0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Feb 25, 2009

POLE DADA KOERO

Ndio maisha dada yangu.

Nimesoma kwa makini sana makala ya dada yetu Koero Mkundi inayelezea changamoto inayomkabili katika maisha. Nimeisoma makala hiyo huku nikiwa na hisia tofauti kwa jinsi alivyojieleza.
Kwanza nilijibainisha na yeye kwa maana ya kusimama katika nafasi yake ili kupata hisia kama mtoto ambaye anatakiwa kumsikiliza mama yake au wazazi wake na kufuata yale wazazi wanayoyataka bila kupewa nafasi ya kujiamulia mustakabali wa maisha yake, halafu nilijibainisha na mama yake ili kujua ni namna gani mama anajisikia pale ambapo ushauri wake unapopingwa na mwanae aliyemzaa mwenyewe.

Sisi tumezoeshwa kwamba wazazi ndio wanawajibika kutuamulia aina ya maisha tunayotakiwa kuishi, kwenda kinyume na maamuzi ya wazazi ni utovu wa nidhamu usioweza kuvumiliwa.Sio kosa la wazazi kuwa hivyo bali ni malezi waliyopitia ambayo kwa mujibu wa mazoea hayo ndio malezi yanayotakiwa kwa watoto, kwa hiyo, kama wao, wanataka na sisi tupitie barabara hiyo hiyo waliyopitia bila kujiuliza kama malezi hayo bado yana nafasi sasa hivi, wakati dunia imebadilika sana?

Labda niwaulize wasomaji wa blog hii, Hivi mfumo wa elimu tulio nao unamuandaa mtoto kukabiliana na changamoto za dunia hii tuliyo nayo leo?

Ukweli unaoumiza ni kwamba mfumo wetu wa elimu hautusaidii katika kufikia malengo yetu na badala yake unatuandaa kuwa waajiriwa, kwa maana ya kuwatumikia matajiri wenye fedha, tunatumia miaka mingi shuleni tulikariri nadharia za wengine zisizo na tija katika kutuwezesha kufikia malengo yetu na matokeo yake ni kujikuta tukitumikia fedha badala ya fedha kututumikia sisi. Kama ulisoma makala ya mazungumzo yangu na Malisa, nadhani utakubaliana na kile alichokisema juu ya udhaifu wa mfumo wetu wa elimu hapa nchini.

Kumshauri mtoto kusomea taaluma fulani, eti kwa sababu ina ajira yenye mshahara mnono na marupurupu mengine, ni ushauri uliopitwa na wakati na usiofaa kwa dunia ya leo. Kama ushauri huu ulitolewa na wazazi wetu miaka ya 60 au 70, ulikuwa na mshiko kwa sababu kipindi hicho nchi ilikuwa na uhaba wa wasomi na nchi ilikuwa ikihitaji wasomi ili kuijenga, lakini ushauri huu kuurudia katika kipindi hiki ni kichekesho.
Kwa nini nasema ni kichekesho, ni kwa sababu, soko la ajira limejaa ushindani mkubwa, tofauti na zamani. Wakati tunawashauri watoto wetu wategegemee ajira, lakini ajira hizo haziwasaidii kufikia malengo yao, sasa ushauri huu una faida gani?

Unasoma elimu ya msingi miaka saba, elimu ya elimu ya sekondari miaka sita, halafu chuo miaka minne mpaka sita, ukimaliza unaajiriwa, kisha unaoa, unazaa watoto unawasomesha unafikia umri wa kustaafu, unapumzika na huenda pia maisha yakawa mabaya zaidi kwa kuwa hukujiwekea akiba ya kutosha matokeo yake unabaki ukigombana na watoto wako kuwa hawakujali pamoja na kwamba umewasomesha. Mlolongo huo unahamia kwa watoto nao kwa mtindo huo huo wa malezi, mduara unaendelea.
Hivi ndivyo wazazi wetu wanavyotaka tuishi, wanataka watupangie mustakabali wa maisha yetu kwa hofu kuwa tukishindwa huenda tukashindwa kuwabeba wakizeeka, zote ni hofu tu za kuhofia kesho.

Pamoja na kwamba dunia imebadilika na inaendelea kubadilika lakini bado wanataka malezi waliyolelewa nayo miaka ya 1947 bado yapewe nafasi. Bado wanataka kufuata mlolongo ule ule wa malezi waliyopewa na wazazi wao. Nadhani kuna haja ya wazazi kuukubali ukweli huu kwamba malezi waliyopitia hayana nafasi tena, kwani dunia imebadilika sana.
Kama mzazi, inawezekana akawa na ushauri kwa mtoto juu ya mustakabali wa maisha yake, lakini kama mtoto anayo malengo yake na anajua ni kitu gani anahitaji katika maisha yake basi apewe ushirikiano katika kufikia malengo yake aliyojiwekea badala ya kuburuzwa kuelekea njia asiyoitaka.

Ningependa kuungana na Kaka Mubelwa Bandio, Nuru Shaabani, Markus Mpangala, Kaka yangu Simon Mkodo Kitururu na wasomaji wengine waliojitokeza kukufariji na kukupa ushauri, nami kama wao naomba urudi nyumbani ukae na mama na baba na kama unao kaka na dada zako ni vyema ukawashirikisha kwenye kikao hicho ili upate kueleza kile kilicho moyoni mwako bila kuficha, weka wazi malengo na matarajio yako na usisite kueleza mafanikio ya biashara yako, kama yapo ili wajue kuwa uko timamu na kile unachokifanya, naamini kwenye watu wengi hapaharibiki neno.

Nakutakia kila la heri, malengo yako yatimie kama ulivyopanga.

3 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Asante sana Kaka Kaluse.
  Nilimpa POLE Da Koero. Nilimpa pole kwa kuwa ana msongo wa mawazo na si kwa kuwa anapambana na apambanayo. Nataka apambane nayo kisahihi na ndio maana sikumpa pole. Labda kwa ufupi ni kwamba sikumpa pole kwa kuwa nampenda na namtakia mapambano mema.
  Akipambana vema atapata suluhisho jema na atakuwa amejifunza kitu na kufundisha kitu pia. Yaani tusimpe mgonjwa dawa kisha tukampa pole. Tumpe pole kama dawa inampa kizunguzungu ama side effect zozote.
  Tumeungana naye kwenye hili, tumempa changamoto mbalimbali za kufuata na sasa atapanga na kuchagua lililo jema kwake na familia yake maana sisi (kama ilivyo kwa mama yake) tuna mitazamo ambayo yawezekana haimfai ama haiiangalii kutoka katika "angle" tuliyopo.
  Koero. Hii ni changamoto na lazima utaipita. Kumbuka, "harder the battle, tougher the fight, SWEETER THE VICTORY"
  Blessings

  ReplyDelete
 2. Hodii mwenyewe hapa. haya nitarudi kutoa yangu maini

  ReplyDelete
 3. Habari za siku kaka Mtambuzi,
  Ningependa kuchukuwa nafasi hii kutoa shukrani zangu za pekee kwako,
  Kwanza kwa kunipa pole na pili kwa yale uliyoyaandika humu.
  Kusema ukweli naona kama umefunga mjadala, kwani sina cha kuongeza kwani ulichoandika utadhani ulikuwa kichwani mwangu, na kwa taarifa yako nime-print hii article ili nikirudi Dar nimpe mama aisome.
  Naamini atakubaliana na hiki ulichokiandika hapa.
  Ahsante sana kwa kutuelimisha ki utambuzi.

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi