake.

Baada ya gazeti hilo kusimama kuchapishwa, amekuwa na wakati mgumu sana, Lakini ujio wa blog hii ya utambuzi umemrejeshea matumaini makubwa, na sasa anaweza kumudu kupambana na changamoto, zozote za maisha zitakazomkabili.

Hata hivyo msomaji huyo alikuja na hoja, anasema kwa muda mrefu amekuwa akijibidisha kufikiri vizuri na pia amekuwa, akivuta anachokitaka akitumia mbinu alizojifunza kupitia katika gazeti la jitambue.
Amekiri kwamba yapo baadhi ya mabadiliko ameyashuhudia kwa kiasi fulani katika maisha yake, ingawa kwa upande wa kufikiri vizuri, zoezi hilo limekuwa gumu sana kwake, kwa sababu ameathirika sana na malezi yake ya utotoni.

Anadai kila akijaribu kufikiri vizuri zinatokea changamoto ambazo zinamtoa kwenye uzingativu hivyo, kuyumba kihisia, kiasi kwamba anatilia mashaka fikra zake, kitu ambacho ni kosa kubwa, katika kanuni hii ya kufikiri vizuri.
Baada ya kumaliza kusoma ujumbe wake niliamua kumpigia simu na kuzungumza nae.

Kufikiri vizuri kuna kanuni zake na kama hukuzifuata kufikiri kwako kutakuwa na walakini. Iwapo maisha yako yatakuwa yamejaa maumivu makubwa kihisia, au hisia zako zilikuwa zimekandamizwa kwa muda mrefu, ni lazima utakuwa unachokozeka kirahisi, kiasi cha kukufanya uwe na hasira za ziada.
Kwa kawaida mtu mwenye hasira za ziada si rahisi kumvumilia mtu au kuvumilia changamoto za maisha.

Ukweli ni kwamba tumechaguliwa kila kitu tulicho nacho katika maisha tunayoishi leo, tumechaguliwa dini za kuabudu, tumechaguliwa taaluma za kusomea, tumechaguliwa aina ya maisha tuanayoishi, tumekuwa sio sisi bali tumekuwa wazazi wetu ndugu zetu au jamii. Utakuta baba anataka uwe yeye, mama nae anataka uwe yeye, shangazi, mjomba, shekh, mchungaji, jirani, rafiki na kila mtu aliyekuzunguka anataka uwe yeye. Sasa wewe ukiwa wao utakuwa na miili mingapi?

Sisemi tusiheshimu maoni ya wazazi wetu, la hasha, bali namaanisha kwamba yapo baadhi ya maamuzi tunapaswa kuamua wenyewe aina ya maisha tunayotaka kuishi. Kwa sababu kila mtu yupo hapa duniani kwa lengo maalum. Tembea dunia yote hii hutakuta mtu yeyote anayefanana na wewe kwa kila kitu, labda sana sana, utasikia “Huyu anafanana na fulani” kwa maana ya kwamba kuna baadhi ya maeneo ameshabihiana na mtu fulani lakini huyo mtu sio yeye.
Kwa hiyo ile kuwa wewe, ni jambo la kujivunia, wewe ni mtu kamili na una umaalum wako, huhitaji kukamilishwa na mtu mwingine

Kimsingi kanuni ya kufikiri vizuri inahitaji mazoezi ya kutosha kwa sababu tumelelewa na kufundishwa kufikiri vibaya, kwa hiyo mawazo yetu yamekandamizwa sana kiasi kwamba hatukuwa na uhuru wa kufikiri tofauti na wazazi wetu.
Kama maisha yako yalitawaliwa na nguvu hasi nyingi, na labda umeshawahi kuwafanyia watu ubaya, kudhulumu au kuwaumiza watu wengine kihisia huko nyuma kutokana na kufikiri kwako vibaya, basi utakuwa umepanda nguvu hasi nyingi ambazo zitakuwa zimekuzunguka.
Kwa kawaida ukipanda nguvu hasi unavuna nguvu hasi, kwani huwezi kupanda mahindi ukavuna mtama, tunavuna kile tulichopanda.

Kwa kuwa ile nguvu hasi inakuwa inakuzunguka, ndio sababu maisha yetu yanakuwa, magumu. Kama mtu umeishi na nguvu hasi kwa muda mrefu, ukiamua kuanza kufikiri vizuri usidhani kuwa ile nguvu hasi uliyopanda kabla hujajitambua itakuacha, ni lazima itaendelea kukuzunguka, kwa hiyo wakati mwingine ukiwa unafikiri vizuri na kujenga uzingativu, nguvu hiyo inaweza ikaja ghafla na kukusomba na hivyo kukutoa kwenye kufikiri kwako vizuri.

Usipokuwa makini, wa kuzipokea changamoto hizo basi hutapata matokeo mazuri, kwa sababu kufikiri kwako vizuri kunategemea na imani uliyonayo juu ya kile unachofikiri na kuamini, kama imani yako ina mashaka, basi na kufikiri kwako kutakuwa hakuna maana.
Kinachotakiwa ni kupokea hizo changamoto, kwa sababu tulizipanda wenyewe kutokana kwamba tulikuwa hatujajitambua.

1 comment:
Andika Maoni Maoni
  1. great post. nikunukuu tena "tumechaguliwa kila kitu, shule, dini etc" kwa kuongzea, tunaendelea kuchaguliwa kila kitu kila siku. tunaendelea kuambiwa cha kufanya na tunaendelea kuishi maisha yetu ili kuiplease jamii au kuwafurahisha wengine kabla ya kuchagua tunayoyapenda sisi kwa hiyo tunakuwa wengine badala ya kuwa sisi.

    thanx

    ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi