0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Oct 1, 2009

UJUMBE WA SIMU: VIFO NA TALAKA


Simu hizi, mara nyingi huleta balaa

Nimekuwa nikisikia kuhusu vurugu za ndoa zinazotokana na simu za mkononi. Kwa upande wangu nilikuwa sijawahi kupambana na tukio lolote la kindoa linalohusu simu hadi hivi karibuni. Nimekuwa nikiamini kwamba simu zinaweza kusaidia mtu kujua kama mwenzake yuko kwenye uhusiano wa nje au hapana. Hadi sasa naamini hivyo, lakini, naamini pia kuwa zinaweza kuzua mtafaruku na kuvunja ndoa wakati hakuna jambo la maana.

Mimi Binafsi kwenye ndoa yangu sijawahi kuwa na uhusiano nje. Lakini kwa mazingira ya kazi yangu, nimezoeana sana na wanawake na pia wanaume. Nataniana sana na wanaume na wanawake, kiasi kwamba, kama mtu hajui anaweza kudhani nina uhusiano na wanawake hao.

Simu yangu hupata ujumbe wa aina mbalimbali ukiwemo wa utani kutoka kwa wanaume na wanawake. Utani huo unaweza kuwa wa kimapenzi, kifamilia, kikazi au mwingine mwingi. Kwa kazi yangu utani huu hunipa nguvu na hisia za ukaribu na watu, lakini kubwa zaidi hunifanya niwe mtani wa wanawake wengi wanaonifahamu kuliko kuwa kitu kingine.

Wiki kadhaa zilizopita kwa bahati mbaya au kwa kusudi, mke wangu alifungua ujumbe ulio kwenye simu yangu. Aliposoma alikutana na ujumbe wenye neno Dear. Bila shaka neno hilo likiwa limeandikwa na mwanamke, lilimfanya kuuliza maana ya neno lile.
Hakujali ujumbe ulisema kitu gani, bali alijali neno Dear. Kidogo lilitutikisa. Lakini mambo yaliisha.

Lakini walisema muonja asali haonji mara moja. Nadhani aliona kusoma ujumbe unaotumwa kwenye simu yangu kunamfanya apate nguvu au kuthibitisha anachotaka kuthibitisha, Siku nyingine tena kwa kile kinachoitwa bahati mbaya, alisoma tena ujumbe kwenye simu yangu.

Ujumbe huu sasa ulikuwa na neno Darling, sio Dear tena. Pamoja na neno hilo kulikuwa na maneno yenye kuonesha kwamba, aliyeniandikia anataka tuwe wapenzi na tushiriki tendo na kwamba, angependa anipeleke mahali kwa siku mbili na nisije nikaanza kumkumbuka mke wangu.

Kwa kweli nadhani ujumbe huu na hasa neno Darling, ulimvunja nguvu mke wangu kiasi kwamba, alilia kwa muda mrefu wa usiku. Nilihuzunika kwa hilo. Lakini nilijiambia na kujiuliza, ‘alikuwa na haki gani kukagua ujumbe kwenye simu yangu?’ Ukweli ni kwamba, simu ni yangu na watu ninao wasiliana nao , nawajua mimi na najua ni kwa nini nawasiliana nao kwa namna fulani. Yeye akisoma ujumbe wa aina yoyote, atafanya majumuisho yake na sio ya hali halisi.

Kwa mfano, mwanamke huyu ambaye, mke wangu alisoma ujumbe wake alianza kuniita Darling, baada ya siku moja kimzaha kuniuliza, ningependa kuitwa nani na yeye, bosi, mheshimiwa, baba fulani, au jina langu. Nilimuuliza, ‘mbona umesahau kutaja neno Darling?’ Kwa utani, kuanzia siku hapo akawa ananiita Darling.

Ujumbe aliousoma mke wangu, ulikuwa ni utani, ambapo alikuwa anasema, akija kunitembelea atanipeleka mahali na kwa sababu mimi najifanya naaminika, nimwombe mke wangu ruhusa ya siku mbili kwamba naenda semina. Tulijibizana kwa muda mrefu kwa ujumbe katika mzaha kama tulivyokuwa tumezoea.

Bila shaka kila mmoja kati yetu alikuwa huru, kwani kila mmoja alijua kuwa anachokifanya ni mzaha. Lakini hata kama mtu mwingine angetulia, ujumbe ule ulikuwa unaonesha utani wa wazi kabisa. Lakini kwa mke wangu ingekuwa vigumu kuona mzaha ndani ya ujumbe ule. Siyo kwake tu, bali hata kwako na kwa mwingine, ingekuwa hivyo. Kwa nini?

Hapa ndipo panawaumiza wengi kwenye suala la ujumbe kwenye simu. Hadi mtu achukue simu ya mpenzi wake na kuanza kukagua ujumbe uliotumwa humo au majina ya watu walio kwenye orodha ndani ya simu hiyo, ni lazima ana wasiwasi na mwenzake. Kwa sababu ya wasi wasi huo, chochote atakachokiona ambacho kinaonesha dalili za kukosa uaminifu, hatatumia akili kukipima, bali ataendeshwa na mihemko.

Ni kweli simu za mkononi zinatajwa kama moja ya vitu vinavyoweza kusema kama mtu anatoka nje. Kwenye kitabu chake, hayati Munga Tehenan cha Mapenzi Kuchipua na Kunyauka, anasema kuhusu mtu kupigiwa simu na kukimbia kwenda kusikilizia mbali na mahali mwenzake alipo.

Nimesoma makala kadhaa zinazohusu madhara ya simu za mkononi, lakini sijaona ujumbe au Message zikipewa uzito. Ujumbe hauna uzito kwa sababu kinachoonekana kwenye ujumbe ni mwendelezo wa jambo ambalo mtu asiyehusika na ujumbe huo hawezi kulijua.

Najaribu kufikiria namna ambavyo mke wangu angejisikia endapo angesoma ujumbe niliokuwa nimetumiwa na rafiki yangu siku nne nyuma kabla ya tukio hilo. Huyu rafiki yangu tunafahamiana sana na alituma ujumbe unaosema, ‘Kama unataka nimwambie mkeo unapomalizia fedha zako sawa. Mwenyewe anajua ana mume mwaminifu kweli, kumbe hajui jitu lina nyumba ndogo kila wilaya ya mkoa wa Dar.

Huu ulikuwa ni mzaha kutoka kwa huyu jamaa yangu. Lakini kwa mke wangu huu usingekuwa mzaha, kama ambavyo haikuonesha kuwa ni mzaha kwenye maelezo ya yule mama. Ndilo tatizo la ujumbe. Unakuwa hujui kitu kimeanzia na kinakwenda wapi.

Ninachotaka kusema hapa sio kuwambia wapenzi kwamba ujumbe wowote wa kimapenzi kwenye simu hauna maana. Kuna wakati ni kweli ujumbe husika una maana hiyohiyo inayosomeka. Kupitia ujumbe, mtu anaweza kumfumania mwenzake. Lakini, kwa sehemu kubwa ujumbe wa simu hauna nguvu na unaweza kusababisha ndoa kuingia doa na hata kuvunjika bila sababu.

Ni jambo la hekima kwa mwanamke au mwanaume kumchunguza au kufuatilia nyendo za mwenzake moja kwa moja. Kama unadhani mumeo au mkeo siyo mwaminifu, ni vyema kutumia mtu au watu wakafuatilia nyendo zake. Kama kweli anatoka nje, hauwezi kuzidi mwezi mmoja kabla hujapata ushahidi kuhusu jambo hilo. Huna haja ya kutegemea robo taarifa kama hizo za ujumbe wa simu. Ni kweli kwamba kuna matumizi mabaya ya simu kutumika kutongozana, kutaarifiana kuhusu uhusiano na mengine. Lakini siyo kila ujumbe wenye kunuka mapenzi una maana ya mapenzi.

Ninachowapenda waislamu kwenye ndoa ni lile suala la fumanizi. Wanasema ili ithibitike kwamba, kweli mtu amezini, ni lazima kitendo hicho kithibitishwe wakati kinatendeka na wanokithibitisha ni lazima wawe watu wanne. Kwa nini nawapenda kwa hilo?

Kuna mazingira mengi ambapo mtu anaweza kuamini kabisa kwamba, mwenzake anatoka nje. Hata anapowasimulia wenzake nao watampambisha moto kwa kumwambia, ‘haiwezekani, ni lazima wana uhusiano,’ wakati hakuna jambo kama hilo. Tunaona sana mambo haya kwenye sinema zinazooneshwa kwenye televisheni zetu.

Kwa upande wangu naweza kusimama na kuzungumzia ukweli kuhusu ujumbe wa simu kwa sababu, nina uzoefu wa kutosha, ambao umenisaidia kujifunza. Hata kabla ya uzoefu huo, nilishapata uzoefu mwingine unaohusu simu ambao unaonesha kwamba, ni lazima kuna ndoa nyingi sana zinayumba au kuvunjika kwa sababu ya simu, iwe ujumbe au kupiga kabisa.

Nikipi kinasema kweli, ni tabia ya mtu kama tunavyoijua au ujumbe tuliouona kwenye simu? Nafikiri kuwa unamjua vipi mume au mke wako, ndilo jambo la msingi kwanza. Kama humwamini, ni lazima utapata mazingira ya kuthibitisha wasiwasi wako. Utachakura kwenye simu yake, utapekua mkoba wake, utakagua mifuko ya nguo zake na hata ‘diary’ yake utaikagua kila wakati. Kwa sababu lengo ni kuthibitisha kwamba siyo mwaminifu, ni lazima utathibitisha.

Kwa uzoefu wangu wa simu za mkononi na uhusiano, ninaingia wasiwasi mkubwa kwamba, kwa kadiri simu hizi zinavyokuwa nyingi mikononi mwa watu na hasa wapenzi, ndivyo ambavyo mapenzi yanaporomoka. Badala ya kusaidia kukuza uhusiano, zinasaidia kuvunja uhusianvo lakini wamiliki wa simu hizi ndio ambao wanapaswa kulaumiwa.

Kushinwa kujua kwamba, simu kila mmoja ni yake na yaliyomo ndani ya simu ni yake na yeye ndiye mwenye kujua maana yake, hilo huwaumiza wengi. Niliwahi kupokea ujumbe kwenye simu ambao unasema, ‘kumbe umeshikwa na mkeo, wewe mpumbavu kweli. Kumbe umekuwa unapoteza bure muda wangu.’ Kabla sijakaa sawa, nikatumiwa ujumbe mwingine na mtu huyo huyo akisema, ‘Kama unaona vipi tuachie hapahapa kabla hatujafika mbali, tusije kuumizana bure.’

Ilibidi nimpigie simu huyo aliyetuma ujumbe huo. Nilipomwambia kwamba huenda amekosea namba , alikiri.
Lakini alisema kuna mtu ameanza kufanya naye biashara na amegundua kuwa kila kitu ni hadi mke wa huyo jamaa aamue. Hivyo ameamua kumwonya, kwani kwa sababu hiyo tayari wameshapata hasara.

Je mke wa huyo jamaa angeuona ujumbe ule kwenye simu ya mumewe angeelewa hivyo? Sio rahisi, angeelewa kwamba huyo mwanamke ni hawara wa mumewe na anataka wavunje uhusiano kwa sababu hampi anachokitaka, yaani kuwa naye muda mwingi au wote.

Ubaya wa ujumbe ni kwamba huwezi kuzuia usiingie, tofauti na kupigiwa,ambapo unaweza kukata simu au unaweza kuacha mtu azungumze wakati simu umeiweka mbali.

Hapo hakuna ushahidi unaoachwa, Ujumbe huacha ushahidi ambao ni dhaifu sana, hata hivyo. Kama nilivyosema awali, kuna kuvunjika kwa ndoa kwingi sana, kutokana na simu za mkononi.

Lakini bahati mbaya ni kwamba, kuna kuuana au kujiua au kuuawa ambapo chanzo ni simu za mkononi. Ni kwa nini binadamu awe kipofu kirahisi kiasi hicho?Kwa nini simu ndio imfundishe kuhusu mwenzake, badala ya mwenyewe kumjua mwenzake?

Habari hii iliwahi kuandikwa katika gazeti la Jitambue

4 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Katika ndoa kwa kweli yataka sana uaminifu. Kwa sababu usipomwamini mwenzako basi raha ya ndoa haitakuwepo hakutakuwa na amani. Ila kuna wakati inabidi mwanamke awe na wivu, akose uaminifu na pia upande mwingine pia. Ila inasemekena kwamba ni rahisi kutambua mwanamume kama anatoka nje kuliko mwanamke akitoka nje. Labda hili ndio tatizo kwasababu wanamume akitoka nje basi mawazo yake yote yanakuwa huko tu. Anaacha kabisa kumthamini mke wake.
  Ni kweli hizi simu zinaletesha sana ugomvi maana kila mtu anatafsiri atakavyo yeye. Lakini Jingine kama unajua mke/mume wako ana tabia ya nini kuacha msg kama hizo na kuleta ugomvi?

  ReplyDelete
 2. Hatari nyingine ya ujumbe wa simu hii hapa: http://matondo.blogspot.com/2009/08/utafiti-kuendesha-gari-huku-ukituma.html

  ReplyDelete
 3. Kaluse, mkeo kabila gani? Duh! Una bahati wewe!!! Angekuwa wangu mulyenchoka huo mkono wenye bandeji angeuvunja ili usipate nafasi ya kubofia...lol

  hauko peke yako dear...oops!!! isije ikaleta tena mushkeli...lol


  Lakini hasa wivu wanini?

  ReplyDelete
 4. Ni kama umemaliza, lakini napenda kuonesha kuunga mkono katika kile kikuu ndani ya makala hii.
  Binafsi nina utani saana na kinadada na kinakaka. Wengine ni hawa ninao-blog nao hapa. Neno Dear na hata Babygal si geni katika jokes za chat na sms.
  Labda kama ulivyosema hapo kuwa "Ni jambo la hekima kwa mwanamke au mwanaume kumchunguza au kufuatilia nyendo za mwenzake moja kwa moja." Lakini napenda kulipeleka hili pande zote za ndoa. Nijuavyo mimi ni kuwa ukioa ama kuolewa UNAPOTEZA SEHEMU YA WEWE na hivyo kutakiwa SEHEMU YA MWENZAKO kujazia pengo unalopoteza kwako. Hii ina maana unastahili kupoteza baashi ya raha zako na hata karaha na kujazia na raha na karaha za mwenzako. Ndio maisha yalivyo.
  Kumjua mwenza wako ni jambo la muhimu kuliko maelezo. Lakini kujua kuwa mwenza wako anaweza kuwa na madhaifu fulani nalo ni la msingi. Kwa hiyo kama pande zote zitajua nyapi yanamkwaza mwenzake na yapi yanaweza kubadilishwa yote na yapi ya kupunguza itasaidia. Kama mtu ana wivu anastahili kuupunguza kwani ukizidi utajikuta unakuwa na suluhisho kabla hujakutana na tatizo. Yaani kwa wivu wako utajua kuwa mumeo ama mkeo analala nje ya ndoa hata kabla hujamuona akisalimiana ama kuongea ama kumtembelea ama kutaniana na mwenzake wa jinsia tofauti. Na ukishajijengenea mazingira hayo, kila kitu kitakuwa utakavyo na kama ulivyosema Kaka Kaluse, mtu ataishia KUDHIHIRISHA KUWA ANATENDA badala ya KUTAFUTA UKWELI KAMA ANATENDA AMA LA.
  Mental pictures determines our actual futures na kama tutakuwa na mawazo kuwa LAZIMA ANATEMBEA NJE YA NDOA basi kila wakati tutamuona akifanya hivyo.
  Niliwahi kuandika kuwa kila kizuri ni kibaya kwa spidi ileile. Na huu ni mfano tosha. Ndege inakwenda kasi na kukufikisha kwa haraka, lakini ikiporomoka wanaokufa kwa kasi ni wengi kuliko treni na yo ni wengi kuliko basi ama gari dogo na inapungua mpaka wale wanaokufa kwa kujikwaa, kwani mwenye kujikwaa ni mwenda pole.
  Sasa tunaona kuwa simu zinaharakisha mawasiliano na kudumisha mahusiano, lakini upande wa pili wake unabomoa mahusiano kwa kasi kuliko barua.
  Ni sehemu ya maisha. Na Mume na mke wote wana wajibu wa kujua mapungufu ya wenzao na kisha kujitahidi kutoyachochea huku wakistahili kuwasaidia kuwa na ujasiri katika hayo.
  Labda mume mwenye mke mwenye wivu na ajitahidi kupunguza matani kwenue jumbe za simu wakati akimueleza mkewe kuwa kuna tofauti kati ya sms na hali halisi ya maisha na vivyo hivyo mke atambue kuwa mumewe alikuwa na utani na hataweza kuuacha wote. Kwa hiyo sehemu ya utani huo itabidi aikabili.
  SOTE TUNAWEZA KUWA SAHIHI KWA KUWA SOTE HATUKO SAHIHI

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi