0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Jan 27, 2009

JE KUNA UKWELI KWAMBA WANAWAKE WAZURI SANA HUWA HAWAOLEWI?

wanaringia uzuri wao


Watanzania wengi wanaamini, kwamba wanawake wazuri sana huwa hawaolewi. Kuamini huku bila shaka hakutokani na utafiti wowote uwe rasmi au sio rasmi. Lakini wengi wanaamini hivyo.

Je, imani hii ina ukweli kwa kiasi gani? Swali hili bila shaka ni gumu kujibika. Labda tu kwa mtu aliyefanya utafiti wa kutosha. Kwani kwa yule anayeamini atakwambia ni kweli na yule asiye amini atakwambia tu sio kweli bila kusema ni kwa vipi na pengine ni kwa nini.

Tunaposema wanawake wazuri tuna maana pana sana na yenye utata kwa kiasi kikubwa kwa sababu uzuri kama dhana dhahania inachanganya sana. Je wanawake wazuri ni wenye sifa zipi na hasa ni wazuri kwa akina nani na sio kwa wengine? Lakini kwa kusudi lakufikisha ujumbe huu tunaweza kusema wanawake wazuri ni wale ambao watu wengi watu wakiwatazama hukuballi kwamba wana maumbile au sura ambazo zinakubaliwa na maoni yao au maana ya uzuri kwa viwango ambavyo akili zao zinaamini.

Kuna ukweli wakutosha kwenye dhana hii kwamba wanawake wazuri hupata matatizo au kujijengea matatizo au vikwazo vya kuweza kuolewa Kwa nini? Kwanza ni suala la mila na desturi zetu sisi binadamu.Watanzania kama binadamu tunaamini kwamba wanawake wana dhima moja tu hapa duniani. Kumstarehesha mwanaume na pengine kusemwa ni pambo la nyumba.

Mtu anaweza kudhani mawazo haya ni ya jamii kama hizi zetu zilizo nyuma kimaendeleo. Lakini ukweli ni kwamba haya ni mawazo ya karibu dunia nzima hata kwa zile jamii zilizoendelea na ndio maana katika nchi hizo uuzaji wa miili kwa wanawake ni jambo lililopewa baraka na serekali na wana jamii wengi.

Kwa kuwa wanaume wa dunia hii wamelelewa na kujengewa dhana kuwa mwanamke ana kazi kubwa moja tu ambayo ni kumstarehesha mwanaume, humtazama mwanamke kama wanavyo tazama ua au mapambo mengine na huenda mbali zaidi na kumtazama mwanamke kama mashine ya kuwakatia kiu ya tamaa ya miili yao. Inakuaje?

Kwa kuwa kwao mwanamke ni mwenye sifa na nafasi hiyo hapa duniani, humtazama mwanamke kwa vipimo maalumu. Vipimo hivyo ni uzuri wake wa sura kama ilivyo ua na uzuri wa mwili kama ilivyo mashine zifaazo zaidi kwa starehe ya kimwili.

Kwa kuwa mwanaume humtazama mwanamke kwa njia hiyo ni wazi pia kwamba humtazama kama kiumbe dhaifu ambaye anahitaji kuhurumiwa, kutunzwa na kuambiwa afanye nini na asifanye kipi kinyume na hayo mwanaume hawezi kamwe kukubali kuwa na mwanamke ambaye ana kauli na anajua kwamba yeye ni mtu kamili na mwenye haki sawa na mwanaume.

Wanaume wengi wanaamini kwamba wanawake wengi wazuri wa sura na maumbile (labda) huwa wana matatizo ya kuwaringia wanaume. Kuwaringia wanaume kuna maana ya mwanamke kutokua tayari kuwa mtumwa wake na kifaa chake cha kukatia kiu ya kimwili. Kwa imani hiyo wanaume huwa waangalifu sana katika kushughulika na wanawake wazuri kwani huogopa kwamba watakua wakiteleza pale watakapokuwa wakitaka kuwabana.

Inawezekana kabisa wanawake wazuri hawana tatizo hilo. Bali wanaume ndivyo wanavyo amini. Kuamini ndiko kunapopelekea waogope kuwaoa.Wanaume huwa wanasema “mwanamke kama yule hafai kuoa labda kuchezea tu kwani ukimwoa atakusumbua sana…” Kauli kama hii ina maana kwamba mwanamke mzuri ukimwoa atataka kuwa na kauli kwa sababu ni mzuri nawe itabidi ukubali hili.

Lakini kwa upande wa pili wanawake wazuri nao wanapogundua kwamba ni wazuri huku wakiwa wanaamini kwamba uzuri wao ni silaha ya kuwapigia wanaume kamwe hawawezi kuolewa au wanaweza kujikuta ndoa zao hazidumu. Hii ni kwasababu kwa kuamini kwao hivyo hufanya mambo kwa kiwango cha kupindukia. Huwatenda wanaume yasiyopendeza kwa kuamini kwamba kwa sababu ni wazuri hawawezi kuachwa na hata wakiachwa wataolewa baada ya mda mfupi.

Bili shaka umeshawahi kusikia hata wanawake wenyewe wakisema “flani anautumia uzuri wake vilivyo anawaburuza kweli wanaume” Hii ina maana kwamba uzuri wao ni silaha nzuri ya kuwashikisha adabu wanaume.

Kwa woga wa kuburuzwa wanaume huogopa kuwafuata wanawake wazuri kwa hiyo unaweza kuona ni kwa vipi wanawake wazuri wanaweza kukosa kuolewa, yote inatokana na dhana potofu walizo nazo wanaume na hata wanawake kuhusu uzuru na mahusiano.

13 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Kaka Mtambuzi,

  Mimi naona hili ni dongo dhidi yetu.
  Mbona mimi nimeona ndoa nyingi za wanawake warembo wameolewa na wanaishi vizuri kwenye ndoa zao?

  Kwa mfano wapo wasichana wengi sana ambao waliwahi kushiriki mashindano ya urembo katika midhania tofauti na kupata mataji na sasa wameolewa na wanaishi kwa amani kwenye ndoa zao.

  kama huamini kamuulize Lundenga atakupa tawimu.
  Nadhani tatizo sio wanawake, bali ni wanaume ambao kwa mtazamo wao wanadhani wasichana warembo wana matatizo kitu ambacho si kweli, kwani wamezoea wasichana ambao watawaburuza lakini wale wenye msimamo, wanawaogopa, na hiyo imetokana na kwamba labda wasichana warembo nao sio wakuchezewa, wanakuwa na misimamo yao.

  Kuna mada zako nyingi nakubaliana nazo lakini kwa hili nakupinga.

  Naomba kuwasilisha.....

  ReplyDelete
 2. Hahahahaaaaa. Dada leo umeniacha. Yaani unaniambia kuwa ndoa ya mtu ni safi wakati hukai naye? Labda nikupe siri. Nimesikia juu ya ndoa ya wazee fulani (ambao wa bahati mbaya wamefariki) ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakilala vitanda tofauti ndani ya nyumba na hata watoto wao hawakujua mpaka mmoja alipofariki. Utamu na amani ndani ya ndoa ya mtu haionekani kwa aliye nje kama walio ndani wameamua.
  Nikirejea kwenye mada niseme kuwa kila kiumbe hujitahidi kutumia kila kilicho na uwezo wa kumpatia mahitaji yake (na ikiwezekana bila kuhangaika). Ni kama alivyoimba Lucky Dube kuwa "this is a give or ake world, so you gotta take what you can, when you can make the best of it". Ndilo lionekanalo hapo kuwa kwa kuwa watu huwachukulia wanawake kama viumbe dhaifu, basi pale wanapokuwa na nafasi ya kuweza kudhihirisha uwezo wao hufanya hivyo. Si wote na si kweli kuwa wanaume wako sahihi kwa namna wawafikiriavyo. Ninalohisi ni kuwa wapo watendao haya na wapo wengi wasiotenda lakini kwa kuwa mazuri mengi hufunikwa na mabaya ndio maana haya huonekana na kutaka kujua haya, hebu tathmini asilimia ya "warembo" duniani na angalia hata kama wote watakuwa na tabia hiyo watakuwa wanawakilisha asilimia ngapi ya wanawake?
  Wacha niwape nafasi wengine

  ReplyDelete
 3. Swala zima la mwanamke gani ni mzuri mimi hunipiga chenga.Naamini kwa wengi uzuri ni kitu cha kujifunza.Ukizaliwa mama aliyekuzaa hakutishi na labda mpaka ukue jamii na mazingira yakufunze ndio labda ugundue ana sura mbaya kwa mitazamo ya watu wengine. Ukizaliwa ulaya ya kasikazini utaaminishwa manamke mzuri ni yule mwenye nywele nyeupe mrefu na asiye na matako. Ukizaliwa Morogoro utasikia mwanamke mzuri lazima awe na tako.

  Wengine wamsifiao mwanamke mzuri mwenye macho ya kulegea, wakati kuna madaktari wa macho wamuonaye ni mgonjwa ahitajiye matibabu.

  Mimi naamini mwanamke mzuri anaoleka kirahisi na kwa kawaida ndiye afukuziwae zaidi na aaminiye huyo ni mzuri.Naamini ukizoea wanawake wa muonekano fulani, wanakuwa wa kawaida machoni. Mwanamke asifiwaye ni mzuri ambaye machoni mwako ni wa kawaida hata akuringie vipi unaweza usistukie.

  Katika ukuaji wangu nilichokuwa nasikia ni kuwa wanawake walioenda shule sana ndio wenye matatizo ya kuolewa kirahisi kuliko wanawake waitwao wazuri ingawa na kwa hili sina uhakika.

  Samahani kwa kuandika harakaharaka kwa mcharazo.

  ReplyDelete
 4. kaka Mubelwa na Kaka Kitururu, hata kama mukiitetea hi mada lakini nitabisha mpaka kesho, kwa mfano kaka kitururu kai divert hii mada kwa kusema kwamba wanawake wasomi ndio wenye matatizo ya kuolewa,nyie wanaume si mmezoea wale illiteracy wasiojua kutetea haki zao, wale wasioweza kusema no kwa wanaume?
  Kwa kulijua hilo mnakimbilia kutafuta miteremko.
  Hata hivyo wapo wanawake wasomi na wameolewa na maisha ya ndoa zao yako shwari.
  Labda nikubaliane na ninyi kwamba wapo wenye matatizo lakini sio wote, hapa naomba tuliweke swala hili kwenye mizani kisha tuangalie ni upande upi wenye kuzidi mwingine?

  ReplyDelete
 5. @Dada Koero:Nikinukuu nilicho sema:''Katika ukuaji wangu nilichokuwa nasikia ni kuwa wanawake walioenda shule sana ndio wenye matatizo ya kuolewa kirahisi kuliko wanawake waitwao wazuri ingawa na kwa hili sina uhakika.'' .

  Sikubadili mada dada kwa nilichosema.
  Nasijawahikufukuzia mdada pale bongo kwa nia ya kuoa bado, kwahiyo sina uhakika. Nafikiri nitakuwa na jibu nikianza kufukuzia wadada hivi karibuni pale Bongo kwa nia ya kuchukua wotewote.

  ReplyDelete
 6. koero mimi naamini wanawake wote ni wazuri ukiwemo wewe kwa sababu wote wana kazi sawa mbele ya mimi mwenye hasira za kuvimba vimba bila kujigonga (tehe tehe teheeeeeee) kama dini yako inasema ni dhambi shauri lako hilo!

  unajua binadamu hupenda kulinganisha saana. unaangalia tako, jicho, nk kama alivyosema MKODO. lakini haturidhiki. aliye na mwembamba anatamani kumjaribu mnene na mwenye mnene hivyo hivyo. mfupi sawa.

  turudi kwenye mada. tatizo ni mawazo yetu ya kingono ngono. koero anadhani nitamtongoza ndio maana anabania namba ya simu. na mimi namwangalia kama dili fulani. hapo ndipo lilipo tatizo kwamba ngono kwetu imekuwa utashi na sio uhitaji. tunazidiwa na wanyama wanaojua ni wakati gani wa kufanya ngono.

  koero unazungumzia haki, kwamba kuna wake wasiojua haki zao, mimi sielewi haki ninini kama ni kujilinganisha au la!

  sijui kwa nini unatanguliza wanawake kusema no kwa wanaume badala ya kujadiliana. huo ni mfumo babe. inabidi tujadiliane na sio kubaniana na kukataliana kila kitu. mwishowe mtazikimbia ndoa zenu harafu mtake kurudi tena.

  mimi naamini wanawake ni wazuri wote kwani sifa tu ya kuwa mke, ni sifa tosha kwa Mume. mingine ni maneno ya mkosaji ya sizitaki mbichi hiizi nk.

  ReplyDelete
 7. naona kama vile wote mnazungusha maneno kama vile wale watu wanojiita wanautambuzi, hawajulikani wamesimamia wapi? (Samahani kaka kaluse kwa kusema hili) Ukweli ni kwamba najitahidi sana kusoma mada za utambuzi lakini naziona kama vile ziko kichwa chini miguu juu.
  Kwa hiyo nikisoma maoni Kamala, naona ni yale yale.

  Nadhani huu mjadala utanishinda kwa kuwa nabishana na midume mitatu ambayao yote imelelewa katika mfumo dume, mpaka leo wanaamini kuwa wao ndio kichwa cha nyumba, sijui nyumba za wajane zinakuwaje maana kichwa kimeshaondoka.

  Naona sitaweza.

  ReplyDelete
 8. koero acha woga, karibu kwenye utambuzi uone mambo kwa picha pana zaidi mtoto

  ReplyDelete
 9. Kamala siutaki utambuzi wenu.
  Mimi nimeshajitambua kivingine.

  Lakini bado nasisitiza kwamba wanawake wazuri wanaolewa tena kwa kasi ya ajabu.

  kama mnataka ndio hivyo na kama hamtaki ndio hivyo hivyo.......

  ReplyDelete
 10. koero ungekuwa na kiboko ungechapa mtu. dah. punguza hasira na misimamo mingine ni bora kuitunza moyoni badala ya kuitoa hadharani kwa sababu kila kitu ubaadirika na vitaendelea kubadilika usije kesho kubadili misimamo harafu ikawa noma

  ReplyDelete
 11. Wadau,

  Naomba niweke wazi kuwa sijakasirika kabisa kuhusiana na huu mjadala, bali huwa nina kawaida ya kuonesha msisitizo wakati ninapowakilisha maoni yangu.
  lakini kama maoni yangu yameonesha aina fulani ya hasira, nadhani hiyo ni tabia mbaya ambayo inabidi niiache.

  Nadhani nilionesha hisia zangu katika kiwango cha juu sana, kitu ambacho si kizuri katika mijadala ya aina hii.

  Basi naoamba kuchukuwa fursa hii kuwaomba radhi kaka Kamala, kaka Mubelwa, kaka Kitururu, na wengine ambao labda kwa njia moja ama njingine wemekwazwa na maoni yangu.
  Hivyo vilikuwa ni vijimambo tu.
  Tusonge mbele.

  ReplyDelete
 12. Hfffuuuuuuu! Imenibidi kupumua kwanza baada ya kusoma mjadala huu. Kushika tama kidogo. Kutafuta namna ya kukaa vizuri maana nusura nidondoke. Mambo ya mjadala na moto wake.

  Wanawake wazuri hawaolewi? Nadhani kama ilivyowekwa bayana na Mkodo, uzuri unategemeana na mtazamo wa jamii na mara nyingine mtu binafsi. Lakini hata hivyo, tafsiri finyu inayotumika na wanaume wengi ni kwamba mwanamke mzuri lazima awe anavutia. Kuvutia huku kunatokana na zingatio la tamaa za mwili kuliko maeneo mengine muhimu katika ukuaji wa mahusiano.

  Mtazamo wangu unaweza kuwa tofauti na watangulizi wangu. Hata hivyo, unatokana na kile ninachokiona katika jamii. Kwamba, kila mwanamke mzuri ninayemfahamu mimi, kaolewa! Kama hajaolewa kuna tatizo jingine lisilohusiana na "uzuri" (soma mwonekano) wake.

  Sababu ni kwamba uzuri ni mtaji mzuri wa mwanamke yeyote kwa wanaume wenye fikra kwamba sura ama maumbile ndicho kigezo pekee cha kuhandisi mahusiano. Sasa iweje mwanamke mzuri, kwa maana ya kuvutia asiolewe?

  Manake kama hivyo sivyo, kwamba wanawake wazuri hawaolewi, basi tukubaliane kwamba wanawake wanaoolewa ni wale wabaya (kama wapo kweli)! Na ikiwa hivyo, wataolewaje wanawake wabaya kama ni kweli kwamba wanaume wanavutiwa na sura?

  Kwa sababu ninachojua mie ni kwamba mwanamke yeyote huamini kwamba yeye ni mzuri. Vyovyote awavyo. Na hii hutegemea na jinsi alivyojengwa na familia yake. Kigezo cha uzuri wake chaweza kuwa tofauti sana na kile cha mwanamke lakini hiyo haimfanyi ajihisi kwamba si mzuri.

  Sasa kama hoja ni kwamba wale wanaoonekana kuwa ni wazuri(wa sura) hujenga kiburi fulani cha kuwaendesha wanaume, basi tuseme kila mwanamke anaweza kuwa na kiburi hicho hicho katika mahusiano kwa sababu, kama nilivyosema, kila mwanamke hujiona kwamba ni mzuri.

  Ninachojaribu kuonyesha hapa ni kwamba tatizo la mwanawake kutokuolewa linaweza kuelezwa kwa maelezo mengine zaidi ya mwonekano wa nje( sura, pua, umbo, kimo, wembamba nk) na kwa maana hiyo lisihusiane na mwonekano wake, uwe mzuri ama mbaya.

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi