0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

http://www.serenahotels.com/serenadaressalaam/default-en.html

Oct 17, 2009

KINDUMBWENDUMBWE CHA MAISHA!!!

  • Ilikuwa ni siku moja Kibaha na mimba ikatungwa sawia.
  • Mama akaiba redio nikimwona, asubuhi akasema ni binti.
  • Picha ikaletwa kimzaha, lakini hali ikabadilika ghafla sana.........................


    Nilikaa na wale jamaa kwa siku tatu tu, lakini niliona mambo ambayo binadamu anaposimuliwa anaweza kudhani kwamba kuna dhihaka anayotakiwa kufanyiwa, yaani haiwezekani.

    Niliondoka Dar Es Salaam siku ya ijumaa kwenda Tanga. Nakumbuka ilikuwa ni August mwaka 1995. Nilikuwa nakwenda kwa jamaa ambaye aliniita kwake kwenda kumsaidia kukagua shughuli fulani ambazo alitaka kuzifanya. Wakati ule nilikuwa najitegemea, nilikuwa sijaingia serikalini kiajira.

    Nilifika mjini Tanga na kumkuta mwenyeji wangu na mkewe wakiwa kituo cha basi wakinisubiri. Tulisalimiana na walisema wamefurahi kunifahamu nami nilisema nimefurahi kuwafahamu. Ilikuwa ni mara yetu ya kwanza kukutana. Walipewa jina na mawasiliano yangu na jamaa yangu mmoja.

    Nilifika nao nyumbani kwao na kukaribishwa vizuri sana. Walikuwa wakiishi Raskazoni. Ilikuwa ni nyumba ya kifahari kwa kweli. Lakini nilibaini kwamba mama au mke wa yule mwenyeji wangu ndiye aliyekuwa na kauli pale nyumbani. Kwa kipindi cha saa moja tu tangu kufika nilipata picha hiyo bila matatizo.

    Wakati wa kula chakula cha usiku, nilitambulishwa kwa watu wa nyumba ile. Haikuwa nyumba ya watu wengi. Kulikuwa na watoto watatu wa yule mwenyeji wangu. Mkubwa alikuwa wa kiume aliyekuwa na umri kama miaka tisa, wa pili wa kike na wa tatu wa kike pia. Halafu kulikuwa na ndugu wa kiume wa mwanamke, kijana ambaye alikuwa ndio kwanza amemaliza kidato cha nne.

    Halafu kulikuwa na msichana wa kumsaidia kazi za ndani au house girl kama wanavyoitwa. Hawa wote nilitambulishwa kwao hapo mezani wakati wa kula. Lakini wakati tunakaribia kumaliza kula msichana mwingine mwembamba mweusi alikuja pale mezani na kukaa kitini, karibu wote tulikuwa tumeshashiba.

    Alianza kujipakulia chakula bila kusema neno. Ilikuwa inaonesha kwamba alikuwa ametoka kufanya kazi kwenye sehemu yenye maji kwani gauni lake lilikuwa na majimaji.
    Nilijua ni msaidizi wa ndani pia. Lakini niliona kwamba sio haki kumtendea vile , yaani kumwacha afanye kazi wakati wengine wanakula . lakini sikuwa nimeenda pale kwa sababu ya upelelezi.

    Nilianza kazi yangu iliyonipeleka pale usiku ule. Nilipewa chumba kilicho karibu kabisa na sebule, ilikuwa nifanye kazi ya kupitia mafaili kadhaa kabla sijaandika tarifa yangu ya kuwasaidia wale jamaa kupata walichokuwa wanahitaji. Naomba nisiseme ni kazi gani hasa. Kwa hiyo nilikuwa nimepania kufanya kazi hadi usiku mkubwa sana kama sio alfajiri.Nilianza kazi kwenye saa nne, nikimwacha mwenyeji wangu na familia yake hapo sebuleni, wakiangalia televisheni. Ilipofika saa sita usiku nilihisi kiu. Niliamua kuvumilia, lakini kiu ilinizidi na niliamua kwamba ningekwenda tu jikoni kutafuta maji ya kunywa.
    Nilitoka chumbani mwangu na kuelekea jikoni ambako bado kulikuwa na taa iliyokuwa ikiwaka. Nilipofika jikoni nilishangaa kukuta kukiwa na mtu. Alikuwa ni yule msichana ambaye sikutambulishwa kwake. Alikuwa anamalizia kuosha vyombo ilikuwa inakimbilia kwenye saa sita na nusu usiku.

    “Pole sana, naomba maji ya kunywa, samahani.” Yule binti aliitika kwa kusema “sawa baba”, huku akiinama kwa heshima. Aliniletea chupa ya maji kutoka kwenye jokofu. “Hapana, napenda ya moto, kama yapo” nilimwambia. Aliitikia kwamba yapo na kunichukulia chupa mezani hapo jikoni nilimwangalia na kugundua kwamba alikuwa analia.

    Kwa kuwa nilishangaa wakati ule wa kula, na hapa saa sita na nusu za usiku mtoto wa miaka 14 au 15 anasafisha vyombo na halafu kule kulia, nilijua kulikuwa na jambo. Nilimuuliza kama analia, na alisema hapana. Nilimwambia, ni usiku na anatakiwa kwenda kulala. Alisema anakwenda kulala.
    Nilikuwa na uhakika alikuwa analia na alikuwa pia anajitahidi kufuta machozi ili nisijua. Kalikuwa ni kasichana kadogo, kazuri sana pamoja na kufujwa kule. Kama ningekuwa kijana bado ni wazi ningeoa msichana wa aina ile. Bahati mbaya zaidi ni kwamba mke wangu alifariki miaka mitano tu nyuma na nilikuwa bado na maumivu. Hisia zile ziliniumiza zaidi.

    Nilirudi kule chumbani nikiwa nimeanza kuingiwa na wasiwasi. Lakini sio wasi wasi tu bali hata huruma. Kwa nini awe yule binti, na kwa nini sikutambulishwa kwake?
    Sikupata jibu

    Sikupata jibu. Ile hali ya kusafisha vyombo hadi saa 6:30 usiku, tena peke yake huku akilia, ilinikera sana, na nilijiambia siondoki pale bila kujua kitu kuhusu binti yule. 8:30 nilisikia kama miguu ya mtu huko sebuleni, nilihisi kwamba angekuwa ni yule binti. Hali hii ilinifanya niwe na hofu kidogo, kwa sababu mawazo yangu yalikwenda kwenye ushirikina hasa kwa kuamini kwangu kwamba, hapo Tanga palikuwa na ushirikina sana.

    Nilizima taa ya chumbani mwangu pole polepole na kuchungulia. Aliyekuwa hapo sebuleni alikuwa ni mke wa yule mwenyeji wangu. Alikuwa amevaa gauni lake la kulalia na alikuwa anachukua kitu juu ya kabati ya sebuleni. Nilivutiwa kutazama zaidi. Niliona akichukua redio fulani ndogo nzuri sana ambayo hata jioni ile niliiona na kuitamani.

    Bila shaka kwa shughuli za yule mwenyeji wangu, kuwa na vitu kama redio ya aina ile lingekuwa ni jambo la kawaida. Yule mama aliichukua redio ile na kuitia kwenye mkoba wake mkubwa wa kike na aliuweka mkoba huo kwenye kabati nyingine ndogo pale sebuleni. Halafu aligeuza na kurudi chumbani mwake.

    Nilirejea chumbani mwangu nikijiuliza ni kitu gani hicho. Nilishindwa kujua yule mama alitaka kuipeleka wapi ile redio, na kwa nini aliiweka kwenye mkoba wake, usiku kama ule. Sikuweza kupata jibu , bila shaka hata kama ingekuwa ni wewe ingekuwia vigumu kupata jibu. Niliamua kuendelea na kazi nyangu.

    Kwenye saa kumi kamili usiku nilisikia mtu huko sebuleni. Nilifungua amlango wangu wa chumba na kugundua kwamba ni yule binti. Alikuwa anafanya usafi. Niliwaza. Kulala saa saba na kuamka sa kumi alifajiri! Lakini kwa nini iwe ni yeye tu. Hilo likawa ndilo swali. Niliamua kulala nikiwa nimeumia sana.

    Kwenye saa 12:30 asubuhi nilishtushwa na kelele za kilio cha mtu. Mtu huyo alikuwa akipigwa hapo sebuleni. Nilitaka kurejea kulala, lakini ilikuwa vigumu kwangu kutokana na kipigo na kelele hizo. Niliamua kufungua mlango wa chumba changu na kwenda sebuleni.

    Yule binti wa usiku na alfajiri ambaye nilikuwa sijajua jina lake ndiye aliyekuwa akipigwa. Alikuwa akipigwa na mke wa mwenyeji wangu kwa mkanda. Kutokana na kauli za mama yule na yule binti mwenyewe , ilionekana kuwa alikuwa akituhumiwa kuiba kitu fulani. Mwenyeji wangu na wanaye pamoja na yule house girl walikuwa wakishuhudia kipigo kile kama vile wakiangalia sinema..

    “Shangazi mimi sikuiba,siwezi kuiba, mimi sio mwizi” Yule binti alikuwa akilia kwa maumivu na alikuwa amelala chini akiwa hoi.
    Yule mama aliponiona aliacha kumpiga na aliondoka kwenda chumbani kwake huku akisema, “Nikija jioni nikute redio yangu, ama marehemu mama yako anilipe”
    “Yaani mtoto kila siku wewe tu ndio kisirani ndani ya nyumba. Nimeshamwambia mjombako wewe ni kibwengo na mikosi haitaisha humu ndani……

    Nilijua ni ile redio ambayo yule mama alikuwa ameiweka kwenye mkoba wake ambao bado ulikuwa pale juu kabati ndogo pale sebuleni. Nilijua kwamba, yule binti alikuwa akipigwa kwa kuonewa kabisa.
    Lakini ni mimi tu na yule mama ndio tuliokuwa tunaujua ukweli huo, halafu na mungu.

    Nilimtazama yule binti pale chini alipokuwa amelala kwa maumivu na nilihisi tu machozi yakinidondoka, Ingawa nilikuwa sijajua, yule msichana ni nani pamoja na kwamba likuwa akimwita yule mama shangazi, kwangu alionekana kuwa binti mwenye adabu na hekima pia.

    Baada ya kunywa chai yule mke wa mwenyeji wangu akiwa hayupo , nilimuuliza yule mwenyeji wangu kuhusu yule binti. Aliniambi yule binti ni mtoto wa marehemu dada yake, ambaye alimzaa na mwanaume ambaye mama yake alikuwa anadai kwamba walikutana tu kwa bahati mbaya na hakujua kama alipata ujauzito. Hivyo hakuwa na anuani yake kamili. Huyo dada yake alifariki miaka sita iliyopita akimuacha yule binti na umri wa miaka minane.

    ‘Ndio nikamchukua, lakini kumbe alishaharibika na kwa kweli anatusumbua sana. Ni msichana ambaye hata shule alikataa, alipomaliza tu la saba. Na kazi yake ndio hiyo ya wizi, kama hakuiba redio, simu, saa, deki basi utapata kesi ya umalaya.

    Kama siyo hivyo basi umbeya mtupu. Mtaa wote unapata habari zinazoenda nyumba hii, basi tu sijui inakuwaje, siju ni laana kutoka huko kwa upande wa baba yake…….!

FUATILIA KISA HIKI CHA KWELI KESHO......................

1 comment:
Andika Maoni Maoni
  1. Ninanukuu “Shangazi mimi sikuiba,siwezi kuiba, mimi sio mwizi” Yule binti alikuwa akilia kwa maumivu na alikuwa amelala chini akiwa hoi.
    Yule mama aliponiona aliacha kumpiga na aliondoka kwenda chumbani kwake huku akisema, “Nikija jioni nikute redio yangu, ama marehemu mama yako anilipe”
    “Yaani mtoto kila siku wewe tu ndio kisirani ndani ya nyumba. Nimeshamwambia mjombako wewe ni kibwengo na mikosi haitaisha humu ndani…… mwisho wa kunukuu.

    Kweli duniani hapa kuna watu wana roho ngumu. Nasubiri muendelezo kesho.

    ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi