0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Dec 13, 2010

FURAHA LAIZER (OHAA MASAI) TUTAKUKUMBUKA DAIMA

Marehemu Furaha Laizer (Ohaa Masai) siku ya Graduation yake

Ni siku ya jumanne ya Disemba 7, 2010, majira ya saa nne asubuhi niko ofisini, nikiendelea na kazi zangu kama kawaida. Nilikuwa na jukumu la kukamilisha ripoti yangu ya juma lililopita ambayo niliilaza kiporo kutokana na kutindikiwa na kazi nyingi siku ya Jumatatu

Nakumbuka nilijihimu sana kufika kazini, nilifika kazini saa kumi na mbili na nusu alfajiri, lakini sijui ni kutokana na uchovu au ilikuwa ni uvivu tu, nilijikuta mpaka kufika saa nne asubuhi nilikuwa sijakamilisha ripoti yangu.
Nikiwa bado naendelea na kazi zangu kivivu-vivu mara simu yangu ikaanza kuita, niliinyanyua na kuangalia jina la mpigaji, hakuwa mwingine, bali ni rafiki yangu aitwae Masudi ambaye nimezoea kumwita Soudy.

Nilipokea simu ile, lakini sauti ya rafiki yangu huyu ilikuwa ni ya huzuni na hata salamu yangu hakuijibu na badala yake alisema tu kwa kifupi “Sir Kaluse, Ohaa Masai hatunaye, amefariki hivi punde” nilibabaika sana nakujikuta nikimuuliza maswali mfululizo. Amepatwa na nini? Amepata ajali au? Ameugua? Lakini kabla Masudi hajanileza sababu ya kifo chake simu yake ilikatika ghafla. Nijipojaribu kumpigia simu yake ikawa haipatikani. Nilichanganyikiwa sana mpaka wenzangu pale kazini wakawa wananishangaa.
Nilianza kuwapigia watu wa karibu na Masudi lakini nilijikuta nikiwa ni mtoa taarifa, kwani hakuna hata mmoja ambaye alikuwa anazo taarifa hizo, na hata mmoja wa wajomba zake ambaye nilikuwa na namba yake ya simu ilikuwa haipatikani.
Wiki iliyopita nilikuwa na huyu kijana niliyeambiwa kuwa amefariki, na nilikutana naye katika Grosary maarufu pale maeneo ya Tabata Bima barabara ya Umoja maarufu kama RN Grosary.
Furaha Laizer ndio jina lake kamili,alikuwa ametimiza umri wa miaka 19 hivi karibuni na ndio amemaliza kidato cha nne akisubiri majibu yake ya mitihani.
Nakumbuka tulizungumza kwa kifupi sana kwa sababu aliniambia kuwa kuna mahali anawahi, na nilikuwa nimemuomba aje kwangu kuniwekea antenna ya TV, na aliniahidi kuwa angekuja mwishoni mwa juma ambapo hata hivyo hakutokea, na badala yake napokea taarifa kuwa amefariki dunia!
Nilikuwa nikijaribu mara kwa mara kumpigia Masudi simu lakini bado ilikuwa haipatikani. Majira ya saa sita nilifanikiwa kumpata masudi na alinijulisha kuwa simu yake iliisha chaji kutokana na kuwapigia watu wengi kuwajulisha juu ya msiba huo mzito, na kutokana na habari hiyo kuwastua watu wengi aliowapigia, alikuwa na wakati mgumu kuelezea sababu iliyopelekea kifo cha Furaha Laizer maarufu kwa jina la Ohaa Masai.
Masudi alinijulisha kuwa siku ya Jumatatu majira ya saa mbili Furaha akiwa amelala, aliamshwa na bibi yake kwenda kumdhibiti mjomba wake ambaye ana matatizo ya akili, kwani alikuwa akifanya fujo mtaa wa jirani. Alikuwa anawafanyia fujo akina mama wauza chapati kwa kumwaga chapati zao.
Furaha alifika katika eneo la tukio na wakati anamsogelea huyo mjomba wake, mjomba wake mwingine aliyekuwepo hapo alimwambia asimsogelee kwa kuwa alikuwa ameshika chupa mkononi, lakini tahadhari ile ilikuwa imechelewa kwani yule mjomba mwenye matatizo ya akili alirusha chupa ile na kumpata Furaha katika paji la uso upande wa juu wa jicho la kushoto.
Furaha alipepesuka na kukaa chini na kwa muda mfupi uso ulivimba kiasi cha jicho moja kufunga. Kwa kushirikiana na majirani mjomba yule mwenye matatizo ya akili aliweza kudhibitiwa na kufungwa kamba na kupelekwa nyumbani.
Furaha aliongozana na mjomba wake aitwae Ibrahim maarufu kwa jina la Timber kwenda Kituo kidogo cha Polisi (Police Post) pale Tabata shule na alikuwa akitembea mwenyewe. Alipofika hapo kituoni aliandikisha malezo yeye mwenyewe na kupewa PF 3 ambapo alikwenda Tabata Hospitali pale pale Tabata shule na hakuonekana kama ameumia sana zaidi ya ule uvimbe.
Alipofikishwa pale na mjomba wake ghafla alianza kupoteza nguvu na hivyo kulazimika kukalishwa chini. Baada ya kumuona daktari walishauriwa wampeleke Hospitali ya Amana, iliyoko Ilala. Waliondoka Tabata na baadhi ya ndugu zake wengine akiwemo bibi yake na jirani yao aitwae Jane Mmari. Walifika Amana majira ya saa nne asubuhi, na wakati huo alikuwa akitokwa damu mdomoni na puani na wakati mwingine alikuwa akitapika damu. Walipomuona daktari waliambiwa wampeleke akapigwe X-Ray.
Baada ya kupiga X-Ray, ikaanza dana dana kutoka chumba kimoja hadi kingine, na kila wanapoingia chumba cha daktari wanaambiwa wamekosea sio chumba hicho wanaelekezwa kumuona daktari mwingine na wakimuulizia daktari walioelekezwa kumuona wanaambiwa ametoka na wamsubiri. Dana dana hiyo iliendelea hadi saa nane mchana bila mgonjwa kupatiwa matibabu, na hadi kufikia wakati huo Furaha alikuwa akizimia na kuzinduka mara kwa mara. Baada ya kuona hakuna msaada wowote wanaoupata tangu wamfikishe mgonjwa pale hospitalini.
Masudi aliamua kumpigia mmoja wa rafiki zake aitwae Elia Ulaya ili afike pale kusaidia. Elia alifika mjira ya saa nane mchana na baada ya kuona hali ya mgonjwa ni mbaya na hakuna msaada wowote wa kitabibu alitoa ushauri warudi Tabata katika Hospitali ya Madona. Walipofika Madona daktari aliposoma ile X-Ray akawashauri warudi Hospitali ya Amana, kwa kuwa ile kesi ni kubwa, lakini kutokana na kukatishwa tamaa na huduma za Hospitali ya Amana wakakata shauri waende Hospitali ya Temeke.
Walifika Temeke majira ya saa kumi na mbili jioni na baada ya kutoa maelezo daktari wa zamu alianza kumuhudumia mgonjwa kwa kumuwekea dripu. Lakini baada kuchungza zile X-Ray akatoa rufaa mgonjwa apelekwe Muhimbili na alitoa ambulance ili mgojwa awahishwe.
Walifika Muhimbili majira saa nne usiku na walikalishwa mapokezi mpaka saa sita usiku na ndipo wakaelekezwa wampeleke katika wadi ya Moi, na wakati huo mgonjwa alikuwa hajitambui kabisa ingawa kuna wakati alikuwa akipepesa jicho moja kwa sababu la pili lilikuwa limefunga kabisa kutokana na uvimbe.
Daktari aliyempokea mgonjwa alichunguza X-Ray waliyokuja nayo na akashauri kuwa mgonjwa anatakiwa kufanyiwa uchunguzi mwingine na kifaa kiitwacho TC Scan. Baada ya kutoa ushauri huo aliwataka wale waliomleta mgonjwa waondoke abaki mtu mmoja ambapo walitoka na kukaa nje na kumuacha mjomba wake na Furaha peke yake. Walikaa pale nje wodini hadi saa kumi alfajiri ndipo wakakata shauri warudi nyumbani.
Masudi anadai kuwa hadi anarudi nyumbani hakuwaza kuwa Furaha angefariki kwani yule daktari aliwatoa wasiwasi kwa kuwaeleza kuwa ile hali a kupoteza fahamu ni tatizo la muda tu kwani kuna wagonjwa ambao hupoteza fahamu kwa wiki nzima na huja kuzinduka na kupona kabisa.
Alipofika nyumbani alilala kidogo na aliamka majira ya saa mbili hivi, akiwa njiani kuelekea Hospitali majira ya saa nne alipigiwa simu na rafikie aitwa Elia na kupewa taarifa kuwa Furaha amefariki muda mfupi uliopita, baada ya kupigania roho yake kwa takriban masaa 26.
Baada ya vipimo vya mwili wa marehemu ilikuja kugundulika kuwa alikuwa amepasuka fuvu la kichwa na hivyo damu kuvuja ndani ya ubongo kitu ambacho, ni vigumu sana kupona, labda kwa miujiza ya mwenyezi mungu.
Tulimzika Furaha Jumatano Disemba 8, 2010 saa kumi na mbili jioni katika makaburi ya Mbagala, mahali ambapo niliambiwa ndipo walipozikwa babu yake na ndugu zake wengine.
Ni msiba ambao umenigusa sana na sitakaa nimsahau kijana huyu Furaha ambaye alikuwa na furaha wakati wote kama jina lake.
Mimi sipendi kutoa sifa za kinafiki eti kwa kuwa amefariki, lakini naomba nikiri kuwa Furaha alikuwa mtu wa watu, ingawa alikuwa ni mdogo kwa umri na mrefu kwa kimo lakini alikuwa amejijengea marafiki wengi wakiwemo wazee, vijana wa rika lake na pia hata wadogo kwake. Alikuwa akimuheshimu kila mtu na alikuwa tayari kutoa msaada pale anapohitajika kufanya hivyo.

Ni jambo la kusikitisha kuwa Dunia imepoteza nguvu kazi na tegemeo la kesho kwani pamoja na kuwa alikuwa akiendelea na masomo yake ya Sekondai lakini pia alikuwa akisaidiana na mjomba wake kazi za ufundi umeme na hadi kifo kinamkuta alikuwa ni fundi umeme mzuri japo hakuhudhuria masomo hayo chuoni.

Katika mojawapo ya mazungumzo yangu na yeye, aliwahi kuniambia kuwa anatarajia kusomea uhandisi hususan wa umeme, hiyo ndio ilikuwa ndoto ya kijana Furaha Laizer.

Ni kweli ametutoka na tutaendelea kumkumbuka daima, lakini pia ametuachia changamoto kuwa na tahadhari na watu wenye matatizo ya akili hata kama ni mtoto wako wa kumzaa. Pia kuna haja ya familia zenye watu wenye matatizo ya akili kuwapeleka katika hospitali zenye wodi maalum za kuwatunza watu hao, kwani kukaa nao majumbani ni sawa na kuishi na bomu ambalo litakuja kutulipukia hapo baadae. Ni kweli tunawapenda na tungependa kuishi nao karibu lakini kuna hatari kubwa kuishi na watu wa aina hiyo.

Ni wengi wameguswa na msiba wa Furaha, na ni vigumu sana kuamini kuwa hatunaye, lakini ni vyema tukikubali matokeo kwani kazi ya Mungu daima haina makosa.

Namuomba Mwenye-Enzi Mungu ailaze roho ya marehemu Furaha Laizer mahali pema Peponi, Amina

8 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Kwa kweli maisha ni mafupi sana. Polni sana wafiwa, ndugu jamaa na marafiki wote kwa kuondokewa na kija huyu Furaha. Mwenyezi
  ungu na aipokee roho yake na aiweke mahali pema peponi Amina. Tutakukumbuka daima.

  ReplyDelete
 2. R.I.P Furaha wewe umetangulia sisi tutakuja. Poleni wafiwa wote ndugu jamaa na marafiki. Inasikitisha sana.

  ReplyDelete
 3. Kila kifo hakikosi sababu, na hiyo ndio njia yetu, mungu amlaze mahali pema peponi. Na pole sana kwa kupoteza rafiki muhimu, yote ni mapenzi yake Muumba!

  ReplyDelete
 4. mimi nikotofauti na wachangiaji waliotangulia kaluse nikuulize hilitukio lilitokea kweli lakini halikutokea dar lilitokea Arusha na aliyesababisha kifo cha huyu mwanafunzi ni kichaa ambaye naye aliuwawa palepale na mwanafunzi huyu hakufia hospitalini alifia palepale alipopigiwa habari ndiyo hiyo

  ReplyDelete
 5. Annony hapo juu, naona unataka kuanzisha mjadala mwingine usio na maana, hivi kuna sababu gani ya mimi kudanganya? Inawezekana lipo tukio ambalo limetokea huko Arusha kama nasibu (Coincidence)likawa linafanana na hili.

  Sitaki kupoteza muda kulumbana juu ya jambo hili. Nimeandika makala hii kama kumbukumbu ya rafiki yangu huyu ambaye ametangulia mbela ya haki. kuanza kubishana kama alifia Arusha au Dar, haiwezi kutusaidia wala kurejesha uhai wake.

  Yatupasa tumuombee apumzike kwa amani

  ReplyDelete
 6. Inasikitisha sana!:-(

  Tatizo huduma ya wagonjwa wa akili kama huduma nyingine ni MBOVU sana Tanzanina.

  Ukifuatilia tukio hili utagundua hilo kwani Mwenye MATATIZO ya akili yuko nyumbani bila msaada wa wataalamu, aliyeumizwa ni shughuli kuhudumiwa.....nk.

  R.I.P Furaha Laizer!

  ReplyDelete
 7. kaluse sina ugomvi na wewe tena hii glob yako napendaga sanab kutembelea haipiti siku sijachungulia mimi sina ugomvi na wewe labda stori zimelingana hembe jaribu kuchunguza hili tukio kama hutaona zimelingana pls kama nimekukwaza nisamehe sion thamiri yangu lakini narudia tena jaribu kuchunguza hili tukio utaona kweli limetokea arusha tena mwaka huuhuu pole kama nimekukwaza sio thamira yangu

  ReplyDelete
 8. Annony, sio kwamba umenikwaza, lakini nilishangazwa na neno la mwisho ulilotumia la kusema "habari ndio hiyo"

  Halikuwa neno zuri kulitumia, hata hivyo naamini pia kuwa kulikuwa na mgongano wa matukio, na ningefurahi pia kupata habari ya huyo kijana wa Arusha kwa undani ili nayo niiweke hapa kibarazani na wengine wapate kujifunza.

  Pia ningependa kukushukuru kwa kuwa msomaji mzuri wa blog hii ya utambuzi, nasikitika kuwa nimekuwa mbali na mtandao kwa muda mrefu sasa lakini nitajitahidi kadri ya uwezo wangu kuendelea kublog kama zamani.

  Ahsante sana kwa kunitembelea na changamoto pia.

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi