0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Mar 18, 2009

NAKUBALIANA NA MAFUNZO YA UTAMBUZI PALE KIMARA

Tunakerwa zaidi na watu tulio karibu nao
Nakubaliana na mafunzo ambayo nimeyapata kwenye madarasa ya Utambuzi ya Kimara. Moja ya yale ninayokubaliana nayo ni lile la kwamba, ukitaka kubadilika kutoka kwenye tabia usizozipenda kwenda kwenye tabia nzuri, anzia kwa watu walio karibu yako zaidi. Anzia kwa mumeo, mkeo, watoto, ndugu au jamaa zako wa karibu sana.

Nakubaliana na hilo kwa sababu, watu wanaotukera kirahisi ni wale ambao tuko karibu nao zaidi. Kwa nini? Kwa sababu, matarajio yetu kwao ni makubwa, kwa maana kwamba, tunaamini kuwa wanatakiwa kututendea vema, kutujali na kutusaidia. Lakini pia ni kwa sababu, kuna wakati tunatarajia watu hawa watujazie mapengo yetu ya kihisia na kiroho ambayo tunayo. Kwa mfano, mtoto wa mjombako akishindwa masomo hutajali na kuumia sana kama ambavyo ingekuwa kwa mtoto wako. Hapa kwa sehemu kubwa unaumizwa na kushindwa kwa mwanao kukupa sifa, kwamba, ‘mtoto wa fulani ana akili.’

Kwa hiyo, kuna ukweli kwamba, maudhi tunayoyapata kwa watu wa familia zetu ni makubwa na yenye maumivu zaidi kuliko yale ambayo tunayapata kutoka kwa watu wengine.
Je, kuna mtu yeyote katika famila yako au ukoo wako ambaye ni kero kwako? Unadhani huyo jamaa yako anayekukera anasababisha kushusha ari yako ya utendaji wako kazini kwa kuwa unapokuwa unafanya kazi anakujia mawazoni mara kwa mara?
Kumbuka tu kwamba, unaweza kutembea na mkeo au mumeo kichwani mwako kutwa nzima. Unaweza kutembea na kero za shemeji yako au dada yako kwa mwaka mzima, kila siku kero zake zinazunguka kichwani mwako kama vile ndizo pekee zilizoko hapa duniani na hakuna kingine cha kuwaza.

Je, katika familia yako kuna mtu yeyote ambaye ana tabia ya kukupinga au anayekupa ushauri mkali wa kudhalilisha na afanyavyo hivyo anakukumbusha hali yako mbaya ya kifedha au ubaya wa umbo na muonekano wako?

Kuna wakati unajiona umechoka kimwili au kuwa katika hali mbaya kutokana na mazungumzo machafu yaliyopita au tatizo ambalo bado halijatatuliwa kati yako na mwanafamilia mwenzio?
Unakumbana na hali hiyo baada ya mazungumzo ya simu au baada ya kutembelewa na mmoja wa ndugu zako wakorofi, na ili kupunguza mawazo unajiingiza katika ‘kulakula’ , unywaji wa pombe, utumiaji wa dawa za kulevya au mambo mengine yafananayo na hayo?
Je, kuna wakati unajikuta huna fedha au huna furaha kwa sababu unajaribu kumsaidia mwanafamilia ambaye haoneshi shukurani zozote kwa msaada unaompa? Inaweza kuwa msaada wa mawazo, fedha au ukarimu wowote wenye lengo la kumfanya ajihisi vizuri.

Je, kisirisiri ungependa familia yako ingekuwa isiwe na migogoro kama ilivyo sasa, au ingekuwa ni familia ambayo mnasaidiana wenyewe kwa wenyewe?
Endapo dalili kama hizi unazo, kuna namna mbili ya kukabiliana nazo. Ya kwanza na ya kawaida ni kukataa. Watu walio wengi wanajaribu kudharau kwamba kuna mambo yanachanganya akili katika familia zao.

Kwa upande mwingine, kuna njia bora ya kukabiliana na hali hii—kutumia mbinu zilizothibitishwa kwa kuboresha uhusiano wa kifamilia.
Kuliko kuyaacha matatizo ya kifamilia yaendelee na kukuathiri kisaikolojia, kuna hatua ambazo unaweza kuzichukua, ikiwa ni pamoja na:

Jenga uhusiano bora zaidi na wanafamilia ambao unadhani ukiwa nao unakuwa na amani. Hakikisha kwamba, unatenga dakika chache kila wiki au kila mwezi kuimarisha uhusiano na watoto, binamu, wakwe na ndugu wengine ambao siyo wakorofi na wanaojali.
Unaweza kumuomba hata mmoja wa wanafamilia ambaye anaheshimika sana kuzungumza kwa niaba yako siku ambayo unakuwa na mzozo wa kifamilia na mmoja wa watu wakorofi sana katika familia yenu.

Jikumbushe kila inapowezekana sababu ya msingi kwa nini unajaribu kujifunza namna ya kuishi na mtu huyu. Inaweza kuwa huyu mwanafamilia ambaye hamuivi, amemwoa mtu katika familia yako ambaye mnaheshimiana sana na hutaki umuudhi. Au yaweza kuwa kuishi na mtu mkorofi na anayekupa changamoto namna hii ni nafasi yako mwafaka ya kujifunza kuhusu utulivu, kujiwekea mipaka n.k.
Au inawezekana kwamba wewe na huyu mtu mwingine wote ni wakorofi na kwa hiyo kikao hicho cha familia kinaweza kutafuta mwafaka. Kumbuka inahitaji watu wawili wakorofi, mambo kwenda ndivyo-sivyo mara zote.

Badala ya kumruhusu mtu huyu kukuchukulia kama busati la kukanyagia mlangoni, simama imara lakini kwa ukomavu. Usimjibu kwa hasira anapokuudhi, njia ya kiutu uzima na yenye nguvu ni kujiwekea ‘mipaka ya huruma.’ Unaweza kuwa na huruma, lakini ukawa imara na kusema, ‘nakujali na najua nawe unanijali. Hebu tuchukue muda mfupi kati yetu mimi na wewe ili kujadili cha kufanya ili mawasiliano yajayo ya simu au kutembeleana kutakakofuata kumfurahishe kila mmoja wetu.’

Badala ya kujibu kwa kupayuka kama mtoto mdogo, nimegundua katika kuzungumza na watu wa karibu yangu, ambao zamani tulikuwa hatuivi, kwamba unapotoa maneno ya kuhurumia unakuwa kama meneja bora anayekabiliana kwa hekima na mfanyakazi mkorofi, na utaonekana umekomaa na ni mtu mzima.

Kwa kuzungumza kwa huruma na upendo, utakuwa unazuia kila mmoja kujiona ni zaidi ya mwenzie kati yako na huyu jamaa yako mkorofi. Badala yake utabadili hali hii kutoka kufokeana na kuwa mjadala ambao utafufua mambo mazuri na ya kujenga kati yenu.

Kama jamaa yako huyu ni mkorofi sana, usijiwekee matarajio makubwa sana kwamba atakubali kukaa kiti kimoja kirahisi. Badala yake Jiwekee malengo madogo ambayo yatakufanya ujisikie umefanikiwa. Kwa mfano, kama maongezi ya simu ya dakika 10 au kumtembelea kwa saa mbili ndiyo muda muafaka katika kujadiliana na mtu mkorofi, usikubali kuongea naye kwenye simu kwa dakika 60 au kumtembelea kwa siku saba mfululizo. Badala ya kujenga itakuwa kubomoa.

Au kama jamaa yako huyo anapenda sana kukupa ushauri mwingi, weka malengo mengine sahihi kwa ajili ya mawasiliano kama: ‘Nitasikiliza kwa kipande cha kwanza cha ushauri na kumwambia, ‘Hilo ni wazo zuri nitalifikiria.’ Inapokuja kwa wanandugu wakorofi, ni vizuri mawasiliano yawe ya muda mfupi, wakati huohuo usisahau kusema, ‘sihitaji kumbadili mtu huyu tabia yake—nahitaji kubaki na afya yangu, mtu niliyetulia bila kujali anafanya nini.’

Kumbuka kwamba, kuna watu wengi wakorofi, ambao hawataki kukubali ukweli wa udhaifu wao. Mara nyingi ni watu wasiojiamini na ambao wamejaa hofu na mashaka na chuki za maudhi ya huko nyuma kutoka kwa watu waliowaamini sana, wawe wazazi au wapenzi.
Kama una mume, mke, au ndugu wa aina hii ni vigumu sana kumsaidia ili abaini kasoro zake. Kwa kadiri unavyojitahidi, ndivyo unavyoharibu, kwani unawatisha zaidi na kuwafanya waamini kwamba, wewe una matatizo. Lakini, wanachoshindwa kukiona ni ukweli kwamba, wenyewe huwa wanakorofishana na kila mtu wanayekuwa naye karibu. Hapa usikubali kuumizwa bure!

Badala ya kurudia mawasiliano kama ya zamani ambayo hayakusaidii kwa miaka na miaka, kwa nini usijaribu kitu kipya safari hii—andaa shughuli fupi ambayo ina uwezekano mkubwa wa kuleta matunda mazuri kwa faida yenu wote wawili.
Kwa mfano, kuna shoo ya muziki mahali mnaweza kwenda pamoja; mnaweza kwenda matembezini pamoja; au mnaweza kupiga picha ya pamoja mkiwa mmekaa kwa amani kama


Kumbukumbu. Hakikisha kwamba unaweka angalau mazingira ambayo anaweza kuona aibu kama anataka kurejea kwenye ukorofi wake. Kumbuka jambo moja muhimu sana kwamba, huwezi kumbadili mtu hapa duniani. Kama yupo mtu unayeweza kumbadili, basi ni wewe mwenyewe. Kwa hiyo, ndugu na jamaa wakorofi, wapenzi na wapendwa wakorofi, huwezi kuwabadili, labda wenyewe watake kubadilika. Hii ina maana unatakiwa wewe kubadilika.

Kubadilika kuliko bora ni kuwaacha hao wakorofi waishi kwenye dunia yao waitakayo bila kukuhusisha.

No comments:
Andika Maoni Maoni

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi